Sheikh Rajab Katimba Kaimu Katibu wa BARAZA KUU Akisoma Taarifa ya Waislam kwa Vyombo Vya Habari Msikiti wa Mtambani |
Kwa
Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu
JUMUIYA
NA TAASISI ZA KIISLAM (T)
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
17 Mfungo Sita 1436
9 Januari 2015
TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA
KIISLAM TANZANIA KUPITIA VYOMBO VYA HABARI KWA WATANZANIA WOTE, JUU YA MUSWADA
WA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI NA.
02, WA MWAKA 2014, HUSUSAN KUHUSU SEHEMU YA MAREKEBISHO KWENYE SHERIA YA TAMKO
LA SHERIA ZA KIISLAM
Awali
ya yote tunapenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu,
Ardhi na vilivyomo, na Rehma na Amani zimfikie Kiongozi wa Ummah Mtume Muhammad
(SAW).
Ndugu wanahabari,
Assalam
Alaykum Warahamatul llah Wabarakatuh.
Tumekuiteni
hapa kwa lengo la kueleza kuhusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
Na. 02, wa mwaka 2014 haswa kuhusu marekebisho kwenye sheria ya tamko la Sheria
za Kiislamu. Tunafahamu kuwa kuanzia tarehe 13 hadi 23 Mwezi huu wadau
mbalimbali wataitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba kwa ajili ya
kuwasilisha mapendekezo yao, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania tukiwa
sehemu ya wadau muhimu tunapenda kuwaeleza kuwa mtiririko wa mchakato wa
marekebisho ya sheria kwa mujibu wa muswada huu unaokusudia kutambua Mahakama
za Kadhi Tanzania bara una kasoro kubwa na kwa dhati unaonesha wazi kuwa
serikali haina nia ya kweli ya kuunda Mahakama ya Kadhi yenye hadhi kamili ya
kimahakama na uthabiti wa kuwepo kwake na kuwa muswada huu ni hadaa nyingine ya
serikali hii ya CCM kwa Waislamu kwa sababu zifuatazo:-
1.
Malalamiko
juu ya Mahitaji ya Mahakama ya Kadhi yana historia ya kupindishwapindishwa na
serikali hii inayoundwa na CCM. Kwa mfano katika Ilani ya CCM
mwaka 2005 iliahidi kuanzisha Mahakama ya Kadhi lakini kwa ghilba nyingi CCM
haikutekeleza ahadi hiyo baada ya kuingia madarakani kwa hoja kuwa hili ni
jambo la Kikatiba.
Hata
hivyo mchakato wa Katiba mpya ulipokuja asilimia kubwa ya maoni ya Waislamu
yalihitaji Mahakama ya Kadhi kuingizwa ndani ya Katiba, mapendekezo hayo
yalikataliwa na Tume ya Jaji Warioba kwa hoja kuwa katiba inayotengenezwa ni ya
Muungano na suala la Mahakama ya Kadhi si la Muungano hivyo lisubiri wakati wa
kuandaa Katiba ya Tanganyika. Waislamu tukavumilia kuisubiri Katiba ya
Tanganyika.
Lakini
Bunge Maalum la Katiba likaikataa Katiba ya Warioba na kutunga Katiba Mpya
Pendekezwa yenye mambo yote ya Muungano na yasiyo ya Muungano bila ya kuingiza
Mahakama ya Kadhi kama ilivyoahidiwa na Tume ya Jaji Warioba. Bunge la Katiba
lililokuwa linaundwa na wajumbe wengi wa CCM hawakuona umuhimu wa kutimiza
ahadi yao ya kuweka Mahakama ya Kadhi katika katiba pendekezwa na kwa makusudi
Mahakama ya Kadhi ikakataliwa na wajumbe wengi wa CCM walishangilia jambo hili
ili hali wanajua dhahiri kuwa Waislamu hawakufurahishwa na uamuzi wao na pia
kukiuka Ilani yao na ahadi kwa Waislamu.
Muswada
huu ni sehemu nyingine ya hadaa kwa Waislamu kwani badala ya sheria kuanzisha
Mahakama ya Kadhi kama ilivyo kawaida ya uanzishwaji wa mahakama zote duniani
muswada huu umeliacha jukumu hilo kwa taasisi binafsi ili hali Mahakama ya Kadhi
kama zilivyo mahakama zingine ni sehemu ya chombo cha dola katika mfumo wa
Mahakama yaani “the Judiciary”, hili limefanywa makusudi kutokana na kutokuwepo
na nia ya dhati ya Serikali ya CCM kuanzisha na kuona Tanzania Bara kunakuwa na
Mahakama ya Kadhi madhubuti na ya ukweli.
2.
MUSWADA umempa mamlaka “Mufti” kuteua makadhi na
kutengeneza kanuni za Uendeshaji wa Mahakama ya Kadhi ili hali Mufti sio chombo
cha kisheria. Hakuna sheria inayounda ofisi ya Mufti isipokuwa uwepo wake
unategemea katiba ya BAKWATA. Maana yake ni kwamba Mahakama ya Kadhi uwepo wake
utategemea uwepo wa Katiba ya Bakwata inayounda ofisi ya Mufti. Kukiwa na
mgogoro wa kikatiba Bakwata athari yake itaikumba na Mahakama ya Kadhi. Hakuna
duniani mtu ambaye ofisi yake haiundwi na sheria kisha sheria ikampa mtu huyo
madaraka ya kuunda chombo chenye mamlaka ya kisheria kama mahakama. Serikali ya
CCM inalijua hili lakini imefanya makusudi kwa kusukumwa na nia yake ya
kutopenda kuona Waislamu wanakuwa na Mahakama ya Kadhi ya ukweli iliyo
madhubuti.
3.
Kama tulivyoeleza hapo juu MUSWADA umempa Mufti
mamlaka ya kutengeneza kanuni za uendeshaji wa Mahakama za Kadhi hili ni jambo
la ajabu sana kwa ofisi ambayo haiundwi na sheria kuwa na mamlaka ya
kutengeneza kanuni za kuendesha chombo cha kisheria ambacho ni Mahakama ya Kadhi.
Hili ni jambo ambalo haliwezekani.
4.
Kwa madaraka makubwa aliyopewa Mufti sheria
haielezi ni nani mwenye mamlaka ya kumuondoa kadhi na wala haiweki sifa za
kadhi na wala haiweki vigezo vinavyoweza kumuondoa kadhi yote hii inadhihirisha
nia ya serikali ya CCM kuunda Mahakama ya Kadhi legelege na kiini macho.
5.
MUSWADA unaeleza Waziri anayehusika na mambo ya
sheria kupewa mamlaka ya kutunga taratibu za kutekeleza hukumu za Mahakama za Kadhi
bila ya kushauriana na wanazuoni wa Kiislamu. Japo katika sehemu ya maelezo ya muswada
Mwanasheria wa Serikali ameeleza kuwa Waziri atashauriana na wanazuoni maelezo
hayo ni hewa kwani si sehemu ya sheria.
6.
MUSWADA umetoa hiyari kwa mtu kufungua shauri
katika Mahakama ya Kadhi. Jambo hili limekusudiwa kuifanya Mahakama ya Kadhi
iwe butu na kutoa mwanya wa kutokea mgongano baina ya Mahakama ya Kadhi na
mahakama za kawaida ikiwa kila upande katika mgogoro utaamua kufungua shauri
katika mahakama tofauti. Hili lisingewezekana kama serikali ingekuwa na nia ya
kweli ya kuunda Mahakama ya Kadhi madhubuti.
7. MUSWADA kuitaka Mahakama ya Kadhi
ijiendeshe yenyewe:
MUSWAAD
huu unaitaka Mahakama ya Kadhi ijiendeshe yenyewe badala ya kuendeshwa na
serikali jambo ambalo halijawahi kutokea sehemu yeyote duniani chombo kama
mahakama kujiendesha chenyewe.
Mahakama
ya Kadhi itafanya jukumu la serikali katika kutafsiri sheria za Kiislamu ambazo
ni sheria halali kutumika Tanzania hakuna mantiki yoyote kwa chombo hicho
kujiendesha chenyewe kama ambavyo serikali ya CCM inataka kufanya.
Isitoshe
uwepo wa hii Mahakama ya Kadhi kutaipunguzia serikali mzigo na msongamano wa
kesi katika mahakama za kawaida jambo ambalo serikali inapaswa kugharamia
uwendeshwaji wake. Serikali kukataa kuigharamia hii Mahakama ya Kadhi ilihali
katika nchi hii upande wa Zanzibar serikali inaiendesha Mahakama ya Kadhi
kunadhihirisha kuwa kuna nia ya kuidhoofisha mahakama hii ishindwe kujiendesha
na kuwa na mahakama isiyokuwa na maana yoyote.
Zipo
mahakama za makundi ya watu maalumu ambazo zinaendeshwa kwa pesa za serikali
ambazo ni kodi za Watanzania wote. Mfano ni kama vile Mahakama ya Kazi, Ardhi,
Biashara n.k. ni kwanini mahakama itakayotafsiri sheria za Kiislamu iwe nongwa?
8. UTAFITI unaonyesha kuwa suala la Mahakama
ya Kadhi huletwa kila unapokaribia Uchaguzi Mkuu bila ya
utekelezaji linazidi kutupa wasiwasi kwani inaonesha serikali ya CCM
imeshazowea kuwacheza shere na kuwalaghai Waislamu na Watanzania kwa ujumla kwa
maslahi yao ya kisiasa. Tabia hii ni hatari sana kwa mustakabali na ustawi wa
taifa letu.
Hitimisho
Ndugu
wanahabari, kwa maelezo yaliyobainishwa katika taarifa hii, tunahitimisha kwa
kusema:
a)
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu (T) zimeukataa na
kupinga mapendekezo ya marekebisho
kwenye sheria ya tamko la Sheria ya Kiislam kama lilivyo katika MUSWADA wa Marekebisho
ya Sheria Mbalimbali na. 02 wa mwaka 2014, mpaka utakapo andaliwa upya kwa
kuhusishwa wanazuoni wa Kiislamu, wanasheria wa Kiislamu waliobobea na kwa
kuzingatia maslahi ya Waislamu na taifa kwa ujumla na pia Mahakama ya Kadhi ni
lazima iingizwe katika Katiba ili kuipa uthabiti.
b)
Kwa kuwa katiba inayopendekezwa haitambui
Mahakama ya Kadhi na inapinga sheria yoyote inayokwenda kinyume na katiba hiyo
ikiwemo Sheria za Kiislamu kwa kauli moja na kwa nguvu kubwa Jumuia na Taasisi
za Kiislamu (T) zitawahamasisha Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuikataa kwa
KUPIGA KURA YA HAPANA katiba inayopendekezwa muda utakapofika wa kuipigia kura.
Ndugu waandishi wa habari,
Ahsanteni sana kwa ushirikiano mliotupa.
Tunawatakia kazi njema katika
ujenzi wa taifa letu.
Kaimu
Katibu
………………………….
Jumuiya na Taasisi za Kiislam
(T)
No comments:
Post a Comment