Saturday, 14 February 2015

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) YABOMOA NYUMBA ILIPOASISIWA TANGANYIKA AFRICAN NATIONAL UNION (TANU)


CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) YAVUNJA NYUMBA ILIPOANZISHWA TANGANYIKA AFRICAN ASSOCIATION NA KUASISIWA (TANU) 1954
 Mohamed Said




Iliyokuwa Makao Makuu ya African Association 1929 – 1954 na TANU 1954 – 1977

Mtaa wa Kariakoo na Mbele ni Mtaa wa Lumumba Mabati Yamezungushwa
Ilipokuwa Ofisi ya African Association, TANU na CCM
Historia ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) haianzi tarehe 5 February, 1977. Historia ya CCM inaanza mwaka 1929 katika nyumba ya Cecil Matola (sasa mali ya marehemu Mzee John Rupia).  Mtaa wa Masasi Misheni Kota. Katika nyumba ile mwaka 1929 ndipo walipokutanika hawa wafuatao kuunda African Association: Kleist Sykes, Ibrahim Hamis, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima, Suleiman Majisu, Raikes Kusi, Mzee bin Sudi, Rawson Watts na Cecil Matola. Wazalendo hawa ndiyo baadae wakaja kujenga Makao Makuu ya African Asociation Mtaa wa New Street na Kariakoo kwa kujitolea. Abdul Sykes katika kumbukumbu zake anasema alikuwa akifuatana na baba yake, Kleist Sykes kila siku ya Jumapili kwenda pale New Street kwa shughuli ya ujenzi. Nyumba ikakamilika mwaka 1933 na ikaja kufunguliwa na Gavana Donald Cameroon.

Katika nyumba hii ndipo palipofanyika mkutano wa TAA wa mwaka 1954 ambako TANU ilizaliwa tarehe 7 Julai. Nyumba hii kwa miaka mingi sana ikijulikana kama ofisi ya TANU ilibeba kumbukumbu nyingi katika mioyo ya Watanganyika. Waafrika ndani ya ukoloni wa Waingereza waliiona nyumba ile kama alama ya matumaini yao ya kuwa, iko siku watakuwa watu huru. Maandamano ya kwenda kwenye mikutano ya TANU Mnazi Mmoja na baadae Jangwani yalikuwa yakianzia pale wananchi wakitembea kwa miguu mbele umetangulia mganda (ngoma ya Wazaramo), njiani ukikumba kila mtu. Kwa yule ambae katoka bara na alikuwa akimsikia Nyerere kwa jina tu na sasa ana hamu ya kumtia Nyerere machoni ilikuwa yeye afike tu pale ofisi ya TANU azubaezubae nje haitapita muda atamuona Nyerere akiwa hayuko majimboni, akishuka kutoka katika gari akiendeshwa na dereva wake Said Kamtawa. Said Kamtawa alikuja kupewa jina akaitwa, “Said TANU,” jina lililomkaa hadi anaingia kaburini. Hawa waliokuwa wanakuja pale New Street kwa nia ya kumuona Nyerere kisha warudi makwao wakahadithie walikuwa wengi.

Waasisi wa TANU Mwaka 1974 Katika Kusheherekea Miaka 20 Toka Kuasisiwa TANU

Photo
Waasisi wa TANU 1954 Wamesimama Mbele ya Makao Makuu ya TAA
Pale ofisi ya TANU ndipo ilipokuwa majlis ya Baraza la Wazee wa TANU wakikutana hapo na halikadhalika ndipo yalipokuwa makao ya Bantu Group chini ya uongozi wa Yusuf Bakis.Hawa ndiyo walikuwa walinzi wa Nyerere. Katika miaka katikati 1970 nikipita nje ya ofisi ya TANU nilikuwa nikimuona Juma Selemani maarufu kama Juma Mlevi, sasa mtu mzima akiwa mlangoni kukaribisha wageni. Huyu Juma Mlevi kwa watoto wa Kariakoo ya 1950 na 1960 alikuwa mtu muhimu sana kwetu kwa kuwa siku za Idd pale Mnazi Mmoja alikuwa akichezesha karagosi na kutuimbisha nyimbo iliyoitwa, “Karagosi Kalewa Tembo.” (Juma Selemani au Juma Mlevi kama alivyojulikana na wengi) alikuwa mmoja wa wajumbe wa mkutano wa Kura Tatu Tabora mwaka 1958.  Sasa ikiwa historia ya CCM itakuwa inaanza kwa kuitanguliza TANU bila ya kuitaja African Association kama inavyostahili kukumbukwa historia ya Tanganyika historia ya CCM yenyewe itakuwa imepunjika. Wengi wa wazalendo hawa hawapo tena wameshatangulia mbele ya haki. Angalau basi na tuwakumbuke kwa kuhifadhi historia yao.
  
Nyerere alianza maisha yake ya siasa katika ofisi ya TANU pale New Street. Lakini ikiwa mtu ataliweka jicho lake pale tu Makao Makuu ya TANU wakati ule bila kuangalia viwanja vingine vya mapambano hakika atakuwa kajihini sana kwani wanaharakati wa wakati ule ukiondoa pale New Street walikuwa na sehemu nyingine walizokuwa wakikutana kupanga mikakati yao. Ajabu katika historia ya TANU ni kule kupuuzwa kwa historia yake ambayo kwa hakika inasisimua. Ningependa msomaji wangu nikupe historia ya nyumba moja iliyokuwa Mtaa wa Aggrey kona na Sikukuu.  Nyumba hii ndiyo alikuwa akiishi Abdulwahid Sykes rais wa TAA 1951- 1953. Mikutano ya siri ya kuunda TANU ikifanyika hapa pamoja na mazungumzo mengine ya kubadilishana mawazo kati ya wanaharakati wa wakati ule.

Hapa ndipo kwa mara ya kwanza Julius Nyerere alikutana na Abdul Sykes, Nyerere akiongozana na mwenyeji wake Joseph Kasella Bantu. Hata Nyerere alipojiuzulu ualimu mwaka wa 1955 nyumba hii ndipo alipoishi kabla TANU haijamtafutia nyumba Magomeni Majumba Sita. Lakini nyumba hii haina historia ya Nyerere peke yake. Nyumba hii ina hitoria nyingine kubwa ya kusisimua ambayo si wengi wanaifahamu. Historia ya Chief David Kidaha Makwaia wa Wasukuma. Baada ya kuchukua uongozi wa TAA mwaka wa 1950 hamu kubwa ya Abdul Sykes ilikuwa kuunda TANU kikiwa chama chenye nguvu na kujumuisha wananchi wote. Ilikuwa fikra yake kuwa kiongozi ambae angefaa kuchukua uongozi wa TAA kisha wakaunda TANU alikuwa Chief Kidaha. Chief Kidaha wakati ule alikuwa katika Baraza la Kutunga Sheria la kikoloni, Legislative Council (Legico). Abdul Sykes ilimjia fikra kuwa Chief Kidaha angeliweza kuwa kiongozi atakaewaunganisha Watanganyika chini ya TANU kudai uhuru wao. Katika nyumba hii Abdul Sykes alifanya mijadala kadhaa na Chief Kidaha kuhusu hili lakini Chief Kidaha hakutaka kubeba jukumu lile.

Inawezekana moja ya sababu zilizomzuia Chief Kidaha kujiweka pembeni na harakati zile za TAA labda ni namna Abdul Sykes, Hamza Mwapachu na Dk. Vedasto Kyaruzi walivyochukua uongozi. Inawezekana pia zilikuwapo sababu nyingine lakini hiki ni kisa kirefu In Sha Allah tutakitafutia siku yake tukieleze. Itoshe tu kusema kuwa uongozi mpya wa TAA uliokuwa wa vijana waliwapindua wazee - Mwalimu Thomas Sauti Plantan aliyekuwa rais na Clement Mohamed Mtamila katibu. Vijana walichukua TAA kwa nguvu kabla Waingereza kuingilia na kusema ufanyike uchaguzi. “Vurugu” hii ndiyo iliyowatia katika uongozi Dk. Vedasto Kyaruzi na Abdul Sykes. Dk. Kyaruzi akiwa Rais na Abdul Sykes katibu. Uongozi huu toka mwanzo haukupendeka kwa Waingereza. Kisa cha uongozi huu mpya kuchukiwa na Waingereza ni kuandika katiba waliyoiwasilisha serikalini na katika waraka ule waliwaeleza Waingereza umuhimu wa kura ya mtu mmoja kura moja kuchagua watu wa kuingia  Legco.Hawakuishia hapo wakamaliza kwa kuwaeleza Waingereza kutoa uhuru kwa Tanganyika baada ya miaka 13.

Inawezekana Chief Kidaha aliona wenzake wanaiepeleka nchi kwa kasi kubwa.  Chief Kidaha alikuwa kipenzi cha Waingereza na heshima yake ilikuwa juu sana kwa wanasiasa wa wakati ule. Kwa ufupi Chief Kidaha aliiachia nafasi ile ikampita. Hivi ndivyo jukumu lile Abdul Sykes akaja kumtwisha Julius Nyerere walipokujajuana mwaka 1952 na mwaka wa 1953 mwezi Juni Nyerere akachaguliwa kuwa rais wa TAA, Abdul Sykes akiwa makamu wa rais. Nyumba hii vilevile ilikuwa kituo kisicho rasmi cha Tanganyika African Government Servant Association (TAGSA) chama cha Waafrika wafanyakazi serikalini. Viongozi wa TAGSA walikuwa - Ally Sykes, Thomas Marealle, Rashid Kawawa, Stephen Mhando, Othman Chande na Leonard Bakuname. Mikutano yao  mingi walikuwa wakifanya katika nyumba hii. Nyumba hii iliyo na historia kubwa ya kupigania uhuru wa Tanganyika leo haipo. Ally Sykes ameivunja na kujenga ghorofa. Nilipomuuliza kwa nini kavunja nyumba ile yenye kumbukumbu kubwa jibu lake lilikuwa, “Hakuna aneitaka historia hii.” Kwa utani nikamwambia,“Baba tunakupeleka mahakamani kwa kuvunja “national monument,” yeye akawa anacheka. 

Ingekuwa nchi yetu inathamini kumbukumbu zake nyumba hii  muhimu katika historia yetu ingekuwa chini ya uangalizi wa mambo ya kale na ndani yake vimehifadhiwa vyote vilivyokuwa mle wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika. Ndani ya nyumba ile zingebakishwa samani zake, vitabu vilivyokuwa katika mashubaka, picha zilizokuwa ukutani nk nk. Kizazi kijacho kingeona chumba alicholala Mwalimu Nyerere kiti alichokalia Chief Kidaha Makwaia, Julius Nyerere na wapigania uhuru wengine wakati wa kupambana na ukoloni. Wakati ule Abbas Sykes alikuwa kijana mdogo na yeye ndiye aliyehamishwa chumba kumpa nafasi Mwalimu Nyerere. Chumba hiki kingehifadhiwa kama kilivyokuwa wakati ule. Hivi ndivyo wanavyofanya wenzetu katika kuenzi historia zao. Turudi kwenye nyumba ya TANU iliyovunjwa. 


Tarehe 10 Oktoba 1953 katika nyujmba hii kamati ya ndani na ya siri ya TAA akiwamo Abdul Sykes na mdogo wake Ally, Dossa Aziz, John Rupia na Julius Nyerere walikutana Makao Makuu ya TAA kujadili vipi wajitokeze wazi sasa kuibadili TAA kiwe chama cha siasa kamili. Wakati ule nyumba ile ilikuwa haina hata umeme. Chumba walichokutania kilikuwa hakina viti vya kutosha. Baadhi ya wazalendo hawa walikuwa wamekaa kwenye viti na wengine kwenye masanduku ya bia yaliyopinduliwa. TAA wakati ule ilikuwa taabani na kuna chumba walikuwa wamempangisha dobi wa Kihindi wapate fedha ya kuendesha ofisi. Mkutano huu muhimu ulifanyika miezi sita baada ya Nyerere kumwangusha Abdul Sykes katika uchaguzi uliofanyika Ukumbi wa Arnautoglo tarehe 17 April. Uchaguzi huu una mengi ya kueleza lakini hapa si mahali pake.

Unapozungumzia ile ofisi ya TANU pale New Street ni lazima uunganishe na “matawi” yake mengine nje ya pale na kote huku kunahitajika kuwekewa kumbukumbu. Shariff Abdallah Attas anamkumbuka Nyerere pale Soko la Kariakoo ambako Abdul Sykes alikuwa akifanyakazi kama Market Master na yeye akiwa Dalali Mkuu wa soko. Shariff Attas anasema Nyerere alikuwa akija pale sokoni ofisini kwa Abdul Sykes na hapo ndipo Nyerere akafahamiana na mmoja wa wazee maarufu wa Dar es Salaam na aliyekuwa mmoja wa wafadhili  wakubwa wa TANU na harakati zote za kudai uhuru, Mzee Mshume Kiyate.


Mzee Mshume Kiyate Akimvisha Nyerere Kitambi Kama Ishara ya
Kuungwa Mkono na Wazee Baada ya Kurudi Madarakani Kufuatia Maasi ya
Tanganyika Rifles Tarehe 20 Januari 1964

Ofisi ya Abdul Sykes ilikuwa Mtaa wa Swahili pembeni kidogo ya soko. Mtaa wa nyuma yake uliokatiza ulikuwa Tandamti na Mbele yake Mtaa wa Mkunguni. Mtaa wa Tandamti ndipo alipokuwa akiishi Mzee Mshume (Mtaa huu ulikuja kupewa jina la Mshume Kiyate kama kumuenzi mpigania uhuru huyu lakini hadi leo wahusika wamekataa kubadili jina). Abdul Sykes aliuza kadi za mwanzo za TANU hapa na nusra afukuzwe kazi na wakoloni. Mimi naikumbuka ofisi ile kama vile naiona. Ilikuwa imezungukwa na mikungu na jirani yake ilikuwa sehemu ya wauza kuku na njiwa. Mmoja wa babu zangu Shariff Mohamed alikuwa na matundu yake ya njiwa pale. Hii ndiyo ilikuwa biashara yake. Huenda vijana wa leo wakashangaa kusikia njiwa wanauzwa. Naam njiwa walikuwa wakiuzwa na walikuwa wakihitajika sana na waganga katika kufanya uganga wao katika kupunga na mengineyo. Tumetoka mbali. In Sha Allah tutafuta siku tuzungumze habari hizi maana siku ya Jumapili ndiyo ilikuwa siku ya kupunga wagonjwa na mashetani kulishwa chano. Haya yalikuwa mambo ya kawaida katika Dar es salaam ya miaka hiyo na kulikuwa na mabingwa wa sifa katika shughuli hizi mmoja ninaemkumbuka alikuwa Mwalimu Bakari na akapewa jina la utani “Seti Khabar,” kwa ubingwa wake.

Mwalimu Nyerere Akifungua Soko Jipya la Kariakoo 1975
Tawi jingine la harakati dhidi ya Waingereza lilikuwa ofisini kwa Hamza Mwapachu Ilala Welfare Centre na tawi jingine nyumbani kwa Dossa Aziz Mtaa wa Mbaruku ambako kila Jumapili vijana hawa wanasiasa walikutana kuzungumza hali ya baadae ya Tanganyika. Nyumba ilipozaliwa TANU haipo tena kama zilivyotoweka sehemu nyingi ambazo zilibeba kumbukumbu nyingi za kupigania uhuru wa Tanganyika. Jambo la kusikitisha ni kuwa hata kabla ya kuvunjwa jengo lile ukiingia ndani ya nyumba ile ilipokuwa ofisi ya CCM, kulikuwa hakuna kumbukumbu yoyote ya wazalendo walioweka misingi ya kuwaunganisha wananchi kupigania uhuru wa Tanganyika. Hapakuwa na picha za waasisi wa TAA wala wa TANU. Hata pale Arnautoglo ambako Nyerere ndipo alipochaguliwa kuongoza TANU pale ukumbini hakuna kumbukumbu yoyote ya uchaguzi ule muhimu si tu katika maisha ya Nyerere bali pia kwa historia ya taifa letu. Ilikuwa katika ukumbi ule ndipo Nyerere alipopiga hatua yake ya kwanza kuingia katika siasa na mapambano ya wazi dhidi ya ukoloni. Lakini ikiwa tutasimama hapa kwa Nyerere peke yake tutajipunja sana. Ukumbi ule wa Arnautoglo una historia nyingine. Naomba niilete hapa. 

Baada ya yale mapinduzi ya Abdul Sykes na Hamza Mwapachu walipoteka ofisi ya TAA na kuchukua madaraka kwa nguvu, Waingereza waliitisha mkutano wa pande zote mbili hapo Arnautoglo na wenyewe wakawepo. Sasa ikawa tabu kwa wanachama kuzungumza kwa uhuru na uwazi kwa kuwahofu wale maofisa Wazungu kutoka serikalini. Hapo ndipo aliposimama Schneider Abdillah Plantan, Mzulu, aliyepigana Vita Vikuu vya Kwanza akiwa katika jeshi la Wajerumani pamoja na Kleist dhidi ya Waingereza na katika Vita Vikuu vya Pili Waingereza wakamkamata na kumfunga kisiwani Ziwa Victoria kama adui. Schneider hakuwa na mengi aliwaambia Waingereza bila hofu kuwa kinachotakikana hapo na Waafrika ni uchaguzi tu. Hivi ndivyo Dk. Vedasto Kyaruzi na Abdul Sykes walivyoingia katika uongozi. Huu ndiyo ukawa mwelekeo mpya kuelekea kuunda TANU mwaka  1954. Uamuzi huu ulifanyika kwenye Ukumbi wa Arnautoglo. Hakika ukumbi ule una historia ya kipekee katika kupigania uhuru wa Tanganyika. 

Naomba nimalize kwa hili. 

Ukumbi ule ulijengwa na George Arnautoglo tajiri wa Kigiriki na akautoa kwa Waafrika wa Tanganyika. TANU ilipoanza Arnautoglo alitoa fedha kwa siri zisaidie chama na hizi fedha akamkabidhi Ali Mwinyi Tambwe.

 
Kushoto Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdulwahid Sykes na Lawi Sijaona Ukumbi
wa Arnautoglo Katika Sherehe ya Kumuaga Nyerere Kwenda UNO Safari ya Pili 1957

Hata hivyo hatujachelewa kuinusuru historia ya Tanganyika. Nyumba ya Mzee Rupia ambayo wakati ikiwa ya Cecil Matola ndipo ulipofanyika mkutano wa kuasisi African Association mwaka wa 1929 ipo. Fikra hii ya kuanzisha African Association Kleist aliipata kutoka kwa Dr. Aggrey alipokuja Tanganyika mwaka wa 1924 kama mgeni wa serikali kuja kusaidia tatizo la elimu kwa Waafrika wa Tanganyika. Si kazi kubwa kwenda pale na kupachika kibao cha shaba kinachoeleza kuwa hapa ndipo palipoasisiwa African Association na majina ya wazalendo wale yakaonyeshwa.  Arnatouglo bado ipo. Inawezekama kabisa kama nia ipo pakawekwa kibao cha kueleza kisa cha ule uchaguzi maarufu kati ya Abdul Sykes na Nyerere. Uchaguzi wenyewe ulikuwa wa kunyanyua mkono. “Aneamtaka Abdul Sykes anyanyue mkono.” Wajumbe wananyanyua mkono wanahesabiwa. “Anaemtaka Julius Nyerere…” Nyumba aliyokuwa akiishi Abdul Sykes sasa haipo badala yake kuna jigorofa kubwa.  Sidhani kama itakuwa shida sana napo kuweka kibao cha shaba na maelezo ya yote yaliyokuwa yakitendeka pale kuanzia Chief David Kidaha Makwaia hadi Julius Nyerere yakaandikwa na kueleza kuwa hapa ndipo alipoishi Baba wa Taifa baada ya kujiuzulu ualimu ili aongoze TANU kudai uhuru. Soko la Karikakoo lipo ingawa si lile la zamani. Halikadhalika hapa pia panaweza kuwekwa kumbukumbu yake. Ilala Welfare Centre nayo ipo. Hatujachelewa ikiwa azma na utashi wa kuiokoa historia ya nchi yetu ipo.



Dr. Kwegyr Aggrey

Mwandishi Mbele ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dodoma

Mwandishi Akihojiana na Balozi Abbas Kleist Sykes Kuhusu Historia ya Ukombozi wa Tanganyika
Ofisi Ndogo ya CCM Shrehe ya Miaka 50 ya Uhuru Pembeni ni Iliyokuwa Ofisi ya TANU

Ofisi ndogo ya CCM kama ilivyo baada ya kujengwa upya


No comments: