Monday, 16 February 2015

TAAZIA YA EBBY "EBRAHIM" SYKES 24 FEBRUARY 1952 - 15 FEBRUARY 2015

Ebby Sykes

Ebby Kwenye Msiba wa Baba Yake Mdogo Ally Sykes 20 May 2013

Dully Sykes
Kushoto:Kleist Abdulwahid Sykes, Ebby Abdulwahid Sykes, Sauti Thomas Plantan na Abdulwahid Ally Sykes


Khitma Nyumbani kwa Kaka Yake Kleist Sykes

Jaji Joseph Sinde Warioba, Paul John Rupia na Mzee Shomari Nyuma Aliyevaa Suti Nyeusi ni
Mohamed Maharage Juma "Contemporary" wa Ebby wote walikuwa Wanamuziki Katika Ujana Wao
Mohamed Maharage ni Mkuu wa Itifaki, Ikulu
Kushoto wa Kwanza Mohamed Maharage Juma Katika Miaka ya 1970
Sheikh Mahdi Akisoma Talakini Kwenye Kaburi la Ebby


Mwinyi Mangara na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Mecky Sadiki (Katikati)
 Kulia kwa Mangara ni Ahmed mwinge na Kushoto ni Kube, Chande na Hussein
Kushoto: Abbas Sykes, Mshike, Abdul Faraj, Mwinyi Mangara na Said Mecky Sadiki

Baada ya Maziko


Katika maisha yangu sijapata kuandika taazia ya mtu aliyekuwa karibu nami. Hii itakuwa ya kwanza In Sha Allah. Hata hivyo sijui kama itakuwa na maneno mengi kwa kuwa mengi niliyonayo ni binafsi zaidi kwa hiyo nahisi kama hakuna ambae atataka kusoma kitu kama hicho.

Ngoja  nijaribu.

Ebby alinitangulia kuja duniani kwa siku moja. Yeye kazaliwa tarehe 24 Februari, 1952 mimi nikazaliwa siku ya pili yake tarehe 25 Februari na mama yangu Bi. Baya biti Mohamed akalala kunizaa mimi kitanda kile kile alicholala jana yake mama yake Ebby Bi. Regina. Nilikuja kumuona mama yetu miaka mingi sana baadae mimi nishakuwa kijana mkubwa nyumbani kwa rafiki yangu Yassin Idd (marehemu) Mtaa wa Bonde ambae alikuwa amemuoa dada yake Ebby, Miski. Miski alikuwa kajifungua mtoto na mama alikuja pale kutoka Morogoro kuja kumkalia binti yake.

Mimi na Ebby tumekuwa pamoja toka utoto wetu tukawa pamoja katika ujana na tukawa watu wazima pamoja ingawa baada ya kutoka katika ujana kila mtu akawa ameshughulika na maisha yake. Babu zetu hata kabla hatujazaliwa sisi wao walikuwa marafiki na bibi zetu wakiwa mashoga. Hiyo ilikuwa katika miaka ya 1930. Ebby alikuwa Kipata karibu na New Street (sasa Lumumba) na sisi tulikuwa Kipata ya Mtaa wa Nyamwezi. Sina mengi ya kusema kuhusu babu zetu ila kuwa walikuwa majirani wakiishi Mtaa wa Kipata (sasa Kleist Sykes) na wote wakifanya kazi Tanganyika Railways lakini nina kumbukumbu nyingi za bibi yake Ebby Bi. Mruguru biti Mussa ambae shoga yake alikuwa bibi yangu Zena biti Farjalla. Tulipokuwa watoto tukipenda sana kula kaukau. Hii ni "snack" inayotengenezwa na unga wa ngano. Kaukau ilikuwa inauzwa katika hoteli ya Mzee Saidi. Huyu alikuwa Mzee wa Kiyemeni na hoteli yake ilikuwa Mtaa wa Narung’ombe na Sikukukuu.

Mtaa wa Kipata Kama Ulivyokuwa Katika Miaka ya 1970 Nyumba zote Hizo Sasa ni Magorofa
Mimi nimezaliwa Hiyo Nyumba Baada ya Nyumba Yenya Rangi Nyeupe Nyumba ya Pili Na. 32
Hii ilikuwa mitaa yetu na dunia yetu yote ikizunguka hapo. Mwenye hela atanunua na tutagawana kisha ikisha tunatazamana kupiga akili vipi tununue kaukau nyingine hadi kifu yetu. Nawakumbuka wenzangu wa wakati ule, Hamza Msanga Mapesa (marehemu), Mohamed Abdulrahman maarufu kwa jina la Mohamed Kitunguu, Ali Hussein (marehemu) maarufu kwa jina la Ali Kioze, Abdu Mgunya na Juma Kube. Basi tukifika hapo kuwa kaukau tumemaliza na bado tuna hamu Ebby atatuchukua hadi kwa bibi yake Bi. Mluguru, Mtaa wa Kirk (sasa Lindi) na Sikukuu. Lakini hatutomsindikiza hadi kwao kwa bibi yake. Sisi tutabana kwenye kona ya mtaa. Hapo alikuwa kinyozi Mzee Mwingereza. Huyu ndiye alikuwa kinyozi wa watoto wote wa Gerezani na barza yake ilikuwa maarufu kwani wakati wa siasa za kudai uhuru katika miaka ya 1950.

Hapo ndipo baba yake Ebby marehemu Abdulwahid Sykes, Dossa Aziz na wanasiasa wengine walikutana kupoteza wakati. Palikuwa hakuna viti wakikaa kwenye kigogo cha mnazi. Ebby atakwenda kwa bibi yake Bi. Mluguru kuomba hela ya kaukau. Bi. Mluguru pale barazani kwake alikuwa na biashara yake akiuza togwa. Siku ikiwa shetani wa kaukau katuondokea tunakwenda kumwamkia Bi. Mluguru na yeye hatatutoa kapa. Atatupa chupa moja moja ya togwa tujiburudishe. Turejee kwa Ebby. Punde Ebby atarudi na hela na safari itaanza kuelekea hoteli kwa Mzee Said kununua kaukau. Ebby alikuwa kiongozi wetu na iko siku ataamua leo tusicheze mpira twendeni sokoni Kariakoo tukaokote mabua tutengeneze miti ya kurukia “high jump.” Ebby ndiye aliyenifundisha mimi “high jump.” Mchezo huu tulikuwa tukifanyia kwetu Mtaa wa Gogo kwa mama yangu mdogo Bi. Mtoro biti Mohamed, kwa kuwa kulikuwa na tifutifu. Haya yote tukifanya wakati wa likizo.

Miaka ikenda sasa tukawa vijana. Michezo ya kitoto tukaiacha. Hiki ndicho kipindi mimi nilishakamana sana na Ebby. Huu sasa ulikuwa ule wakati Waingereza waliuita, "The Roaring 60s." Ebby alizaliwa katika nyumba ya muziki. Baba zake wakati wa ujana wao walikuwa na bendi iliyoitwa, "The Skylarks." Hii ilikuwa katika miaka ya 1950 wakati sisi tunazaliwa. Ebby katika miaka ile ya 1960 katikati yeye tayari akiwa kijana mdogo wa miaka kama 14 hivi tayari alikuwa amekwisha kuwa mpiga gitaa mzuri. Alikuwa Ebby ndiye alinifunza mimi "chords" za gitaa. Ebby alikuwa na gitaa lililokuwa kwao. Nalikumbuka hili gitaa aina yake ilikuwa “Gibson.” Gibson lilikuwa gitaa mashuhuri Marekani na Marekani ya Kusini kwa ajili ya sauti yake ya kuvuma tofauti na magita yaliyokuwa yakitumika Ulaya ambayo yalikuwa yanaitwa, “solid” yakitoa sauti kavu, maarufu katika haya lilikuwa, “Hofner.”

Siku moja nazugumza na Balozi Mohamed Maharage nyumbani kwake Makongo, akanambia, "Unajua Sidney (hii ilikuwa nickname yangu) wewe ndiye ulionifunza mimi "chords.” Ebby alikuwa mwimbaji mzuri pia. Akiwaiga waimbaji wa wakati ule - Percy Sledge, Wilson Picket, Ottis Redding na wengineo. Mimi nilichelewa kuhama nilikokuwa wakati "Soul" ishaingia Dar es Salaam. Mimi bado nilikuwa kwa Elvis Presley na Cliff Richard. Nakumbuka wakati ule nikifanya mazoezi na rafiki yangu Abdul Yusuf kuupiga mwimbo wa Cliff Richard, "You and I," wakati Ebby rafiki yangu akishika gitaa anapiga, “Hold On,” ya Sam and Dave. Abdul Yusuf  tulisoma darasa moja St, Joseph's Convent na wakati ule umri wetu ulikuwa miaka 15. Abdul Yusuf alikuja kuwa Aeronautical Engineer.  Ebby akizisikiza "soul" kwenye "record player," nyumbani kwao kisha akizikopi na kuzipiga kwa "key" ile ile waliopigia wenyewe. Wakati huo baba yake, Bwana Abdul Sykes alikuwa kajenga nyumba Magomeni Mikumi na wamehamia hapo.

Kushoto: Kamili Mussa, Yusuf Zialor (marehemu), Abdallah Mgambo, Othmani Chande
Aliyekaa Kleist Sykes, Ebby Sykes, Miriam Max, Janeth Zebedayo, Erica Kissa, Elizabeth Frisch (1960s)
(Picha kwa Hisani ya Abdallah Mgambo)

Mitaa hiyo kwa wakati ule wazee wetu wengi walijenga hapo, Chifu Fundikira alikuwa na nyumba Mikumi, Mzee Mzena, Chihota, Mzee Amri, Mzee Mgone, Mzee Muhuto, Ally Sykes, Abbas Max, Mzee Mwakinyo ili muradi mitaa hiyo ilikuwa na uchangamfu wa aina yake kwa ajili ya watoto wa wazee hawa, wa kike na wa kiume. Sisi tuliokuwa tukiishi, Upanga, Karikoo, Temeke na kwengineko mchezo wetu ulikuwa Mikumu na tukapaita, "Soulville." Hii ni kwa sababu wakati ule muziki uliokuwa ukitamba dunia ulikuwa "soul" na bingwa wa "soul music," alikuwa James Brown. Ikawa sasa tukijifunza kupiga muziki kwa staili ya Motown. Hii ndiyo ilikuwa “record label,’ mashuhuri ya muziki wa “soul,” kutoka Detroit. Miaka mingi sana baadae naingia Marekani na “entry point” yangu ilikuwa Detroit. Nilipokuwa nimesimama kwenye foleni kusubiri kugonga pasi yangu, fikra zangu zilinirudisha nyuma sana.


Kushoto: Adam Kingui, Vuli, Ebby Sykes, kwenye drums Khalid,
Kulia Bob Dean, Nasser (Mick Jagger), Choge Sly 
Siku ya Jumatano shule mwisho saa sita. Hiyo ndiyo ilikuwa siku tunakutana Magomeni Mikumi nyumbani kwa akina Mohamed “Captain Mike” kufanya mazoezi ya nyimbo zetu. Ebby siku zote alikuwa "centre stage." Huu ndiyo wakati Adam Kingui, katika vijana waliokuwa na kipaji kikubwa cha muziki akiwa na kundi la The Rifters pamoja na Simon Ngocho (Simon alikuja akawa Civil Engineer) sasa ni marehemu, Mohamed Ali Abbas (marehemu), Vuli kijana kutoka Afrika Kusini, Nassoro maarufu kwa jina la Mick Jagger, na vijana wengine siwakumbuki.  Leo nikiangalia nyuma naona wakati ule ulikuwa mgumu sana kwetu lakini sioni sababu ya sisi kujilaumu tulikuwa tunaitika mazingira ya wakati uliokuwapo. Miaka ya 1970 tunamaliza sekondari. Sasa tunaanza kuwa na akili zilizotulia. Ebby akaenda Mombasa kujaribu bahati yake katika muziki. Hakukaa sana Mombasa akenda Piraeus Greece. Huo ulikuwa wakati vijana wengi wanatafuta kazi ya ubaharia. Ebby hakukaa sana Ugiriki akarudi Dar es Salaam.  Miaka ikapita...
Kushoto: Dimitri, Vyas, Kleist Sykes, Abdallah Mgambo na Adam Kingui 1965

Ebby alikuwa mpole lakini alikuwa na uwezo mkubwa wa kumdhibiti mbabe yoyote. Siku zile za madansi ya mchana tukiita "Boogie," tukimaliza dansi wakati wa kurudi nyumbani tunachokozana. Kulikuwa na “gang,” za vijana wa Temeke, Magomeni na kwengineko. Ukiwa umefuatana na Ebby jua uko salama. Wababe wakimjua hivyo wakimfanyia staha. Ebby Mungu alimjaalia mshipa wa kula. Alikuwa anaweza kula sana kiasi ilikuwa zamani tukienda kula chips haikuwa ajabu Ebby kupiga sahani mbili za chips kwa samaki au kuku peke yake kisha akashushia na soda. Nakumbuka siku moja naingia kwenye kimgahawa kimoja kilikuwa Maggot hii ilikuwa hoteli maarufu katikati ya mji. Ebby alikua ameshaniona toka nakuja akawa kapiga oda yangu. Nafika tu tunasalimiana muhudumu namuona ananiwekea kilima cha kababu. Mimi nimeshangaa. “Ebby akanambia, “Sidney yako hiyo nimekuodea.” Sasa nikaanza kulalamika kuwa siwezi kumaliza na nini. Ebby hakusema kitu. Alinyanyua ile sahani yangu akajipunguzia kababu kwenye sahani yake ambayo tayari ilikuwa ni kilima akaendelea kula.

Buriani ndugu yangu, rafiki yangu Ebby. Si haba Allah katukadiria umri wa kutosha na tushukuru kwa hilo. Miaka 63 si haba ingawa mwenzangu ulibakisha siku tisa tu kukamilisha hiyo miaka 63.

Allah akuweke mahali pema peponi.

Amin


Ebby na Mimi 2010

No comments: