.jpg)
Imekuwa Hamkani Sio Shwari Tena
Kituo Kikuu cha Daladala Kuhamia Kiswandui
Na Ben Rijal
Hamkani
sio shwari tena, kumekuwa hakukai sawa na kila kukicha yanakuwa hayo kwa hayo
maji ya futi na nyayo. Kusema kweli tunaambiwa kuwa ili tuweze kuendelea na
kujua hapa tulipo kama kuna mustakbala mwema huko mbele ni muhimu kuzingatia
kufanya utafiti katika nyanja mbalimbali kuanzia kilimo, afya, kijamii,
mazingira, elimu, mawasiliano, n.k.
Tafiti
nyingi za nchi za Ki-Africa zinakosa kupatiwa fedha za kutosha na matokeo yake
huwa kinyume na matarajio ya matokeo ya hizo tafiti, inaelezwa kuwa kila
kukicha katika nchi za Africa badala ya kuongezewa bajeti za tafiti matokeo
yake huwa fedha za tafiti hupunguzwa. Kwa mfano nchini Africa Kusini nchi
ambayo ina uchumi imara kati ya nchi za Ki-Africa mwaka wa 2014 iliripotiwa
kuwa fedha za kufanyiwa tafiti zimeporomoshwa na serikali kuu kwa asilimia 0.71
kutokana na pato la kila mtu (GDP), unaposikia haya unapata kiwewe na kujiuliza
Africa inaelekea wapi?
Najaribu
kuzungumzia tafiti kijuu juu kwasababu mengi yanayotupeleka kombo nikutokana
kuwa hatufanyi tafiti, tunaulizana kwanini siku hizi Polisi wamekuwa
wakimkamata mtu huanza kumtwanga vya kutosha hata akifika kituoni huwa yupo hoi
au kama huku tusemavyo chicha kabisa. Kuna sababu ya haya kutendeka na ili
tuweze kupata jawabu kunatakiwa kufana utafiti, suala la magari ya daladala
kupiga nyimbo kwa sauti kubwa na madereva wake kuuweka uhuni mbele koliko
ustaarabu, kwanini yanakuwa hayo?
Kuna
sababu ulufu ndani yake, wakati mmoja nchini Kenya waliwahi kufanya utafiti juuya
makondakta na maderva kujua kwanini
wanafanya mambo yalio sio ya kikawaida, tafiti ilikuja kufichua kua zaidi ya
asilimia 80 kati ya madereva na utingo wa matatu huwa wanavuta bhangi. Nchini India walikuja
kupata soko la kuuza vyura nchini Sweden na vyura vyote vilikuja kutokomea
katika mashamba ya mpunga, wakulima walipata tija ya muda mfupi, bada ya mwaka
tu, uliingia ugonjwa wa mpunga kukunyaa na kushindwa kuvunwa, utafiti
ulipofanyika ilikua kujulikana sababu ya maradhi hayo kua vyura walikuwa wakila
bakteria ambao bakteria hao ndio waliokuja kuleta madhara, kwa kukosekana kukuweko kwa vyura bacteria
wakaja juu na kuogezeka na kushambulia mpunga. Tafiti ni muhimu sana sana na
kukosekana kufanyika tafiti matokeo yake ni kuendelea kuwa na kilema
kisichoponyeka ikiwa kilema hicho kinaponyeka.
Nimejaribu
kujenga hizi hoja kutokana na azma ya makala haya juu ya kituo cha Daladala
kilichohamishwa kutoka hapo Darajani na kuhamishiwa Kiswandui na eneo hilo lilokuwa
kituo cha daladala hivi sasa ni sehemu ya kuegesha magari ambao watu hutozwa
ada. Nitanena kama wanenavuo wengine kunena
kuwa kuondolewa kwa kituo cha Darajani kulifanyika pasina kufanywa utafiti ila
tu jazba na utashi wa wahusika ndio walikurukupa na matokeo yake kwa sasa kuwa kuna
kila aina ya adha, baa na belwa mtaa wa Kiswandui.
Kama
wakuu wa Baraza la Mji wangefanya utafiti ingebidi kubakia na kituo kile cha
Darajani na huku wanatafuta njia nyengine ya kudumu, lazima mwenye kuhusika na
watu ajuwe idadi yao ni wangapi na wangapi wenye vipando vyao hawategemei
vipando vya Umma na wangapi wanatumia magari ya serikali n.k.
Aidha
mtafiti anaangalia kukua na kuongezeka kwa watu nini kinahitajika kufanyika,
kwa mfano kisiwa cha Zanzibar katika mwaka wa 1964 idadi ya watu wake ilikuwa
ni watu laki tatu (300,000) lakimbili ikiwa imestakimu Unguja na laki moja ipo
Pemba na kutokana na Sensa iliopita ya mwaka wa 2012 inatueleza kuwa idadi ya
watu wa Zanzibar kwasasa ni Milioni moja na laki tatu (1,300,000) ongezeko hili
la watu linaingia katika masafa yaleyale ya kisiwa ambacho watu wameongezeka
lakini masafa ya kisiwa ndio yale yale au unaweza kusema hata yanapungua kwani
tunafahamishwa kuwa kuna maeneo yasiopungua 125 yamevamiwa na maji ya chumvi
baadhi ya maeneo hayo yalikuwa ni ya kilimo, mengine ni makazi ya watu.
Katika miaka
ya sitini kituo hicho cha magari kiliopo Darajani kilikuwa kinapokea magari kwa siku nzima magari yasiozidi 15
yakiwa ya Makunduchi mawili, Fuoni moja, Jumbi mawili, Nungwi moja, Mkokotoni
moja, Kizimkazi moja, Chwaka moja, Ndijani moja, Bumbwini, Mangapwani moja,
Bwejuu moja, Matemwe moja n.k hio ni miaka ya sitini. Kwa mfano gari kutoka
Makunduchi likiingia mjini linabakia hapo hadi mchana ndio linarudi huwa na
safari moja tu kwa siku, leo gari hizo zinafanya hata safari tatu kwa siku
kutokana na mahitaji ya watu. Magari yameongezeka kutokana na idadi ya watu
kuongezeka ambao wanahitajia usafiri mathubuti, kwa siku ingia toka ya magari
hapo Darajani yanafikia idadi ya magari mia na khamsini au nazaidi.
Kituo
cha Darajani kilikuwa kinachukua abiria wa Bububu, Saateni, Mwanakwerekwe,
Kiembe Samaki, Chukwani, Mombasa, Amani, Daraja bovu n.k. Kwamatafiti atapotaka
kukiondosha kituo kama kile cha Darajani kwanza atatafakari kujua anahamisha
kukipeleka wapi? Atataka kujua kwa wastani wa magari mangapi kwa siku yanaingia
hapo kituoni, ataangalia katika saa magari mangapi yanaingia na ni wakati gani
kunakuwa na abiria wengi wanaovutana kutaka usafiri.
Baada
ya kujiuliza hayo anakuchukua takwimu na kuzichambua na jawabu atakayoipat atachokifanya
ni kujaribu kukihamisha gari la eneo moja tuseme Mwanakwerekwe atakihamishia
kwa muda sehemu moja kisha atapima adha na urahisi wa abiria na atapata sura halisi
bada ya majaribio hayo kusema kupunguza msongamano wa Darajani itakuwa vyema
kuhamisha magari yaendao Kiembesamaki, Mwanakwerekwe na Chukwani kuwahamishia
sehemu ya iliopata kuwa Baraza la wakilishi au tuite jina lilozoeleka Peoples
Club.
Mtafiti
huyo hatosita hapo bali atatoa na Dodoso au tuite Hojaji (Questionnaire)
kuwauliza abiria wanaokusanyika hapo nini mapendekezo yao juu ya kuhamishwa
kituo. Zaidi ya hapo wahusika ambao ni wa Baraza la Mji watatakiwa wakae na
watu wa Mipango Miji na Vijiji kuangalia njia iliokuwa mbadala, isitoshe watatakiwa
wafanya vipindi vya Radio na TV kuwaelimisha wananchi kuweza kufahamu sababu ya
kuhamishwa kwa kituo hicho na wao watasema nini kuhusu uamuzi huo? Watafiti hao
hapo tena ndipo watapokuja na suluhisho ambalo litakuwa la kisayansi kabisa lisioleta
adha.
Waswahili
wana msemo wao ambao mie nitausema kwa njia ya tarwia nayo ni unaruka kukimbia kukanyaga
haja ndogo huku unakanyanga kinyesi. Ikiwa ilikuwa kupunguza kelele na adha kwa
skuli za Darajani na Vikokotoni basi kituo hicho kimehamishiwa kwenye skuli ya
Kiswandui ambayo hapo ndipo panapotakiwa kuwepo utulivu wa hali ya juu kwani
wale watoto taahira (Mongoose) ndipo wanaposoma aidha Makao Makuu ya Chama cha
CCM ndipo yalipo. Lakujiuliza ndio kipi kilichofanyika? Jengine ambalo linawapa
watu mashaka nikuona kituo kilekile cha Darajani kilichofikiriwa kunampango
mwengine unataka kuratibiwa sasa kinaegeshwa magari ya watu binafsi na kutozwa
shilling alfu moja kwa saa, aah, hii ni Hamkani Sio Shwari Tena.
Abiria
wa daladala wapo tafshanini hawajui la lufanya hawajui la kutenda inagwa
wamegubikwa na maudhi ambayo hawajui jawabu yake litatokana na nini wapo
wanaona ni Hamkani isiokuwa na ushwari.
Narudia
tena utafiti ni jambo la muhimu, ikiwa watu wataongezeka kila kitu cha
mahaitaji juu ya watu hao nacho kitaongezeka, sasa watu wameongezeka na magari
yameongezeka, afana alek unaingia mjini hujui wapi uegeshe gari lako utapata
upenyu uliweke utakuja kukuta umeshatiliwa chuma na hao hao watu wa Baraza la
Mji ulipe alfu kumi ndio ufunguliwe gari yako upate kuondoka na wiki iliopita
magari yakibebwa juu kwa juu sijui yakipelekwa wapi? Unajiuliza hawa wahusika
wamefanya tafiti? Wametembea nchi za visiwa kama Mauritius na Seychelles
wakaona taratibu za wenzetu wazifanyazo? Nimeshuhudia kule Mauritius hata hizo
sehemu za pembeni ambazo huku kwetu ni dhambi kuegesha gari huko wao huegesha
na zimeekewa michoro wa ukomo wa gari za kuegeshwa, wenzetu hao wa visiwa walikuja
na fikra hizo kwa kujua wao ni watu wa visiwa na vipi ardhi ilivyokuwa
inapungua, wakajiuliza vipi wataweza
kuondoa adha na kuwa na matumizi bora ya sehemu ndogo ya ardhi walionayo.
Hapa
Unguja imekuwa mashaka na adha baina ya wenye vipando na watu wa Baraza la Mji.
Jengine ambalo halijafanyiwa utafiti ni kuona kuwa baada ya kuchwa jua bado
watu hao wa Baraza la Mji katika eneo la Forodhani wanaendelea kukusanya fedha
za maegesho pamoja na siku za mapumziko jambo hilo halipo popote pale duniani,
ndio nikasema Hamkani Sio Shwari Tena mambo yapo mchafu koge, msege mnege.
Tatizo
la kuegesha magari katika maeneo ya mjini na Darajani ni adha tupu, bado
nawanasihi wakuu wa Baraza la Mji kufanya utafiti wa juu ya suala hili,
watafiti Alhamdulillahi wamejaa kama pishi ya mchele iwe SUZA, Chuo cha Fedha
ChChwaka, Chuo cha Elimu Chukwani, Zanzibar University hata watafiti mmoja mmoja wanaweza kusaidia pakubwa,
jambo hili linahitajia kuangaliwa kwa makini kwani linawakosesha utulivu wakazi
wanaotegemea vipando vya daladala.
Wakazi
wa Kiswandui hawana raha kuanzia asubuhi ya saa moja hadi nne ya usiku kwa
makelele na moshi wa magari wanajiuliza hayo yataendelea mpaka lini? Watoto wao
wamo kujifundisha matusi yanayoporomoshwa na madereva na utingo, wanapambana na
uchafuzi wa mazingira ya moshi na maeneo hayo kwa kuwa hayana vyoo vya kwendea haja
ndogo watu hujikojolea ovyo, wakazi wa Kiswandui hujiuliza “tumekosa nini?” Mie
nitawambia hamjakosa kitu wala hamtiwi adabu bali tafiti zimeonekana sio lolote
wala sio chochote kile amua, amua twende mbele ndio hayo yanayowatesa wakazi
hao.
Tabu ya
watu wetu nayo nikuwa wanashindwa kuhoji kila kitu utasikia kimeandikwa sijui
kimeandikwa na nani na hio kamwe sio Tawhidi.
Aaah Hamkani Sio Shwari Tena.
No comments:
Post a Comment