Annur Na.187- Feb.5-11, 1999
Hotuba ya Mh. Kitwana Kondo (MB) aliyoitoa Bungeni
Dodoma
| Kitwana Selemani Kondo |
Mh. Kitwana S. Kondo: Mheshimiwa
Spika, naomba nikushuru sana.
Mheshimiwa Spika, naomba na mimi nimpongeze
Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake aliyoitoa tarehe 4 Novemba, 1998 hapa Bungeni.
Hotuba hii Mheshimiwa Spika ina ukweli, ina usahihi na pia ina uungwana.
(Makofi).
Mimi nataka ninukuu vifungu viwili katika hotuba
hii, navyo ni vifungu vya mwisho. Lakini kabla sijafanya hivyo, nataka
nimwambie rafiki yangu, mpenzi wangu Dr. Msina kwa manung’uniko yake ya mambo
aliyofanyiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, mimi ninazo habari na sio mimi tu, watu
wengi wanazo habari kwamba Wasukuma na Mkuu wa Mkoa wa Tabora ni Msukuma na
Wanyamwezi na kidogo Wadigo wana tabia ya wizi. Kwa hiyo yaliyomkuta ni mahali
pake. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ningependa
sasa niende kwenye vile vifungu nilivyosema kuwa nitavinukuu. Katika hotuba hii
ya Mheshimiwa Rais, mwisho inasema hivi, "Mheshimiwa Spika, baada ya miaka
mitatu ya Urais, nathubutu kubadili maneno ya msanii mashuhuri wa visiwani,
Siti bint Said na kusema Tanzania ni njema atakaye na aje. Nchi yetu Mwenyezi
Mungu ameibariki sana. Ni nchi ya umoja, amani, upendo, bashasha, ukarimu
uliopindukia. Ni nchi ya wapenda usawa na haki. Umoja wetu wa Kitaifa unatokana
na imani yetu ya dhati juu ya usawa wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu na
mbele ya sheria. Umoja unaoimarishwa na sera sahihi za kujenga jamii na kuandaa
mazingira ya maendeleo ya haki, amani na utulivu kwa wote". (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, Mheshimiwa Rais
anaendelea. Anasema hivi, "Umoja unaotahadhari sera, kauli, tabia na
vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za mfarakano, chuki na kutoaminiana miongoni
mwa Watanzania". Ningependa niyarudie maneno haya. "Umoja
unaotahadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za
mfarakano, chuki na kutoaminiana miongoni mwa Watanzania. Umoja unaolindwa kwa
vita vya kudumu dhidi ya ukabila, udini, ubaguzi wa rangi, jinsia au majimbo".
Mheshimiwa Spika, miaka mingi iliyopita, kwenye 1658
A.D. Mtu mmoja Galileo alisema, "Dunia ni mviringo". Makuhani
wakamwambia huyu anakufuru, akashitakiwa akahukumiwa kuuawa na akachomwa moto.
Leo Galileo amekuwa Vindicated. Kwa bahati mbaya Galileo mwenyewe hayupo
kujua kwamba amepata Vindication. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni hiki cha
umoja unaotadhari sera, kauli, tabia na vitendo vinavyoweza kupanda mbegu za
mfarakano. Nimesema mara nyingi hapa kwako. Mheshimiwa Rais, hivi karibuni
aliwahutubia Waislamu kwenye Baraza la Idd, akawaambia kwamba manung’uniko yao
na malalamiko yao yote atayatazama na atayashughulikia akishirikiana na Baraza
lake la Mawaziri.
Sasa nina mambo mawili au matatu ambayo nataka
kuyasema ambayo yanaweza kuleta mfarakano. Yanapandwa na serikali. Moja,
karibuni hivi katika mwezi wa Ramadhani, mwezi wa Ramadhani kwa Waislamu ni
mwezi Mtukufu, ni mwezi wa toba.
Wale jamaa zangu wasiojua toba ni mwezi wa kurudi
kwa Mungu. Wakati wa ukoloni na mimi nilisoma wakati wa Ukoloni mwezi wa
Ramadhani shughuli zote zinafungwa, baadaye kwenye serikali yetu wenyewe shule
hazifungwi. Lakini baada ya muda wanaachiwa watoto kurudi majumbani kwao au
kwenda kwenye mabweni. Lakini mwaka jana na mwaka huu serikali ikaamua kuwa mitihani
ya watoto wa kidato cha nne ifanywe mwezi wa Ramadhani na iendelee mpaka siku
za Idd. Hiyo ni moja ya cheche za mifarakano.
Kwa Rehema ya Mungu Alhamdulillah, baada ya
kunung’unika Waislamu, Waziri wa Elimu na Utamaduni alitoa maelezo. Maelezo yale
yakawaridhisha Waislamu na Mheshimiwa Rais akakubali kwa siku za Iddi, watoto
wasifanye mitihani na haikufanywa mitihani. (Makofi)
Lakini mimi ninalouliza ile sababu ya kuamua mwezi
wa Ramadhani ifanywe mitihani ni nini? Ni Insensitivity, ni jeuri, ni kiburi,
kwa sababu kuna wengine ambao ni wazito tuliwasikia wakisema, wakitaka kufanya
mtihani na wafanye hawataki basi. Mimi nasema watu kama hao ndiyo watu
wasioitakia kheri nchi hii. Siyo sisi tunakuja kusema hapa hadharani. Hao
wanaosema wakitaka kufanya na wafanye na hawataki kufanya basi. Hao ndio
wasioitakia kheri nchi hii. (Makofi)
La pili, linaloweza kuleta mfarakano ni tabia ya
serikali ya kuchelewesha makusudi kuandikisha taasisi za Kiislamu. Taasisi
yoyote ya Kiislamu ikitaka kuandikishwa serikalini itachukua miaka miwili au
mitatu. Sababu hazitolewi, hata kama kuna uchunguzi, watu waende wakatafute
habari kwa nini inachukua miaka miwili, miaka mitatu?
Mheshimiwa Spika, nilipata kusema hapa kwamba mimi
ni mlezi wa Baraza la Maimamu Tanzania. Tumeomba Baraza la Maimamu
kuandikishwa, sasa ni miaka mitatu, sababu haijulikani. Wengine kila wakiomba
wanasema lazima kipatikane kibali toka BAKWATA. Leo ningependa nijue ipo sheria
inayosema hivyo? Au ni matakwa tu ya wakubwa? Hilo la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la tatu, Sura ya 33 Aya ya 30 na
ya 31 ya Qur’an inamtaka mwanamke akifika umri wa miaka 9 avae hijabu. Hijab
maana yake avae nguo ya mikono mirefu, avae shungi, avae gwanda zuri na avae
suruali inayoficha mapaja na mpaka magoti. Mimi najua ya kwamba serikali imetoa
agizo kwa watoto wa shule kwamba wafanyiwe hivyo wale wa Kiislamu wanaotaka,
sheria zote zinavunjwa. Dini ya Kiislamu inakataza pombe, Waislamu wanakunywa
pombe. Sasa hilo anafanya mwenyewe.
Lakini ninajua pia ya kwamba kuna shule nchini huku,
kuna viongozi wa Idara ya elimu ambao wanakataa kutekeleza sheria hii au agizo
hili na serikali imekaa kimya, nataka nijue ni kwa sababu gani? Tujue ni kwa
nini. Hii ni amri ya Mwenyezi Mungu na serikali, Rais anasema tusifanye chochote
kinachoweza kuleta mifarakano.
Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba huu mwaka wa 30
wa uhuru. Siku ya Ijumaa ni siku muhimu kwa Waislamu kama ilivyo kwa siku ya
Jumamosi ni siku muhimu kwa Wasabato kama ilivyokuwa siku ya Jumapili ni siku
muhimu kwa Wakristo wengine. Lakini siku ya Ijumaa ingawa kuna agizo la
serikali kwamba Waislamu waachiwe waende wakasali. Kuna viongozi siku ile ndiyo
siku ya kufanya Board Meeting, ili kumzuia Mkurugenzi ambaye ni Muislamu
ambaye anapenda kazi yake aogope. Shule zinafungwa saa 7. Jumapili vitoto
vidogo vidogo vya Kikristo vinakwenda kusali. Jumamosi vitoto vidogo vidogo vya
Kikristo vinakwenda kusali. Siku hizi vitoto vidogo vidogo vya Kiislamu
vinataka kwenda na wazazi wao. Naomba utaratibu ufanywe wa dhamiri kabisa kwamba
Ijumaa saa 6 kazi basi kwa Waislamu. Wale wanaofanya Board Meeting
waache wafanye saa 8, wafanye saa 9 na shule zote za Primary na Secondary
zifungwe saa 6 ili kuwapa nafasi watoto wa Kiislamu waende wakasali.
Mheshimiwa Spika, nina mengi lakini nitakuambia
mwisho. La mwisho, Rais aliwaambia Waislamu wote pale Dar es Salaam kwamba
atalishughulikia suala la elimu. Lakini akawashauri kwamba wale wafadhili ambao
hivi sasa wanatujengea Misikiti wajenge pia shule. Hilo jambo zuri, na Waislamu
wamelisikia na ninajua ya kwamba Waislamu wanataka hivi karibuni kumwendea Rais
kwenda kumshukuru. Ila nina jambo moja, natoa mfano wa Dar es Salaam, Waislamu
wanafikia asilimia 70 au zaidi. Kwenye magereza Dar es Salaam wengi kuliko
Wakristo au watu wengine. Hawa wengi, hawana kazi, jela watakuwa wengi.
(Kicheko)
Lakini tuende kielimu. Ninayo ripoti ya mwaka huu.
Waliofanya mtihani wa darasa la saba kuingia darasa la tisa, asilimia 71
Waislamu. Asilimia 29 ni wengine. Walioshinda katika wale asilimia 71 ni
asilimia 21. Katika wale 29 walioshinda tena sema mwenyewe. Katika asilimia 29
waliokwenda shuleni ni asilimia 79. Katika asilimia 71 waliokwenda darasa la
tisa ni asilimia 21.
Sasa kuna moja, ama Waislamu wajinga ama akili yao
haifanyi kazi, ama mtu ukiwa Muislamu wewe huna kitu, ama kuna kitu. Sasa
namwomba Waziri anayehusika, anaposema aseme ya kwamba kwa hali ilivyo Waislamu
wameumbwa wajinga. Au kwa hali ilivyo kuna sababu kadha, kadha. Mwalimu Nyerere
alisema zamani ifanywe bidii ya kuwanyanyua waliokuwa chini. Sasa bidii hii
siyo ya kuwanyanyua waliokuwa chini. Bidii hii ni ya kuwakandamiza waliokuwa
chini.
Mheshimiwa Spika, Rais Mkapa anawasaidia Waislamu.
Tulimwendea, mimi mmojawapo kwa mambo mengi ambayo ameyashughulikia. Nina
hakika ya kwamba mambo haya tuliyoyasema na aliyoambiwa na viongozi wa Kiislamu
kule bungeni atayashughulikia. Lakini ninaamini kabisa ya kwamba hataweza peke
yake bila ya msaada wa viongozi wangu hao walioko hapa. Wakisema hawa kwamba
ndiyo kawaida yao hiyo. Atapata tabu Rais wangu.
Mheshimiwa Spika, kengele ya pili imelia. Nashukuru
sana. Lakini nataka niseme kwamba haya niliyoyasema, nasema kwa sababu najua
mimi kwamba suala hili la mfarakano ni suala kubwa. Penye mfarakano hakuna
maendeleo. Penye mfarakano hakuna cha uchumi. Kwenye mfarakano kuna ghasia. Kwa
kuwa Rais ameomba tufanye kila jambo mfarakano usiwepo, basi serikali imsaidie
Rais katika kutekeleza wajibu wake kwa makundi yote ili pawepo na usawa.
(Makofi)
| Kitwana Selemani Kondo akifanya kipindi cha televisheni (TV Imaan) ''Walioacha Alama Katika Historia,'' nyumbani kwake Upanga tarehe 12 Septemba, 2012 akihojiwa na Mohamed Said |
No comments:
Post a Comment