Wednesday 4 February 2015

MAHAKAMA YA KADHI: TAMKO LA TAASISI 11 ZA KIISLAM


TAMKO LA TAASISI 11 ZA KIISLAMU KWENYE MAENEO AMBAYO YAMEPOTOSHWA NA MATAMKO YA BAADHI YA TAASISI ZA KIDINI NA MAGAZETI IKIWEMO MAASKOFU, BAKWATA NA GAZETI LA MIZANI KWENYE MCHAKATO WA KUTOA MAONI JUU YA  MUSWADA UNAOHUSU MAHAKAMA YA KADHI

Utangulizi
Sisi waislam, kupitia Jumuiya na Taasisi zetu za Kiislamu chini, tumepitia matamko kadhaa yaliyotolewa na taasisi mbalimbali, watu binafsi, viongozi wa serikali na magezeti, hususan, maaskofu, jukwaa la Wakristo Tanzania, gazeti la Mizani, Sheikh Jongo na Sheikh Mohammed Idd kutia kipindi cha Ar-risala kinachorushwa na Kituo cha TV cha Channel 10.

Matamko hayo yana malengo ya kupotosha baadhi ya maeneo ya maoni yaliyotolewa na Waislamu, kupitia Jumuiya na Taasisi zao kuhusu muswada wa marekebisho ya sheria yanayohusu mahakama ya kadhi kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala tarehe 19/01/2015.

Muhtasari wa Maoni ya Taasisi Kumi na Moja
Kwa muhtasari maoni ya Waislamu ambayo matamko tuliyoyataja hapo juu yanalenga kuyapotosha yalibainisha makosa, kasoro na udhaifu mwingi ulioko kwenye muswada unaohusu Mahakama ya Kadhi kiasi cha kutia shaka juu ya uthabiti wa nia ya Serikali wa kutaka kuleta sheria itakayowezesha mfumo wa utoaji haki wa sheria za Kiislamu kufanya kazi hapa nchini kwa ufanisi zaidi kulio mfumo wa sasa unatoa nafasi kwa maafisa wa mahakama kama majaji na mahakimu kuhukumu masuala ya sheria za Kiislamu ambapo mara nyingi maafisa hao hawana sifa, ujuzi, maarifa na uzoefu wa kushika nafasi ya kuhukumu chini ya utaratibu wa sheria za Kiislamu.

Maoni hayo, ya Waislam, kupitia jumuiya na taasisi zao Kumi na Moja, yalidhihirisha dosari kubwa kwenye muswada huo kwenye maeneo yanayohusu, kutokuwepo kwa kifungu kinacho anzisha na/au kuitambua Mahakama ya Kadhi; kutokuwepo muundo wa mahakama ya kadhi inayokusudiwa; kutoelezwa sifa za kadhi; upungufu kwenye utaratibu wa uteuzi wa makadhi; kukosekana maelezo ya ajira na usalama wa ajira ya makadhi; mapungufu yanayoambatana na kuweka mamlaka ya kutengeneza kanuni za mahakama ya kadhi kwa ‘Mufti’ na ya kukazia hukumu kwa Waziri; kukosekana kwa utaratibu wa kudhibiti nidhamu, mwenendo na maadili ya makadhi; mapungufu kwenye uwigo wa mamlaka wa mahakama; hiyari kwa mdaawa Muislamu kufungua shauri lake la sheria ya Kiislamu katika Mahakama ya Kadhi; upungufu wa dhana ya Mahakama ya Kadhi kujiendesha;  mamlaka ya Waziri kutoa matamko ya sheria za Kiislamu; na ulazima wa Mahakama ya Kadhi kutajwa kwenye Katiba.

Kwa hoja hizo, Waislamu kupitia taasisi zao hizo Kumi na Moja, walishauri kwa kupendekeza muswada mbadala kwamba serikali iuondoe muswada huo ili uboreshwe kabla ya kuwasilishwa bungeni kwa mjadala.

Upotoshaji Uliofanywa na Matamko Yaliyotolewa
Upotoshwaji wa maoni ya waislamu yaliyotolewa kupitia taasisi zao kumi na moja, uliofanywa na matamko yaliyotolewa na taasisi mbalimbali, watu binafsi, viongozi wa serikali na magezeti, umejikita kwenye maeneo haya ya fuatayo: (i) Kuwa taasisi 11 zilizowasilisha maoni ya Waislamu juu ya muswada wa mahakama ya kadhi zinawakilisha wachache; (ii) Kuwa asasi hizo 11 ni za Wahabi na hivyo maoni yao hayawakilishi waislamu wote; (iii) Kuwa Mufti ndiye kiongozi mkuu wa Waislamu; (iv) Kuwa Mufti ndiye anastahiki kuteua makadhi; (v) Kuwa BAKWATA ndiyo taasisi baba, nyingine watoto wake; na (vi) Kuwa Mahakama ya Kadhi italeta hukumu za kukata mikono, kuhukumu wasio kuwa Waislamu, na kubagua wasio kuwa Waislamu. Matamko ambayo yamebeba upotoshaji huu yametolewa kwa makusudi kwa lengo la hadaa kwa Waislamu, wananchi na serikali kwa jumla ili wasitilie maanani maoni yaliyotolewa na taasisi hizo Kumi na Moja ambayo kama yatafanyiwa kazi na Serikali yatawezesha kupatikana kwa Mahakama ya Kadhi inayokidhi matakwa ya sheria za Kiislamu na wajibu wake kama mamlaka ya kutoa na kutenda haki.

Tamko Letu Dhidi ya Upotoshaji Uliotolewa
Hivyo basi, kwa lengo la kuweka sahihi kumbukumbu na kuondosha uwezekano wa upotoshaji huu kuchukuliwa kuwa ni kweli, ni vyema tukabainisha ukweli kama ifuatavyo:
1.   
 JJumla ya taasisi kumi na moja (11) ziliwasilisha maoni ya Waislamu juu ya muswada wa Mahakama ya Kadhi. Hizi ni pamoja na taasisi ambazo zinatambulika, zimesajiliwa na zenye uwakilishi na mtandao wa kitaifa. Baadhi ya taasisi hizo ni Baraza Kuu, TAMPRO, BASUTA, JASUTA, IPC, HAIYAT ULAMAA, Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania; na Shura ya Maimam Tanzania. Maoni juu ya muswada wa Mahakama ya Kadhi yalipatikana baada ya mchakato uliohusisha wanachama na wawakilishi wa asasi hizo Tanzania nzima. Hivyo, siyo kweli kuwa asasi hizi Kumi na Moja (11) zinawakilisha maoni ya wachache. Ni wazi pia kuwa upotoshaji huu unadhihirisha kuwa waliotoa kauli za upotoshaji huu wanaona uzito wa umoja huu wa asasi za Kiislamu na maoni yao kweye suala hili la mahakama ya kadhi.

Hawa wanaosema taasisi hizi zinawakilisha maoni ya wachache na ya wahabi, hawatuambii kuwa maoni yao yanawakilisha taasisi ngapi za Kiislamu na ya madhehebu yepi. Ukweli ni kwamba hoja hii inadhihirisha hofu ya mshikamano wa asasi za Kiislamu katika kukabiliana na suala hili la Mahakama ya Kadhi. Ndiyo maana badala ya kujibu hoja na mapendekezo yaliyotolewa na asasi hizi, matamko hayo yamejikita kwenye kushambulia taasisi husika kwa hoja ambazo zina misingi ya kuwagawa Waislamu.

2.    Madai kuwa Mufti ndiye kiongozi mkuu wa Waislamu hapa Tanzania na kwamba ndiye anaye stahili kuteua makadhi nchini siyo sahihi. Inawezekana kwa taasisi kuwa na muundo wa uongozi ambao unamfanya Mufti kuwa kiongozi mkuu wa Waislamu wa taasisi hiyo na hapa huyo Mufti atakuwa mkuu wa taasisi husika na siyo Waislamu wote wa Tanzania. Mfano wa taasisi ambazo kiongozi wake mkuu ni Mufti ni BAKWATA. Hii haina maana kuwa kiongozi huyo ndiye kiongozi wa Waislamu wote nchi nzima. Tulieleza kwenye kamati ya Bunge kama tunavyoeleza hapa  kuwa zipo taasisi nyingi za Kiislamu zilizoandikishwa na mamlaka mbalimbali za uandikishaji wa asasi huru na vyama vya kijamii (NGOs) zenye maafisa wenye cheo cha Mufti. Kwa hivyo, siyo vyema sheria kuweka mamlaka yoyote  inayohusu mahakama ya kadhi (mfano uteuzi wa makadhi) kwa Mufti wa taasisi binafsi kwa kuwa kunaweza kukatokea mgongano na mgogoro mkubwa  kwa kila asasi kutaka kutumia mufti wake kuteua makadhi.

3.    Madai haya kwamba Mufti ndiye kiongozi mkuu wa Waislam na anaye stahili kuteua makadhi yanalenga kupotosha hoja ya msingi kwamba siyo sahihi kwa sheria kumpa Mufti mamlaka yeyote yahayohusu mahakama ya kadhi kwa kuwa mufti huyu, ama wa BAKWATA au wa taasisi nyingine yeyote, siyo chombo kinachoundwa na sheria yoyote (bali katiba ya taasis husika) na wala hakuna sheria inayounda ofisi ya Mufti.  Mahakama ya Kadhi kuwekwa chini ya Mufti ni kuifanya mamlaka hiyo muhimu ya kutoa haki kuwa chombo kilicho chini ya Taasisi binafsi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Kwa mfano, siyo kila Muislamu wa Tanzania Bara ni mwanachama wa BAKWATA na yuko chini ya Mufti wa BAKWATA. Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa kujumuika na kujiunga katika jumuiya mbalimbali. Kuwalazimisha Waislamu wawe chini ya Mufti wa BAKWATA au Mufti wa taasisi nyingine yeyote ni kuvunja Katiba ya nchi. Hivyo basi si sahihi mamlaka ya kutoa haki kuhusishwa na MUFTI anayetokana na Katiba ya Taasisi binafsi.

4.   Kama tulivyokwisha eleza kwenye maoni yetu tuliyowasilisha kwenye kamati ya Bunge juu ya muswada wa mahakama ya kadhi, kwa istilahi ya Kiislamu “Mufti” maana yake ni alim (msomi) mwenye upeo mkubwa wa elimu ya dini na sheria. Ni mtu aliyebobea katika taaluma za dini na sheria. Si afisa wa Serikali wala hana dhima ya utawala au uongozi. Alim hutambuliwa kuwa Mufti na maulamaa wenzake wa eneo husika kwa kutambua upeo wake mkubwa katika fani za elimu ya dini na sheria. Alim akitambuliwa na kupewa hadhi ya mufti huchukuliwa kuwa ni marejeo kwa ajili ya kutolea ufafanuzi masuala ya elimu ya dini na sheria. Kwa hiyo Mufti jukumu lake ni kufutu mas’ala ya dini na sheria. Si kuwa mtawala au mpangaji wa masuala ya utawala. Ni dhahiri kuwa madai yaliyotolewa kuwa Mufti ndiye kiongozi Mkuu wa Waislam hayana mashiko kilugha wala kiistilahi.

5.   Hatuamini hata kidogo kuwa wanaotoa madai haya na upotoshaji huu hawajui nafasi ya Mufti katika mfumo wa sheria za Kiislam na kilugha. Tunashawishika kuamini kuwa wanafahamu ukweli kama tulivyouweka hapo juu, bali wanapotosha kwa malengo mahsusi kwa sababu baadhi yao ni wasomi wenye shahada mpaka shahada za juu katika fani mbalimbali za dini ya Kiislamu.

6.      Madai kuwa BAKWATA ndiyo taasisi baba na taasisi nyingine ni watoto wake  hayana mashiko yeyote ndiyo maana hata Kamati ya Bunge haikutoa mualiko kwa BAKWATA pekee bali kwa taasisi nyingi za Kiislamu ikiwemo BAKWATA. Ifahamike kuwa BAKWATA ni taasisi ya kidini kama zilivyo taasisi nyingine lakini pia BAKWATA ni taasisi dhaifu na iliyopoteza imani kwa Waislamu wengi nchini. Jina la taasisi hiyo haliifanyi taasisi hiyo kuwa ndiyo kubwa na yenye hadhi kuliko taasisi zingine za Kiislamu. Hata hivyo, kimuundo na kiuwakilishi, taasisi hii haina sifa ya kuwa ni taasisi kubwa na yenye mamlaka dhidi ya taasisi nyingine za Kiislamu kwa sababu zifuatazo;(i) BAKWATA haina wanachama tofauti na taasisi zingine ambazo zina wanachama; (ii) mara kadhaa BAKWATA imetoa matamko kuwa haiwakilishi Waislamu wote wa Tanzania; (iii) Asili yake BAKWATA haijaundwa na Waislamu kwa umoja wao. Ndiyo maana uhalali wa BAKWATA kuwa ndicho chombo kikuu cha uongozi wa Waislamu nchini umehojiwa na Waislamu mara nyingi.

7.      Kama tulivyoeleza kwenye maoni yetu juu ya muswada wa Mahakama ya Kadhi, tunarudia kusema tena kuwa iwapo Serikali itafuata upotoshaji huo kuwa BAKWATA ndiyo chombo kikuu kinachowakilisha Waislamu wote na hivyo kuipa BAKWATA nafasi ya kuwawekea Waislamu Mahakama ya Kadhi itahesabiwa na Waislamu kuwa ni hila ya Serikali kutaka kulazimisha mamlaka ya BAKWATA juu ya Waislamu hata wale wasioikubali taasisi hiyo.  Jambo ambalo litakuwa limekiuka haki ya msingi ya kila Mtanzania kujumuika kwa uhuru bila kutezwa nguvu au kushinikizwa. Inasikitisha kwamba, wakati mchakato wa maoni juu ya muswada wa Mahakama ya Kadhi unaendelea, baadhi ya viongozi wa juu wa serikali wametoa kauli ambazo zinaoana na hoja dhaifu kuwa BAKWATA ndicho chombo cha uwakilishi cha Waislamu na kwamba serikali imeuandaa mchakato wa Mahakama ya Kadhi kwa kuishirikisha BAKWATA kwa karibu kama chombo kinachowakilisha Waislamu wote. Hili ni kosa kubwa kwa kuwa BAKWATA siyo chombo cha Waislamu wote nchini..

8.      Kuna matamko yametolewa na taasisi na watu binafsi ambao wanatumia muswada huu wa mahakama ya kadhi kuleta hoja zinazokusudia kuleta faraka za kimadhehebu kwa propaganda ambazo hazina msingi au ukweli wowote katika dini ya Kiislamu hasa suala la kupinga Mufti kuwa ndiye mteuzi wa makadhi na utengenezaji wa kanuni za Mahakama ya Kadhi. Tunaotoa udhaifu wa kumpa madaraka hayo Mufti tumezingatia hoja za kisheria, kidini na kimantiki. Hivyo si kweli kuwa tunapinga Mufti kupewa madaraka hayo kutokana na tofauti za madhehebu ndani ya Uislamu. .

9.      Kadhalika, wapo viongozi wa dini ambao si Waislamu (mfano maaskofu) wametoa matamko ya kupinga Mahakama ya Kadhi kwa hoja kuwa italeta hukumu za kukata mikono, kuhukumu wasio kuwa waislamu, kubagua wasio kuwa waislamu nk. Hoja hizo zote siyo za kweli na watoaji wa hoja hizo wanajua ukweli kuwa mahakama ya kadhi inayokusudiwa ni mahakama itakayotumia sheria za Kiislamu ambazo zinatumika kwenye mahakama za kawaida toka enzi za ukoloni mpaka leo. Inajulikana wazi kuwa mahakama ya kadhi itashughulika na mambo binafsi ya watu kwa mujibu wa sheria za Kiislamu ambazo ni sehemu ya sheria halali zinazotumika hapa nchini, mfano mambo kama ndoa, talaka mirathi, wakfu na malezi ya watoto. Kinachofanywa na viongozi hao wa dini wasiokuwa waislamu ni kuivunjia heshima jamii ya Kiislamu na kupotosha ukweli ambao uko wazi.



…………………………………………………………………………
        Sheikh Suleiman A. Kilemile
Mwenyekiti  wa Hay Atul -Ulamaa

03/02/2015

No comments: