ALI SONGEA MBANO
Nje kidogo ya mji wa Songea kuna kitongoji kinaitwa Mahenge, hapo kuna sehemu ya kumbukumbu ya vita vya Majimaji. Jambo kubwa la mahala hapo ni kaburi kubwa la halaiki ambamo askari zaidi ya sitini na… (sitini na saba) walizikwa kwa pamoja. Na kando ya kaburi hilo la pamoja kuna kaburi la Ally Songea Mbano ambae yeye alizikwa peke yake.
Kwa mara
ya kwanza nilitembelea makumbusho hayo mwishoni mwaka 2007. Baada ya kusaini
kitabu cha wageni na kulipa ada ya kituo muhudumu wa kituo hicho alitupa
karatasi yenye orodha ya majina ya wale wote walionyongwa na kuzikwa hapo. Ukiitazama
orodha hiyo na hasa ukiwa Mwislam jambo moja litakustuwa. Robo tatu ya
walionyongwa na kuzikwa hapo ni Waislaam. Linaanza jina lake la Kiiislam, kisha
kwenye mabano kuna jina la Kikristo na mwishoni linaishia jina la kiasili,
mfano Abdulrahman [Dominic] Mputa Gama.
Muhudumu
akatueleza kuwa hawa mashujaa wa vita vya Maji Maji kabla ya kunyongwa
alikuwako padri ambae aliwabatiza na kuwapa majina ya Kikristo na baadae
kunyongwa, wengi walibatizwa kwa hadaa kuwa wakibatizwa wataachiwa huru, wote
katika hao walionyongwa walikuwa ni Waislam. Uzuri ni kwamba katika orodha hiyo
kulikuwa na jina na sahihi ya yule padri aliyewabatiza, na kwa mkono wake
[huyo padri] aliiyaandika hayo majina. Karatasi yenyewe ilihifadhiwa vizuri
kwenye fremu ngumu ya kioo. Tuliomba kwa nguvu zote kupatiwa hiyo karatasi ya
majina hata kwa kununua lakini haikuwezekana pamoja na kuwaona na kuwaona
wakubwa wa kituo hicho. Niliporudi kwa
mara ya pili mwezi July 2009 nilipata mstuko.
Karatasi
iliyohifadhiwa kwenye fremu ngumu ya kioo, iliyokuwa na majina ya Kiislaam
ya mashujaa wa vita vya Maji Maji, haikuwapo,na badala yake imewekwa karatasi
nyingine ombayo ndani ya karatasi hiyo majina ya Kiislaam ya mashujaa hao wa
vita vya Maji Maji yameondolewa na kuachwa majina ya ubatizo na yale ya kiasili
tu, jina la padri, sahihi yake na wadhifa wake katika Kanisa Katoliki pia
vimeondolewa na karatasi yenyewe haikuwa kwenye fremu ya kioo na ilikuwa katika
fotokopi tu.
Nilimuuliza
muhudu kulikoni? Akasema, “Songea pana mzee mmoja maarufu sana katika historia
ya TANU na historia ya kuasisiwa Bakwata anaitwa kwa kifupi M. S. Mzee
huyu ana binti yake ambaye ameolewa na Mzungu wa Kijerumani. Binti huyu na na
mumewe wa Kijerumani walikuja hapa Songea matembezi. Hivyo kwa shinikizo la
huyu mzee M.S. karatasi hiyo alipewa huyu Mzungu kwa ahadi kwamba anaipeleka
Ujerumani na atairudisha. Hivyo ndivyo karatasi ile asilia ilivyotoweka. Kubwa
katika karatasi ile ni ule ushahidi wa majina kuwa wote katika wale walionyongwa
na kuzikwa hapo ni Waislaam, wengi katika hao walihadaiwa kuachwa huru hivyo
wakabatzwa ispokuwa wachahe sana waligoma kama shujaa Abdulrauf Songea Mbano. Huyu
kwa ushujaa wake wa kupambana na Wajerumani aligoma na akasumbua sana kiasi
akanyongwa siku yake na peke yake na ndio sababu akazikwa peke yake.
Ukiingia
ndani ya kinyumba cha ghorofa, unaanza kuona picha za mashujaa wa Maji Maji
wakiwa wamevaa mavazi ya vita mithili ya mahujaji wanavyovaa Ihraam wakati wa
hija. Kinachoongezeka kwao ni vilemba kichwani. Chini ya kila picha kuna jina
la aliyekuwa kwenye picha ile. Ukipanda gorofani utaona silaha za kiajadi kama
mikuki, pinde, ngao n.k. Kinachosisimua zaidi ni mavazi ya vita. Mavazi ya vita
ya askari wa Maji Maji wengi walivaa kanzu za Kiislaam na vilemba. Jambo
jingine linalosisimua ni kile ambacho watu wa kituo hicho wameandika ”rosary”
hili ni jina la Kikristo, hasa la Kikatoliki, ni zile shanga ambazo
huning’inia msalaba lakini unapotazama hicho kilichoitwa “rosary” utaona si “rosary,”
bali ni tasbihi hasa ya Kiislaam yenye kupangika hasa shanga zake, 33, 33, 34.
Maneno yaliyoandikwa kuelezea “rosary” hizo ambazo ni tasbihi ni:
“Hizi ni
rosary ambazo wapiganaji wa majimaji walikuwa wakitumia KUTAMBIKA kabla ya
kwenda vitani kwa kuamini kwamba zitawakinga na risasi.”
Ukweli
ni kwamba hawa askari wa Maji Maji wengi walikuwa ni Waislaam hivyo hawakuwa
WAKITAMBIKA bali walikuwa wakitumia tasbihi hizo kufanya dhikri kwa Allah kabla
ya kwenda vitani. Midhali sisi Waislaam hatujawa tayari kuandika historia yetu
kama Waislaam wanaotuandikia watapotosha na kupindisha na
kutuzulia wanavyotaka. Hapo gorofani kuna
jambo jingine la kusisimua. Kuna magudulia na makopo. Wameandika kuwa, haya
ndio makopo ambayo askari wa Maji Maji walikuwa wakiyatumia KUNAWA kabla ya
kwenda vitani [kushika udhu na sio kunawa] pia kwa kuamini kuwa maji hayo
yatawakinga. Muhudumu alitueleza kuwa kumbukumbu nzuri na za kuaminika ziko
Jimbo Kuu la Wakatoliki Peramiho.
Tulikwenda
jimboni lakini hatufanikiwa kwa sababu za ki-urasimu tu.T ulitakiwa tupate
kibali cha Askofu Mkuu. Hatukukipata. Kwa yale tuliyoyaona na kuyashudia yafuatayo:
Vita vya
Maji Maji havikuwa ni vita vya kizalendo, kwamba wazalendo walikuwa wakipigania
nchi yao. La. Vilikuwa ni vita vya Waislaam wakipigana na Wakristo wa Kijerumani
waliovamia maeneo asilia ya Waislaam kwa lengo la kuuwa Uislam na kusimamisha
Kanisa kwani mazingira yote utayoyaona ya mashujaa wa vita vya Maji Maji ni mazingira
ya Kiislaam, kingine ni kwamba hukuti mahala yalipo makaburi ya askari wa Kijerumani
ila katika miji ya Waislaam kama Kilwa, Bagamoyo n.k. Kwa nini wauliwe maeneo
ya Waislaam tu? Walifuata nini huko?
Kuna
upotoshaji mkubwa sana wa historia ya vita vya Maji Maji. Vinaoneshwa kama ni
vita vya wazalendo wakipigana na wakoloni wa Kijerumani, wakati ukweli si
hivyo. Ukweli ni kwamba vita vya Maji Maji vilikuwa ni vita baina ya Waislaam
na Wakrito wa Kijerumani, Waafrika Wakristo wa Songea walijiunga na Wakristo
wenzao wa Kijerumani dhidi ya Waafrika wenzao wa Kiislam.
Wakristo
wameitafiti hakika hii na wakaijua kisha wameificha kwa maslahi yao.
Kuna haja ya wasomi wetu wa Kiislaam
kufanya juhudi za makusudi za utafiti wa historia yetu ili kukifanya kizazi
hiki cha Kiislaam kujitambua zaidi na kujenga ujasiri. Taasisi za Kiislaam na
watu binafsi [matajiri] wawawezeshe kiuchumi wasomi hawa kufanya kazi hii.
Mwaka 2008 nimetembelea Kilwa Kisiwani, huko
nikamkuta Mzungu wa Kifaransa akiandika historia ya Kilwa Kisiwani akiitwa Thiery,
ameweka kambi na majenereta ya umeme, solar power na makompyuta. Kazi nyingine
kubwa alokuwa akifanya ni kukarabati yale magofu ambayo mengi ni misikiti na
majumba ya mawe ya wafalme wa kale. Kilwa Kisiwani ni moja kati ya dola kubwa
za Kiislaam katika mwambao wa Afrika Mashariki, ndio dola ya mwanzo kuwa na
sarafu yake ambayo iliandikwa jina la Allah. Tuliposoma kazi ile ya Yule
Thiery Mfaransa tayari alikwisha ipotosha kwa kiasi kikubwa. Sikuwa na la
kumfanya. Kizazi cha vijana wa Kiislaam hakitopata historia ya kweli ya Kiislaam
kama tutawaacha akina Thiery waandike na hivyo vijana wetu hawatajitambua na hawatokuwa na ujasiri katika Uislam wao.
Ilunga Hassan Kapungu
Jumanne 19 Oktoba 2010


No comments:
Post a Comment