TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI

TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA
KUHUSIANA NA MUSWADA WA MAHAKAMA YA KADHI
Sisi,
Maaskofu kutoka TEC, CCT na CPCT tumekutana leo tarehe Machi 30, 2015 hapa Dodoma ili kuomba kwa pamoja juu ya mgawanyiko
unaodhihirika wa dini za Kikristo na Kiislamu kutokana na muswada wa Mahakama
ya Kadhi. Maaskofu tuliokutana hapa hatuna hasira na wala hatuongozwi na hasira
wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine
wanavyotutafsiri. Tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na sala na tunasukumwa
na upendo kwa wananchi ili kujenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na
maelewano.
Pia
tumekuja kufuatilia kwa kina Muswada
wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo
mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964. Muswada
huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ambao utawasilishwa Bungeni
April 01, 2015 kwa hati ya dharura
na hivyo kuufanya umma wa Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada
huo wakati bado hoja zetu za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na
Sheria ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa.
Tangu tulipokutana Machi
10, 2015 ambako tulitoa tamko letu kuhusiana na Mahakama ya Kadhi na Katiba
Inayopendekezwa, tumekuwa tukiendelea kutafakari juu ya yale tuliyokuwa
tumesema katika matamko yetu mbalimbali na jinsi amani na utulivu wa nchi yetu vinavyoendelea
kumomonyoka siku zinavyokwenda.
Kwanza tumeshangazwa na tabia ya viongozi wa serikali ya kuitisha
na kuendesha mikutano wanayodai ni ya viongozi wa dini lakini isiyo rasmi. Machi 03, 2015 Waziri Mkuu aliitisha
mkutano kupitia Mchungaji mmoja ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au
Kanisa aliyeshiriki. Jambo la kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, 2015 ambapo Mhe. Rais
alishiriki kikao cha kikundi ambacho sio rasmi yaani Kamati ya Amani ya Mkoa wa
Dar es Salaam. Tunasema kamati hiyo siyo rasmi kwa sababu haina baraka za
viongozi wa ngazi za juu wa kidini wa Mkoa huo na haina mwongozo wa kazi zake.
Mikutano ya jinsi hii kati ya serikali na wale ambao imewaona kuwa ndio
viongozi wa dini sio sahihi kwani viongozi wa dini wana taratibu zao za
kualikwa au kuwakilishwa katika mikutano na viongozi wa serikali au wa dini au
madhehebu mengine. Tunawashauri wanaohutubia na wanaoshiriki mikutano hii wajue
kwamba washiriki hawana uwezo wa kuamua au kukubaliana na jambo lolote kwa
niaba ya viongozi wao wa juu na pia viongozi husika wa serikali wasifurahi
kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini kwani hao washiriki sio wawakilishi
rasmi na hawana uwezo wa kutoa maamuzi au kukubaliana juu ya jambo fulani la kitaifa.
Pili, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu juu ya muswada wa
Mahakama ya Kadhi na tumebainisha dhahiri kwamba kile tulichokuwa tunasema
kitatokea kimeaanza kutokea bayana. Yale yaliyotokea kwenye semina kuhusu
Mahakama ya Kadhi kwa Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Machi 29, 2015 ambao ni
wasomi, ni ishara ndogo sana ya kile kitakachotokea maeneo yote ya nchi yetu. SERIKALI KWA NIA MOJA NA KWA SABABU
TUSIZOZIJUA INAANZISHA VITA VYA KIDINI KATI YA WATANZANIA WAKRISTO NA WAISLAMU.
Tunashangazwa kuona jinsi serikali inavyonuia jambo hili ovu litakaloleta balaa
kwa nchi yetu wakati huu wa kuelekea kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na
baadaye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kutokana na mambo hayo makuu mawili hapo juu, sisi
Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunatamka kama ifuatavyo :
- Matamshi ya Mhe. Rais akihutubia aliyowaita viongozi
wa dini tarehe Machi 28, 2015
kuwa Mahakama ya Kadhi ni ya Waislamu wenyewe na serikali haitajihusisha
wala kugharamia yanakinzana na kile kinachoendelea bungeni na nchini. Hapa
tunajiuliza, endapo maneno ya Rais ni kweli, mbona Bunge linaendelea kujadili
kitu ambacho serikali haitajihusisha wala kukigharimia ? Kwa mantiki
hiyo, tunamtaka Mhe. Rais aagize muswada huu uondolewe Bungeni na
usijadiliwe tena kwa kuwa Utafiti wa Tume ya kurekebisha sheria ulishaonyesha
madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi. Vinginevyo, kuendelea
kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba serikali inajihusisha na
itagharimia mahakama hiyo.
- Serikali ijue kuwa endapo Wabunge wa dini za
Kikristo na Kiislamu watapigana na kisha baadaye wananchi nao wakafanya
hivyo katika maeneo yao, SERIKALI ITAKUWA
NDIYO CHANZO CHA MAPIGANO HAYO. Kama tulivyotamka hapo juu, kuhusiana
na jambo hili tunamtaka Mhe. Rais aiepushe nchi yetu na kuingizwa kwenye
mapigano ya kidini ambayo kuyadhibiti itakuwa vigumu sana (tafadhali rejea
kinachoendelea huko Nigeria). Pia tunamwomba Mhe. Rais akumbuke na kutafakari
kile kilichotokea na kinachotokea nchi ya Afrika ya Kati kati ya kundi la Seleka
(Waislam) na kundi la Anti Balaka (Wakristo).
- Tunaamini kuwa viongozi wa serikali wanafahamu
viongozi rasmi wa dini na madhehebu ya dini. Kwa mantiki hiyo tunawashauri
viongozi wa serikali waache kabisa kutumia vikundi visivyo rasmi kualika
mikutano wanayodhani kuwa itakubalika na waumini wa dini hizo. Mikutano
yote ya jinsi hiyo itakayoitishwa ni batili na maamuzi yake hatuyatambui na
hatutayatambua.
- Bado Maaskofu tunasimamia Tamko letu la Machi 10, 2015 na tunawahimiza
Wakristo wajitokeze kwa wingi katika kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la wapiga Kura na zaidi wajitokeze kwenda kupiga kura ya HAPANA wakati wa kura ya maoni
kwani Katiba inayopendekezwa ilifikia hapo kwa njia ya ubabe, ilikosa
uadilifu na mbaya zaidi ni RUSHWA YA
AHADI YA MAHAKAMA YA KADHI ya iliyotolewa na Waziri Mkuu kwa Waislamu
wakati wa kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Tunafanya hivyo kwa dhamiri
safi kwa sababu ya imani yetu na kwamba sisi ni raia wa nchi hii na tuna
haki ya kueleza mawazo yetu bila woga kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
mwaka 1977 inavyotupa haki.
- Mwisho tunawaomba Wakristo wote waendelee kufunga na
kuomba kwa ajili ya utulivu na amani ya nchi yetu.
‘Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, atavunjika
ghafla, wala hapati dawa .’Mithali 29 :1
Imetolewa na

No comments:
Post a Comment