Wednesday, 1 April 2015

Sheikh Muhammad Bin Umar Al-Khatibu - Hamza Z. Rijal

Baadhi ya Masheikh Waliopita Zanzibar na Kuweka Msingi wa Elimu ya Dini ya Kiislamu
Sheikh Muhammad Bin Umar Al-Khatibu
Na Hamza Z. Rijal
Katika mfululizo wa makala za wanavyuoni wetu hii leo tutamuangalia alimu mwengine wa visiwani humu kwa jina ni Sheikh Muhammad Bin Umar Al-Khatibu.

Sheikh Muahammad Bin Umar kama watu walivyopenda kumwita bwana wa Shangani/Shakani, alizaliwa mwaka wa 1239 A.H (1876). Unapojaribu kutaka kumzungumza Sheikh inakubidi kwanza umtizame ni nani mwalimu wake? Katika wanafunzi wengi wa Sheikh Abdallah Bakathir (1860-1925) aliowasomesha pale alipokuwa keshastakimu Unguja alikuwa ni Sheikh Muhammad Bin Umar.

Sheikh Muhammad Bin Umar alipelekwa kupiga goti na kupinda shingo (kusoma) kwa Sheikh Abdallah Bakathir na hapo aliweza kuonyesha jitihada kubwa ya kujifunza, na Sheikh Bakathir akatokea kumpenda mno na kumfanya kati ya watu wa aila yake na alikuwa akiandamana naye popote pale alipokuwa anakwenda na Sheikh anahakikisha kuwa Sheikh Muhammad Bin Umar yupo naye popote pale aendapo.

Sheikh Muhammad Bin Umar alipokuwa anajifunza na wanafunzi wenzake ikiwa wa makamo yake na wengine waliomzidi hirimu, kilimchukua kipindi cha muda mfupi sana kutokana kuwa mwanafunzi hodari na aliweza kuwa taliisha wenziwe na muda usio mrefu, aidha alipata makamo ya kusomesha darasa ndogo ndogo hapo Ukutani.

Ukutani katika nyakati hizo ilikuwa ni sawa na "College’ yeyote ile kubwa ya kidini hivi sasa duniani, kwani wanavyuoni takriban asilimia kubwa walipitia hapo na kusomesha Ukutani na wasomi hao walikuja kukubalika nje ya Afrika Mashariki ikiwemo Hadharmout, Makka na Misri.

Sheikh Muhammad Bin Umar inasemekana kuwa alikuwa na wake wawili, mmoja akikaa mjini na wa pili akiishi naye katika mtaa wa kikwajuni ambako alikuawa akidarasisha baadhi ya siku za wiki katika Msikiti wa Kikwajuni ukijulikana kwa saa Msikiti wa Ahli-Sunna.

Kilimchukua kipindi kifupi cha kusomesha watu wa hirimu yake ambacho kilidumu miaka saba kabla ya kupewa makamo kamili ya kudarasisha darasa zote alikuwa akianza kudarasisha mara tu baada ya sala ya alfajiri, hadi saa tano za asubuhi, wanafunzi wakibadilishana kwa makundi.

Kundi hili likimaliza kundi jengine linaingia, na hivi ndivyo walivyokuwa wakisoma watu na namna walivyokuwa wakisomesha. Na wengi wa wanavyuoni wetu walipitia mkondo huu kusoma na kutalii na wenzao kuanzia asubuhi hadi Isha.

Suala la kujiuliza ni vipi wakijiendesha kimaisha? Kila mmoja alikuwa na sampuli yake, wengine walikuwa wametolewa makwao na kila haja zao zilikuwa zikikidhiwa makwao, wengine walikuwa na mali za kurithi nyumbani, wengine walikuwa wafanya biashara, na wengineo hawajakuwa na lolote ila wakijifunza na kuangalia bahari ya maisha itawachukua vipi na kuwaweka wapi.

Msikiti Gofu ni kati ya misikiti michache visiwani humu kuwa wanasali sala ya Tarawehe na Sala za witri kwa mtindo wa kusomwa juzuu kamili, jema linaloendelea hivi sasa ni misikiti isiopungua 20 hivi visiwani inakwenda na mtindo wa kusali Tarawehe na Witri kwa usomaji wa juzuu nzima. Msikiti wa pili kusali Tarawehe na Witri kwa kusoma Juzz nzima ulikuwa Msikiti wa Chwaka katika Karne ya 19.

Sheikh Muhammad Bin Umar alipewa makamo ya kusalisha Tarawehe na Witri wakati walimu wake wakuu wa hai na wakiwa nao wakihudhuria sala hizo, hao sio wengine ila ni Sheikh Abdallah Bakathir na Sayid Ahmed Bin Sumeit.

Sheikh Muhammad Bin Umar alidumu kuzisalisha sala hizi hadi pale alipokuja kupokewa na Sheikh Abdallah Bin Farsy katika mwaka wa 1933.

Sheikh Muhammad alikuwa akiisoma Quran kwa hukmu zake na kwa ukamilifu, jambo ambalo lilimfanya achaguliwe kuwa Khatibu wa Msikiti Ijumaa wa Malindi na Sheikh Abdallah Saleh Farsy anatueleza kuwa "hakutokea Khatibu katika Unguja, Pemba, Mrima, Mombasa na Lamu mwenye sauti ya juu na kali kama Sheikh Muhammad Bin Umar."

Sheikh Muhammad Bin Umar alidumu kusomesha Msikiti wa Kikwajuni, na alihamia Msikiti Gofu kusomesha darasa zake zote katika mwaka wa 1927 alipokufa Sheikh Muhammad Bin Abdallah Al-Hinzwany.

Alikuwa na darsa nyingi akizisomesha hapo Msikiti Gofu na alizidi kutwikwa mzigo na mzigo kumuelemea pale Sheikh Muhsin Barwany aliposhindwa kuzisomesha darsa pale Ukutani kuzidiwa na maradhi na kupokewa na Sheikh Abubakar, na mwisho Sheikh Muhammed Bin Umar akaendeleza darsa na watu wakawa wanajihisi kuwa zimeondoka sura tu za watangulizi wake lakini taaluma waliokuwa wakiipata ni ile ile.

Darsa zake zilikuwa zikihudhuriwa na watu ambao walikuwa wa madhehebu nyenginezo, lakini waliyaweka madhehebu upande na kwenda kuchota elimu kwake, kwani alikuwa ni kisima chenye kina kirefu na maji yake yapo saa zote na kila yakitekwa basi huzidi kuja juu.

Alipokufa Sheikh Abubakar alikuwa yeye ndiye mwenye amri zote za nyumba mbili za Ukutani kwani, bwana huyu alipata bahati nzuri ya kumuoa mtoto wa Sheikh wake, kwa hivi ni kusema kuwa Sheikh Abdalla alikuwa mkwewe na Sheikh Abubakar na ndugu zake wanakuwa shemegi zake, ni Sheikh Muhammad Bin Umar aliyetoa shauri ya kufanya nyumba mbili za ukutani kuwa ni nyumba za wakfu na kila mmoja wao akaridhia (soma makala ifuatayo juu ya tarekhe ya Ukutani).

Wengi wa Masheikh waliopita walikuwa na muandiko mzuri, naye Sheikh Muhammad Bin Umar alikuwa na muandiko wenye kupendeza kuusoma na yeye ndiye aliyeandika "Muswada" (Manuscript" wa baadhi ya vitabu alivyovitunga Sayyid Ahmad na Sheikh Abdalla; na kavisoma mbele yao, na wao wakamsikiliza).

Sheikh Muhammad Bin Umar alifunga macho usiku wa kuamkia Jumaane tarehe 30 Mfunguo Tisa 1377 A.H (21.1.57).

Msikiti Gofu na Ukutani kama nilivyokwishaeleza wanavyuoni tele wakisomesha hapo na kusomea hapo, na mwahali humu mulikuwa ndio chimbuko la elimu hapa visiwani, Leo Msikiti Gofu darsa ya pekee iliyo na wanafuzni wengi ni ile ya mwezi wa Ramadhani baada ya sala ya Alasiri ya tafsiri ya Quraan isomeshwao na Mufti Sheikh Harith Bin Khelef, lakini Gofu haina tena darasa nzito nzito zilizopata kuweko ingawa kuna darsa ndogo ndogo tu, na Ukutani nayo imepoteza mkondo wa taaluma iliyopata kuweko ingawa elimu bado inasomeshwa.

Wako wapi watakaochukua jukumu la kuirejesha hadhi na mkondo wake uliopata kuweko mwahali humo mwenye historia kubwa ya elimu ya dini visiwani, yaani Msikiti Gofu na Ukutani.

Tunamuomba "Allah" azirejeshee Unguja na Pemba yake elimu ya Kiislam kama walivyokuwa nayo kina Sheikh Muhammad Bin Umar na wengineo "Ameen. ’’

No comments: