TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU 11
KUHUSU HATIMA YA MAHAKAMA YA KADHI NA HALI YA AMANI YA TANZANIA – MARCH 2015
| Naibu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu Sheikh Rajab Katimba Akitoa Tamko la Waislam |
Hivi karibuni baada ya Serikali
kuandaa Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali, hususan sehemu ya muswada
unaohusu Mahakama ya Kadhi kumekuwa na matamko toka kwa Maaskofu na Wachungaji kupitia
Jukwaa la Wakristo Tanzania linaloundwa na taasisi za BARAZA LA MAASKOFU
KATOLIKI TANZANIA (TEC), JUMUIYA YA KRISTO TANZANIA (CCT), BARAZA LA MAKANISA YA PENTEKOSTE TANZANIA
(CPCT) zikiitaka Serikali na Bunge kuacha mara moja kuendelea na utaratibu wa
kuwasilisha, kujadili na kupitisha sheria ya utambuzi wa Mahakama ya Kadhi
Tanzania kwa hoja kuwa hilo ni jambo la kidini liachwe kwa wanadini husika.
Imedaiwa na Maaskofu na Wachungaji hao kuwa muswada wa Mahakama ya Kadhi
unakiuka katiba na ni rushwa iliyotolewa na Serikali kwa Waislamu ili kupata
ridhaa ya Waislamu kuipitisha Katiba Pendekezwa wakati wa Bunge Maalum la
Katiba.
Sisi Waislamu chini ya mwavuli
wa Jumuiya na Taasisi Kuu za Kiislamu Tanzania zipatazo 11 (ambazo ni Hay
Atul-Ulamaa, Shura ya Maimamu, DUMT, BASUTA, AN-NAHL TRUST, BARAZA KUU, Jumuiya
na Taasisi, JASUTA, TAMPRO, IPC, AL-MALID) kwa azimio la kikao cha dharura cha
tarehe 21/03/2015 tunapenda kutamka
yafuatayo:-
1. Kama
inavyojulikana Tanzania ni nchi yenye kuongozwa kwa sheria za aina nne (sheria za
Kiislamu, sheria za Kimila, sheria zilizorithiwa toka kwa waingereza (yaani
common law) na sheria za kutungwa na Bunge). Hivyo basi Sheria za Kiislamu ni
sehemu ya sheria halali za nchi hii. Sheria hizo za Kiislamu zimekuwa zikitumiwa
na mahakama kabla ya uhuru na baada ya uhuru. Kwa kipindi chote hicho zaidi ya
miaka 100 Maaskofu na Wachungaji hawakuwahi kupinga matumizi ya sheria hizo za Kiislamu
katika mahakama za Serikali ilihali wamekuwa wakijua fika kuwa sheria hizo ni
za kidini. Tunasikitishwa na hali hiyo kubadilika sasa. Hakuna mantiki yoyote
kwa maaskofu na wachungaji kuipinga Mahakama ya Kadhi ambayo itaendelea kutumia
sheria hizo za Kiislamu zinazotumiwa na Mahakama za kawaida.
2. Maaskofu
na Wachungaji kulitaka Bunge kuacha kujadili muswada wa Mahakama ya Kadhi ni
kuingilia uhuru na utawala wa Bunge jambo ambalo serikali na Bunge linapaswa
kukemea bila ya kuwa na kigugumizi.
3. Serikali
iwachukulie hatua za kisheria Maaskofu na Wachungaji kwa kutoa matamko yakichochezi
yaliyokusudia kuumiza hisia za kidini kwa Waislamu kinyume cha sheria ya Kanuni
ya Adhabu Sura ya 16, ikiwemo kuwakamata, kuwafikisha mahakamani na kuzuia
dhamana kama inavyofanya kwa masheikh pindi wanapotoa kauli zinazopingana na
mtazamo wa serikali.[AK1]
4. Kwa
kudai kuwa serikali imetoa rushwa kwa Waislamu kama kundi maalum kwa kukubali
sheria itakayounda Mahakama ya Kadhi ili kuipitisha Katiba Pendekezwa ni
kuidhalilisha dini ya Mwenyezi Mungu, kuwadhalilisha Waislamu na ni kuumiza hisia
za Waislamu na kuhatarisha amani na utangamano.
5. Serikali
isipofanya kama tulivyoeleza hapo juu utakuwa ni ushahidi MWINGINE kwetu Waislamu
kuwa hakuna usawa mbele ya serikali kwamba iko tofauti katika kushughulikia
kauli za masheikh na kauli za maaskofu na wachungaji Wakristo. Vile vile
hatutokuwa na cha kuzuia imani za Waislamu kuwa maaskofu na wachungaji walitoa
tamko lao kwa kushauriana na serikali na wengine kwenda mahakamani kuizima Mahakama
ya Kadhi kama mpango maalum.
6. Serikali
iendelee na mchakato wa uundwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa kufuata maoni
yaliyotolewa mbele ya Kamati ya Sheria na Utawala ya Bunge kwa kuzingatia mambo
muhimu yafuatayo:-
i. Serikali iache njama au hila za kuigeuza Mahakama
ya Kadhi inayohitajika kuwa miliki ya taasisi ya BAKWATA na MUFTI wa BAKWATA.
ii. Serikali iache njama za kutaka kutumia
kisingizio cha uundaji wa Mahakama ya Kadhi kuihalalisha kupitia sheria ya Mahakama
ya Kadhi BAKWATA kuwa chombo rasmi kwa mujibu wa sheria chenye kuwakilisha na
kusimamia mambo yote ya Waislamu. Hii ni
kwa sababu (a) BAKWATA imekosa uhalali (legitimacy) kwa ummah wa Waislamu (b)
BAKWATA haiaminiki tena kwa Waislamu wa ndani na nje ya Tanzania (c) BAKWATA ni
baraza lililosajiliwa kama taasisi ya kijamii, hivyo kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ni marufuku kuwalazimisha watu kujiunga au kuwa wanachama
wa jumuiya au taasisi bila ya ridhaa (d) Serikali itajiingiza katika mgogoro wa
kikatiba na Waislamu kwa kuvunja Katiba ili kutimiza mapenzi yake kwa BAKWATA.
iii. Serikali iwache kufanya vikao na BAKWATA peke
yake kwa upande mmoja na maaskofu kwa upande mwingine katika mchakato wa
kuandaa muswada wa Mahakama ya Kadhi na itupilie mbali maafikiano yeyote
yaliyofikiwa tokana na vikao hivyo, na badala yake izingatie maoni
yaliyokwishatolewa mbele ya Kamati ya Sheria na Utawala ya Bunge.
iv. Endapo serikali itaendelea na kuwasilisha
muswada wa Mahakama ya Kadhi unaoipa mamlaka BAKWATA kuunda, kusimamia, kuteua
makadhi nakadhalika kinyume cha maoni ya Waislamu walio wengi itakuwa
imethibitika kuwa serikali haikuwa na nia ya kweli kuunda na kuanzisha Mahakama
ya Kadhi.
v. Tunataka Mahakama ya Kadhi iliyo huru,
inayoanzishwa na sheria na siyo kuanzishwa na taasisi au chombo binafsi.
Mahakama hiyo iwe chini ya tume maalum itakayowajibika kwa mujibu wa sheria
kuteua makadhi, kutengeneza kanuni za uendeshaji mashauri, kudhibiti maadili na
nidhamu ya makadhi, nakadhalika
vi. Iwe na muundo kuanzia ngazi ya tarafa, wilaya,
mkoa na taifa ambayo zaidi itashughulikia rufaa.
vii. Igharamiwe na serikali kama ambavyo serikali hivi
sasa inavyogharimia uendeshaji wa mashauri yaliyopo kwenye mahakama za kawaida
yanayohusu sheria za Kiislamu ambayo mara nyingi yanaamuliwa kwa makosa. Na pia
igharimiwe na serikali kama ambavyo serikali hii hii inavyogharamia huduma za
makanisa chini ya mkataba maarufu Memorandum of Understanding (MOU) mkataba
ambao haukuwahusisha wala kutaka ridhaa ya Waislamu (miongoni mwa wadau wakuu) ambao
umeendelea kunufaisha wakristo fedha za walipa kodi.
viii. Hoja ambayo inaweza kuzushwa kuwa Waislamu
wenyewe wanakhitilafiana kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ni sababu
tosha ya kuuodoa Muswaada huu, haina mashiko kwa sababu tulizozitaja hapo juu.
7. Iwapo
serikali haitopeleka muswada bungeni unaokidhi matakwa ya Waislamu wengi kama
ilivyopendekezwa kwenye Kamati ya Sheria na Utawala ya Bunge, Waislamu
wataendelea na msimamo wao wa kususia kushiriki kwenye mchakato wa kuipigia
kura katiba pendekezwa.
Imetolewa na Jumuiya na Taasisi
za Kiislamu Tanzania leo tarehe 23.03.2015
NAIBU KATIBU MKUU
SHEIKH RAJAB KATIMBA
Tunawashukuru sana na ahsanteni.
No comments:
Post a Comment