Friday, 20 March 2015

TAMKO LA TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA KUFUATIA TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MAHAKAMA YA KADHI





                                                                       TAREHE: 18 MACHI 2015

PRESS RELEASE

TAMKO LA TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA KUFUATIA TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MAHAKAMA YA KADHI

Ndugu Wanahabari,

Assalaam Alaykum,

1.            Madhumuni ya Tamko la Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania

Kufuatia Tamko la Maaskofu la tarehe 10 Machi 2015, liliotolewa kwa kutumia “mwamvuli” wa Jukwaa la Wakristo Tanzania (T.C.F) kuhusu Katiba inayopendekezwa, Mahakama ya Kadhi na Hali ya Usalama na Amani ya Nchi, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania ilifanya kikao chake jana Jumanne tarehe 17 Machi 2015 kwa lengo la kulitafakari tamko hilo. 

2.            Muhtasari wa Yaliyojitoleza Katika Tamko la Maaskofu

Taasisi imezipitia kwa kina nukta zote nne za Tamko hilo pamoja na hitimisho lake na kubaini yafuatayo:

(a)           Maaskofu “wamejisahau” kwamba wao ni viongozi wa kiimani na kiroho ambao wanatakiwa wawe tayari kumpokea yeyote na kumpa neno la hekima lililojazwa faraja, bila hata ya kujali itikadi au chama chake cha siasa. Badala yake wameamua kutoa faraja kwa waumini wao kwa kuzingatia utashi wa kisiasa.

(b)           Maaskofu wameamua kutumia msukumo wa kiimani pamoja na kuzitumia nyumba zao za ibada ili kuwazuilia Waislamu wasipate haki yao ya kuwa na Mahakama ya Kadhi na kutoa madai ya “Waislamu kupewa rushwa” ili kufanikisha mchakato wa Katiba inayopendekezwa.

(c)            Maaskofu wameamua kuanzisha utamaduni mpya wa kuyaendea mambo ya kisiasa kwa misingi ya kiimani na hivyo kutoa tishio la kuwagawa Watanzania kwa misingi hiyo.

3.            Nasaha za Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania

Baada ya Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania kujiridhisha na yaliyomo katika Tamko hilo la Maaskofu chini ya mwamvuli wa Jukwaa la Wakristo Tanzania (T.C.F), imeona itoe “nasaha” zifuatazo:

(a)        Kwa kuwa Serikali ina vyombo makini vyenye wataalamu wenye uwezo wa kufahamu na kuelewa uvunjifu wa Katiba na Umoja wa Kitaifa, tunaiomba Serikali ilipuuze tamko hilo la Maaskofu na iendelee na mchakato wa Mahakama ya Kadhi na Maaskofu wawe wavumilivu kwani Serikali hii ni ya Watanzania wote.

(b)        Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imesikitishwa sana na Tamko la Maaskofu lililowadhalilisha Waislamu kwa kudai kuwa wamepewa “rushwa ya Mahakama ya Kadhi”. Madai haya yanaonesha dharau, kiburi na kutowaheshimu Waislamu, jambo ambalo lina athari mbaya kwa mahusiano baina ya Waislamu na Wakristo nchini.

(c)         Suala la Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu na haliwahusu wala halihitaji ridhaa ya wasiokuwa Waislamu kama ambavyo waislamu hawajapata kuombwa ridhaa yao katika yale ambayo Serikali imekuwa ikiwafanyia wakristo na makanisa yao.

(d)       Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inapinga kwa nguvu zote madai ya Maaskofu kuwa Waislamu kuwa na mahakama ya kadhi ni uvunjifu wa Katiba, kwani Sheria za Kiislamu ni moja ya vyanzo vya Sheria ya Tanzania kama ilivyo kwa “Common Law of England” na ndio maana Mahakama za Tanzania zimekuwa zikizitumia sheria hizo kuhukumu kesi za Waislamu kuhusu Ndoa, Talaka, Mirathi na kadhalika toka mwaka 1963 ilipopitishwa Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Magistrates Courts Act) ya mwaka 1963, kufuatiwa na Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu ya mwaka 1964 (The Islamic Law(Restatement) Act of 1964) na kuhitimishwa na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971. Jambo la msingi hapa ni kuwa kesi hizo zinahukumiwa na Mahakimu wasio na elimu wala ujuzi na sifa za kuwa Makadhi kwa mujibu wa Sheria  za Kiislam na ndio msingi wa Waislamu kudai uwepo wa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara. 

(e)         Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawakumbusha Maaskofu kuzingatia kuwa madhara ya kuwagawa Watanzania kwa misingi ya kiimani, dhambi yake haitoishia kwenye kadhia ya Mahakama ya Kadhi wala Katiba Inayopendekezwa, bali itaendelea kukita mizizi yake katika kila jambo linalowahusu Watanzania.

(f)          Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawasisitizia Watanzania kwa ujumla wao kuwa wapate elimu ya Katiba Inayopendekezwa kwa kuisoma kwa makini na kuielewa vilivyo ili wawe na uwezo na uhuru wa kuchagua kile wanachikiona kina manufaa kwao bila kuwepo shinikizo la kiimani.

(g)        Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawanasihi Watanzania wote kuendelea kudumisha udugu wao kama Watanzania bila ya kujali rangi, dini, kabila na itikadi za kisiasa, na tumkemee yeyote yule anayetaka kutugawa kwa kutumia misingi ya kidini, kikabila, kisiasa, kiuchumi na kadhalika.

(h)        Kuhusu hali ya usalama wa nchi, viashiria vya ugaidi na mauaji ya Albino, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania inawakumbusha Watanzania kuwa suala la kulinda na kudumisha Amani na utulivu nchini ni wajibu wa kila mtanzania. Hivyo inawaomba Watanzania wote kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika kuzikabili changamoto hizo.

(i)          Ifahamike kwamba mauaji ya Albino, tishio la ugaidi na uhalifu mwengine, kamwe havitoweza kukomeshwa kama hatujengi utamaduni wa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Ahsanteni sana.



_________________________________
SHEIKH KHAMIS SAID MATAKA
KATIBU MKUU

No comments: