Sunday 24 May 2015

TAARIFA YA KIFO: MOHAMED OMARI MKWAWA 1922 - 2015

TARIFA YA KIFO
MOHAMED OMARI MKWAWA 1922 - 2015
Mohamed Omari Mkwawa Akiwa Amekishika Kitabu: "Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru," kitabu kilichoandikwa na
Dr. Harith Ghassany

Mzee Mohamed Omari Mkwawa au kwa jina lingine Tindo alilopewa na Karume wakati wa harakati za ukombozi Zanzibar katika miaka ya 1950 amefariki dunia usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili tarehe 5 May 2015 nyumbani kwake Mwahako Tanga. Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho Jumatatu Tanga mjini. Mzee Mkwawa alipata umaarufu mwaka 2010 baada ya kutoka kitabu cha Dr. Harith Ghassany, “Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru,” kitabu kilichokuja kueleza historia ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa usahihi kuliko vitabu vyote vilivyopata kuandikwa kabla. Ilikuwa Mzee Mkwawa ndiye aliyefichua siri kubwa iliyokuwa imefichwa kwa miaka mingi ya jeshi la askari mamluki wa Kimakonde waliochukuliwa kutoka mashamba ya mkonge ya Sakura wakapewa mafunzo katika mapori ya Kipumbwi na kuvushwa kwenda Zanzibar kusaidia mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964. Mzee Mkwawa ndiye alikuwa akilivusha jeshi hili kwa majahazi kutokea Kipumbwi kwenda Zanzibar usiku wakiwa wamevaa mavazi kama wavuvi. Mzee Mkwawa alikuwa na mchango mkubwa katika kutegua kitendawili cha mchango wa Tanganyika katika mapinduzi ya Zanzibar kiasi mwandishi Dr. Ghassany alipatapo kusema kuwa, "Ufunguo wa  kitabu changu anao Mzee Mkwawa." In Sha Allah taazia kamili ya marehemu ikieleza mchango wake katika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar itafuatilia. 



Inalilah Wainailaih Rajiuun
Nyongeza:
Mzee Mkwawa amezikwa makaburi ya Sharif Haidar Msambweni leo Jumatatu tarehe 25 May 2015 asubuhi saa nne.

Mohamed Omari Mkwawa
Mwaka 1995 wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vyingi Tanzania, nilibahatika kufuatana na mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, katika kampeni za uchaguzi katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Alipokuwa Tanga, Prof. Lipumba alifanya mkutano mkubwa sana Tangamano kiasi cha kuishtua CCM. Baada ya mkutano ule, Prof. Lipumba na ujumbe wake walialikwa nyumbani kwa mama mmoja akijulikana kama Mama Ummie (sasa ni marehemu), ambako walifanyiwa dhifa kubwa. Kote tukipita mitaa ya Tanga msafara wetu ulikuwa ukishangiliwa kwa nguvu sana. CUF ilikuwa imeingia Tanga kwa kishindo kikubwa.
Mimi kazi yangu ilikuwa kuangalia niliyokuwa nayaona na kupiga picha. Kwa hakika nilikuwa nikishuhudia historia ikijiandika. Historia ambayo ilikuwa imeshahibiana sana na ile ya wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika katika miaka 1950. Lakini ninalotaka kusema si hili, bali ni picha ambayo niliipiga ndani ya nyumba ya Mama Ummie. Picha hii ilikuwa inamuonyesha mzee mmoja wa makamo aliyevaa fulana ya CUF, mbele ikiwa na picha ya Prof. Lipumba. Mzee huyu alikuwa amekaa nyuma ya Prof. Lipumba. Kwa wakati ule picha hii haikuwa na maana yoyote kwangu, na hata nilipokuwa naitazama mara kwa mara sura yake, si iliyokuwa inanivutia bali ile fulana ya CUF aliyovaa ambayo ilikuwa na picha ya rafiki yangu, Prof. Lipumba.
Mungu ana mipango yake. Mahangaiko ya kutafuta riziki yakanihamishia Tanga na nikawa karibu sana na baadhi ya viongozi wa CUF na wanachama wake. Sasa hapa ndipo nilipokuja kuonana uso kwa uso na mzee yule kwenye picha yangu niliyoipiga hata kwa wakati ule ilikuwa miaka mingi iliyopita. Jina la mzee wangu huyu ni Mohamed Omar Mkwawa. Ilikuwa katika barza yetu ya kawaida ya kunywa kahawa na kula pweza huku tukijadili historia ya Tanzania ambako siku moja Mzee Mkwawa alinambia, “Mohamed nataka nikuambie kitu. Unajua mimi nimehusika sana katika mapinduzi ya Zanzibar?”

Kushoto: Mohamed Omari Mkwawa, Juma Duni na Prof. Ibrahim Lipumba
Nilimuangalia Mzee Mkwawa kwa makini. Fikra yangu ya utafiti na uandishi ishashtuka haipo tena usingizini. Mzee Mkwawa aliendelea, “Mimi ndiye niliyekuwa nikiwavusha Wamakonde kutoka Kipumbwi kwenda Zanzibar kuipigia kura ASP na wakati wa mapinduzi mie ndiye niliyewavusha Wamakonde kwenda kuipindua serikali ya Jamshid.” Sasa moyo wangu ukaanza kudunda kwa nguvu. Naisemesha nafsi yangu, “Huyu mzee anajua uzito wa maneno haya?” Tuishie hapa.

Dr. Harith Ghassany na Mohamed Omari Mkwawa, Tanga

Kushoto: Mohamed Omari Mkwawa, Maulidi Sheni (Mmoja wa Wanamapinduzi) na Mwandishi, Dar es Salaam (Picha Imepigwa na Dr. Harith Ghassany), Dar es Salaam 2009
Kuanzia siku ile nikawa sasa namtazama Mzee Mkwawa kwa jicho jingine na heshima yangu kwake ikawa imepanda maradufu. Nilikuwa nimeshatambua kuwa Mzee Mohamed Omari Mkwawa alikuwa mmoja wa wanahistoria waliosahaulika katika historia ya Tanganyika na Zanzibar. Juu ya hayo nilishangazwa na kitu kimoja. Iweje leo huyu mwanamapinduzi wa ASP ambae Abeid Amani Karume alimpa jina la “Tindo” kwa ujasiri wake amekuwa mstari wa mbele CUF, chama ambacho kinanasibishwa na Hizbu, hasimu mkubwa wa ASP?



Mimi na Mzee Mkwawa Tukiwa Kipumbwi

No comments: