
Zakatul-Fitri na Funga ya Siku Sita
Na Ben Rijal
Zakatul-fitri
ni Zakka ambayo inamlazimu Muislamu bada ya kufunga Ramadhan. Zakkatul-fitri
inamlazimu kila Muislamu mkubwa na mdogo, mwanamume na mwanamke alio huru na
mtumwa.
Maana
ya Zakat-Fitr ni Sadaqa ya utakaso kwa yule ambaye amefunga mwezi mtukufu wa
Ramadhani. Zakka hio hutolewa pale mwezi unapoandama mpaka pale inapomalizika
kusaliwa sala ya Eid.
Maana ya Zakka
Maana
ya Zakka kilugha ni kukuwa, kuzidi na kujitakasa kwa upande wa Kisheria Zakka
ni kutoa kiwango maalumu kwa mali iliyopitiwa na mwaka na kuwapa khasa khasa
masikini na mafakiri.
Hekima ya kutoa Zakatul-Fitri
Hekima
ya kutoa Zakatul-fitri ni kuwatakasa wale waliofunga kwa kuweza kuzisafisha
sawmu zao kutokana na makosa ya hapa na pale, aidha Zakatul-fitri ni kuwalisha
Waislamu maskini na wao wawe kwenye furaha kwa siku ya Eid.
Wamepokea
Bukhari na Muslim katika vitabu vyao vilivyo sahihi kutokana na Ibn Umar RA amesema:
“Amefaradhisha Mtume SAW Zakatul Fitri pishi ya tende au pishi
ya shairi kwa Mtumwa na muungwana mwanamume na mwanamke na mdogo na mkubwa wa
katika waislamu.” Aidha imepokewa tena na Ibn Umar amesema: “Hukmu Za Zakatul
Fitri Katika Sunna iliyotakaswa.” Aidha imepokewa na Ibn Abass RA “Mtume SAW amefaradhisha
Zakatul Fitri kwa ajili ya kumsafisha mwenye kufunga kutokana na maneno yake
machafu na ya upuuzi, na kwa ajili ya kuwalisha maskini.”
Utowaji
Alivyokuwa
akifanya Mtume SAW na Masahaba zake ni kutoa kwa njia ya chakula. Abu
Sa'id al-Khudri RA: "Katika wakati wa Mtume SAW tulikuwa
tukitoa Zakatul-fitri Sa' moja ya chakula, Sa' moja ya Shayiri, Sa'
moja ya Tende, Sa' moja ya Aqit (maziwa makavu), au Sa' moja ya Zabibu kavu.
Wakati huo chakula chetu cha kawaida kilikuwa ni Shayiri, Zabibu kavu,
Aqit na Tende.
Wanazuwoni
wanatafautiana kuna wanaosema kuwa nikutoa chakula na kuna wengine wanaoelezea
kuwa unaweza kutoa chakula au thamani ya chakula, hawa wa kauli ya pili
wanafahamisha kuwa ikiwa kila mtu atampelekea chakula na mtu huyo anahitajia
vitu vyengine kuweza kupika kile ulichompelekea ndipo walipoeleza kuwa unaweza
kutoa thamani.
Anayoongoza
familia ndio inayomlazimu kutoa, kwa kujitolea yeye na wale wote waliokuwa
chini ya mamlaka yake ambao wanamtegemea pamoja na mfanya kazi wa nyumbani,
aidha ikiwa anawangalia wazee wake na wao bado wapo hai itamlazimu aidha nao
kuwalipia.
Viwango
na namna ya kutoa
Sa’
ni sawa na pishi na pishi ipo Kilo 2.75, Pishi ni kiwango ambacho kilikuwa
kinatumika huko nyuma na kwasasa pishi sio kiwango ambacho kinatumika lakini
imefanyiwa kazi na kujulikana kiwango chake.
Imepatikana ikhtilafu baina ya wanavyuoni kuhusu neno "twa'am" (chakula) lililotajwa kwenye riwaya iliyotangulia hapo juu. Vilevile ni rahisi kutambua yakuwa neno hilo limehusu nafaka na aina nyengine ya chakula kinachoweza kupimwa kwa chombo. Jambo hilo limedhihirishwa na baadhi ya riwaya kutoka kwa maswahaba. Kwa mfano Ibn Abbas RA amesema: "Sadaka ya Ramadhan ni Sa' moja ya chakula, kwa hivyo yule atakaeleta ngano, atakubaliwa nayo, kwa yule atakaeleta shayiri, atakubaliwa nayo; kwa yule atakaeleta tende, atakubaliwa nayo; kwa yule atakaeleta nafaka (kama ngano) atakubaliwa nayo; kwa yule atakaeleta zabibu kavu, atakubaliwa nayo."
Sa’
ni kilo kuna wanayoielezea kuwa ni sawa na 2.5 Kg au 2.75 Kg na wengine nikuona
awla bora kutoa kilo 3Kg kamili.
Namna
ya kutoa
Vyema
kutumia Formula ambayo itakuelekeza namna ya kutoa.
N=namba ya
watu waliokulazimu, P=Pishi, B=Bei ya chakula hicho kinacholiwa katika mji.
Tutoe
mfano familia ya watu 5 na uchukulie pishi ni 2.5 na gharama ya chakula ni
shillingi 2,000. Kwahio ni sawasawa na Zakatul Fitri : 5 x 2.5 x
2,000=25,000
Mtu mmoja : 1 x 2.5 x 2,000=5,000.
Jadwedi iliopo hapo chini itakusaidia katika kufanya mahesabu yako
Idadi, N=Watu
|
Pishi (2.75)
|
Gharama ya Chakula
|
Jumla yote (N*P*B)
|
2
|
2.75
|
2,000
|
2 x 2.75 x 2,000=11,000
|
4
|
2.75
|
2,000
|
4 x 2.75 x 2,000=22,000
|
2
|
2.75
|
4,000
|
2 x 2.75 x 4,000=22,000
|
2
|
2.75
|
4,000
|
2 x 2.75 x 4,000=44,000
|
Sawmu ya Siku sita baada ya Ramadhani
Tumeelezwa
kuwa funga zetu kuwa zitakuwa zinaninginia baina ya mbingu na ardhi na
hazitofika kukubaliwa mpaka kwa kuzitolea Zakatul-fitri, ni vyema tukaelewa
wajibu huu kuwa tulikaa kwa mwezi mzima tukafunga kwa kuwa na matarajio ya
kupata mafanikio, itakuwaje sisi ya malipo ukaja kujikuta kuwa hukuwa na malipo
yoyote katika funga zako, ikiwa sawa na mwanafunzi aliofanya mtihani wa kuingia
darasa jengine na kujenga matumaini kafanya vizuri katika mtihani aje kujikuta
mwisho wa siku kuwa kaaunguka na kila somo ana sufuri, mwanafunzi huyo
atakuwaje?
Anasema
Sheikh Sayed Sabiq katika kitabu chake kiitwacho ‘Fiq -hi Sunnah’ kwamba
wamesimulia Maimam wote wa Hadithi isipokuwa Bukhari kuwa; Ameelezea Abu Ayoub
Al Ansari (Radhiya Llahu anhu) kwamba Mtume SAW
"Atakeyefunga Mwezi wa Ramadhani kisha akafuatilia (kufunga) siku sita
katika mwezi wa Shawaal, (anakuwa) kama aliyefunga maisha yake yote,” na
mapokezi mengine yanasema ni kama aliyefunga mwaka.
Wengine
wamepiga mahesabu kusema kuwa tumeelezwa kuwa kila jema tulifanyalo huongezwa
ujira wake kwa mara kumi, kwa hio mwezi wa Ramadhani unasiku 30 ukizidisha mara
kumi unapata 360 na siku 6 za mwezi wa mfungo mosi ukafunga siku 6 ukizizidisha
mara 10 utapata 60 kwa hio 300 ukiongeza 60 ni sawa na 360 ikiwa ni siku za
mwaka.
Hesabu:
30 x 10= 300 na 6 x 10=60 ukijumlisha 300+60=360
Waislamu
tuzingatie masomo tulioyapata katika mwezi wa Ramadhani na tuzikamilishe Sawm
zetu kwa kutoa Zakatu-fitri pamoja na kufunga siku Sita za mfungo mosi tuzidi
kupata mafanikio.
Natanguliza
kutoa mkono wa Eid kwa Waislamu wote, Eid Said, Wakulu Aum Wa Antum Bil Kheir.
No comments:
Post a Comment