Sheikh Abdallah Rashid Sembe |
KIFO cha Abdallah Rashid Sembe
kilitokea Hospitali ya Bombo, Tanga tarehe 22 Mei, 1999. Siku ya pili yake,
Jumapili asubuhi kwa wale waliokuwa wanasikiliza Radio One walisikia
katika matangazo ya vifo Mwalimu Julius
Kambarage akiarifiwa msiba ule. Kisha jina lililofuata likawa la Rais wa
Zanzibar Dk. Salmin Amour na baadae mtangazaji akasema habari za msiba
ziwafikie ndugu na jamaa wote.
Hili halikuwa tangazo la kifo la
kawaida. Si kila siku wananchi wanapata bahati kama hiyo ya kusikia Mwalimu
Nyerere akitangaziwa taarifa ya kifo kwenye radio. Ni wazi kuwa wananchi wengi
walikuwa wamepigwa na mshangao. Pana uhusiano gani kati ya Sheikh Abdallah
Rashid Sembe na Mwalimu Nyerere kiasi ya kifo cha Sheikh aarifiwe.
Wengi hawamfahamu Sheikh Abdallah
Rashid Sembe na wengi wataendelea kutomjua hadi hapo Mwalimu Nyerere,
wana-historia na CCM yenyewe itakapoamua kuandika upya historia yake na
kuwaenzi wale wote waliopigania uhuru wa nchi hii. Hata pale makaburini
Msambweni katika makaburi ya Sharif Haidar, CCM walipokuwa wakieleza habari za
mchango wa Sheikh Rashid Sembe katika kuasisi TANU na kupigania uhuru wa
Tanganyika habari zilizotolewa zilijaa makosa matupu.
Msomi maarufu na makini, Juma
Mwapachu katika taa'zia aliyomwandikia marehemu Dossa Aziz katika gazeti la the
african kwa uchungu alisema kuwa, wakati mwingine inakuwa aibu na
fedheha unapowasikia viongozi wa CCM wakijaribu kwa shida sana kueleza mchango
wasiojua wa mzalendo aliyefariki dunia. Juma Mwapachu akamaliza kwa kumwuliza
Mwalimu Nyerere kuwa hadi lini atanyamaza kimya bila ya kuwataja wenzake
aliokuwa nao katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Hali kadhalika akawauliza
wasomi wazalendo kwanini hadi leo hakuna juhudi ya kutafiti na kuandika
historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika.
Hadi hapo Mwalimu Nyerere
atakapofungua kinywa chake kuwaeleza wananchi habari za mashujaa wenzake
aliokuwa nao katika harakati za kudai uhuru, wananchi na hasa kizazi cha hivi
karibuni kitakuwa kinamtukuza yeye pekee kama shujaa wa uhuru wa Tanganyika. Na
wenzake wengi waliomsaidia watabaki hawafahamiki na mwishowe historia nzima ya
uhuru wa Tanganyika itatoweka.
Mchango wa Abdallah Rashid Sembe
katika kuasisiwa kwa TANU, Tanga 1955
Mwaka 1955 Sheikh Abdallah Rashid
Sembe alikuwa na miaka arobaini na mbili akijishughulisha na biashara ya kuuza
nazi katika soko la Ngamiani mjini Tanga.
Hali ya siasa katika jimbo la Tanga
ilikuwa ni ya kipekee kabisa ukilinganishwa na jinsi hali ilivyokuwa sehemu
nyingine za Tanganyika. Ilikuwa ni Tanga tu katika historia ya Tanganyika kuwa
dhana mpya ya siasa zaidi ya ule ubwana wa Waingereza, uliongezeka katika
uhusiano baina ya Waafrika na watu wa rangi nyingine.
Katika jimbo la Tanga kwa bahati
mbaya sana Uarabu ulichukua nafasi ya tabaka la utawala juu ya Waafrika. Dhana
hii ilitiwa nguvu na wakoloni ili kuwagawa wananchi na kuwakandamiza Waafrika.
Hiki kilikuwa kitu ambacho Waafrika walikuwa hawajapambanacho. Kwa zaidi ya
karne moja walikuwa wamezoea ubwana wa Waingereza. Uongozi wa siasa kupitia
African Association ulikuwa chini ya watu waliojinasibu kuwa asili yao ni
Uarabu zaidi kuliko Uafrika ingawa wengi wao walikuwa na damu ya Kiafrika.
Katika hali kama hii African Association Tanga haikuwa na nguvu ya
kuwaunganisha wananchi kupambana na ukoloni kama ilivyokuwa sehemu nyingine.
Mara chache sana watu waliihusisha ofisi ya TAA Tanga na siasa. Ofisi ya TAA
inakumbukwa na kuhusishwa na mahakama ya kadhi ambako Kadhi, Sheikh Ali bin
Hemed alihukumu jamii ya Waislamu kwa kutumia sharia.
Mwaka wa 1875 UMCA ilikuwa imehama
kutoka Mkunazini Zanzibar kwenda Magila katika Jimbo la Tanga. Ukristo
ulianzishwa na kustawi katika nchi ya Wabondei, na vivyo hivyo nafasi za elimu
kwa watoto wa Wabondei ambao wengi walibatizwa katika lile wimbi la kuwania
nafasi za elimu. Jimbo la Tanga likabarikiwa na kuwa na Waafrika walioelimika
sana. Vijana wengi kutoka Ubondei waliingia Makerere College na siasa za
kizalendo zilizoanza baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Wabondei walikuwa
wamejaa katika utumishi wa serikali ya kikoloni.
Katika hali kama hii ingelitegemewa
kuwa hawa wasomi wa Makerere ambao wengi walikuwepo pale Tanga mjini wakifanya
kazi wangetoa uongozi katika African Association na kuanzisha harakati za kudai
uhuru wa Tanganyika.
Hawa Waafrika wasomi kutoka shule za
misheni na Makerere badala ya kuwa wapigania haki wakawa watiifu kwa taasisi
mbili zenye nguvu, serikali ya kikoloni na Kanisa. Wasomi hawa waliunda vikundi
vyao kwa kushawishiwa na Waingereza vilivyokuwa vikijulikana kama Discussion
Groups yaani vikundi vya majadiliano. Vikundi hivi vilijitenga na
siasa. Kwa ajili hii basi, ilibakia kwa Waislamu "wasiokuwa na elimu"
kuunda TANU na kuongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Hapa ndipo
unakutana na Shekh Abdallah Rashid Sembe.
Kikundi cha wafanyabiashara wadogo
wadogo katika soko la Ngamiani, Abdallah Rashid Sembe akiwamo kiliitisha
mkutano katika ukumbi wa Tangamano Septemba 5, 1955. Waliohudhuria mkutano huo
walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Hamis Heri, Peter Mhando, Mohamed Kajembe, Tuwa
Abdallah, Dhili Mgunya, Victor Mkello, Mohamed Sadik, Hassan, Peter Ramadhani
Jembe na Ali Mohamed. Peter Ramadhani tayari alikuwa mwanachama wa TANU huko
Arusha na alikaribishwa mkutanoni ili waasisi wa TANU wanufaike kutokana na
uzoefu wake.
Wasomi wa Makerere, uongozi wa TAA
na Mwalimu Kihere mmoja wa wanasiasa wa wakati ule hawakuwepo kwenye mkutano
huu muhimu. Mkutano ulifunguliwa na Hamis Heri na ulifungwa kwa uamuzi kuwa
mkutano mwingine wa kuchagua viongozi wa chama ufanyike tarehe 23 Oktoba.
Mkutano uliamua vile vile kuwa juhudi zifanyike kupata wanachama wengi
iwezekanavyo. Kiasi kidogo cha fedha kilikusaywa na Harir Omari Siagi alipewa
aende makao makuu ya TANU, Dar es Salam kununua kadi sabini za TANU. Abdallah
Rashid Sembe alikuwa mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU.
Tarehe 23 Oktoba, wanachama wa
mwanzo wa TANU huko Tanga walikutana kuchagua viongozi wao wa kwanza. Hamisi
Heri alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Peter Mhando Katibu. Jumla ya watu
arobaini na tano walihudhuria mkutano huo na wakapewa kadi za TANU. Mwalimu
Kihere alihudhuria mkutano lakini hakuchaguliwa katika nafasi yoyote ya
uongozi. Kamati ya wanachama iliundwa kutokana na wale wanachama kumi na moja
waasisi waliokutana katika ule mkutano wa kwanza mwezi uliopita.
Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe
wafuatao: Abdallah Rashid Sembe, Mohamed Kajembe, Victor Mkello, Dhili Mgunya,
Ali Mohamed, Abdallah Mohamed na Mohamed Sadik. Peter Mhando alijitolea nyumba
yake kuwa ofisi ya kwanza ya tawi la TANU mjini Tanga. Mara tu baada ya mkutano
huu wazee wa Tanga wakiongozwa na Makoko Rashid, mwanachama wa zamani wa TAA
walianza kufanya kampeni kwa ajili ya TANU. Chama kilipata msukumo mwingine na
kuongezeka nguvu wakati Sadik Ali Patwa Muasia tajiri alipoingia TANU.
Baada ya kufungua tawi la TANU mjini
Tanga, uongozi wa chama ulimwalika Julius Mwalimu Nyerere, Bibi Titi Mohamed,
John Rupia na Mbutta Milando. Mwalimu Nyerere alifikia nyumbani kwa Hamis Heri.
Huu ndiyo ukawa mwanzo wa urafiki kati ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Abdallah
Rashid Sembe. Wazee wa Tanga wanakumbuka kuwa wakati wa harakati Mwalimu
Nyerere alipata kufanya mikutano mingi ya siri nyumba ya pili kutoka nyumba ya
Sheikh Sembe barabara ya kumi na nne Sheikh Sembe akiwa mwenyeji wake. Nyumba
hii sasa hivi inamilikiwa na ukoo wa Salim Mbaruku, moja ya koo maarufu mjini
Tanga. Baada ya kushindwa kupata nafasi yoyote katika chama, Mwalimu Kihere alipoteza
shauku ya siasa. Mwalimu Nyerere alipokuja Tanga kuifanyia kampeni TANU ndipo
Mwalimu Kihere alikaribishwa na Mwalimu Nyerere kujiunga na chama. Matokeo ya
ziara ya Mwalimu Nyerere Tanga ilikuwa ni kumrudisha tena Mwalimu Kihere katika
siasa.
Mabingwa wa kuhamasisha wa TANU enzi
zile, Julius Mwalimu Nyerere, Bibi Titi Mohamed walihutubia mkutano wa hadhara
kwenye uwanja maarufu wa Tangamano. Hii ilikuwa hatua kubwa sana kwa TANU, na
kwa harakati dhidi ya ukoloni katika jimbo la Tanga. Haya yalikuwa mapinduzi
makubwa kutoka enzi za zile siasa za wasomi katika Discussion Group ambazo
kama akina Sembe na wenzake wangeziendekeza uhuru ungelichelewa sana. Baada ya
hapo, Mwalimu Kihere alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tanga badala ya Hamis
Heri, na Amos Kissenge alichaguliwa Katibu. Abdallah Rashid Sembe mmoja wa
wanachama wasisi wa mwanzo kabisa wa TANU alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati
Kuu ya Taifa ya TANU akiwakilisha Jimbo la Tanga. Sheikh Abdallah Rashid Sembe
alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 1969 akiwa mmoja wa viongozi waliopitisha
Azimio la Arusha mwaka wa 1967.
No comments:
Post a Comment