Utangulizi
MWAKA 1958 serikali ya kikoloni
baada ya kushindwa ilikubali ufanyike uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria
ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya rangi. Kulikuwa na viti kwa
ajili ya Wazungu, Wahindi na Waafrika. Masharti mengine ya kumwezesha Mwafrika
kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi mia nne za Kiingereza kwa mwaka,
awe na kiwango cha elimu ya darasa la kumi na mbili na awe ameajiriwa katika
kazi maalum. Haya yalikuwa masharti magumu na yaliyoonekana kama hayataweza
kukubalika na TANU. TANU ilifanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa 1958 mjini
Tabora kuanzia tarehe 21-26 Januari, 1958 kujadili miongoni mwa mambo mengine ikiwa
ishiriki katika uchaguzi chini ya haya masharti ya kibaguzi yaliyowekwa au
isusie uchaguzi.
Mkutano huu wa Tabora ulitishia
kuigawa TANU katika kambi mbili hasimu. Kambi moja ni ile ya wenye siasa za
wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ile ya pili ni ile ya wenye
msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa. TANU ilinusurika na kile
ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye
msimamo mkali kama Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa
TANU katika makao makuu, Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa TANU,
kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama mapande mawili kama isingelikuwa
busara ya Mwalimu Nyerere, Abdallah Rashidi Sembe, Hamisi Heri na viongozi wa
TANU wa Tanga ambao walipanga mkakati wa kuwashinda 'siasa kali' katika chama.
Lakini ili kuzielewa hisia za
wanachama wa TANU, uongozi wake na nguvu zilizokuwa zikidhibiti siasa
Tanganyika wakati ule wa ukoloni, na ili kuelewa kwa nini Kura Tatu ilizua
mgogoro na kutoelewana katika uongozi, inatubidi turudi nyuma. Tunahitaji
kuyatazama mambo kwanza kuanzia Tanga mahali ambapo Mwalimu Nyerere na uongozi
wa TANU Tanga walikutana kwa siri kuweka mikakati ya mkutano wa Tabora. Baada
ya kufanya hivyo tufichue jambo moja baada ya jingine katika mkakati wa Sheikh
Abdallah Rashid Sembe, Mwalimu Kihere na Mwalimu Nyerere uliofanya wafuasi wa
siasa za wastani wawashinde wale waliokuwa na msimamo mkali. Inasikitisha kuwa
kisa hiki cha ujasiri na mbinu za hali ya juu kama zilivyoonyeshwa na watu wa
Tanga hadi leo kimebaki siri kuu. Wanaokifahamu kisa hiki wengi wao
wameshakufa.
Baraza la Wazee wa TANU |
TANU kwa hakika kilikuwa chama cha
Waislamu; kwa hiyo ilikuwa ni dhahiri kuwa kuyakubali masharti yale ya kibaguzi
ya upigaji kura ilikuwa sawa sawa na kuwasukuma Waislamu ambao ndiyo walikuwa
wafuasi wakubwa wa TANU nje ya wigo wa siasa. Ujumbe wa Mwalimu Nyerere
mwenyewe kutoka makao makuu ulikuwa na wajumbe wengi ambao wasingeweza hata
kidogo kusimama kama wagombea katika uchaguzi chini ya masharti yale. Makao Makuu ya TANU yalikuwa yanawakilishwa kwenye mkutano mkuu na Mwalimu Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Elias Kissenge, Dossa
Azizi, Julius Mwasanyangi, Michael Lugazia, Ramadhani Chaurembo, Hussein
Mbaruk, Clement Mtamila, Idd Tulio, Mzee Salum, Idd Faiz Mafongo, Idd Tosiri,
Haidari Mwinyimvua na Rajabu Diwani.
Hii ilikuwa na maana uongozi wa Waislamu kule Dar e Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine nchini Tanganyika usingeweza kusimama kama wagombea uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Baraza la Wazee wa TANU likiwa na wajumbe takriban mia mbili na sabini Waislamu watupu, walikuwa hawawezi kupiga wala kupigiwa kura. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi.
Hii ilikuwa na maana uongozi wa Waislamu kule Dar e Salaam, Tanga, Tabora, Dodoma na mahala pengine nchini Tanganyika usingeweza kusimama kama wagombea uchaguzi ili wachaguliwe kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria wala wasingeweza kuwapigia kura wagombea wanaowataka. Baraza la Wazee wa TANU likiwa na wajumbe takriban mia mbili na sabini Waislamu watupu, walikuwa hawawezi kupiga wala kupigiwa kura. Kwa hiyo ilikuwa ni jambo la wazi kabisa kuwa TANU ingesusia uchaguzi.
Serikali ya kikoloni, ikishirikiana
na wamishionari, walikuwa wamewanyima Waislamu elimu, sharti lile lile ambalo
sasa linawekwa kuwazuia Waislamu kushiriki katika siasa. Hakuna kumbukumbu
zozote zinazoeleza mawazo ya Mwalimu Nyerere katika suala la Kura Tatu wala
hakuna nyaraka inayoweza kueleza kuwa alipata hata kuzungumza suala hili kwa
faragha pale Makao Makuu na washirika wake wa karibu kama Sheikh Suleiman
Takadir, Zuberi Mtemvu, Rajab Diwani, Idd Faiz, Haidar Mwinyimvua, Dossa Azizi
au Bibi Titi Mohamed. Kwa ajili hii ni vigumu kuweza kujua ni kwa kiasi gani
Mwalimu Nyerere alikuwa amejizatiti katika msimamo wa TANU kuingia katika Kura
Tatu katika masharti yale. Lakini ikiwa utafanya tathmini kutokana na hali ya
hewa ya siasa kama ilivyokuwa katika miezi ya mwisho ya mwaka 1958, si vigumu
kuona kwa nini Mwalimu Nyerere ilibidi afiche msimamo wake katika suala la Kura
Tatu kama TANU ilivyotwishwa na serikali. Mwalimu Nyerere alikuwa anafahamu
hatari iliyokuwa ikinyemelea TANU kutokana na Kura Tatu. Alijua wazi ili
kukinusuru chama na mgawanyiko kulikuwa na haja kubwa ya yeye kufanya uamuzi
haraka na kwa makini kabla ya kwenda kwenye mkutano Tabora.
Siku chache kabla ya kusafiri kwenda Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa TANU, Mwalimu Nyerere na Amos Kisenge, Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda Tanga kushauriana na uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga, kuhusu matatizo yaliyoletwa na uchaguzi wa Kura Tatu. Mkutano huu baina ya Mwalimu Nyerere, Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa siri sana. Tanga iliwakilishwa na Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Ng'anzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makatta. Mwalimu Nyerere alizungumza waziwazi na kwa dhati ya moyo alikiambia kikao kile kuwa amekwenda Tanga kuomba wamuunge mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU lazima ishiriki katika ule uchaguzi wa Kura Tatu uliokuwa unakaribia hata masharti yakiwaje. Mwalimu Nyerere aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa makini kuwa alikuwa amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa ufasaha wa lugha na kwa uwezo wa kuzungumza vizuri. Mwalimu Nyerere alisema angehitaji hiki kipaji adimu cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko Tabora. Mwalimu Nyerere alitoa hoja kwamba TANU lazima ishiriki katika uchaguzi kwa sababu kuususia ni sawasawa na kukipa chama hasimu UTP ushindi bila jasho kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa sauti katika maamuzi yatakayotolewa na seriakli katika siku zijazo.
Kufichuka kwa msimamo wa Mwalimu
Nyerere wa kutaka TANU iingie katika Kura Tatu kulishtua uongozi wa Tanga.
Majadiliano makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha upinzani wao kwa
msimamo wa Mwalimu Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu Mwalimu Nyerere
alifanikiwa kuwashawishi wote wawili Hamisi Heri na Mwalimu Kihere ambao ndiyo
walikuwa wapinzani wakubwa wa msimamo wa Mwalimu Nyerere na uchaguzi wa Kura
Tatu. Mwalimu Nyerere aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya Kura
Tatu itakapokuja anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko
Tanga kwenyewe, TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP iliyokuwa
na nguvu Tanga kwa sababu ya walowezi waliokuwa wakimiliki mashamba ya mkonge
katika jimbo hilo. Kwa ajili hii akina Rashid Sembe walikuwa wameelemewa na
mashambulizi kutoka kwa wapinzani.
Maili tatu kutoka Tanga kipo kijiji
cha Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU lillilokuwa na nguvu sana
likiongozwa na Mmaka Omar kama mwenyekiti na Akida Boramimi bin Dai akiwa
katibu. Hawa wote ni marehemu na mchango wao hadi leo haujathaminiwa. Mwalimu
Nyerere na Kissenge walichukuliwa hadi Mnyanjani ili ifanyike tawaswil. Waliohudhuria
kisomo hicho walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Sheikh Dhikr bin Said, Mzee Zonga,
Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa mshairi maarufu, Akida Boramimimi bin
Dai na Mmaka Omari. Aliyechaguliwa kusoma Qur'an Tukufu alikuwa mjomba wa
Mwalimu Kihere, Sheikh Ali Kombora.
Mara baada ya dua ile Mwalimu
Nyerere aliondoka kwenda Tabora akiongoza ujumbe mkubwa sana kutoka makao
makuu. Ile agenda ya uchaguzi wa Kura Tatu ilipoanza kujadiliwa, mkakati wa
Tanga uliofanyiwa dua maalum kwa Mwenyezi Mungu katika kijiji cha Mnyanjani
ukaanza kutekelezwa. Mwalimu Nyerere aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano aliomba
amwachie kiti Mwalimu Kihere ili apate fursa ya kushiriki katika mjadala na
kutoa mchango wake. Mara tu baada ya Mwalimu Kihere kuchukua kiti aliutuliza
mkutano na akamchagua Sheikh Abdallah Rashid Sembe kuwa msemaji wa kwanza kama
vile walivyopanga kule Tanga majuma machache yaliyopita. Sembe alihimiza TANU
kushiriki katika uchaguzi. Kama vile Baba wa Taifa alivyotabiri mapema, zogo
kubwa lilizuka. Wajumbe walipiga makelele, wakagonga meza kwa hasira, wengine
wakawa wanaburuza meza na viti kwa makelele kudhihirisha hamaki zao. Jumanne
Abdallah, Bhoke Munanka kutoka Jimbo la Ziwa walisimama na kumlaani Abdallah
Rashid Sembe wakimwita msaliti. Sheikh Sembe alishikilia msimamo wake kuwa TANU
ni lazima iingie uchaguzi unaokuja ili ishinde uchaguzi na katika ushindi huo
iwe na uwezo wa kufutilia mbali mfumo huo wa dhulma. Mwalimu Nyerere alisimama
na akamuunga mkono Sheikh Sembe. Mwalimu Nyerere alitoa hoja katika misingi hiyo hiyo
kuwa ili TANU iweze kuondoa Kura Tatu ni lazima kwanza iingie kwenye Kura Tatu.
Wajumbe hawakuafiki hoja ya Mwalimu Nyerere. Wote walishikilia msimamo wa TANU
kususia uchaguzi. Hamaki za watu zilikuwa wazi ndani ya ukumbi wa mkutano wa
Mwalimu Kihere aliahirisha kikao hadi siku ya pili ili kuwapa wajumbe muda wa
kutuliza hamaki zao.
Siku iliyofuata ustadi wa Mwalimu
Nyerere katika mjadala ulitumika. Mwalimu Nyerere akizungumza kwa vitendawili
na methali, aliwauliza wasikilizaji wake, je, ingewezekana kwa mkulima mwenye
busara, aliyelima na kupanda shamba lake kwa taabu, angesita kuvuna mazao yake
kwa kuhofia kuchafua nguo zake, kwa sababu tu, ili afike shambani kwake itabidi
avuke mto wenye matope. Watu wangelimuonaje mkulima kama huyo? Mwalimu Nyerere
aliwaeleza wale wajumbe kuwa, TANU iko njia panda, ingekuwa kazi bure kwa
wakati huu kwa TANU kususia uchaguzi baada ya kufanya kazi yote ile kwa shida
kubwa hadi kufika hapo walipofika. Kususia uchaguzi ingekuwa ni kujiingiza
katika mtego. Adui angefurahi kuona imenasa katika mtego, TANU ikisimama
pembeni na UTP ikiingia katika uchaguzi na kuchukua viti vyote katika Baraza la
Kutunga Sheria. Serikali ya kikoloni ingefurahi sana kuona kitu hiki kinatokea.
Mwalimu Nyerere na Sheikh Abdallah
Rashid Sembe ambaye alihatarisha uhai wa yeye kuwapo katika TANU katika suala
la uchaguzi wa Kura Tatu walikuwa washindi. Hata hivyo agenda ya Kura Tatu
ilibidi ipigiwe kura. Kura ilipopigwa kundi la akina Sheikh Suleiman Takadiri
waliotaka kuususia uchaguzi walishindwa: kura 37 zilipigwa
kuunga mkono kushiriki uchaguzi wa Kura Tatu dhidi ya 23 zilizotaka ususiaji. Mwalimu Nyerere alitia sahihi Azimio la Tabora ambalo
baadae lilikuja kujulikana kama 'Uamuzi wa Busara.'
Siku ile Mwalimu Nyerere alipokuwa akiweka sahihi yake watu hawa wafuatao ndiyo walikuwa wamemzunguka: kwa upande wa kulia wa Mwalimu Nyerere alikuwa amesimama makamu wa rais wa TANU, John Rupia; upande wake wa kushoto alikuwepo Amos Kissenge, aliyekuwa kakaa nyuma ya Mwalimu Nyerere akiwa amevaa kofia ya mkono, koti na kanzu alikuwa Mzee Jumbe Tambaza mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU, upande wake wa kulia alikuwa kijana Juma Selemani maarufu kwa jina la lake la utani, 'Juma Mlevi', katibu wa Bantu Group. Mwisho wa meza wakitazamana alikuwa Bibi Titi Mohamed kwa upande wa kulia wa Mwalimu Nyerere na Sheikh Suleiman Takadir kwa upande wake wa kushoto.
Siku ile Mwalimu Nyerere alipokuwa akiweka sahihi yake watu hawa wafuatao ndiyo walikuwa wamemzunguka: kwa upande wa kulia wa Mwalimu Nyerere alikuwa amesimama makamu wa rais wa TANU, John Rupia; upande wake wa kushoto alikuwepo Amos Kissenge, aliyekuwa kakaa nyuma ya Mwalimu Nyerere akiwa amevaa kofia ya mkono, koti na kanzu alikuwa Mzee Jumbe Tambaza mjumbe wa Baraza la Wazee wa TANU, upande wake wa kulia alikuwa kijana Juma Selemani maarufu kwa jina la lake la utani, 'Juma Mlevi', katibu wa Bantu Group. Mwisho wa meza wakitazamana alikuwa Bibi Titi Mohamed kwa upande wa kulia wa Mwalimu Nyerere na Sheikh Suleiman Takadir kwa upande wake wa kushoto.
Mohamed Jumbe Tambaza |
Baada ya kutia saini kwa Azimio la
Tabora Mwalimu Nyerere alimpigia simu Zuberi Mtemvu makao makuu Dar es Salaam
kumuagiza awatangazie wananchi kuwa TANU imepiga kura kuingia katika uchaguzi
wa Kura Tatu. Siku iliyofuata wakati mkutano bado ukiendelea Mtemvu alituma
simu ya maandishi kwa rais wa TANU, Mwalimu Nyerere kupitia ofisi ya TANU
Tabora, akitangaza kujiuzulu kwake kutoka TANU na kuanzishwa kwa chama chake
cha upinzani - African National Congress (ANC) Chama cha Mtemvu kilikuja
kujulikana kama 'Congress' neno ambalo kwa mtazamo wa vyama hivyo pinzani
lilikuja kunasibishwa na usaliti. Mtemvu akimshutumu Mwalimu Nyerere kwa
kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na TANU na wananchi kwa kuwatumbukiza katika
Kura Tatu; na Mwalimu Nyerere akimshutumu Mtemvu kwa kujitenga na mapambano na
kujiunga na upinzani ili kudhoofisha TANU, na hivyo kusaliti harakati za kudai
uhuru. Hadi leo Mzee Mtemvu na wazee wengi wa TANU hawafahamu kuwa mkakati wa
Tabora ulipikwa Mnyanjani.
Kabla ya kuondoka Tabora Mwalimu
Nyerere lifanya mkutano wa hadhara soko kuu la Tabora na kuelezea maamuzi ya
mkutano mkuu. Hotuba ya Mwalimu Nyerere ilijaa hisia kali. Aliwaambia
wasikilizaji wake kuwa endapo Waingereza watakaidi kutoa uhuru basi wananchi
wataelekeza kilio chao kwa Mwenyezi Mungu. Wakati ule TANU ilikuwa na dini
hakukuwa na lugha ya sasa ya 'chama chetu hakina dini'. Mwalimu Nyerere
alipotamka maneno haya hakuweza kujizuia, akaangua kilio na vilio vya wananchi
waliouelewa uchungu wa dhulma vikatanda uwanja mzima. Baada ya hotuba hii
iliyowaliza watu, wananchi wengi ambao walisita kujiunga na TANU sasa waliingia
kwa wingi. Ni vigumu kuamini lakini watu huko Tabora walisimama msururu
usikukucha kukata kadi za TANU.
Huyu ndiye Sheikh Abdallah Rashid
Sembe, muasisi wa TANU ambae amekufa akiwa mwanachama mtiifu wa CCM na kwa
viongozi wake. Mkutano wake wa mwisho aliohudhuria wa CCM ulikuwa Mkutano Mkuu
uliofanyika Dodoma Novemba, 1997 ambao alihudhuria kama mwalikwa. Kwa bahati
mbaya sana mkutano huu ulimalizika kwa fedheha kwa upande wa Sheikh Rashid
Sembe. Bila ya kujali umri wa Sheikh Sembe na nafasi yake ya usheikh, msichana
mcheza ngoma akiwa nusu uchi alikwenda kucheza ngoma mbele yake na huku
akinengua alimkalia Sheikh Sembe mapajani. Gazeti moja la kila siku bila ya
tafakuri ikachapisha picha ile ya Sheikh Sembe akiwa katika mavazi yake ya
Kiislamu ya kanzu, koti, kofia na kilemba katika ukurasa wake wa mbele.
Waislamu wengi walikasirishwa na kuhuzunishwa na picha ile. Wapo waliomlaumu
Sheikh Sembe kwa kuhudhuria mikutano ya kitwaghut na wapo
walioilaumu CCM kwa kuachia Sheikh Abdallah Rashid Sembe avunjiwe heshima na
halikadhalika wapo waliolilaumu gazeti.
Wengi wa wanasiasa wa sasa katika
ukumbi ule wa mkutano walikuwa wakimpita Sheikh Sembe bila ya kujua kwa hakika
yule mzee aliyevaa Kiislamu katika ukumbi ule alikuwa nani na nini ulikuwa
mchango wake katika siasa za Tanganyika. Hata hivyo historia ya uhuru wa
Tanganyika na hata maisha ya Mwalimu Nyerere yatakapoandikwa hayatakamilika
bila ya kumtaja Sheikh Abdallah Rashid Sembe.
Picha ya wana TANU Waafrika, Waasia na Wazungu kabla ya uhuru wagombea wa Kura Tatu 1958 |
No comments:
Post a Comment