Thursday, 22 October 2015

KUMBUKUMBU ZA IDDI TOSIRI MWANACHAMA WA TANU KADI NO. 24

Mwaka wa 1954 wakati TANU inaasisiwa Iddi Tosiri na ndugu yake Iddi Faiz Mafongo walikuwa na umri wa miaka 40 na zaidi kidogo na tayari walikuwa katika siasa za TAA na Al Jamiatul Islamiyya. Ndugu hawa wawili ni kati ya wanachama wa mwanzo kabisa kujiunga na TANU. Iddi Tosiri kadi yake ya TANU ni no. 24 na Iddi Faizi kadi yake ni no. 25. Iddi Tosiri alikuwa akiishi Mtaa wa Livingstone na Amani mwendo wa kama dakika 10 hivi kufika ofisi ya TANU New Street. Ndugu hawa wawili walikuwa na kaka yao mkubwa Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo, Khalifa wa Tariqa Qadiriyya. Katika kuipa nguvu TANU na kumtambulisha Nyerere kwa watu maarufu, Iddi Tosiri na Iddi Faizi walimchukua Julius Nyerere hadi Bagamoyo kwenda kumtambulisha kwa kaka yao Sheikh Mohamed Ramia. Sheikh Mohamed Ramia alikujakuwa rafiki mkubwa sana wa Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika. Nimebahatika kuonyeshwa na mtoto wa Iddi Tosiri, Maulid ‘’Chubby’’ Tosiri picha alizoacha marehemu baba yake Mzee Tosiri zikumuonyesha yeye mwenyewe na Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika. Nami kwa hisani ya familia hii naziweka hapa kama kumbukumbu ya mashujaa wa uhuru wa Tanganyika picha hizi tatu zilizofuatana.

Idd Tosiri na mgeni wake kutoka Congo
Wakwanza kushoto mbele ni Iddi Tosiri, watatu ni Julius Nyerere akifuatiwa na Kaluta Amri Abeid,
Mstari wa mwisho wapili kulia ni Rashid Sisso. Picha hii ilipigwa miaka ya mwishoni 1950 New Street
mbele ya ofisi ya TAPA (Tanganyika African Parents Association)

Kushoto: Idd Faiz mafungo, Sheikh Mohamed Ramia, Julius Nyerere
Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu Dodoma 1956


No comments: