Abdilatif Abdalla... nikimuona
Abdilatif Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam
katika miaka ya 1980 lakini kwa mbali. Hatukuwa na mazoea yoyote baina yetu.
Wakati ule alikuwa Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Baadae
nikajakutana na Abdilatif BBC Bush House London BBC Club ambako nikenda pale
nikifuatana na Ahmed Rajab. Hii ilikuwa miaka ya mwanzoni 1990. Wakati ule mimi
nilikuwa mmoja wa waandishi wa jarida lililokuwa likiitwa Africa Events likichapwa
London na kuhaririwa na Mohamed Mlamali
Adam. Pamoja na Ahmed RajabA bdilatif alikuwa mmoja wa waandishi wa Africa Events
na pia mtangazaji BBC Idhaa ya Kiswahili vilevile pamoja na Ahmed Rajab. Abdilatif kipindi kile
tayari alikuwa keshajenga jina kama mwandishi na mshairi wa kutajika baada ya
kufungwa na serikali ya Kenyatta katika miaka ya 1970 na kuchapisha kitabu
kilichokuja kuwa maarufu sana, ‘’Sauti ya Dhiki.’’
|
Abdilatif Abdalla |
|
Gazeti la Africa Events |
Pale London sasa
ikatokea kuwa nimepata nyumba mbili za kutembelea kila nikiwa mjini hapo
nikitokea Cardiff nililokuwa mwanafunzi – Bush House Idhaa ya Kiswahili na
ofisi ya Africa Events. Nami ni mpiga porojo kwa hiyo jamaa wakiniona pale huwa
wana hamu ya kupata ‘’mpya,’’ kutoka Tanzania na hii ikimuhusisha hadi
aliyekuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Mzee Neville Hermes. Huyu bwana alikuwa
hajui neno moja la Kiswahili lakini ndiyo akiongoza idhaa ile. Nishaingia
ofisini kwake kupiga soga na akanipa ofa ya kazi ya utangazaji lakini hiki ni
kisa kingine. Nawakumbuka jamaa
waliokuwa pale siku zile ukiwatoa Abdilatif Abdalla na Ahmed Rajab – Suluma Kassim,
Eric Munene, Mohamed Abdillah, Aisha Yahya, Ali Attas, Ali Saleh, Tido Mhando, Othman Matata, Ali
Mutasa na wengineo. Africa Events ukiwatoa tena Abdilatif na Ahmed kulikuwa na Mohamed
Mlamali Adam na Ahmed Saleh Yahya. Hawa wote Wazanzibari na mabingwa wa lugha
ya Kiingereza. Usomapo makala zao hujui kipi kilichokupendeza zaidi ni maneno
katika makala au wanavyocheza na lugha.
|
Kushoto: Ali Saleh, Mwandishi, Chama Omari Matata na aliyesimama ni Balozi Mohamed Maharage Juma BBC Club 1991 |
|
Tido Mhando Nje ya Bush House |
|
Ahmed Rajab |
|
Mwandishi akiwa studio za BBC Glasgow, Scotland akifanya kipindi ''Barua Kutoka Glasgow'' |
Siku moja siku ya Eid
Abdilatif akanialika kwake. Hapa ndipo nilipokuwa napataka. Sijui kwa nini
lakini siku zote nikamfananisha Abdilatif na Malcolm X mmoja wa mashujaa zangu
enzi za utoto wangu nikikua katika mitaa ya Kariakoo Dar es Salaam. Kuna mwandishi
mmoja alipata kuandika na kusema kuwa yeye kila akimuona Abdilatif
anamfananisha na mcezaji mpira wa kikapu kutoka Marekani. Kilichonistaajabisha nyumbani kwa Abdilatif
pale London ni wingi wa vitabu. Sijapatapo kuona vitabu vingi kiasi kile ila
katika Maktaba ya Taifa, Mtaa wa Titi Dar es Salaam au Maktaba ya Chuo Kikuu
Cha Dar es Salaam. Huu ulikuwa mshtuko wa kwanza. Mshtuko wa pili. Katika
maktaba ile ya Abdilatif nikakuta cassette nyingi sana za muziki wa jazz (miaka
ile CD zilikuwa bado) nami ni shabiki wa muziki huo pia. Sasa ikawa mimi na
Abdilatif tumeunganishwa vizuri sana, uandishi, kupenda vitabu na muziki wa jazz.
Katika mazungumzo yetu ya muziki wa jazz Abdilatif akanambia kuwa yeye
anamuusudu sana Miles Davis.Miaka ikenda na kurudi nikawa nimepoteana na
Abdilatif kiasi cha miongo miwili.
|
Kushoto: Ridder Samsom wa Chuo Kikuu Cha Humburg, Kai Kresse wa Zentrum Moderner Orient (ZMO) Berlin |
Sasa niko Ujerumani
Berlin katika taasisi moja ya utafiti inaitwa Zentrum Moderner Orient (ZMO)
niko mbele ya hadhira najitayarisha kutoa mada lakini tunasuburi muda wa
kuanza. Hii ni miaka ya 2000 mwanzoni. Nimeinama lakini nahisi kuna mtu
kanifata mbele yangu kaniinamia. Nanyanyua kichwa… Abdilatif huyu hapa. Katokea
Humburg kaja nisikiliza ndugu yake nikibwabwanya ughaibuni. Wakati ule Abdilatif alikuwa akifundisha Chuo Kikuu Cha Leipzig. Dunia hii ni ndogo.
Mwaliko niliopata kutoka ZMO aliyenialika alikuwa Kai Kresse ambae ni mmoja wa
wahariri wa kitabu hiki, ‘’Abdilatif Abdalla Poet in Politics.’’ Ilikuwaje nikaalikwa ZMO hiki ni kisa kingine
lakini napenda nikiseme lau kwa muhtasari. Nilishiriki katika kipindi cha Meza
ya Duara kilichoendeshwa na Sauti ya Ujerumani, Bonn mwenyekiti wake akiwa
Othman Miraj. Maudhui yalikuwa ‘’Miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar.’’ Washiriki
wenzangu walikuwa Harith Ghassany akiongea kutokka Washington DC, Ahmed Rajab
akiwa London, mimi nikiwa Tanga na Salehe Feruzi mmoja wa viongozi wa CCM
Zanzibar akiongea kutoka visiwani. Kipindi hiki walivyodai wasikilizaji wengi
ni kuwa mimi nilikichangamsha kwa maelezo yangu ambayo hayakuwa yamezoeleka
katika masikio ya wasikilizaji wengi. Katika kipindi kile nilikataa nadharia ya
mapinduzi Zanzibar kuwa ni sababu ya ‘’maendeleo,’’ visiwani kama alivyoeleza
Salehe Feruzi. Kubwa ni pale niliposema kuwa CCM Zanzibar wanaogopa uchaguzi na
nikaeleza sababu za kusema hivyo. Ndipo Kai Kresse baada ya kusikia msimamo
wangu ule aakanialika nikatoe mada katika taasisi yake Berlin.
|
Abdilatif na Mwandishi Humburg |
Abdilatif akanialika nyumbani
kwake Humburg na nikenda kumtembelea. Pale nyumbani kwake nikakuta maktaba
kubwa sana imeshona kila aina ya vitabu. Nami nikiwa na muda napita kitabu
kimoja hadi kingine kusoma maudhui kasha kukirejesha shubakani. Abdilatif
akanambia kuwa ile maktaba yake ya London bado ipo vilevile hapa Ujerumani
kaanzisha nyingine mpya. Nguvu ziliniishia. Kipindi nilichokuwa Humburg nikapata mwaliko wa kutoka kwa Ridder Samsom. Nilifatana na Abdilatif na hakika ilikuwa siku nzuri sana. Ridder Samsom ingawa ni Mholanzi lakini ni bingwa wa lugha ya Kiswahili. Baada ya chakula Ridder alisogea kwenye piano yake na hapo nikashuhudia maajabu mengine. Alinipigia nyimbo moja niipendayo sana ya Abdullah Ibrahim mpiga jazz maarufu kutoka Afrika Kusini. Abdullah Ibrahim kabla ya kusilimu na kuwa Muislam jina lake lilikuwa Dollar Brand. Abdilatif ni mtu wa mambo mengi na vipaji chekwa. Wakati mwingine akiniburudisha kwa habari za Muyaka Bin Haji mshairi mkubwa wa Kenya aliyeishi karne ya 18. Kipindi nilichokaa kwa Abdilatif
pale Humburg nilipata muda wa kujifunza mengi katika maisha yake kiasi
nilimuomba aandike kumbukumbu za maisha
yake. Alinifahaisha kwa ufupi maisha yake akiwa kifungoni jela ya Shimo la Tewa Mombasa na vipi aliweza kupata karatasi kuandika kitabu chake, ''Sauti ya Dhiki.'' Kama kawaida ya watu hawa wakubwa waliofanya mengi majibu yao hayapishani
hupenda kusema kuwa wao si lolote si chochote hakuna la kueleza muhimu katika
maisha yao nk. nk.
|
Juu Abdilatif Abdalla na Juma Mwapachu na chini akiwa na Jenerali Ulimwengu New Africa Hotel katika kuzindua kitabu c
cha Mwalimu Nyerere: Nyerere The Early Years kilichoandikwa na Thomas Molony |
Nashukuru kuwa wapo
walioona umuhimu wa Abdilatif Abdalla na wameamua kumuandika. Naamini kitabu hiki kitakuwa na mengi ya
kusisimua na kuelimisha.
Nikikutana na Abdilatif Insha
Allah nitamuuliza ni wazo lake au la mchapaji kuweka picha staili ya Alfred Hitchcock?
|
Alfred Hitchcock
|
No comments:
Post a Comment