Maandamano ya Waislam Dhidi ya NECTA Chini ya Dr. Joyce Ndalichako |
Ndugu Waziri,
Kwa muda mrefu
sasa, kumekuwa na maswali mengi wakijiuliza Waislamu, moja likiwa
inakuwaje katika maeneo yenye Waislamu wengi ambapo idadi ya wanafunzi Waislamu
inakuwa zaidi ya asilimia 70, lakini wanapochaguliwa kwenda sekondari, idadi ya
watoto wa Kiislamu huporomoka na kuwa chini ya asilimia 20.
Swali na
kitendawili hiki kimekuwepo kwa muda mrefu bila kupatiwa majibu. Hata
lilipofikishwa Bungeni mwaka 1999 na aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni, Mzee
Kitwana Selemani Kondo, bado halikupatiwa jibu.
Kitwana Selemani Kondo |
Akihoji juu
hali hiyo, Mzee Kitwana Kondo alitoa mfano jinsi hali ilivyokuwa katika shule
ya Pembamnazi iliyokuwa na Waislamu watupu na kwa miaka mingi mfululizo
kulikuwa hakuna hata mtoto mmoja aliyekuwa akichaguliwa kwenda sekondari kutoka
katika shule hiyo. Aidha alisema kuwa, katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani,
takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wa Kiislamu katika shule za msingi
ilikuwa zaidi ya asilimia 70 lakini inapokuja kuchaguliwa kwenda sekondari,
idadi ya Waislamu iliporomoka na kuwa chini ya asilimia 20.
Akizungumza
Bungeni tarehe 2 Februari, 1999 alisema kuwa katika watoto waliofanya mtihani
wa darasa la saba mwaka 1998, idadi ya Waislamu ilikuwa asilimia 71 na Wakristo
29%. Hata hivyo akasema, ilipotoka orodha ya waliochaguliwa kwenda sekondari,
idadi ya Wakristo ikawa asilimia 79 (79%) na Waislamu 21%.
Je, hiyo
ilikuwa na maana kuwa watoto wa Kiislamu kwa asili yao hawana akili? Alitaka
kujua Mzee Kitwana Kondo. Lakini hakuweza kupata jibu.
Mheshimiwa
Waziri,
Ni wazi kuwa
Waziri wa Elimu au Waziri Mkuu ambaye ndiye msimamizi wa mambo ya serikali
Bungeni asingeweza kutoa majibu ya uhakika kwa sababu swali lilihitaji
kufanyika uchunguzi huru wa kina na makini kwanza.
Mheshimiwa
Waziri,
Mwaka 1987
aliyekuwa Waziri wa Elimu, Profesa Kighoma Ali Malima, aliweka utaratibu mpya
wa ufanyaji wa mtihani wa darasa la saba ambapo namba zilitumika toka kufanya
mtihani, kusahihisha na kuchagua wanafunzi wa kwenda kidato cha kwanza. Namba
zilivishwa majina baada ya taratibu zote hizo kukamilika. Mwaka huo idadi ya
watoto wa Kiislamu waliokwenda kidato cha kwanza iliongezeka kwa asilimia 40
ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Hata hivyo,
mara aliondolewa Waziri Malima katika wizara hiyo na utaratibu wa zamani
ukarejeshwa ambapo yalikuwa yakichaguliwa majina na idadi ya Waislamu
ikaporomoka na kurudi chini ya asilimia 20.
Mheshimiwa
Waziri,
Hali kama hii
hapana shaka inazua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu na majibu hayo
hayawezi kupatikana bila ya kufanyika uchunguzi.
Labda tuongeze mifano ili kuliweka wazi zaidi jambo hili. Mwaka 1983 mwanafunzi
aliyekuwa akiitwa Kopa Abdallah akisoma katika shule ya msingi Kichangani,
Kilosa, alikosa kuchaguliwa kwenda sekondari. Yeye binafsi, wazazi wake na hata
walimu wake hawakuamini matokeo yale kutokana na alivyokuwa akifanya vizuri
kuliko wanafunzi wote. Baadae ilikuja kugundulika kuwa nafasi yake alipewa
mwanafunzi aliyekuwa akiitwa Antoni Samirani ambaye alikuwa na uwezo mdogo sana
ikilinganiswa na Abdallah. Kilichofanyika ni kuwa jina la Abdallah lilifichwa
na baadae Antoni akapewa jina hilo kimya kimya na kwenda kusoma sekondari
akitumia jina Abdallah wakati yeye ni Antoni.
Taarifa
zinasema kuwa Kopa Abdallah alipogundua hakuweza kufanya kitu akaishia kuwa
dereva.
Hali kama hiyo
ilimkuta pia Adam Ramadhani aliyekuwa akisoma shule ya msingi Rutihinda jijini
Dar es Salaam na kumaliza darasa la saba mwaka 1999. Yalipotoka matokeo ya
mtihani wa darasa la saba na kuonekana kuwa Adam hakuchaguliwa, baba yake
hakuamini kuwa mtoto wake anaweza kufeli kutokana na uwezo aliokuwa nao na
zaidi akitizama walivyochaguliwa watoto ambao Adam alikuwa mwalimu wao shuleni
na mitaani.
Katika
kufuatilia suala hilo wizarani, ilikuwa aibu kwa wizara baada ya kuonekana kuwa
walichaguliwa watoto wa Kikristo wenye alama za chini kabisa huku akiachwa Adam
Ramadhani aliyekuwa na alama za juu kuliko wote.
Mheshimiwa
Waziri,
Mifano kama hii
ni mingi mno na ipo katika ngazi zote kwa maana kutoka elimu ya msingi kwenda
sekondari, kutoka kidato cha nne kwenda kidato cha tano na kutoka kidato cha
sita kwenda Chuo Kikuu. Kwamba hata kutoka kidato cha nne kwenda kidato cha
tano, wapo watu waliopata kushuhudia majina ya wanafunzi wa Kiislamu yakiwekwa
pembeni japo walikuwa na sifa za kuchaguliwa.
Mheshimiwa
Waziri,
Ukiacha hujuma
katika kuwaacha wanafunzi Waislamu wenye sifa kuendelea na masomo, matatizo
huanzia kwenye kuamua nani amefaulu na nani kafeli. Tuhuma zilizopo ni kuwa
wapo wanafunzi wanapewa madaraja ya juu wakati alama zao ni za chini na wapo
wanaopewa madaraja ya chini wakati alama zao ni za juu. Na hii ni kwa masomo
yote.
Mheshimiwa
Waziri,
Kumekuwa na
utamaduni katika nchi hii wa kukataa ukweli. Kufuatia uchunguzi uliofanywa na
Kamati za Bunge, tumeshuhudia wizi na ufisadi wa kutisha ukifichuliwa Bungeni
hivi karibuni hali iliyopelekea mpaka Mheshimiwa Rais kubadili Baraza lake la
Mawaziri.
Sasa baada ya
kuyasema yote hayo, tunasema kuwa Baraza la Mitihani la Tanzania, limekuwa
likilalamikiwa kwa zaidi ya miaka 30, lakini malalamiko hayo yamekuwa
yakipokewa kwa sikio la uziwi. Imefikia mahali tunasema kuwa hatuna tena imani
na Baraza hilo.
Mheshimiwa
Waziri,
Ilikupata
ukweli wa malalamiko na shutuma hizi, na ili kujibu lile swali juu ya watoto wa
Kiislamu ambalo halikupata jibu Bungeni, tunaitaka serikali kufanya yafuatayo:
- Tume huru iundwe kuchunguza Baraza la Mitihani la
Tanzania na utendaji wake kazi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.
- Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA)
ajiuzulu mara moja ili kulinda heshima ya serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzaani na Baraza la Mitihani. Watendaji
wakuu wa kitengo cha mitihani na wanaohusika na mfumo wa Kumputa ya Baraza
la Mitihani nao wawajibishwe mara moja.
- Hatua za kisheria na kibinadamu zichukuliwe
dhidi ya watumishi wa Baraza la Mitihani watakaothibitika kuhusika na
kashfa hii.
- Muundo wa Baraza la Mitihani uzingatie uwiano wa
kidini, kitendo cha chombo nyeti kama hiki kujazana watu wa dini moja
kunaliondolea Baraza la Mitihani sura ya kitaifa, kwani takwimu
zinaonyesha Makatibu Wakuu Watendaji na Manaibu Katibu Wakuu wamekuwa
Wakristo na Wenyeviti wa Baraza hilo ni Wakristo tangu lilipoanzishwa
mwaka 1973, mpaka hii leo na takwimu tunazo.
Mheshimiwa
Waziri,
Tunaomba
ieleweke kuwa tunachotaka ni kupatikana haki na kufanyika uadilifu kwa watu
wote. Hatudai wala hatutaki upendeleo kwa Waislamu na wala hatutaki kuona mtu
yeyote anaonewa au kuporwa haki yake, awe Mwislamu au mtu wa dini nyingine.
Tunachoamini
ni kuwa kama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haina cha kuficha, basi
itaunda Tume hiyo kwa haraka na kuhakikisha kuwa ni Tume ya kuaminika
itakayofanya kazi yake kwa umakini, kwa kina na kwa uadilifu wa hali ya juu
kabisa.
Lakini
kama Wizara yako itaona kuwa haiwezi kuunda Tume ya uchunguzi, tunacho
kuhakikishia ni kuwa sisi tutafanya kila liwezekanalo na kwa namna yoyote
kuhakikisha kuwa Tume hiyo inaundwa. Na ikigundulika kuwa kuna hujuma
zinafanyika katika utendaji wa Baraza, basi itabidi uwajibikaji uanze kwenye
Wizara kabla ya kuwawajibisha watendaji wa Baraza la Mitihani.
Ni
imani yetu kuwa utayapokea madai ya Waislamu na kuyafanyia kazi kwa umakini na
kwa haraka ili kujenga mustakbali mwema wa nchi hii na watu wake.
Tunaomba
kuwasilisha,
Mwenyekiti
Baraza
Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Juni 8, 2012
No comments:
Post a Comment