Monday 11 January 2016

AZAM TV: MAPINDUZI YA ZANZIBAR KUTOKA KUMBUKUMBU ZILIZOZIKWA



Faraja Sendegea akifanya mahojiano na Mohamed Said
Ingia hapa kusikiliza kipande cha mahojiano:
Leo asubuhi nilifanyiwa mahojiano na mtangazaji Faraja Sindegea wa Azam TV kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar. Mtangazaji alifungua kipindi kwa utangulizi kuhusu historia ya mapinduzi na umuhimu wa kuyaenzi mapinduzi. Nilimtaka radhi kwa kumwambia kuwa itafaa kama tutayazungumza mapinduzi kutoka kumbukumbu ya mashujaa waliopigania uhuru wa Zanzibar lakini michango yao haitambuliwa na nchi yetu. Nilikwenda moja kwa moja kwenye kumbukumbu za Aman Thani kueleza yale ambayo si wengi wanayafahamu. Watazamaji nadhani kwa mara ya kwanza waliona picha ya Aman Thani kwenye televiseheni zao na picha ndiyo hiyo hapo juu. Nilieleza kuwa nimezisoma kumbukumbu za Aman Thani na niligusia umuhimu wa nyaraka zake kwa mwanafunzi yoyote yule anaejifunza historia ya siasa za Afrika hususan historia ya Zanzibar na mapinduzi yaliyokuja kutokea mwaka wa 1964. Nimesema kuwa kumbukumbu za Aman Thani zinakuja na picha nyingine kabisa ya mapinduzi ambayo si wengi wanaijua. Nilieleza kuwa ni Aman Thani peke yake katika wafungwa wa siasa wa Zanzibar aliyeweza kueleza kwa kirefu kuhusu Jela za Mateso zilizoundwa baada ya mapinduzi na jinsi alivokabiliana na Mtesaji Mkuu Hassan Mandera.

Niliwaonyesha watazamaji baadhi ya vitabu muhimu vya historia ya Zanzibar pamoja na kitabu, ''Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha,'' kitabu ambacho nilisema mwandishi Minael- Hosanna O. Mdundo amepotosha mambo mengi.

Mtangazaji Faraja alitaka kujua John Okello ni nani. Nilimweleza kuwa John Okello hakuwa chochote katika mapinduzi ila alitumiwa kutoa matangazo ya kuwatisha wananchi. Kwa lugha ya wenye mapinduzi yao ni kuwa, ''Walimvisha blanketi la U-Field Marshall na likamwenea na yeye mwenyewe akaamini khasa kuwa hakika ni ''Field Marshall,'' Hapa kuhusu, ''Blanketi la Okello,'' niliwapeleka watazamaji wangu kwenye rejea ya kitabu cha Dr. Harith Ghassany, ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.'' Nilimtaja Abdallah Kassim Hanga kuwa ndiye aliyepanga mapinduzi akishirikiana na serikali ya Tanganyika chini ya Julius Nyerere. Katika muktadha huu niliwarejesha tena watazamaji kwenya kumbukumbu za Aman Thani aliposema kuwa hayakuwa ''mapinduzi,'' bali mavamizi. Aman Thani nikaeleza kuwa ametoa changamoto katika picha maarufu ya Okello hapo juu kuwa atokee mtu awaonyeshe Wazanzibari khalis katika picha ile.

Baadhi ya mawaziri wa serikali iliyopinduliwa
Kushoto: Ibun Saleh, Juma Aley, Mohamed Shamte, Dr, Baalawy na Ali Muhsin Barwani







Niliendelea kusema kusema kuwa hatujapatapo kusheherekea Mapinduzi ya Zanzibar katika hali ya majonzi kama mwaka huu. Moja kwa moja nikawafahamisha watazamaji kuwa tunasheherekea mapinduzi tukiwa katika hali ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar wamepanda jahazi la ubaguzi wa rangi kwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuonyesha bango la kibaguzi wakiwabagua Wazanzibari ambao hawakuzaliwa na ngozi nyeusi habari ambazo zimezagaa katika mitandao ya kijamii kama moto wa makumbi. Nilimweleza mtangazaji kuwa sitaki kuamini kuwa CCM Zanzibar imefilisika kiasi hiki. Nilieleza maana ya ''Hizbu,'' kuwa ni neno la Kiarabu lenye maana ya ''Chama'' na ''Watan,'' maana yake ni ''Taifa.''

Hapa nikaeleza historia ya Tanzania kuwa katika kupigania uhuru wa Tanganyika kulikuwa na Wazungu na Wahindi waliokuwa viongozi wa TANU na wakisimama kugombea nafasi za uongozi na wakishinda bila ubaguzi. Nilimtaja Sophia Mustafa, Ratansey, Amir Jamal, Dereck Bryceson na nikaeleza kuwa katika Bunge la Tanzania kuna kila aina ya wabunge mpaka Makalasinga.

[​IMG]
Baraka Shamte kada maarufu wa CCM na mtoto Waziri Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar Mohamed Shamte akifanya mahojiano na Mwandishi nyumbani kwake Mkunazini, Zanzibar
Nikaeleza kuwa huko Zanzibar tumekuwa na rais Amani Abeid Karume ambae baba yake asili yake ni  Mnyasa na mama yake ana asili ya Kihindi. Nikawauliza hawa wabaguzi kuwa hivi ndugu zetu kama Mansour Yusuf Himid na Mahamoud Thabit Kombo na wengi wao Amani Karume mwenyewe na binti yake Fatma watajisikiaje kwa kauli kama hizi za ugozi? Nilifanya rejea za Ton Ton Macout wa Papa Doc wa Haiti ambae alitumia mbinu za vitisho kwa wananchi wake mfano wa Mazombie wa Zanzibar halikadhalika nilitahadharisha hatari ya kuwatumia vijana kama walivyotumiwa na Adolf Hitler kwa kutengeneza ''Stormtroopers,'' au ''Brown Shirts,'' kuwatisha wananchi. Nikawaeleza viongozi waisome historia ili wapate mafunzo nini ilikuwa hatima ya mambo haya.

Nilieleza kuwa historia nyingi ya mapinduzi ya Zanzibar imo katika vifua vya watu wengi wao wameshatangulia mbele ya haki. Wengi katika hao kwa njia moja au nyingine walishiriki wakiwa Bara katika kuiangusha serikali ya Zanzibar. Lakini kutokana na mauaji yaliyotokea katika mapinduzi na baadae wengi wao walifunga midomo yao na hawakutaka watu wajue kuwa walihusika. Mfano mmoja niliouleza ni wa Ali Mwinyi Tambwe. Nilieleza kwa uchache kuwa Ally Sykes alimgusia Dr. Harith Ghassany kuwa wao ndiyo walimjulisha Nyerere kwa Karume.


Mtangazaji alitaka tuhitimishe mahojiano yetu kwa mimi kueleza hali ya baadae ya Zanzibar. Nilimueleza kuwa Wazanzibari wamefanya uchaguzi na CCM Zanzibar imeshindwa kwa ufupi ni kuwa, ''The people of Zanzibar have spoken,'' hakuna njia yeyote nyingine ila kwa walioshindwa kukubali kushindwa na maneno ya Ali Mohamed Shein kuwa kesi yake ipelekwe mahakamani ni jambo linalotufedhehesha. Itakuwa kichekesho cha mwaka mtu ashindwe uchaguzi dhahiri na anapoelezwa hivyo aseme, ''Nenda mahakamani mimi ni rais halali.''






No comments: