Monday, 11 January 2016

TUMETENGENEZA MAKABURU WATOTO ZANZIBAR


Vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM wakipita  mbele ya mgeni rasmi  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akipokea matembezi ya Vijana hao waliotembea katika Mikoa Minee ya Kichama katika kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyomalizia leo katika viwanja vya maisara Suleiman Mjini Unguja,[Picha na Ikulu.]

Picha hiyo hapo juu ni bango la Kikaburu katika mwaka wa 2016 bango linalotukuza ubaguzi wa rangi. 


Sitaki kuamini kama Ali Mohamed Sheni na uongozi wa juu wa CCM Zanzibar wamewatuma vijana hawa kufanya haya. 

Akili yangu inanikatalia kabisa. 

Sitaki kuamini kuwa tumeanza kuwatengeza akina Hendrik Verwoerd na Eugene Terre Blanche weusi katika visiwa vya Zanzibar. 

CCM Zanzibar inamuiga nani katika hili?
Hitler na Manazi na vijana wao waliojulikana kama Stormtroopers ukipenda waite Brown Shirts?

Hilo bango mbona litawagusa wengi katika safu ya uongozi wa siasa katika Zanzibar na wengine walipatapo hata kuiongoza nchi? 

Machotara?
Nani huyu chotara?

Tumehama kwa Waarabu sasa tuko kwa Machotara!
Lakini huyo chotara si ana wajomba, babu, bibi na mama wakubwa na wadogo Waafrika?

CCM imefilisika kiasi hiki?

Nini hiki ni kiwewe cha CCM kushindwa uchaguzi au ni kitu gani? 
Nini khasa tafsiri ya mambo haya? 

Tusubiri In Sha Allah wakati utatupa jibu.

Kasema Mwalimu Nyerere karne ya ishirini na moja kuna watu wanapanda basi la ukabila...
Hawa wanapanda jahazi la ugozi.

No comments: