Mimi ni zao la Zanzibar. Ni matokeo ya maelfu ya pepo za msimu zilizowapeperusha watu wa madau kutoka duniani kote kuja kwenye visiwa hivi viduchu vilivyochipuka katika maji vuguvugu ya Bahari ya Hindi mashariki mwa bara la Afrika.
Wakati wafanyabiashara wa Bahari ya Hindi wakisambaza bidhaa zao, lugha ya Kiswahili ikaibuka sambamba na Waswahili pamoja na utamaduni wao. Ninaona fahari kuitwa Mswahili. Mimi ni mchanganyiko wa makabila yote yaliyokuwa na uthubutu na nguvu za kuivuuka Bahari ya Hindi na bara la Afrika na kuja kuhamia Zanzibar.
Mfano ni bibi yangu, Bi Amina, ambaye akiwa na umri wa miaka 10 tu, alitekwa nyara kutoka kijiji kimoja Afrika ya Kati na wafanyabiashara ya utumwa na akamudu kutembea na kuvuuka bara hilo na kisha safari ya dau kutoka Bagamoyo hadi Zanzibar. Babu wa babu yangu alikuja akiwa mfanyabiashara kutoka Jimbo la Kutch, India. Babu wa babu wa babu yangu alikuja Zanzibar kwa dau akitokea Maskati akitumia pepo za msimu za wakati huo, kitambo tu baada ya kuwasili Seyyid Said bin Sultan, Simba wa Oman. Na nyuma ya hapo, babu wa babu wa babu wa babu yangu aliingia Zanzibar kwa dau akitokea Uajemi.
Mimi sina tafauti na maelfu ya Waswahili wengine. Sisi ni watu wa upwa huu, watu ambao muundo wa vinasaba vyetu ni mchanganyiko wa Wabantu, Waarabu, Waajemi na Wahindi. Tumeishi kwenye upwa wa Uswahilini na Zanzibar yenyewe kwa karne kadhaa. Sisi ndio agano kwa historia ya upwa wa Afrika ya Mashariki – na bado Jumapili iliyopita, wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) walikuwa na uthubutu wa kutuambia kuwa hatutakiwi Zanzibar.
Jumapili ya tarehe 10 Januari 2016, zikiwa ni siku mbili tu kabla ya sherehe za maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliohudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, wanachama wa UVCCM walibeba mabango mawili. Yote mawili yaliiambia nchi na dunia kwamba watu wenye rangi mchanganyiko, ambao wao waliwaita kwa jina la kejeli la ‘machotara’, hawatakiwi Zanzibar kwa sababu sisi tunaonekana kuwa watumwa wa Sultan, na wao kwa mtazamo wao, Zanzibar ni kwa ajili ya Waafrika tu.
Picha za mabango hayo zikatwaliwa na mitandao ya kijamii na hadi kufikia Jumanne ya tarehe 12 Januari 2016, zikawa zimeshazagaa kote. Kila mwenye intaneti alijuwa kuwa UVCCM hatimaye ilikuwa imeonesha rangi zake halisi. Jioni ya siku hiyo, Kaimu Mkuu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Daniel Chongolo, akajikalifisha kwa heshima na adhama kuomba radhi kwa niaba ya chama chake kutokana na mabango hayo ya ubaguzi yaliyooneshwa na vijana wa CCM.
Kwenye ukurasa wa mbele ya gazeti la Daily News la Alhamisi ya tarehe 14 Januari 2016, umma ukaelezwa kwamba “CCM ilikuwa mbioni kuwatambua na hatimaye kuwachukulia hatua muafaka watu waliohusika na bango la uchochezi lililooneshwa na mmoja wa wanachama wake Zanzibar mapema wiki hii,” na Nape Nnauye, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, alinukuliwa akieleza, “ningependa kusisitiza kwamba CCM inapingana na aina zote za ubaguzi, na hili linafahamika duniani kote. Ni bahati mbaya kwamba chama kinalaumiwa kwa makosa yaliyofanywa na kundi dogo tu la wafuasi wetu.”
Siku ya Alhamisi ya tarehe 13 Januari 2016, Shaka Hamdu Shaka, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa niaba ya chama hicho. Ni jambo la kuzingatia kwamba taarifa hiyo ilijitenga na tamko la kuomba radhi kutoka UVCCM na badala yake ikautuhumu upinzani kwa kuzusha chuki za kikabila na kuwahakikishia wananchi kwamba CCM, kwa kushirkiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na polisi, ingechukuwa hatua za kisheria dhidi ya wote waliohusika.
Kwa hivyo, si ajabu hivi karibuni tutaona wimbi jengine la kamatakamata linachochewa na CCM dhidi ya wanachama wa upinzani kwa kuthubutu kutueleza utovu adabu wa wanachama wa UVCCM, huku wale wakosaji hasa wakiwachwa bila kuguswa na wakingojea nafasi nyengine kuonesha mabango yao ya chuki. Taarifa ya Shaka iliwataka wanachama wa CCM waliochanganya damu kuendelea kuwa wavumilivu. Kuvumulia nini, sijui.
Na vipi kuhusu raia wa nchi hii waliochanganya damu na ambao si wanachama wa CCM – je wao ndio ‘wasaliti’ waliotajwa kwenye ujumbe huo?
Inavyoonekana, UVCCM inaamini kuwa uvumilivu na kuwaamuru polisi kuwashughulikia wapinzani ni dawa ya uovu huu. Tumewaona wanachama wengi wa upinzani wakati wa uchaguzi wakikamatwa na kwa upande wake Shaka hakuwazuia wanachama wa UVCCM kuchapisha matamko ya kibaguzi. Na hili ndilo linalonifanya nione kuwa inachofanya CCM ni danganya-toto tu. Yumkini kinachopaswa hasa kufanywa na polisi ni kuwakamata wanachama wa CCM wenye makosa haya, na pengine hilo lingeliweza kukomesha tabia hii ovu.
Kabla ya CCM haijaweza kushughulikia ubaguzi ndani yake yenyewe, inahitaji kuwa tayari kukubaliana na mambo rahisi yenye ukweli. La kwanza kuliko yote, siku ya Jumapili ya tarehe 10 Januari 2016, kulikuwa na mabango mawili ya kibaguzi yaliyooneshwa na wanachama wa UVCCM na sio moja kama inavyodaiwa na CCM. Pili, mabango haya yalioneshwa mbele ya Makamu Mwenyekiti wa CCM na wanachama wa ngazi za juu wa chama hicho, na hatukuwasikia wakiyalaani, ama iwe kwenye mkutano huo wa hadhara au baada ya hapo. Tatu, tafadhalini musitupumbaze kwa kutuambia kuwa ‘muko mbioni’ kuwatambua wanachama waliohusika na mabango hayo kwa sababu picha zao ziko kwenye mitandao yote ya kijamii. Kwa hakika, ninayo moja wao kwenye simu yangu; mukitaka naweza kuwatumia bure kwa njia ya ‘WhatsApp’. Nne, hii si mara ya kwanza kwa wanachama wa CCM kutoa matamshi ya kibaguzi. CCM ina ubao wake maarufu uitwao ‘Sauti ya Kisonge’ nje ya maskani yake iliyopo Michenzani, Zanzibar, ambayo katika siku za karibuni imekuwa ikiandika matamshi ya kibaguzi yanayowalenga Waarabu na watu wenye damu mchanganyiko na, hapana shaka, Wapemba.
Watu wanaotokea kisiwa cha Pemba wamekuwa wahanga wakubwa wa kila mashambulizi mabaya ya kibaguzi mikononi mwa CCM. Bahati nzuri, kuna watu ambao wameweka rikodi ya propaganda hizi za chuki. Sijawahi kusikia hata siku moja kauli rasmi ya kulaani tabia hii kutoka CCM.
Mwisho, kuna viongozi wa juu wa CCM ambao wanatoa kauli za kibaguzi na zilizo dhidi ya Uislamu kwenye mikutano ya hadhara. Na hili nalo pia liko kwenye rikodi. Hakuna hata mtu mmoja kati yao aliyewahi kuonywa na CCM. Badala yake, wamekuwa wakizawadiwa vyeo vikubwa zaidi kwenye chama na serikalini.
Kwa hivyo, sikubali kuwa kuilaumu CCM ni jambo la bahati mbaya, badala yake naamini inastahiki, na ikiwa CCM haitakuwa na ushujaa wa kuikata saratani hii iliyomo ndani yake – badala ya kuwalaumu wapinzani – hakuna uwezekano wa chama hicho kutenganishwa na tabia hii ya chuki.
Kati ya mwezi Aprili na Juni 1994, wanamgambo wa kundi la Intarahamwe na washirika wao waliwauwa kiasi cha Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani. Mauaji ya maangamizi nchini Rwanda yalipangwa na kutayarishwa na wanaadamu waovu kama hawa waliokuwa wakitumia maneno kupitia magazetini, likiwemo gazeti la ‘Kangura’, na redio, kama ‘Radio Television Libre des Mille Collines’, kutangaza na kusambaza propaganda za kibaguzi na chuki. Watutsi walipewa majina kama vile mende na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliokuwa wameoana na Watutsi waliitwa wasaliti. Ubaguzi wa ukabila ukawa sehemu ya utamaduni wa Rwanda.
Je, sisi tuna tafauti yoyote na Rwanda ya kabla ya mauaji hayo ya maangamizi? Tuna tafauti gani, ikiwa polisi wanawaruhusu wanachama wa CCM kuendelea kuchapisha matamshi ya kibaguzi na uchochezi kwenye mabao na mabango yanayooneshwa hadharani na kutoa hotuba cha chuki kwenye mikutano ya hadhara bila kuwachukulia hatua za kisheria? Tuna tafauti gani, ikiwa mwanachama wa ngazi za juu wa CCM anawaelezea Wazanzibari kuwa ni tatizo kwa kuwa tu asilimia 95 ya watu wake ni waumini wa dini ya Kiislamu? Bahati njema ni kuwa kuna watu wanaoiona tabia hii haikubaliki, lakini hawathubutu kusema wakihofia kushushiwa mashambulizi na chama hiki kikuu na kikongwe.
Sitanukuu hapa hotuba maarufu ya Mwalimu Nyerere kwa sababu nyote munaijuwa, na kwa hivyo ujinga wa kutojuwa si kisingizio cha tabia hii ovu. Lakini itoshe tu kusema kwamba pale wanachama wa CCM wanapotoa kauli dhidi ya Uislamu, maelfu ya Wazanzibari na mimi nikiwemo tunakuwa tumeshambuliwa kwa kuwa zaidi ya asilimia 95 ya watu wetu ni waumini wa Kiislamu. Pale wanachama wa CCM wanapotoa kauli za kibaguzi dhidi ya Wapemba, maelfu ya Wazanzibari na mimi tunakuwa tumeshambuliwa kwa kuwa tuna jamaa wa karibu ambao ni Wapemba. Pale wanachama wa CCM wanapotoa kauli za chuki dhidi ya Waarabu, maelfu ya Wazanzibari na mimi tunakuwa tumeshambuliwa kwa kuwa tuna jamaa wa Kiarabu. Pale wanachama wa CCM wanapotowa kauli za kibaguzi dhidi ya watu wenye damu mchanganyiko, CCM inakuwa imeipoteza Zanzibar kwa kuwa baba na mama zetu ni Waafrika na wao pia wanakuwa wameshambuliwa.
Andiko hili ni ushuhuda wangu wa wakati huu ambao utadumu muda mrefu hata baada ya mimi kuondoka ili wanangu na watoto wao waje waujuwe ukweli kuliko hekaya za CCM. Watajuwa namna CCM ilivyojiruhusu kuvamiwa na ubaguzi wa kikabila na wa kidini. Hadithi hii haijesha. Ni ama chembechembe za kibaguzi ndani ya CCM zitakimaliza chama hicho na nchi yetu au CCM itapata ushujaa wa kuukomesha uoza huu uliokivamia.
Ninaishauri CCM ijiangalie vyema yenyewe na ianze kusafisha uchafu wa kibaguzi kutoka chama hicho kwa maslahi ya kila mmoja wetu na, zaidi ya yote, kwa maslahi ya demokrasia visiwani Zanzibar, kwa sababu tukatake tusitake, tunahitaji kuwa na CCM imara na yenye uwezo kuwa mizania ya CUF. CCM inayobakia madarakani kwa msaada wa mtutu wa bunduki haina faida kwa yeyote, hasa kwa Zanzibar.
TANBIHI: Makala hii ya Mwanasheria Fatma A. Karume ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Kiingereza la The Guardian la tarehe 16 Januari 2016 ikiwa na kichwa cha habari ‘Why CCM should shun racists for the sake of democracy in Zanzibar’. Imetafsiriwa kwa Kiswahili na Mohammed Ghassani kwa idhini ya mwandishi.
No comments:
Post a Comment