Simon Noel |
Ni miaka 52 sasa imepita tangu Mapinduzi ya
Zanzibar yatokee. Tuna mengi sana ya kujifunza Kutokana na Mapinduzi hayo ya
january 12 mwaka 1964 yaliyouondoa utawala wa Sultan Jamshed bin Abdulah pamoja
na serikali ya Zanzibar huru iliyokuwa chini ya waziri mkuu Sheikh Mohammed
Shamte. Mapinduzi hayo yalifanywa na vijana wa ASP wakishirikiana na makomredi
wa chama cha UMMA party.
Mengi sana yamesemwa kuhusiana na Mapinduzi hayo
yaliyofanyika kwa mtindo wa aina yake kiasi cha Zanzibar kupewa hadhi ya kuitwa
Cuba ya Afrika. Katika makala haya tutajadili hali ilivyokuwa baada ya
Mapinduzi kwa wale waliopindua na wale waliopinduliwa.
Mpaka sasa bado hapajawa na historia kamili juu
ya nani hasa alikuwa kiongozi mkuu wa Mapinduzi hayo ya january 12 mwaka 1964.
Historia rasmi inamtambua sheikh Abeid Karume kama jemadari mkuu wa Mapinduzi
hayo. Mwandishi Harith Ghassan amemtaja Kasimu Hanga kuwa ndie alikuwa kinara
mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar akimuelezea kuwa alifanya mpango na rafiki zake
kina Oscar Kambona na Ali Mwinyi Tambwe wa kuwasafirisha askari mamluki
waliokuwa wakifanya kazi ya Manamba kwenye mashamba ya mkonge ya Sakura na
Kipumbwi yaliyoko huko mjini Tanga.
Wanahistoria wengi wa kigeni walioandika historia
ya Mapinduzi ya Zanzibar wamemtaja field Marshall John OkeLlo kama ndie alikuwa
kiongozi mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar akishirikiana na vijana wa ASP kina Seif
Bakari, Faki Haji, Abdalah Natepe, Yusupj Himid, Mfarinyaki pamoja na wengineo
waliounda kamati ya watu 14.
Mara tuu baada ya Mapinduzi hayo Sheik Abeid
Karume aliongoza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kisha akishirikiana na
viongozi wengine wa serikali wakamtimua field Marshall John Okelo na akapigwa
marufuku kutokukanyaga tena Zanzibar. Akiwa nchini kwao Uganda John Okelo
aliandika kitabu cha Mapinduzi ya Zanzibar akieleza kuwa yeye ndie aliyeyapanga
na kuyaongoza Mapinduzi hayo. Akiwa na masikitiko sana John Okelo alinukuliwa
akisema kuwa anajutia sana aliyoyafanya kwani hayakumsaidia chochote na badala
yake yamemletea matatizo maishani mwake. Wakati fulani field marshall John
Okelo alinukuliwa akisema kuwa " mimi ndie nilifanya hadi Sultan akapoteza
ufalme wake lakini yeye mwenzangu hali yake ni nzuri kuliko mimi. Yeye
alipokelewa Uingereza na anaishi huko raha mustarehe lakini mimi ndugu zangu
wamenifukuza na nimebaki natanga tanga" alisikika akilalamika Okelo.
Baadae field marshall John OkelLo aliuawa kikatili na dikteta Iddi Amin pale
aliposema kuwa Uganda pana mafield marshall wawili yani yeye na Iddi Amin.
Huo ukawa mwisho wa field marshall John Okelo
aliyejiita shujaa mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Shujaa mwingine wa Mapinduzi hayo Kasimu Hanga
ambaye baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar aliteuliwa kuwa balozi huko
nchini Guinea miezi michache kabla ya kifo chake alisikika akisema kuwa
anajutia sana yale aliyoyafanya akimaanisha kuwa anajutia sana ushiriki wake
katika mapinduzi ya zanzibar. Kwa mujibu wa Harith Ghassan ameeleza kuwa Kasimu
Hanga akiwa nyumbani kwa Oscar Kambona London Uingereza alisikika akisema kuwa
" Sisi tumeua watu, tumedhulumu watu, tumechukua wake za watu. Nami najuta
kwa niliyoyafanya na namuomba Mungu anisamehe ". Baada ya hapo Hanga
alirudi nchini ambapo alikamatwa kwa amri ya serikali ya muungano. Na kabla ya
kupelekwa Zanzibar aliwekwa hadharani na kudhalilishwa mbele za watu katika Uwanja wa Mnazi Mmoja
huku akiwa katika hali ya kufungwa. Baada ya hapo akapelekwa Zanzibar ambapo
yeye pamoja na mashujaa wengine wa Mapinduzi kina Othman Sharif, Jaha Ubwa na Mdungi Usi
waliuawa kikatili. Jaha Ubwa alikuwa ni shujaa wa Mapinduzi aliyekuwa Msaidizi
mkuu wa field marshall John Okelo na Othman Sharif alikuwa ni msomi kutoka chuo
kikuu cha makerere ambaye alisaidia sana katika kuyafanya Mapinduzi hayo
kutambulika kimataifa. Jambo la kushangaza ni kuwa mashujaa hawa waliuawa
kikatili na serikali waliyoipigania iingie madarakani.
Historia rasmi inamtambua sheikh Abeid Karume
kama kiongozi mkuu wa Mapinduzi ya Zanzibar. Lakini jambo la kushangaza ni kuwa
sheikh Abeid Karume aliuawa kwa risasi na makomredi wa UMMA party ambao
alishirikiana nao katika kuuondoa utawala wa Sultan Jamshed bin Abdulah.
Mashujaa wengine wa Mapinduzi hayo kanali Seif
Bakari, Brigedia Faki Haji pamoja na Rais mstaafu wa Zanzibar Aboud Jumbe nao
pia wakikutwa na dhahama inayofanana na hizo ingawa wao hawakuuawa ila misuko
suko waliyoipitia kipindi kile cha kuchafuka kwa hali ya hewa Zanzibar ilitosha
kabisa kumfanya kanali Seif Bakari atoe kauli ya kujutia maishani mwake kuingia
katika maswala ya maisha
Lakini jambo la kushangaza ni kuwa wale
waliopinduliwa waliishi maisha mazuri tena ya raha mustarehe.Sultan Jamshed bin
Abdulah anaishi hadi leo nchini Uingereza akiwa ni Mzee Mwenye miaka 86 na
hajawahi kukumbwa na tatizo lolote tangu
alipopinduliwa. Aliyekuwa kiongozi mkuu wa chama cha ZNP sheikh Ali Muhsin
Barwan aliondoka nchini mwaka 1974 baada ya kuachiwa toka kifungoni na alienda
Muscat Oman ambapo aliishi raha mustarehe hadi alipofariki mwaka 2006.
Swali la kujiuliza kama kweli Mapinduzi hayo
yalikuwa na baraka za wananchi wa Zanzibar ni kwa nini viongozi na mashujaa wa
Mapinduzi hayo walikuja kupata matatizo makubwa kiasi hicho.
Simon Noel
B.A Development Studies
University of Dodoma
0767001000
No comments:
Post a Comment