TAMKO LA JUMUIYA MAIMAMU ZANZIBAR (JUMAZA) KWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI
ZA KIISLAM ZANZIBAR KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MGOGORO WA KISIASA ZANZIBAR
TAREHE 6 JANUARI 2016
Awali tunamshukuru Mwenyezi Mungu
aliyetuwezesha kukutana katika hafla hii hali ya kuwa ni wazima; sala na salamu
zimfikie Mtume wetu Mtukufu Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake na
wote wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya Malipo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Tunawashukuru sana kwa kuitikia wito wetu wa kuhudhuria katika mkutano huu muhimu wenye lengo la kutafuta maslahi na mustakbali mwema wa nchi yetu.
Tunawashukuru sana kwa kuitikia wito wetu wa kuhudhuria katika mkutano huu muhimu wenye lengo la kutafuta maslahi na mustakbali mwema wa nchi yetu.
Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislamu
Zanzibar tunawashukuru sana Wazanzibari wote kwa kuendelea kudumisha amani na
utulivu katika nchi yetu pamoja na kukabiliwa na mtafaruku mkubwa wa kisiasa
ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Zanzibar uliotokana na hatua ya
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha kuufuta Uchaguzi
wote uliofanyika tarehe 25 Octoba, 2015 na matokeo yake katika tangazo lake la
tarehe 28-10-2015.
Kitendo hicho cha kuufuta uchaguzi
huo, kimepelekea nchi yetu kuingia katika mgogoro mkubwa wa kikatiba na
kisiasa. Wananchi wa kawaida ambao ndio wapiga kura wanaathirika kisaikolojia
kwa kushindwa kujua khatima ya kura walizozipiga. Kwa upande mwengine kumekuwa
na ongezeko la ugumu wa maisha visiwani Zanzibar unaotokana na mfumuko wa bei
kwa bidhaa muhimu na mzunguuko wa pesa kuwa mdogo kutokana na baadhi ya Wafanya
biashara kuwa na khofu ya kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa khofu ya
kutokea vurugu.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Sisi tukiwa viongozi wa jamii
tumeshughulishwa sana na mtafaruku huu wa kisiasa unaotukabili ambapo hadi sasa
tumechukua hatua zifuatazo kusaidia kufikia ufumbuzi:-
Tuliwaandikia
barua za nasaha viongozi wote wakuu wa kisiasa wanaoshiriki katika mazungumzo
ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo huu wa kisiasa.
Tuliwaandikia
barua mabalozi wa nchi sita waliopo Tanzania kuomba wasaidie katika kuutafutia
ufumbuzi mgogoro huu katika kuhakikisha kuwa demokrasia inachukua mkondo wake.
Mabalozi wahusika ni kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Norway
na Sweden.
Tulimwandikia
barua Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe
Magufuli kumkumbusha dhima yake ya kuingilia kati mgogoro huu ili kupatikana
ufumbuzi wa haraka. Kupitia khutuba za Ijumaa katika misikiti mbali tumekuwa
tukiwanasihi wananchi wawe na subra ili watoe fursa kwa viongozi wa kisiasa
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu kwa njia za amani.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wananchi wa Zanzibar tulipata
matumaini tulipoona kuwa viongozi wakuu wa kisiasa wanakutana kuzungumzia hali
ya kisiasa nchini, tuliamini kuwa katika vikao hivyo Viongozi hawa wenye
kuheshimika wakitawaliwa na busara, hekima, uadilifu na wakiweka mbele maslahi
ya taifa badala ya vyama vyao basi muda si mrefu tungepata ufumbuzi wa mgogoro
huu. Bahati mbaya tunaambiwa ni vikao 8 sasa vimeshafanyika tokea kikao cha
mwanzo cha tarehe 9 Novemba, 2015 hakuonekani kuwa matumanini yale wananchi
waliyoyajenga kwao kuwa yatatimia. Tunasema hivi kwa sababu kwanza vinaendeshwa
kwa usiri mkubwa mno na hadi leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa umma.
Hali hii inawafanya wananchi kutoelewa kinachoendelea na hivyo kuishi maisha ya
wasi wasi na kukosa utulivu hata wa kufanya shughuli zao za kimaisha.
Kasoro nyengine ni kuwa vikao
hivi vimechukua muda mrefu sana na hivyo kuibua maswali mengi na shaka kwa
wananchi. Pia tabia iliyojitokeza ya baadhi ya wajumbe wanaoshiriki mazungumzo
hayo kutoa kauli zinazoshabikia msimamo wa upande mmoja kunawatoa imani
wananchi juu ya kuwepo kwa nia njema katika mazungumzo hayo na kwamba
mazungumzo hayo yanaweza kuivusha nchi yetu katika mkwamo huu wa kisiasa
unaohatarisha usalama wa nchi yetu.
Kutokana hali hii sisi Viongozi
wa Dini ya Kiislam Zanzibar tunatamka kwamba:-
JUMAZA na
Taasisi za Kiislam Zanzibar zinawataka viongozi wakuu wa kisiasa wanaoshiriki
katika mazungumzo kuwajibika kwa kuweka mbele maslahi mapana ya nchi,
kuhitimisha mazungumzo yao haraka iwezekanavyo na kutoa maamuzi rasmi ikiwa ni
muongozo wa kutukwamua hapa tulipo kwa njia ya amani na salama.
Tunawatanabahisha kuwa jamii yetu kwa sasa ni mfano wa bomu linaloweza kuripuka
wakati wowote ule. Ukimya na uvumilivu wa Wazanzibari uliopo kamwe usichukuliwe
kuwa wao ni Malaika bali ni binaadamu kama walivyo wengine ambao wanaweza
kufikia hatua ya kushindwa na uvumilivu na kutoa maamuzi magumu yanayoweza
kutufikisha pahala pabaya na kuigharimu sana nchi yetu.
Hatuombi jambo
hili kutokea lakini likitokea viongozi wakuu wa kisiasa watabeba dhima mbele ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hivyo basi, tunawaomba Viongozi wakuu wa kisiasa wanaoshiriki
katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi, ni wakati muwafaka sasa watoke
hadharani na watoe taarifa kwa umma juu ya hatua iliyofikiwa na ikiwezekana
lini mazungumzo hayo yatakamilika na Wazanzibari watarajie nini kutokana na
mazungumzo hayo. Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislam Zanzibar, tunapinga kwa nguvu
zetu zote kauli za uchochezi zinazoendelea kutolewa na wanasisa ambazo zinazidi
kujenga khofu, hamasa na chuki miongoni mwa wananchi.
Aidha,
tunasikitika kuona kuwa kauli hizo zinatolewa bila ya kujali mazungumzo
yanayoendelea ya viongozi wakuu ya kutafuta ufumbuzi.Sisi Viongozi wa Dini ya
Kiislam Zanzibar, kwa heshima kubwa tunamuomba sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dk. John Pombe Magufuli ambaye
ameonesha dalili njema za uadilifu na uwajibikaji mkubwa achukue hatua za wazi
na za haraka katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu kabla nchi yetu
haijatumbukia pahala pabaya. Aidha, tunamuomba kusimamia kwa udhati na ujasiri
kuona haki inachukua mkondo wake na maamuzi ya Wazanzibari walio wengi
yanaheshimiwa.
Katika Uchaguzi
wa tarehe 25 Oktoba, 2015 JUMAZA ilikuwa na waangalizi katika majimbo yote ya
Unguja na Pemba, kasoro zilizoripotiwa katika uchaguzi huu ni kasoro ndogo
ndogo mno na kwa hakika ni afadhali kuliko chaguzi zote zilizopita huko nyuma
tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vyangi.
JUMAZA
inashangazwa sana na hatua ya kufuta Uchaguzi huu iliyochukuliwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha.
JUMAZA inauliza
kwanini wakati tulipokuwa na kasoro kubwa zaidi katika chaguzi za mwaka 1995,
2000, 2005 na 2010 Uchaguzi haukufutwa na kutakiwa kurejewa tena iwe Uchaguzi
wa mwaka 2015 tu? Na jee kama uchaguzi utakaorejewa nao ukawa na kasoro
zitakazolalamikiwa, utafutwa tena? Tutafanya chaguzi ngapi kwa mtindo huu? Taasisi
za Kiislam Zanzibar zinawaomba Waislamu wote kuendeleza dua ili kuitakia mema
nchi yetu na kumkabidhi Mwenyezi Mungu kwa wale wote wanaokusudia shari.
Aidha,
zinawaomba Maimamu na Makhatibu kukemea kauli zinazohatarisha amani na mshikamano
wa jamii.
JUMAZA na
Taasisi za Kiislam Zanzibar zina khofu kubwa juu ya kurejewa kwa uchaguzi,
uzoefu unaonesha kuwa nchi zilizorejea uchaguzi katika Bara la Afrika kama vile
Nigeria, Zimbwabwe, Malawi na kwengineko hatimaye zilitumbikia katika machafuko
makubwa. Kama hilo halitoshi Zanzibar tuna historia mbaya ya kurejea uchaguzi.
Wengi tunakumbuka katika historia ya Zanzibar kile kinachoitwa ‘vita au
machafuko ya Juni. ‘
Uchaguzi wa Januari mwaka 1961 ulilazimika
kurejewa mwezi wa Juni 1961, ambapo ulipelekea machafuko makubwa ikiwemo vifo
vya watu 68, maelfu kujeruhiwa, nyumba kuvunjwa na kuchomwa moto. Kwa historia
hii JUMAZA na Taasisi za Kiislam Zanzibar hazioni kuwa ni busara kurejewa kwa
Uchaguzi uliofanyika kwa ufanisi na kukamilika. Penye nia njema na utashi wa
kisiasa basi njia ya uadilifu iliyo wazi ya kutukwamua hapa tulipo ni kwa
Viongozi wakuu wa kisiasa kufikia ufumbuzi na makubaliano haraka iwezekanavyo.
Mola wetu Mtukufu tunakuomba kwa
rehma zako utuwezeshe kufikia ufumbuzi unaofaa juu ya tatizo linalotukabili na
uziunganishe nyoyo za Wazanzibari kuwa pamoja, kupendana na kuweka mbele
maslahi ya nchi yao. Amiin.
Ahsanteni
………………………………..
Muhiddin Z. Muhiddin
KATIBU MTENDAJI
JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR (JUMAZA)
No comments:
Post a Comment