Mwandishi na Dr. Harith Ghassany, Muscat Oman |
Utangulizi
Dr. Harith Ghassany ana
''sense of homour,'' kama wasemavyo Waingereza mbali ya kuwa msomi makini. Hata
pale unapozungumzanae jambo zito kama la Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964
na roho zilizoteketea atakutafutia jambo akuchekeshe. Ngoja nikupe mfano mmoja.
Tuko Kipumbwi Tanga katika
fukwe ya Bahari ya Hindi tumetoka kuangalia zile sehemu ambazo mamluki wa
Kimakonde kutoka mashamba ya mkonge ya Sakura walipokuwa wakivushwa kwa
majahazi kwenda Unguja tayari kushiriki katika kuiangusha serikali ya Waziri
Mkuu Mohamed Shamte.
Siku ile daktari alikuwa na
furaha kubwa sana kwa kuwa kitendawili kikubwa katika historia ya mapinduzi
kilikuwa kimeteguliwa. Hakuna mtafiti yeyote katika historia ya mapinduzi
aliyewahi kufika pale. Tulikuwa tushamaliza kupiga picha na zingine za video.
Ile video camera kanikabidhi mimi tulipokuwa pangoni huko ambako mamluki
walikuwa wakijificha na kupanda majahazi kiza kiingia wakivushwa na Mohamed
Omari Mkwawa au kwa jina lingine ''Tindo,'' (jina alilopewa na Mzee Karume), kwenda
Unguja wamejivika mavazi kama wavuvi wa Kidigo. Basi mimi napiga picha huku
nafanya, ''narration.'' Yeye ananitia moto kwa kunisifia ati nahadithia vizuri.
Nami bichwa linavimba kwa kusifiwa na msomi wa Harvard.
Sasa tuko juu pwani na upepo
wa bahari unatupiga. Dakari ananiuliza, ''Guy sasa katika kazi hii nikuandike
wewe nini kazi yako katika utafiti huu?'' Mimi najua daktari ananitania kwa
kuwa kazi yangu yeye anaijua sana. Mimi shughuli yangu kuu ilikuwa ni dereva,
nikimuendesha. Nami kwa maskhara na bila kufikiri nikamjibu, ''Mimi kazi
yangu Guy ni ''Research Assistant.'' Kwa anaejua kazi hii katika utafiti atajua
uzito wake.
Nimesahau ya Kipumbwi na yeye
kesharudi Marekani nami nimebaki Tanga. Baada ya miaka kama miwili hivi 2010
kitabu kimechapwa. Ndani ya kitabu nakuta picha yangu na cheo changu, ''Mtafiti
Msaidizi.'' Kila nikileta hii ''subject,'' kwake yeye anashikilia kuwa hiyo
ndiyo ilikuwa kazi yangu na wala sikupatapo kuwa dereva wake. Mimi na yeye
humaliza ubishi huu kwa vicheko na kwa kweli ''the joke is on me.''
Zanzibar 1950s |
Huyu ndiye Dr. Harith
Ghassany.
Sasa hebu msome hapo chini
akilihadithia baibui la Abdulrahman Babu
na kinachonichekesha mie ni
kule kufikiri zile sharubu za Babu ndani ya baibui
la ukaya:
Assalam Alaykum,
Inna Lillah wa Inna Ilayhi Raajiun -
Mzee Ahmed Badawi Qullatein ametutangulia kunako haki.
Mara yangu ya kwanza kuonana na marehemu
Mzee Badawi ilikuwa pale alipokuja Zanzibar kwa matembezi kutoka Dar es Salaam. Nilikwenda kuonana nae nyumbani kwake
Malindi na ilikuwa tarehe 26 Julai 2005.
Ilibidi nimsubiri kidogo kwa sababu alikuwa
anasoma Qur'an nyakati za asubuhi. Tulizungumza kiasi na alinikaribisha
nikipata wasaa nende nikaonane nae kwake Dar es Salaam lakini sikujaaliwa.
Nilionana nae tena mara pili alipokuja Uroa
na Bwana Ali Mohamed Yahya ambaye alikuwa ana tabia ya kumtembelea marehemu
baba yangu. Nakumbuka vizuri marehemu Mzee Badawi kuniambia kuwa suluhisho la
matatizo ya Waislam ni kuanzishwa kwa Dola ya Kiislam, na si jengine.
Tumebahatika wakati wa maombolezi ya kifo
cha almarhum Mzee Badawi kupata maelezo ya mchango wake wa kisiasa kama ni
kipande cha sehemu ya mwanzo wa maisha yake ya ujanani. Sheikh Salim Msoma
ametueleza kuwa marehemu alifariki Makka wakati alipokwenda kufanya Hijja.
Ingelipendeza zaidi kama Salim Msoma
angetueleza pia mabadiliko ya nafsi na ya kimtazamo ya marehemu Sayyid Ahmed Badawi
alietokana na ukoo wa Masharifu, akawa mmoja wa waasisi wa "Marxist Umma
Party of Zanzibar", na akafika kuipata bahati ya kufariki Makka wakati
akiweko huko kwa ajili ya kufanya Hijja.
Salim Msoma ana uhuru wake lakini
hakumtendea haki marehemu Mzee Badawi ambaye pia inasemekana aliomba
"Tawbat Nasuha" kabla ya kufariki kwake dunia ambayo ndio kilele cha
kujuta na kuomba maghfira kutoka kwa Muumba. Hilo ni jambo binafsi baina ya
muumbwa na Muumba wake lakini linatuambia kitu sisi waja wake kuhusu hali ya
marehemu Mzee Badawi kabla ya kurudi kwa Mola wetu sote. Wa Allahu Yaalam!
Sasa nakuja pale Salum Msoma alioitumia
nafasi ya maombolezi ya kifo cha marehemu Mzee Badawi kutoa dukuduku lake juu
ya kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Bado jini mkali
wa historia anaendelea kuwasumbua baadhi ya Makomred na ndio maana hata
marehemu Mzee Badawi aliefariki Makka akiwa na umri wa miaka 80 wanaona bora
wamrudishe nyuma alipokuwa kijana mbichi kwenye umri wa miaka 30.
Hakuna kitu kilichowaudhi baadhi ya
Makomred kama pale marehemu Mzee Aboud “Mmasai” aliposema na alivonukuliwa
akisema “Tukaingia ndani, Migombani huku, buibui la Sauda akavaa Babu, sasa
tunamwambia “wewe tukitoka uringeringe kidogo.” Dereva wa gari alikuwa Ali
Saidi, taxi-driver, tulimchukuwa, kwa sababu yeye huyu alikuwa ni
memba wa mapinduzi. Alikuwa ni mwenzetu. Tukampita asikari, akaingia ndani ya
gari ile, tukatoka tukenda Kizingo. Kizingo Babake Fuko, mzazi, alikuwa na
ngarawa na mwanawe mdogo Huseni, ndo akapakiwa Babu kupelekwa…kateremkia
Mlingotini. Akateremshwa pale, sie tukarudi huku.”
Kabla ya Salim Msoma, yuko
Komred mwengine (jina nalihifadhi) ambaye tuliwasiliana mwaka jana na alinipa
uoni wake juu ya kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! kwa
kusema “Ninachotaka kusisitiza hapa, bila ya kuigeuza barua hii pepe na kuwa
insha, ni kwamba zipo hizo tofauti kati ya wenye kukumbuka” na akatoa mfano:
“Tofauti nyingine ya makumbusho
niliyoiona ni katika maelezo ya jinsi Babu alivyokimbizwa kutoka Unguja. Nijuavyo
mimi hakuvalishwa buibui wala mke wa Marhemu Saleh Saadallah hajakuwako kwa
Babu wakati wa yeye Babu kukimbizwa kama alivyohadithia Aboud Mmasai. Waliokuwapo
hapo walikuwa Saadallah, Twala, Ashura aliyekuwa mkewe Babu...”
Mwaka jana nilibahatika kupokea mualiko
jijini Washington DC ambao wageni rasmi walikuwa ni Bibi Ashura na mumewe.
Nikajiambia kuwa hii itakuwa fursa ya kuusikiliza upande wa pili wa shilingi na
kujua kama maelezo ya kutoroshwa marehemu Abdulrahman Babu ya marehemu Mzee
Aboud “Mmasai” yalikuwa sahihi au yanahitajia marekebisho. Bi Ashura hakutaka
kuingia katika mazungumzo haya na mie nikayawacha.
Maelezo ya Salim Msoma
yanapingana na yale ya marehemu Mzee Aboud “Mmasai” juu ya mahala alipotoroshwa
Babu kupelekwa Dar es Salaam kwa msaada wa kina marehemu Saleh Saadalla na
Abdulaziz Twala. Mzee Aboud anasema ilikuwa ni Kizingo, Salum Msoma anasema
ilikuwa Fumba.
Sijui kwanini Salum Msoma akangojea
mpaka Mzee Badawi akafariki dunia ndio hii leo akaamua kutuletea kumbukumbu
muhimu kama hii. Jambo la kutia tamaa ni Msoma anasema kuwa mtu alioiendesha
gari iliomchukua Babu na Badawi Fumba yuhai na anaishi Dar es Salaam.
Kulia: Abdulrahman Mohamed Babu na Abdallah Kassim Hanga |
Sasa lilobaki ni kumuomba Bwana Msoma
atuletee, hadharani au hata kwa pembeni, jina na maelezo ya dereva aliyempeleka
marehemu Babu Fumba ili tuyahakiki maneno yake na yale ya marehemu mzee Aboud
“Mmasai” tuweze kuiweka rekodi sawa katika toleo lijalo la kitabu cha Kwaheri
Ukoloni, Kwaheri Uhuru!
Muhimu katika maneno ya Bwana Msoma ni
kukiri kwake kuwa marehemu Mzee Badawi alipewa taarifa ya mapinduzi na
waandalizi wa mapinduzi ambao walikuwa kina marehemu Abdalla Kassim Hanga,
Saleh Saadalla, na Abdulaziz Twala. Ameongeza kuwa Umma Party waliarifiwa
kwanza hata kabla kuarifiwa marehemu Mzee Karume na viongozi wengine wa chama
cha Afro-Shirazi.
Mungu amlaze mahala pema marehemu Mzee Ahmed Badawi
Qullatein – Amin.
Dr. Harith Ghassany na Mzee Mohamed Omari Mkwawa wakati wa utafiti wa kitabu picha ilipigwa 2009 Tanga |
Mwandishi picha kapiga Dr. Harith Ghassany na nyuma ni kijiji cha Kipumbwi Tanga |
No comments:
Post a Comment