Salim Ahmed Salim na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 1964 |
Mara baada
ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapo mwaka 1964, Mambo ya Nje ni
moja ya mambo yaliyokubalianwa kuwa yawe ya Muungano, hivyo nafasi kama za
Ubalozi katika Nchi mbalimbali Washirika na Taasisi za Kimataifa ilibidi
zigawanywe kati ya Watanganyika na Wazanzibari ili dhana ya Utanzania ipate
kuonekana dhahiri.
Ni katika
wakati husika ndipo Rais Julius Nyerere, Kama Mkuu wa Nchi na mtu mwenye
Mamlaka ya Uteuzi wa Mabalaozi alipoomba majina ya wale ambao walionekana kuwa
na sifa za kuteuliwa kuwa Mabalozi kutoka Zanzibar kwa Rais Abeid Amani Karume.
Miongoni
mwa majina yaliyoletwa na Sheikh Karume kwa Mwalimu Nyerere ni jina la Kijana
mdogo wa miaka 22 Salim Ahmed Salim, jambo ambalo lilimfanya Mwalimu Nyerere
amuulize mara ya pili Rais Karume juu ya umri wa Kijana huyo, majibu aliyopewa
ni kuwa huyo ni Kijana wa Zanzibar mwenye vigezo na uwezo, apewe nafasi.
Bila hiyana, Mwalimu Nyerere
akamteua Kijana huyo Salim Ahmed Salim kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri
ya Uarabu ya Misri, nafasi ambayo aliitumikia kwa muda wa Mwaka mmoja kati ya
Mwaka 1964 na 1965 kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Nchini India.
Unaweza kudhani kuwa Salim
Ahmed Salim alipewa nafasi husika kwa upendeleo, au kwa kuwa Chama chake cha
Ummah Party kilikuwa na mahusiano ya karibu na Chama cha ASP cha Karume.
Uwezo wa Dkt Salim Ahmed
Salim katika kuieneza Diplomasia ya Tanzania kwa muda wa miaka 50 ya Muungano
wetu unaonyesha dhana ya upendeleo isivyo na mashiko, lakini hata uzoefu na
Ukindakindaki wake wakati akiteuliwa kushika nafasi hiyo pamoja na kuwa alikuwa
na umri mdogo vinaonyesha kuwa aliistahili nafasi hiyo.
Salim
hakuwa mgeni wa Siasa za Zanzibar, alichipukia katika Chama cha Zanzibar
Nationalist Party, ZNP chini ya ulezi wa Komredi mahiri, Profesa Abdulrahman
Mohammed Babu na bega kwa bega naye alishiriki katika kukiasisi Chama cha
Kwanza chenye kufuata Mrengo wa Kijamaa katika Afrika, Chama cha Ummah Party,
Chama ambacho kilishirikiana na Chama cha ASP katika kutekeleza Mapinduzi ya
Zanzibar ya mwaka 1964 yaliyomuingiza madarakani Karume.
Ni Chama hiki cha Ummah Party
ndicho kilichotoa wanamapinduzi Majemedari kama Komredi Ali Sultan Issa, Kanali
Ali Mahfoudh, Komredi Sharifu Ahmed Badawyi Qullatein na wengineo ambao
walikuwa chachu ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kijana mdogo Salim Ahmed Salim
alishirikiana na kulelewa na wote hao, jambo lililompa uzoefu, uwezo na
mafunzo. Mpaka leo rekodi zinamuonyesha Dkt Salim A Salim aliyezaliwa Januari
23, 1942 kuwa ndiye Mtanzania mwenye umri mdogo zaidi kuteuliwa kuwa Balozi wa
Tanzania nje ya Nchi.
Pichani (juu) ni Kijana wa Miaka 17
wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Ndugu Salim Ahmed Salim wa Chama cha ZNP akiwa
pamoja na Rais wa Chama cha TANU, Ndugu Julius Kambarage Nyerere. Picha husika
inaonyesha uzoefu na ushiriki wa Kijana huyu katika Siasa za Ukombozi tangu
akiwa na umri mdogo tu.
No comments:
Post a Comment