Saturday, 27 February 2016

BARUA KUTOKA KWA MSOMAJI WA KITABU CHA ABDULWAHID SYKES




Assalam Alaykum Sheikh Mohamed, 

Miaka saba iliyopita niliwahi kununua kitabu ulichokipa jina ‘’Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes.’’

Kwa wakati ule nilikuwa nimezongwa sana nikakosa utulivu wa kukisoma kitabu kile, bahati mbaya au nzuri akatokea swahib wangu ambaye ni mwanaharakati katika dawaa na khatibu katika misikiti mbali mbali Zanzibar akaniomba nimuazime.

Bila hiyana nilifanya hivyo nikiamini kupitia kwake watafaidika Waislamu wengi zaidi. Nikampa sikuwa nimekisoma kitabu kile.

Ni kama mwezi mmoja uliopita nikaranda katika maduka yanayouzwa vitabu nikijiandaa kwa ajili ya watoto wangu kuanza mwaka mpya katika madarasa mapya,  nikasadifu kukikuta tena kitabu hiki.

Nikakinunua.

Katika wakati Alhamdullilah nimepata wasaa wa kusafiri nacho nikiwa India ndani ya wiki tatu nimeweza kukiosoma mara mbili.

Kwa hakika nimefaidika na mengi, kitabu kimeniwezesha kujibu masuala niliyokuwa nikijiuliza siku zote hasa nilipokuwa chuoni nikifanya BA, Edn (History).

Masuala yaliyokuwa yakinitanza ni harakati za uhuru Tanganyika kabla ya jina la Nyerere kutajwa ziliongozwa na nani ambao hawatajwi tena katika historia ya nchi hii? 

Pili kupitia taarifa tofauti tunajifunza kuwa Waislamu walikuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru, kipi kiliwasibu baadaye mpaka wakapotea. 

Haya yote nimepata majibu vizuri.

Pia wakati nasoma chuoni nilikuwa nikibishana sana na Mwalimu wangu Dr. Mayanja  Kiwanuka leo namkuta humu,  sawa nimeelewa kwanini tulikuwa tukibishana.

Sheikh Mohamed, 
Kitabu kimejaa mafunzo si tu kwa watafiti na wanahistoria lakini zaidi kwa Waislamu wenyewe wa Tanzania.

Kuna sehemu zinahuzunisha sana zimenitoa machozi hasa ninapokutana na aina ya Waislamu kama kina Adam Nasibu.

Inasikitisha kuona namna Waislamu tulivyorahisi kutumika na kumalizana wenyewe kwa wenyewe.

Inasikitisha zaidi kuona kuwa hali ya Waislamu wa leo matokeo yaliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na Waislamu wenyewe.

Sheikh Mohamed, sitaki nikuchoshe kwa maelezo marefu,  kwa ufupi nikupe pongezi zangu za dhati kwa namna unavyojitolea kusimamia UKWELI na UADILIFU katika maandishi yako. 

Nakuombea Mungu akulipe kila la kheir na kwa maandishi yako haya iwe nj sababu ya kukufutia madhambi yako na kukuingiza katika pepo yake. 

Nduguyo katika Uislamu,

Kwasasa nipo India ila mastakimu yangu ni Zanzibar.
Jina langu si geni katika masikio wala macho ya dada hapo (Ahli wako) Mhe Riziki. 

Naomba nisalimie.
Nikutakie kila kheir.

Wakatabah
Issa Kheir Hussein


Wakwanza kulia ni Dk, Mayanja Kiwanuka


Toleo la kwanza kwa Kiingereza 1998

No comments: