Wednesday 17 February 2016

JAMAL YASSIN: NILIKAMATWA, NIKAWEKWA RUMANDE, NIKATESWA NIKISHUTUMIWA GAIDI

Jamal Yassin

Barua ya Uthibitisho Kutoka BAKWATA
Mwandishi akizungumza na Jamal Yassin na Ali Mbaruk Seboy Katibu wa Kamati
ya Maafa Shura ya Maimam Tanzania

Kushoto Mwandishi akizungumza na Jamal Yassin kulia na Ali Mbaruk
''Jina langu ni Jamal Yassin na ni mtu wa Pemba, Ole Kiyanga ambako nilizaliwa mwaka wa 1978. Shughuli zangu za kujiendeshea maisha ni mfanyabiashara wa dagaa ninazotoa Pemba kuzileta Dar es Salaam kwa usafiri wa majahazi. Nimefanya biashara hii kwa karibu miaka mitano sasa. Mwezi Juni 2015 nikiwa natoka kuwatembelea wateja wangu nikirejea nyumbani Kigamboni nilipanda daladala Mbagala Rangi Tatu ambako nilikuwa nimesali sala ya L’Asr. Nilishuka BP Kurasini karibu na daraja na mzunguko wa barabara ya kuelekea Kariakoo na nyingine Posta. Nilikuwa na abiria wenzangu wawili wote akina mama. Tulipokaribia ule mzunguko tukakuta   gari ya polisi Landrover Defender imeegeshwa pale. Mara wakatokea askari wawili wakiwa na silaha na kutuambia kuwa tuko chini ya ulinzi. 

Tukakalishwa chini na palepale askari akanikanyaga began a buti za polisi alizovaa. Nilikuwa nimevaa kanzu na kichwani nimepiga kilemba. Haya ndiyo mavazi yangu ya kawaida siku zote. Hapo tukaanza kuulizwa dini zetu. Wale akina mama mmoja akasema yeye ni Msabato na akaachiwa aendelee na safari yake. Mwenzake akasema yeye ni Muanglikana nay eye pia akaachiwa. Mimi nikasema ni Muislam na kwahakika hapakuwa na haja ya kujitambulisha hivyo mwonekano wangu ulikuwa dhahiri unanitambulisha mimi dini gani. Jibu lililotoka kwa askari ni kuwa, ’’Huyo mwenye ndevu ndiye tunaemtaka. 

Hapo hapo nikaanza kurushwa kichurachura kuvuka barabara huku nikipigwa. Baada ya kuvuka barabara nikafungwa pingu. Hapo nikaingizwa ndani ya gari ile ya polisi hadi Central Police. Nikiwa nje ya jingo nikavuliwa nguo zote nikabaki na chupi. Nikalazwa kifudifudi pembeni ya barabara wakisema wananipekua kuangalia kama nina mabomu. Wakati wakifanya upekuzi wakawa wanakoki silaha na kuulizana kama wanimalize au vipi. Hapo hapo nikamuelekea Allah na kutoa shahada kumpwekesha Mola wangu na kushuhudia kuwa Mtume Muhammad ni Mjumbe Wake. Wale askari wakawa wanaambizana wenyewe kwa wenyewe kuwa, ‘’Hawa Waislam ni magaidi tu tummalize huyu.’’

Akatokea afande mmoja anaitwa Mohamed. Huyu akauliza mbona wale wengine mmewaachia? Mwingine akajibu akasema, ‘’Hawa wenye ndevu si wakuachia hawa wanavunja vituo vya polisi.’’ Kiza kilikuwa kjmeingia nikaingizwa ndani ya jingo la Central Police ilikuwa kama mida ya saa mbili usiku hivi. Wakati nilipokuwa nasulubiwa pale nje ya jingo wapiti njia  wote walikimbia sehemu ile pakawa patupu huoni mtu. Sasa nikafungwa pingu kwa nyuma na nilipofika ndani nikafungwa mnyororo kiunoni na miguuni.  Askari mmoja akaleta ‘’tape measure’’ akawa anapima kanzu yangu hadi ilipoishia na akapima pale ilipoishia kanzu hadi unyayoni. Nikaulizwa kwanini navaa kilemba na kuweka ndevu. Mimi niajibu kuwa hayo ni mafundisho ya dini ya Kiislam kama alivyofundisha kiongozi wetu Muhammad (SAW) yeye katunasihi tujifananishe na yeye. Majibu haya yangu wakawa wanayaandika. Wakaleta kiti wakaniweka kisha wakaniamrisha kunyanyuka na nikaingizwa kwenye chumba kidogo wakafungua maji wakaanza kunimwagia. Maji yale yalikuwa yakitoka katika ‘’pressure’’ kali na ya  baridi na yalikuwa yanawasha.


Askari walikuwa nje ya kichumba hiki wananiangalia. Haya maji yaliniumiza sana. Ngozi yangu ikaanza kuvimba. Haukupita muda nikawa hoi nguvu zimekwisha na akili yangu naihisi inapotea. Wkati wote huu mimi nilikuwa uchi. Walipoacha kunitesa wakaanza kunihoji na wakanambia kuwa nikikubali yale wanayotaka. Wkasema kuwa kuwa kwangu na ndevu na kanzu fupi kwao wao ni kiashiria kuwa mimi Al Qeda. Wakanambia kuwa mimi ndiye niliyeongoza mashambulizi ya Sitakishari. Wakaniuliza zile bunduki nimezipeka wapi? Wakataka niwaeleze nani nilishirikiana nao katika shambulio lile. Wakanambia kuwa mimi  lengo langu  ni kutaka kuweka sheria za  Kiislam Tanzania. Wakambia niwaonyeshe wapi nimezificha wakazichukue. Wakasema kuwa nikiwaeleza wapi silaha zilipo hawatanifanya chochote kwa kuwa rafiki yao. Wakaniahidi kunijengea nyumba Oysterbay na kunipa gari. Nikaanza kuwajibu kuwa sijaiba silaha wala sijavamia kituo chochote cha polisi mahala popote. Hapo wakaanza kunipiga makofi, mateke, ngumi na kunipiga shoti za umeme. Nilipoteza fahamu. Nilipozinduka ilikuwa tayari kumekucha.

In Shaallah itaendelea...


Kushoto: Sheikh Ali Mbaruk na Jamal Yassin

Nilipozinduka ndipo wakanipekeka shimoni. Panaitwa shimoni kwa sababu hizo seli zipo chini ya jengo hilo na hata magari yanapopita nje barabarani unayasikia kwa juu. Hapo shimoni nilikuta Waislam wengi na baadhi yao nikawafamu. Nilimkuta Abubakar ambae tulijuana kwa ajili ya kuwa pamoja katika shughuli za Uislam. Walikuwapo vilevile Kudra Same na Ismail Abubakar. Nilikakaa shimoni nikiuguza majeraha niliyopata mgongoni, ubavuni, miguuni na kifuani kutokana na vipigo nilivyopata. Sikuweza kulala kwa masiku. Baadae nikapelekwa kituo cha polisi cha Shitakishari, Buguruni na Msimbazi pamoja na wenzangu niliowakuta shimoni tukiwa tukihamishwa siku baada ya siku. Baadae tukarudishwa shimoni pale tulipotoka Central Police. Kutoka hapo sasa ndipo tukapelekwa Oyster Bay kwa mahojiano na Task Force ambacho ni kitengo maalum kwa jaili ya ugaidi. Walionihoji hapo Task Force waliniambia kuwa mateso niliyokwishapata huko nilikotoka ni madogo, hapo nitapata mateso makubwa zaidi. Wakanitahadharisha kuwa itabidi nionyeshe silaha ziko wapi kabla hawajanishughulikia zaidi.

Maswali yakawa ni yale yale na nikaanza kupigwa safari hii miguuni baada ya kufungwa katika kitu kama pipa ambacho kinashikilia miguu. Nilipigwa hadi nikawa siwezi kusimama. Adhabu zikawa zinaeendelea maswali ni kuhusu silaha. Majibu yangu yakawa ni yale yale kuwa sihusiki na mambo hayo. Kutoka hapo sasa nikapelekwa Mikese, Morogoro. Wakati napelekwa huko nilikuwa nimefungwa kitambaa cheusi usoni. Hapo Mikese ni sehemu ya wazi hatukuwa ndani ya majengo. Hapo panaitwa ‘’gereji,’’ kwa kuwa hapo ni sehemu makhsusi ya kuwashughulikia Waislam. Hapo nilionyeshwa kaburi na nikaambiwa kuwa katika kaburi lile amezikwa mvaa kanzu fupi, kilemba na mfuga ndevu kama mimi. Nilivuliwa nguo na kuanza kupigwa bakora nyingi sana huku mahojiano yakiendelea na mimi nikiwa uchi. Waliniambia nikiri kuwa mimi ni gaidi. Mimi nilikataa.

Kuna mwenzetu alivunjwa mkono katika mahojiano na baada ya kuvunjwa mkono kwa ajili ya maumivu yale alikiri kuwa yeye ni gaidi. Alinieleza kuwa yeye hakuwa anahusika na yaliyotokea Sitakishari lakini aliambiwa kuwa asipokiri atavunjwa mkono wa pili na baba na mama yake watakamatwa na kuteswa kama alivyoteswa yeye. Kwa ajili ya kuwanusuru waazazi wake aliona bora awakubalie wanalolitaka. Hapa tulikuwa kama watu 18 kisha wakaletwa wanawake watatu. Siwezi kueleza yaliyowafika hawa wanawake. Nilipigwa sindano ambayo kwa kweli sijui ya nini na kuanzia hapo nilipoteza fahamu. Nilipozinduka niliambiwa na walioniokota kuwa walinikuta Mbezi Barabara ya Morogoro na walidhani ni maiti. Hivi sasa mimi ni mgonjwa kwa ajili ya kipigo kile. Natokwa na damu katika sehemu zangu mbili za siri.


Nimewaona mara mbili watesaji wangu mara ya kwanza Msikiti wa Mtambani na mara ya pili Msikiti wa Buguruni. Tulitazamana uso kwa macho na walijua kuwa nimewatambua. Ningeliweza kupiga kelele pale msikitini kuwa hawa hapa watesaji wa Waislam lakini Allah alinielekeza kwenye busara. Laiti ningelifanya vile na kwa kuwa mkasa wangu unafahamika na ndugu zangu Waislam wale askari nina hakika wangeuliwa mle msikitini. Nilijizuia nikabaki kimya nikawa nawaangalia wakitoka nje ya msikiti kwa haraka na kukimbia. Kama ungeliwaona wakiwa katika himaya yao usingeamini kuwa wale walikuwa waoga wanaogopa kukabiliana na Waislam. Sihitaji kulipiza kisasi kwa dhulma niliyofanyiwa mimi na Waislam wengine. Sihitaji kulipiza kisasi ingawa kisasi ni haki yangu. Allah anatosha kwani yeye ni hakimu muadilifu.''

Jamal Yassin akiwa amefuatana na Sheikh Ali Mbaruk ameonana na Mufti wa BAKWATA Sheikh Abubakar Zubeir na kumfahamisha yote aliyoshuhudia wakifanyiwa Waislam mikononi mwa polisi na yaliyomfika yeye kwa ajili ya Uislam. Mufti Zubeir ameahidi kulifikisha suala hili kwenye vyombo husika.

No comments: