Monday, 8 February 2016

MWL. JULIUS K. NYERERE, KANISA KATOLIKI NA UISLAM: DOLA NA TATIZO LA UDINI TANZANIA



Mwalimu Julius K. Nyerere, Kanisa Katoliki na Uislam
Dola na Tatizo la Udini Tanzania
Mohamed Said 
Utangulizi
Baada ya kifo cha Julus Kambarage Nyerere tarehe 14 Oktoba 1999 mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusu msimamo wake na uadilifu kuhusu Uislam Tanzania.
Nia ya kitabu hiki ni kueleza jinsi Mwalimu Nyerere katika kipindi chake cha uongozi  alivyoshughulikia suala la Uislam na Waislam wa Tanzania.
Hii ni historia ya uhusiano wa Mwalimu Nyerere na Waislam kwa kipindi cha takriban robo karne toka pale aliposhika madaraka ya nchi mwaka 1961 hadi alipoachia madaraka mwaka 1985.
Ni mategemeo ya mwandishi kuwa kitabu hiki kidogo kitaweka wazi yale ambayo hayafahamiki kwa wengi.
Mohamed Said
Sura ya Kwanza
Uislam Katika Tanzania
Siasa za Uislam, Kanisa, Dola na Mwafrika Mkristo
Uislam umekuwepo Afrika ya Mashariki toka karne ya nane. Hata hivyo wana-historia wameghitilafiana kuhusu ni lini hasa Uislam uliingia. A.A. Ahmed akinukuu mswada ambao haujachapishwa wa Muhammad B. Sharif Al-Baidh, Stages in East African History, anasema kuwa, ‘Uislam uliingia wakati wa Khalifa ‘Abd al Malik bin Marwan, katika mwaka wa 702/80H. Al-Baidh anasema Uislam uliletwa Afrika ya Mashariki na kundi la Waomani, miongoni mwao wakiwemo waungwana wawili Sa’id na Sulaiman. Sa’id inasemekana alikuja Lamu na Sulaiman alikwenda Mombasa’. [1] Lakini wanahistoria wengi wazalendo wanaamini kuwa Uislam ulifika Afrika ya Mashariki wakati wa uhai wa Bwana Mtume (SAW), hata kabla haja hajiri kwenda Madina. Pamoja na Uislam ikazuka lugha ya Kiswahili, lugha ianyozungumzwa Afrika ya Mashariki na ya Kati na utamaduni wa Kiswahili ambao unanasibishwa na Uislam. Nembo ya Muislam katika Afrika ya Mashariki na Kati ni kuikubali lugha ya Kiswahili kama lugha yake ya asili.
Theluthi mbili ya Waislam wote wa Afrika ya Mashariki wanaishi Tanzania [2] ambayo ndiyo nchi yenye watu wengi kuliko zote katika Afrika ya Mashariki, yaani Kenya, Uganda na Tanzania. Hii ni pamoja na Zanzibar  – nchi ya Kiislam yenye Waislam takriban asilimia tisini na tisa na kuna wakati ilikuwa ndiyo kitovu cha maarifa ya Kiislam katika Afrika ya Mashariki na Kati. Kutokana na sensa ya mwaka 1957, kwa kila Waislam watatu walikuwepo Wakristo wawili. Kwa wakati ule hii ilionyesha kuwa Tanganyika ilikuwa na Waislam wengi katika nchi zote Kusini ya Ikweta. Lakini katika sensa ya kwanza mwaka 1967 baada ya uhuru jumla ya Wakristo Tanzania Bara ilikuwa asilimia thelathini na mbili na Waislam asilimia thelathini na Wapagani asilimia thelathini na saba. Sensa hii inaonyesha kuwa Wapagani ndiyo walio wengi Tanzania. Sensa hii ya mwaka 1967 haikueleza kwa nini katika kipindi cha miaka kumi kwa ghafla Waislam wamepungua nchini au kwa nini ghafla Wapagani wameongozeka katika nchi ya waumini.
Hii ndiyo ilikuwa sensa ya mwisho iliyokuwa ikionyesha mgawanyo wa dini. Inaaminika kuwa matokeo ya sensa hii yalifanyiwa mabadiliko kwa ajili ya sababu za kisiasa pale ilipobainika kuwa Waislam Tanzania walikuwa wengi kupita Wakristo. Upo ushahidi kuwa mwaka 1970, ilipobainika kuwa Waislam ni wengi Tanzania serikali iliiamrisha Idara ya Takwimu kuchoma moto matokeo yote ya sensa ya mwaka 1970.[3] 
Bahati mbaya mgao wa madaraka katika siasa Tanzania umewatupa nje Waislam, ingawa inafahamika kuwa usalama na utulivu wa nchi yeyote unategemea mizani hii kuwa sawa. Vyanzo tofauti vya takwimu vinatoa takwimu tofauti zinazopingana kuhusu hesabu ya Waislam na Wakristo katika Tanzania. Hii inatokana na ukweli kuwa somo hili ni nyeti. Katika nchi za Kiafrika ambazo zina wafuasi wengi wa dini hizi mbili, kwa mfano Tanzania na Nigeria,[4] uchunguzi wa kuwa ni dini gani ina wafuasi wengi kupita mwenzake ni chanzo cha mgongano na mzozo. Tatizo hili lipo Tanzania. D.B. Barret [5] anasema kuwa Waislam Tanzania ni wachache wakilinganishwa na Wakristo. Takwimu zake zinaeleza kuwa Waislam ni 26%, Wakristo 45% na Wapagani ni 28%. Takwimu za Tanzania National Demographic Survey za mwaka wa 1973 zinaonyesha kuwa Waislam ni wengi kidogo kupita Wakristo wakiwa 40%, Wakristo 38.9% na Wapagani 21.1%. Lakini takwimu za Africa South of the Sahara,[6] zinaonyesha Waislam ni wengi Tanzania kwa 60%. Takwimu hizi zimebaki hivyo bila ya mabadiliko toka mwaka 1982. Kwa kuwa utafiti wa Waislam wenyewe katika suala hili ni mdogo sana au haupo kabisa, suala la wingi wa Waislam katika Tanzania halijafanyiwa utafiti na Waislam wenyewe.[7]
Mgao wa madaraka na kugawana vyeo haikupashwa kuwa sababu ya migongano na mifarakano katika Afrika. Lakini kwa bahati mbaya sana hii imekuja kuwa sababu ya mifarakano katika serikali za wananchi wenyewe. Jambo hili limekuwa ni suala nyeti kwa sababu ukabila, udini na kujuana ni kitu muhimu katika serikali za Afrika. Mgawanyo wa madaraka na wingi wa wa wafuasi katika dini au kabila havikuwa vitu vilivyokuwa vikiwashughulisha wananchi wakati wa ukoloni kiasi cha kuleta mifarakano katika jamii. Kwa bahati nzuri ukabila hauna nguvu Tanzania lakini dini imekuwa chanzo cha ubaguzi toka zama za ukoloni, tofauti ni kuwa wakati wa ukoloni waliokuwa wakiwabagua Waislam hawakuwa Wakristo weusi bali Wazungu.
Ukristo ni dini mpya Tanzania kwa kuwa uliingizwa katika karne ya kumi na nane na wamisionari. Kanisa na Mwafrika Mkristo ni matokeo ya ukoloni.  Kwa ajili hii basi historia ya Kanisa katika Afrika ni ile ya kuhirikiana na kuwa tiifu kwa serikali ya kikoloni. Chini ya ukoloni, taratibu Kanisa likaweza kujenga uhusiano maalum kati yake na serikali pamoja na Mkristo Mwafrika ambae imemuelimisha katika shule zake. Mwafrika Mkristo akawa ananufaika na mfumo wa kikoloni. Waislam wakawa wanataabika kwa kuwa dini yao ilikuwa inapingana na dini ya mtawala. Mwafrika Mkristo akawa mnyeyekevu kwa serikali wakati wa ukoloni na baada ya kupatikana kwa uhuru akaja kushika madaraka ya serikali.  Waislam wakatengwa na kuteswa katika ukoloni kwa kubaguliwa na kunyimwa elimu hivyo kuwaondolea fursa ya maendeleo. Kuwepo kwa Waislam kama raia na ili kuinusuru dini yao ilibidi Waislam wasimame kuutokomeza ukoloni. Baada ya uhuru Kanisa likabaki na msimamo wake wa enzi ya ukoloni wa kutii na kujipendekeza kwa serikali mpya iliyokuwa madarakani. Ushirika huu kati ya Kanisa na serikali, uliojengwa na tabia ya Kanisa ya kukubaliana na mfumo wowote wa serikali ulililelewa vyema na umeisaidia sana Kanisa. Kanisa likaweza kujijengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zake bila ya kipingamizi wala wasiwasi. Kutokana na uhusiano huu maalum Kanisa likajifanyia msingi imara wenye nguvu  kutokana wa Wakristo waliowasomesha katika shule zao. Kanisa likatumia nafasi na uhusiano huu kwanza na serikali ya kikoloni kisha na serikali ya wananchi kujijengea himaya ambayo wafuasi wake wakaja kushika nafasi zote muhimu katika uongozi wa juu wa serikali, bunge na mahakama katika Tanzania. Katika miaka yake mia moja tu Kanisa likaweza kupata safu yake ya viongozi ambao wanadhibiti kila sekta katika jamii ya Watanzania.
Waingereza walipoja kuitawala Tanganyika (kama Tanzania inavyojulikana) baada ya kuondoka  Wajerumni baada ya Vita Kuu ya Kwanza, Wajerumani walikuwa wameshafanya kazi ya kutosha ya kuiweka Tanganyika ndani ya mamlaka mbalimbali za Kikristo. Tanganyika ilikuwa imegawanywa katika mamlaka mbalimbali za Kikristo kutoka nchi tofauti za Ulaya. Kanisa Katoliki ambalo ndilo lenye nguvu zaidi, lilikuwa tayari limeshajikita Tanganyika. White Fathers walikuwa wapo Tabora, Karema, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Bukoba; Holy Ghost Fathers walikuwa Morogoro na Kilimanjaro; Benedictine Fathers walikwepo Peramiho na Ndanda; Capuchin Fathers walikuwepo Dar es Salaam; Consolata Fathers walikuwepo Iringa na Meru; Passionist Fathers walikuwa Dodoma; Pallotine Fathers walikuwa Mbulu; Maryknoll Fathers walikuwapo Musoma; na Rosmillian Fathers walikuwa Iringa. [8]
Wamisionari [9]hawa walipotia mguu pwani ya Afrika ya Mashariki, nia yao hasa ilikuwa kuufuta Uislam. Wakazi wa pwani hii iliyokuwa ikijulikana kama Zanj waliuona Ukrsto kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1498 Wareno walipofika sehemu hizo. Mwaka 1567 wamishionari wa Augustinian waliingia Afrika ya Mashariki ili kupambana na Uislam ili Ukristo uwe dini ya dunia nzima. Kadinali Lavigirie alianzisha The White Fathers, taasisi ya Kanisa Katoliki kwa kusudi maalum la kuupiga vita Uislam[10] Wakati huo huo Church Missionary Society (CMS) ilikuwa imjitwisha kazi ya kuondoa ulimwengu kutokana na Uislam, ujinga na giza.[11] Hadi hii leo White Fathers wapo Tanzania wapo Tanzania wakiendelea kufanya kazi iliyowaleta Tanganyika zaidi ya miaka mia iliyopita.
Wajerumani walipofika Tanganyika waliwakuta Waislam wanafahamu kuandika, kusoma na walikuwa wameelimika katika hesabu. Mmishionari Ludwig Krapf alipofika kwa Chifu Kimweri wa Usambaa mwaka 1848 alimkuta yeye na wanae wote wanajua kusoma.[12] Herufi walizokuwa wakitumia zilikuwa za Kiarabu. Wajerumani kwa ajili hii basi waliwaajiri Waislam kama walimu, wakalimani na makarani serikalini. Wamisionari na wakoloni waliona wivu kwa maendeleo haya waliyoyakuta kwa Waislam. Kubwa zaidi ni kuwa walikuwa wamekuja kustaarabisha watu ‘washenzi' badala yake wamewakuta watu walistaaarabika na wanye utamaduni wa kupendeza. Elimu hii yote na utamaduni huu wa hali ya juu ulikuwa unatokana na Uislam na shule zake – madras. Hapo ndipo zilipoaanza mbinu ya kuvunja maendeleo haya yote.
Herufi za Kiarabu zikapigwa marufuku kutumika na badala yake watu wakalazimishwa kujifunza herufi za Kirumi. Muislam ambae jana alipoingia kulala alikuwa anaitwa ameelimika akaamka asubuhi yake mjinga, hana elimu, hajui kusoma wala kuandika. Njama hizi zote dhidi ya Uislam ilikuwa sehemu ya makubaliano kama ilivyoandikwa katika kifungu IV  cha Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884. Kifungu hicho kilikuwa kinasema kuwa Ukristo ni lazima ulindwe dhidi ya Uislam. [13] Kati ya mwaka 1888-1892 katika kutekeleza kifungu hicho kama ilivyokubalika katia Mkutano wa Berlin, Imperial British East Africa Company ilitumia nguvu za kisiasa na kijeshi kuulinda Ukristo katika Afrika ya Mashariki.[14]  Ombwe lililoachwa na elimu ya Kiislam ikajazwa na elimu ya Kanisa chini ya usimamizi wa Waingereza. Kanisa hivi sasa linaeneza uongo na propaganda kuwa lenyewe ndilo lililoweka msingi wa kwanza wa elimu Tanganyika. Ukweli ni kuwa Wamisionari walifuata nyayo za madras na walimu wa kwanza katika shule za misheni walikuwa Waislam ambao hawakusoma katika shule za kanisa bali katika madras.[15] Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mia moja Kanisa likaelekeza nguvu zake katika katika kuwatayarisha raia ambao wengi wao walikuwa Wakristo, watakaokuwa watiifu kwa Kanisa na serikali. Ni katika mtandao huu ndiyo Wakristo wanaimiliki serikali na Chama Cha Mapinduzi na kuiamrisha ifanye linavyopenda Kanisa, wakati Waislam na Uislam ukifanywa kama vitu visivyokuwa na maana yoyote.

Hadi kufikia mwaka wa 1960 Kanisa likawa taasisi kubwa inayomiliki mamilioni ya dola ya misaada inayopokelewa kutoka wahisani na wafadhili walioko katika ulimwengu wa Kikristo. Kanisa sasa hivi linahodhi mahospitali, misururu ya ndege binafsi, viwanja vya ndege, makampuni ya uchapaji na mitambo ya kupiga chapa, stesheni za radio na magazeti. Kanisa limekuwa na nguvu na udhibiti wa mambo kiasi kwamba wakati mwingine watendaji, hasa Wakristo katika serikali na ndani ya chama tawala CCM hawajui utii wao upo kwa nani, serikalini au katika Kanisa?  Ni katika kuchanganyikiwa huku kwa watendaji wa serikali kuhusu uhusiano wao na Kanisa na serikali ndiko kulikoamsha kutoaminiana kati ya Waislam na serikali mara tu baada ya uhuru kupatikana. Serikali ikaonekana kama moja ya taasisi za Kanisa na Waislam wakiwa ni watazamaji tu. Mara baada ya uhuru Kanisa likaangalia nafasi yake na serikali mpya iliyokuwa madarakani. Wakati wa kudai uhuru Kanisa lilijiweka mbali na siasa na ikaonekana kuwa Kanisa lilikuwa likiheshima ule mpaka kati ya dini na siasa. Wakati ule mgongano kati ya Kanisa na serikali haukupata kusikika hata kidogo. Baada ya uhuru kupatikana tu na serikali ikawa mikononi mwa wananchi, Kanisa likaanza kusikika likisema kuwa lina haki na wajibu kuwa na ushawishi ndani ya serikali, kuikosoa serikali na kuingooza pale inapoona serikali haifanyi mambo sawa kwa matarajio yake. Katika msimamo huu mpya, Kanisa likajipa fursa ya kuwa msemaji wa watu. Huu ulikuwa ni mwelekeo mpya katika mambo ya siasa na utawala.
Katika Uislam siasa na dini ni kitu kimoja. Vitu hivi viwili havitenganishwi. Lakini mwaka wa 1955 wakati wa siku za mwanzo kabisa za TANU, tuliona jinsi Waislam katika TANU walivyoweza kukiogoza chama katika misingi ya kisekula na utaifa ili kulinda umoja wa wananchi.. Kutochanganya dini na siasa ikawa moja ya maadili makuu ya TANU. Kuanzia hapa ndipo sasa tunaweza kuelewa mapambano kati ya Waislam kwa upande mmoja na serikali na Wakristo kwa upande wa pili yalivyokuja kugubika Tanzania mara baada ya uhuru.
Uislam: Itikadi ya Kupinga Ukoloni
Uislam siku zote umekuwa kikwazo cha utawala wa kikoloni na kipingamizi kwa mamlaka yoyote ambayo imejaribu kuwakandamiza Waislam. Kwa ajili hii basi, hakuna serikali iliyokuwa madarakani, iwe ya wananchi au ya kikoloni ambayo imepata kuwa na uelewano mwema na Uislam, hivyo basi Waislam wamekuwa daima wakipambana kulinda dini yao na kupigania haki zao.
Ukristo ulipingwa na Waislam tokea mwanzo. Katika kila pambano la silaha dhidi ya ukoloni, Waislam walichukua nafasi hiyo kuwashambulia wamishionari na taasisi zao.[16] Waislam waliwaona wamishionari na wakoloni kama washirika wakishirikiana kupiga vita Uislam na kwa hiyo wote ni maadui. Ukakamavu wa Uislam dhidi ya ukoloni na Ukristo una historia ndefu. Ukristo ukawa kama kibaraka ukijikurubisha na kujinasibisha na ukoloni hata Wakristo kupigana vita pamoja na wakoloni dhidi ya majeshi ya wazalendo. [17] Kuelewa hali ya Uislam wakati ule, unahitaji kusoma barua iliyoandikwa na Chifu Songea bin Ruuf wakati alipokuwa akikusanya nguvu za raia wake dhidi ya majeshi ya Wajerumani na huku akijaribu kupata ushirika wa machifu wengine katika sehemu za kusini ya Tanganyika na ng’ambo ya Mto Ruvuma katika Msumbiji. Barua hii aliyoandikiwa Sheikh, Sultan Mataka bin Hamin Massaninga inasema:
Sultan Songea bin Ruuf anasema: Kwa Sheikh Sultan Mataka bin Hamin Massaninga. Asalaam Aleikum, Ninakuletea barua kupitia Kazembe. Tumepata amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa Wazungu lazima waondoke nchini. Tupo katika kupigananao hapa. Naamini tumeshapatana muda mrefu, (kwa hiyo) niletee wanao, ili tufanye ushirikiano. Nilitaka kukuletea mifugo kama zawadi, lakini sipo katika hali ya kuweza kufanya hivyo, kwa kuwa vita ambavyo Mwenyezi Mungu amevitaka vinaendelea. Niletee watumiaji bunduki mia moja, na niunge mkono katika kulivamia Boma (Songea).
Ninakuletea chupa ya Mtume Muhammad, ambayo ndani yake ipo nguvu ya kuwashinda Wazungu. Usiwe na shaka nayo, ina uwezo mkubwa. Tutakapoliteka Boma (Songea), tutakwenda kwenye vituo katika Nyasa pamoja, mimi na wewe. Hivi sasa tusahau ugomvi wetu wa zamani.
Chupa hii, na da’wa, imeletwa na Chinyalanyala mwenyewe, kiongozi wa vita. Ameleta vilevile kombe, na anakupa salamu nyingi.
Endapo watu wako watakuja, Chinyalanyala mwenyewe atafika na atakupa vitu vingi vilivyo vitukufu.
Hassan bin Isma’il anakusalimu.
Salam nyingi,
Sultan Songea bin Ruuf. [18]
Kitu cha kuangalia katika barua hii, nzuri kama ilivyo, ni kuwa inatiliwa shaka na Becker, ambae msimamo wake ni kuwa chanzo cha barua hiyo ni cha kutatanisha.
Mkutano wa Kwanza wa Waislam, 1962
Baada ya uhuru kupatikana mwaka 1961 Waislam waliamini kuwa hali yao ya baadae katika serikali huru itakuwa nzuri. Mwaka 1962 ukaitishwa mkutano wa Waislam wa nchi nzima kujadili nafasi ya Uislam katika Tanganyika huru. Taasisi zifuatazo zilihudhuria mkutano huo: East African Muslim Welfare Society (EAMWS), Daawat Islamiyya, Jamiatul Islamiya fi Tanganyika, Jamiatul Islamuyya ‘A’[19] na Muslim Education Union. Mkutano ule ulikubaliana pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuanzisha idara ya elimu chini ya EAMWS. Waislam hawakusubiri serikali itimize ahadi yake ya kurekebisha upogo uliokuwepo wa elimu kati ya Waislam na Waislam. Waislam walianzisha mipango yao wenyewe ili isaidiane na juhudi ya serikali. Mipango ikatayarishwa ya kujenga shule Tanganyika nzima na mwishowe kujenga Chuo Kikuu cha kwanza kwa Waislam katika Afrika ya Mashariki. Mkutano ukamchagua Tewa Said Tewa waziri wa serikali, mwanasiasa wa TAA na mmoja wa wale wazalendo kumi na saba walioanzisha TANU kuwa mwenyekiti wa EAMWS kwa upande wa Tanganyika.
Huu ndiyo ukawa mwanzo wa uadui kati ya Waislam na serikali ambayo ilikuwa mikononi mwa Wakristo. Uelewano uliodumu wakati wa kudai uhuru ukaanza kutoweka na siasa zikachukua sura mpya ya uhasama, kutoaminiana na kutafutana kati ya jamii hizi mbili. Kisa cha hali hii mpya ikiwa ni sababu ya Waislam kutaka kuondoa hali ya kikoloni iliyowakandamiza kwa miaka mingi. Waislam waliona kuwa hili lilikuwa ni jambo lisilokuwa na pingamizi kufanyika. Uhuru ili uwe na maana ni lazima Waislam wajitoe ndani ya unyonge waliogubikwa na wakoloni. Kwa upande wa Wakristo hali hii ilisababisha hofu kuu nyoyoni mwao.
Pingamizi Katika Kuleta Mabadiliko Yatakayonufaisha Waislam na Uislam
Uhuru ulipopatikana kulikuwa na makundi makubwa mawili yaliyokuwa yanatawala siasa Tanganyika. Kwanza kulikuwa na Waislam ambao tegemeo lao kubwa lilikuwa kuona ile hali yao ya unyonge iliyodumu kipindi chote cha ukoloni ikitoweka. Nguvu ya pili ilikuwa vyama vya wafanyakazi. Makundi haya yote yalikuwa na mategemeo makubwa kwa serikali ya TANU kuwa itawapa haki zao bila ya matatizo yoyote. Pamoja na makundi haya palikuwapo na vyama vya upinzani, AMNUT na Congress [20] ambavyo kwa kweli havikuwa na nguvu yoyote ya kuweza kupambana na TANU. Miezi michache kabla ya uhuru, Nyerere alitoa onyo ambalo dhahiri lilikuwa limeelekezwa kwa makundi haya. Mwezi Mei, 1961 Nyerere alionya kuwa hatosita kuwaweka kizuizini viongozi wa vyama vya wafanyakazi, viongozi wa dini na wengineo endapo watakuwa tishio kwa serikali yake. [21] Hapa ieleweke wazi kuwa viongozi wa dini aliowakusudia Nyerere kuwaweka kizuizini hawakuwa viongozi wa kanisa, bali masheikh[22]. Hawakuwa viongozi wa kanisa kwa kuwa mpaka uhuru unapatikana makanisa yalikuwa yamejitenga na siasa kwa ukamilifu. Huenda Nyerere alitoa onyo hilo kutokana na shutuma alizotoa mpinzani wake rais wa Congress, Zuberi Mtemvu. Akiwahutubia wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Karl Marx mjini Leipzig, Ujerumani ya Mashariki, Mtemvu alibashiri kuwa kutolewa kwa uhuru wa Tanganyika kwa uongozi wa TANU, hautabadili chochote kwa kuwa wanaoingia madarakani wameamua kushirikiana na walewale wanyonyaji wa zamani na hii itavunja nguvu za wazalendo na matumaini yao. [23]
Haiwezekani kuielewa ahadi ya Nyerere katika haki na usawa kwa raia wote kama alivyoahidi wakati wa kudai uhuru, hadi usome hotuba yake aliyoitoa tarehe 10 Desemba, 1962 katika Bunge wakati Tanganyika inakua jamuhuri. Hotuba ya Nyerere ilijikita kwenye matatizo ya upogo kati ya Waislam na Wakristo. Nyerere alifanya hivi labda akijua kuwa ingawa yeye alikuwa Rais Mkatoliki lakini waliomuweka madarakani kuitawala Tanganyika walikuwa Waislam. Nyerere alikuwa na haya ya kusema:
Hakuna njia nyepesi ya kuondoa tafauti baina ya raia wetu Waafrika na wasio Waafrika; hakuna njia nyepesi ya kuondoa tofauti za elimu kati ya Wakristo na Waislam, au baina ya wachache wenye elimu na wengi wa watu wetu wasio kuwa na elimu; hakuna njia nyepesi ambayo Wamasai na Wagogo wanaweza wakalingana na Wahaya na Wachagga na Wanyakyusa.[24]
Hii ilikuwa kauli ya serikali ya kudhihirisha nia yake njema. Kauli hii ilikuwa ya kuwapa matumaini na kuwahakikishia Waislam na wale wote walioathirika na dhulma ya wakoloni, kuwa serikali ilikuwa inatambua shida zao na itachukua hatua zifaazo kurekebisha hali hiyo. Wakati Nyerere anatoa kauli hii ya kutia moyo, serikali iliyokuwa imejaa viongozi wa Kikristo na taasisi za Kikristo zilikuwa imejaa hofu wakiogopa harakati za Waislam za kujiletea maendeleo zilizokuwa zinatapakaa nchi nzima kwa kasi. Walifahamu fika nguvu na umoja wa Waislam ukitumiwa vyema hapana shaka Waislam watakuja juu. Kwa viongozi wa Kikristo waliokuwa wameshika madaraka ya serikali hii ilimaananisha kugawana madaraka sawa na Waislam, kwao wao harakati hizi mpya ziliashiria kuanguka kwa himaya yao katika madaraka kama viongozi.
Hii ilionekana kama harakati za pili za Waislam, safari hii kuchukua serikali kutoka kwa Wakristo. Harakati za kwanza zilikuwa zile za kumng’oa Mwingereza katika ardhi ya Tanganyika. Bila ya kutegemea, serikali ikajikuta inakabiliana ana kwa ana na na jumuiya ya Kiislam iliyokuwa na nguvu ambayo kwa dhahiri yake kila Muislam alikuwa ni mwanachama, na ndani yake imejumuisha wana-TANU shupavu pamoja na wapinzani wa TANU. Wakati huo huo Baraza la Wazee wa TANU katika nafasi yake ya ushauri likawa linaishinikiza serikali ifanye mabadiliko haraka kutokomeza mabaki ya ukoloni. Serikali ikaona harakati hizi ni sawasawa na kuendesha nchi katika misingi ya Uislam. Baraza la Wazee wa TANU lilikuwa sasa limejigeuza kutoka kundi dogo la wazalendo na kuwa kundi lililokuwa likishinikiza serikali ndani ya TANU. Serikali ilikuwa ama ikubali matakwa ya Waislam au ikatae na ipambane na upinzani kutoka kwao. Kuanzia hapa mambo yakaanza kwenda kwa kasi ya kushangaza.

Tarehe 11 Machi, 1963, Kamati Kuu ya TANU iliyokutana Dar es Salaam ilipiga kura kuvunja kamati ya wajumbe kumi na moja ya Baraza la Wazee wa TANU chini ya Mwenyekiti wake Idd Tulio. Wazee walikusanyika katika ukumbi wa Arnautoglo na wakasomewa uamuzi wa Kamati Kuu ya kulivunja Baraza la Wazee. Taarifa ilisema wazee hao ni kero kwa sababu ‘dini na siasa vilikuwa vitu viwili tofauti na hawa wazee walikuwa wanachanganya dini na siasa.’ [25] Hiki kilikuwa chombo cha ushauri ambacho wajumbe wake wote walikuwa Waislam; chombo kilichokuwa ndani ya TANU ambacho kilimuunga mkono Nyerere na TANU tangu siku za mwanzo kabisa, kwanza chini ya uongozi wa Sheikh Suleiman Takadir na kisha chini ya Idd Tulio baada ya kufukuzwa kwa Sheikh Takadir kutoka TANU. Wakati haya yote yakitendeka Kanisa ambalo wakati wa kudai uhuru lilijiweka mbali na halikutoa msaada wowote sasa likawa linanyemelea kujiingiza katika siasa likiwa na agenda yake: kuwaweka viongozi Wakristo katika nafasi za uongozi na kuutoa nje ya uongozi Waislam ambao Kanisa liliwaona hawana elimu.[26] Jumuiya za Kiislam kama Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na EAMWS zilikuwa sasa zinapigwa vita na serikali ya Nyerere kama vyombo ambavyo havikuwa na umuhimu wowote katika Tanganyika mpya. Katika kumuhakikishia utiifu wao juu yake, Waislam walijitahidi mwisho wa uwezo wao kuziweka taasisi zao kando na chuki za kidini dhidi ya Wakristo. [27] Juhudi hizi hazikuthaminiwa. Serikali ilifanya juhudi za siri kuhakikisha kuwa jumuiya zote za Waislam zinapigwa marufuku. [28]
Huu ndiyo ukawa mwanzo wa kampeni za kufuta historia ya Uislam katika TANU na mwisho wa Waislam kuwa na sauti katika siasa baada ya uhuru kupatikana. Baada ya kupatikana kwa uhuru, ile nguvu ya Waislam iliyotumika kupambana na Waingereza kuleta uhuru, ikaonekana haina maana yoyote na haifai kitu tena. Kuvunjwa kwa Baraza la Wazee ndiyo ilikuwa kishiko cha mwisho cha Waislam katika TANU. Baada ya hapo Kanisa lililokuwa pembeni wakati wa kudai uhuru sasa likajitokeza waziwazi kuwapiga vita Waislam katika TANU. Katika kitendo ambacho kanisa halikupata kufanya, Kanisa Katoliki Bukoba liliteua wagombea wake wenyewe wapambane wa wagombea Waislam walioteuliwa na TANU kugombea nafasi katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Kanisa lilisema limeweka wagombea wake binafsi kwa kuwa wana elimu kupita wagombea wa TANU Waislam. Kampeni kama hii ilifanyika vilevile Kigoma. Hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa Nyerere, serikali au TANU yenyewe ilichukua hatua zozote dhidi ya Kanisa kwa kuchanganya ‘dini na siasa’.
Mkutano wa Pili wa Waislam, 1963
Ulipoitishwa Mkutano wa Pili wa Waislam Dar es Salaam matatizo haya mazito yaliwekwa kwenye agenda ili yajadiliwe. Mkutano ule ulithibitisha bila wasiwasi wowote kuwa kulikuwapo na njama za sirisiri ndani ya TANU kuhujumu Waislam na njama hizi zikienda sambamba nchi nzima na kampeni dhidi ya Waislam na viongozi wa EAMWS.[29] Nyerere alialikwa kufunga mkutano ule na Waislam wakamueleza masikitiko yao kwa hali ile iliyojitokeza. Nyerere alizungumza kwa kirefu matatizo ya Waislam na kwa kiasi aliweza kutuliza mambo. Lakini kulikuwa hapana shaka katika fikra za viongozi wa EAMWS kuwa kulikuwa na njama zilizopangwa na Kanisa mahsusi kwa minajili ya kupiga vita Uislam na Waislam, uongozi wa Wakristo katika TANU, serikali na Nyerere binafsi akitumika kufanikisha azma hiyo. Uongozi wa Kikristo katika taasisi za umma sasa ukawa unatumia nguvu za dola kulipa Kanisa madaraka ili liweze kudhibiti serikali na TANU.
Tarehe 20 Januari, 1964 kulitokea maasi katika Tanganyika Rifles. Nyerere alirudishwa madarakani na jeshi la Waingereza lililoletwa kumaliza maasi.[30] Baada ya mambo kutulia Nyerere akachukua nafasi hiyo kuwaweka kizuizini viongozi wa vyama vya wafanyakazi na masheikh maarufu katika Tanganyika. Kesi ya uhaini wa wanajeshi ilipofikishwa Mahakama Kuu hapakuwa na ushahidi wowote ule kuwa masheikh walihusika kwa njia moja au nyingine katika uasi wa Tanganyika Rifles. Uvumi uliokumba mji wa Dar es salaam ni kuwa masheikh hao walikuwa wanapanga njama za kupindua serikali. Shutuma hii kwa masheikh kwa hakika ilikuwa ni kiroja. Baada ya hapo, mwanazuoni maarufu, Sharif Hussein Badawiy na mdogo wake Mwinyibaba, walipewa notisi ya kuondoka nchini kama wahamiaji wasiotakiwa. Kilichofanya Shariff Badawiy afukuzwe nchini ni kauli aliyotoa Mwinyibaba katika maulid. Akiwahutubia Waislam katika maulid yale, Sheikh Abdallah Chaurembo alisema kuwa Waislam wanapashwa kuishukuru serikali kwa kutoa ruhusa kwa Waislam kuondooka kazini mapema siku ya Ijumaa ili wapate fursa ya kuswali swala ya Ijumaa. Ilikuwa ni kauli ya kawaida tu, lakini kwa kuwa wakati ule tayari palikuwa na upasi kati ya Waislam na serikali baadhi ya Waislam waliokuwapo pale waliona kama kwamba Sheikh Chaurembo alikuwa akijikomba kwa serikali ili apate umaarufu wa bure na kwa ajili hiyo afaidike kisiasa. Iliamuliwa kuwa Waislam lazima waijibu hotuba ya Sheikh Chaurembo usiku ule ule bila ya kungoja.
Mwinyibaba akisukumwa zaidi na hamasa za ujana, alipanda kwenye membar ile ile ambayo muda mfupi uliopita Sheikh Chaurembo alihutubu. Mwinyibaba aliwaeleza Waislam kuwa wao hawahitaji kumshukuru yeyote kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, vyovyote iwavyo sala ya Ijumaa ni fardh inayomuwajibikia kila Muislam na hana khiyari ila kuitekeleza, serikali iwe imetoa ruhusa au vinginevyo. Sheikh Abdallah Chaurembo alikuwa hapo mwanzoni mwanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir na alikuwa chini ya Sheikh Hassan hadi ilipotokea mtafaruku baina yake na mwalimu wake mwaka 1961. Chanzo cha mtafaruku ilikuwa ni kuhusu mambo ya akida katika siasa za TANU. Kwa ajili hii ikabidi Sheikh Chaurembo ajiondoe kwa sheikh na akajihusisha katika siasa hadi akachaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU. Jibu kama lile alilotoa Mwinyibaba likaonekana kama ni kuonyesha fedhuli kwa serikali na TANU. Siku ya pili yake serikali ikatoa amri Shariff Hussein afukuzwe nchini pamoja na mdogo wake Mwinyibaba ingawa yeye Shariff Hussein hakuwepo hata kwenye hafla ile ya maulid kwa kuwa alikuwa nje ya Dar es salaam.[31] Shariff Hussein na Mwinyibaba ikabidi waondoke na kurudi kwao Kenya. Lakini ili ieleweke sababu ya kutiwa kizuizini hawa masheikh inabidi turudi nyuma katika mkutano wa mwaka wa EAMWS ukiofanyika mwaka 1963.
Jaribio la mwanzo la Nyerere kutaka kuivunja EAMWS lilikuwa mwaka 1963. Lakini jaribio hilo halikufanikiwa kwa sababu ya mpango uliopangwa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir na kutekelezwa na Bilali Rehani Waikela, katibu wa EAMWS Tabora. Mwaka huu wa 1963 EAMWS ilifanya mkutano wake katika ukumbi wa Shule ya wasichana ya Aga Khan. Wajumbe wa mkutano huo walipowasili mjini Dar es Salaam walikuta uvumi kuwa wajumbe wa mkutano wa EAMWS watakamatwa na kuwekwa kizuizini. Chanzo cha uvumi huu hakikufahamika lakini haikuwa vigumu kuhisi. Baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka ule ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa amewatupa mkono washirika wake wa zamani na sasa alikuwa akitafuta wapya ili kujenga upya msingi wake wa siasa. Kutokana na mambo yalivyokuwa yakienda ilikuwa ni dhahiri washirika wake wapya hawatakuwa Waislam.
Katibu wa EAMWS Tabora, Waikela alipowasili Dar es Salaam kuhudhuria mkutano aliitwa na Sheikh Hassan bin Amir. Mufti Sheikh Hassan bin Amir mbele ya Mzee Ali Comorian, alimfahamisha Waikela kuwa kulikuwa na njama zilizokuwa zikipikwa na Nyerere kumuungamiza yeye na Tewa Said Tewa ili kuvunja EAMWS ipatikane nafasi ya kuanzishwa jumuiya ya Kiislam ya Watanganyika itakayokuwa chini ya wanafiki. Sheikh Hassan bin Amir alimwambia Waikela kuwa harakati za uhuru zilikuwa zinatekwa nyara na Wakristo kwa manufaa ya makanisa yao. Sheikh Hassan alimfahamisha Waikela kuwa ni lazima yeye afanye kila linalowezekana ili njama za Nyerere zishindwe. Waikela alimuuliza Sheikh Hassan bin Amir kwa nini amechaguliwa yeye kufanya kazi ile. Sheikh Hassan bin Amir alimuambia kuwa yeye ana imani na uwezo wake. Baada ya maneno hayo Sheikh Hassan bin Amir alinyanyua mikono yake juu na kumuombea dua Waikela. Nyerere alikuwa anamfahamu Waikela  kwa kuwa alikuwa muasisi wa TANU na alikuwa ametoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru.
Nchi nzima hasa sehemu za Waislam kulikuwa mpango wa serikali wa kuwavunja Waislam nguvu na kuwakatisha tamaa. Waikela, kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wa EAMWS alikuwa anasuguana na Mkuu wa Mkoa wa Jimbo la Magharibi, Richard Wambura. Kulikuwa na ujeuri kwa upande wa serikali walipokuwa wanashugulikia matatizo ya Waislam, mbali na mategemeo ya Waislam waliyokuwanayo kabla ya uhuru. Subira ya Waikela ilifikia kikomo pale Wambura alipowatukana Waislam katika mkutano wa hadhara. Baada ya kuhutubia Wambura, Waikela alipanda jukwaani na akaikumbusha serikali isiwe mwizi wa fadhila kwa kusahau jinsi Waislam walivyojitolea muhanga katika kudai uhuru. Serikali ikachukulia hotuba ya Waikela kama usaliti na yenye kuwashawishi Waislam wasiitii serikali. Ilikuwa katika hali hii Waikela mwanachama shupavu wa TANU alijitoa kwenye chama na akaamua kutumia nguvu zake kuwatumikia Waislam kupitia EAMWS. Ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa na habari za msuguano kati ya serikali na Waislam kule Tabora na mtu ambae alikuwa akihusika na msuguano huo.
Siku kabla ya mkutano wa EAMWS, Nyerere aliwaalika wajumbe wa mkutano Government House kwa chakula cha usiku. Hao waalikwa walikuwa wajumbe waliochaguliwa mahsusi. Waikela hakuwa mmoja wa hao waalikwa. Nyerere alichukua nafasi ile kuwashauri wajumbe wale waanzishe jumuiya ya Waislam wa Tanganyika ichukue nafasi ya EAMWS. Wajumbe hawa walipoleta katika mkutano hoja ya kuanzisha jumuiya ya Waislam wa Tanganyika, Waikela alisimama na kuipinga hoja ile. Alizungumza vilevile kuhusu uadui wa serikali kwa Waislam na Uislam. Waikela alimaliza hotuba yake kwa kutoa changamoto kwa wajumbe wamuite Nyerere kwenye ufunguzi wa  mkutano ili aje awaeleze wajumbe msimamo wake kuhusu kadhia hii ya chinichini baina ya serikali na Waislam.
Baada ya kushindwa kwa hoja ya kuivunja EAMWS wajumbe wa mkutano ikaonekana kuwa ingekuwa vyema Nyerere aitwe kufunga mkutano ule na asomewe makubaliano yaliyofikiwa. Nyerere alifika kufunga ule mkutano na akakutana uso kwa uso na Waikela, ambae alimsomea maazimio ya mkutano. Waikela alimfahamisha Nyerere kuwa umoja kwa Waislam ni fardh – wajibu wa lazima. Ni kwenda kinyume na maamrisho ya Allah kuwagawa watu. Baada ya utangulizi huu Waikela huku akimnyooshea Nyerere kidole alieleza uadui unaoonyeshwa na serikali dhidi ya Waislam. Waikela alimaliza hotuba yake kwa kitisho. Alimwambia Nyerere ikiwa Waislam watamgeuka kupambanana yeye hatakuwa na uwezo wa kuwashinda. Nyerere alitulia tuli pembeni mwa Rais wa Baraza la Tanganyika la EAMWS Tewa Said Tewa akimsikiliza Waikela. Aliposimama kujibu hotuba ya Waikela Nyerere kwa upole alisisitiza msimamo wa serikali wa kutoa haki na usawa kwa raia wake wote. Kwa kiasi fulani Nyerere alikuwa amefanikiwa kupunguza joto kati ya Waislam na serikali. Hotuba ya Waikela na ya Nyerere zikapewa umuhimu mkubwa katika radio. Waislam wengi wakajitokeza stesheni ya gari moshi Tabora kuja kumpokea shujaa Waikela. Alipewa heshima ile kwa kuwa na ujasiri wa kuweza kusimama kidete dhidi ya wale waliodhani kuwa wanaweza kuwakalia Waislam vichwani. Nyerere alihisi ameumbuka na hili lilimchoma moyo sana. Kuanzia hapa Nyerere hakumtazama Sheikh Hassan bin Amir kwa jicho jema. Alingoja nafasi yake ili alipize kisasi. Mwaka ukiofuata, tarehe 20 Januari, 1964 jeshi liliasi. Nyerere alichukua fursa ile kuwatia kizuizini masheikh walioonekana wanapinga serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi. Waikela alikuwa mmoja wa wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. [32] Nyerere kwa wakati ule hakuwa na nguvu ya kumgusa Mufti Sheikh Hassan bin Amir.
Wakati ule mwaka wa 1963 shughuli za kueneza dini za EAMWS zilikuwa zikienda vizuri sana. Tabligh ilikuwa chini ya Sheikh Amir bin Juma kutoka Tanga na Wakristo wengi walikuwa wakirudi katika Uislam. [33] Tabligh ilikuwa ikiongozwa kutoka kwa masheikh wa mikoa na wilaya. Fedha za kufanyia shughuli hizi zilikuwa zikichangwa na Waislam wenyewe. Mufti Sheikh Hassan Bin Amir yeye alikuwa akisomesha fikh, mantik, tauhid, na tafsir ya Qur’an katika misikiti mbalimbali ya Dar es Salaam Wakati ule Katibu Mkuu wa EAMWS kwa Afrika ya Mashariki alikuwa V.M. Nazarali.
Juhudi za Kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiislam Chini ya EAMWS, 1964
Mwezi Aprili 1964 ujumbe wa hali ya juu wa EAMWS ndani yake wakiwemo Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Said Omari Abdallah, Tewa Said Tewa, Katibu wa EAMWS Abdul-Aziz Khaki na mzee wa TANU Mzee Mwinjuma Mwinyikambi; Makisi Mbwana, Issa Mtambo, Omari Muhaji na Saleh Masasi waliondoka kwenda ziara ya nchi za Kiislam kutafuta msaada wa kujenga Chuo Kikuu cha Kiislam na kuanzisha uhusiano na nchi za Kiislam. Gamal Abdel Nasser alifurahishwa sana na ujumbe wa Tanganyika kiasi kwamba ingawa alikuwa katika matayarisho ya mapokezi ya Waziri Mkuu wa Urusi Kruschev, na ingawa ujumbe wa EAMWS ulikuwa wa kidini zaidi kuliko wa kiserikali, alikutana na ujumbe ule akaupatia ofisi, huduma za simu, na makatibu muhtasi ili waweze kutayarisha mipango yao kwa serikali ya Misri bila shida. Halikadhalika alimuagiza makamu wake Sharbasy afanye makubaliano na EAMWS kwa niaba yake.
Serikali ya Misri ilikubali kugharamia ujenzi wa chuo hicho. Mkataba wa makubaliano ukatiwa sahihi mjini Cairo kati ya Tewa Said Tewa kwa niaba ya EAMWS na Makamu wa Rais wa Misri, Sharbasy kwa niaba ya serikali yake. Serikali ya Misri iliahidi kujenga Chuo Kikuu cha Kiislam ambacho kitamilikiwa na kuendeshwa na EAMWS. Gharama ya mradi mzima uliuwa pauni milioni hamsini na tano za Ki-Misri. Baada ya kukamilisha kazi ile ujumbe ule uliondoka Cairo kuelekea Makka kufanya ibada ya hija. Baada ya kumaliza hija wajumbe wanne walirudi nyumbani na Tewa, Aziz Khaki, Sayyid Omar Abdallah wakaendelea na safari kwenda Aman, Jordan ambako walifanya mazungumzo na Mufti na Waziri wa Aukaf. Kutokea hapo ujumbe ulikwenda  Kuwait ambako walikutana  na Sheikh wa Kuwait kisha wakaenda Bhaghdad, Iraq na kukutana na rais wake, Abdisalama Arifek. Kutoka hapo ujumbe ulielekea Beirut, Lebabon ambako ulifanya mazungumzo na viongozi wa harakati za Kiislam. Baada ya kutoka Beirut ujumbe ule ulirudi tena Cairo kwa ajili ya kukamilisha makubaliano ya kujenga Chuo Kikuu. Tarehe 20 Mei, 1964 ujumbe ulirejea Dar es Salaam na kupokelewa na viongozi wa EAMWS na Waislam kwa ujumla. Mkutano wa Halmashauri Kuu ya EAMWS ukaitishwa na Tewa Said Tewa akatoa taarifa yake kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu Cha Kiislam. Siku ya pili Tewa akaitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutoa habari za kufurahisha za kujengwa kwa Chuo Kikuu Cha Kiislam kwa vyombo vya habari na kwa Waislam kwa ujumla.[34] Kwa mafanikio haya Tewa akawa amejichimbia kaburi. Matokea haya yalijaza hofu kwa viongozi wa Kanisa. Kampeni za chinichini dhidi ya Tewa binafsi na uongozi mzima wa EAMWS zilianza.
Mara baada ya ujumbe wa EAMWS kurudi kutoka ziara yake, Nyerere alifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na Tewa Said Tewa, Mwenyekiti wa EAMWS upande wa Tanzania akajikuta nje ya serikali. Nyerere akamteua Tewa balozi wa Tanzania katika Jamuhuri ya Watu wa China. Mwezi Januari, 1965 Tewa alikwenda China kuanza kazi yake mpya. Inasemekana uteuzi wa wa Tewa kwenda China ulisababishwa na juhudi zake za kutaka kuwaunganisha Waislam kuwa kitu kimoja chini ya jumuiya moja yenye nguvu. Wakati ule ile mipango iliyopitishwa na mkutano wa Waislam mwaka 1962 ilikuwa ikitekelezwa vyema, shule zilikuwa zimejengwa Ilala, Kigogo na Kurasini, Dar es Salaam; shule zilikuwa zimejengwa Ruvu na Maneromango. Shule hii ya Maneromango ilikuwa na umuhimu wa pekee kwa sababu hii ndiyo ilikuwa shule ya kwanza ya Waislam kujengwa Uzaramo. Shule za upili zilikuwa zikijengwa Dar es Salaam, Kinondoni na Moshi, Kibohehe. EAMWS ilikuwa vilevile imetiliana mkataba wa makubaliano na serikali ya Misri kuipa scholarship thelathini na tano kila mwaka kwa wanafunzi wa Kiislam kusoma Misri. EAMWS ilikuwa imejenga shule, misikiti, shule za ufundi na hosteli kwa ajili ya wanafunzi katika sehemu nyingi za Afrika ya Mashariki. Kwa hakika EAMWS ilikuwa ikifanya mambo ya maendeleo kwa Waislam.


Uganda
Tanzania
Kenya
Shule
77
70
28
Misikiti
67
53
29
Shule za Ufundi
3
-
-
Hosteli
1
-
-
Chanzo: Utafiti
Baada ya Tewa kuondoka Bibi Titi Mohamed akachaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa tawi la EAMWS la Tanzania ili kuongeza nguvu makao makuu kwa kuwa mwenyekiti hakuwepo. Kutokuwepo kwa Tewa nchini kulileta ombwe ambalo ilibidi lijazwe. Ghafla palizuka uvumi kuwa Sheikh Abdallah Chaurembo alikuwa achukue uongozi wa EAMWS. Inasemekana nia yake ilikuwa ni kwanza kupata urais wa EAMWS na kisha achaguliwe kuwa Mufti wa Tanzania. [35] Uvumi huu ulidumu kwa karibu mwaka mzima hadi pale Tewa aliporudi kutoka Peking baada ya kujiuzulu ubalozi kuja kugombea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965. Aliporudi Tewa alihojiwa na waandishi wa habari kuhusu uvumi ule na yeye jibu lake lilikuwa kuwa Muislam yeyote mwenye sifa ya maadili mema ana haki ya kugombea nafasi yoyote katika uongozi wa EAMWS. Neno alilolitumia Tewa katika kumueleza mtu ambaye angeweza kuwaongoza Waislam lilikuwa takwa, neno zito la Kiarabu kueleza mtu mcha-mungu.
Nikuanzia katika matukio haya ndipo tunaweza sasa kuanza kuchunguza jinsi Nyerere akiitumia serikali livyoanza kuuhujumu umoja wa Waislam kwa kutumia njama, hujuma za dhahiri na za kificho, magendo na kueneza uongo dhidi ya uongozi wa EAMWS, ambao ulionekana ni tishio kwa utawala wake. Wakati ule serikali nzima ilikuwa mikononi mwa Wakristo. Ukiwatoa Wazanzibari walioikuwa katika serikali ya muungano – A.M. Maalim, Waziri wa Biashara na Viwanda; Aboud Jumbe, Waziri Nchi; A.M. Babu, Waziri wa Ardhi, Makazi na Maji; Hasnu Makame, Waziri wa Habari na Utalii; Rashid Kawawa ambae alikuwa mtu wa karibu sana na  Nyerere, waziri Muislam katika baraza la mawaziri kumi na tano alikuwa Said Ali Maswanya, Waziri wa Mambo ya Ndani. Hali kama hii ya Wakristo kushika nyadhifa takriban zote za serikali ilikuja vipi? Jibu la swali hili linapatikana katika historia ya Tanganyika wakati wamisionari wa kwanza walipowasili nchini kuja ‘kulistaarabisha bara jeusi’ na halikadhalika katika historia ya TANU .











Sura ya Pili
‘Mgogoro’ wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) wa Mwaka wa 1968 [36]
Uchochezi wa ‘Mgogoro’ wa BAKWATA
Kutokana na katiba ya mwaka wa 1957 lengo kuu la EAMWS ilikuwa ni ‘kuutangaza Uislam katika Afrika ya Mashariki’. EAMWS yenyewe ilikuwa ikijigamba kuwa uti wake wa mgongo ilikuwa ni tabligh, yaani utangazaji wa dini. [37] Jumuiya hii iliyoanzishwa mwaka 1933 ilikuwa ya Waislam wa mataifa yote katika uanachama na katika uongozi wake. Katika uhai wake wa miaka thelathini na tano EAMWS ilijiweka mbali sana na siasa. Jumuiya hii ilishughulikia kuutetea na kuueneza Uislam katika Afrika ya Mashariki. Lakini baada ya kutokea maasi ya Tanganyika Rifles mwaka 1964 yaliyopelekea viongozi wengi wa Kiislam kuwekwa kizuizini, EAMWS ikawa imepoteza mwelekeo wake na kudhoofika. Baadhi ya matawi yaliyokuwa katika majimbo yakafungwa kwa woga na kukosa viongozi thabiti na kwa matawi mengine yalifungwa kwa sababu viongozi wake walkuwa wakichimbwa chinichini na serikali. Waislam wengi walihisi vitisho vya serikali kwa hiyo waliogopa kuchukua uongozi wa EAMWS. Wengi waliogopa kuitumikia EAMWS kwa kuwa walihisi ofisi za jumuiya hiyo zilikuwa zikichukuliwa na serikali kama vituo vya upinzani dhidi yake. Kwa zaidi ya miaka mitatu toka ule mkutano wa mwaka 1963, EAMWS haikuweza kufanya mkutano wowote.
EAMWS ilipokuja kuitisha mkutano wake wa mwaka mjini Arusha mwaka 1966 kikajitokeza kikundi kutoka upande wa Tanzania kikidai EAMWS ijigawe, kila nchi iwe na mamlaka yake na ijitegemee yenyewe, yaani Tanzania, Kenya na Uganda zote ziwe mbalimbali. Kikundi hiki kilichokuwa kikidai utengano vilevile kikadai kuwa katiba ya EAMWS nayo iwe ya ‘kizalendo’[38] Hii ilikuwa na maana kuwa uongozi itabidi iifanyie katiba marekebisho ili kuiwezesha Tanzania kuwa huru ndani ya EAMWS. Wajumbe waliokuwa wanaona mbali kutoka Tanzania na wengine kutoka Kenya na Uganda, na kwa hakiaka mkutano mzima kwa ujumla walipinga kitendo hicho, wakidai kuwa kwa kufanya hivyo Waislam wa Tanzania watakuwa wametengwa na umma wa Kiislam wa Afrika ya Mashariki. Jambo hili likitokea, si tu litakuwa limewadhoofisha Waislam wa Tanzania peke yao, bali Waislam wa Afrika ya Mashariki nzima. Wajumbe wa Kenya na Uganda walikuwa wanatambua kuwa kulikuwa na shinikizo kubwa kutoka serikali ya Tanzania kwa Watanzania kujitoa kutoka EAMWS. Halikadhalika ilikuwa inafahamika kuwa wajumbe wa Tanzania walikuwa wakifanya kazi chini ya shinikizo kali kutoka serikali ya Nyerere.
Haikuwa siri sana kuwa baadhi ya viongozi wa EAMWS walikuwa kisirisiri wakiandamwa na serikali. Lakini mkutano ule haukuzungumzia matatizo haya kwa kuwa hayo yalichukuwaliwa kama matatizo ya ndani ya nchi. Hata hivyo kwa ule moyo wa Kiislam wa kuhurumiana, wajumbe wa Kenya na Uganda kwa faragha walionyesha masikitiko yao kwa Tewa kuhusu ile hali iliyokuwa ikiwakabili Waislam wa Tanzania. Wajumbe walipokuwa wakiondoka kurejea makwao, ilikuwa wazi kuwa serikali ya Tanzania ilikuwa ikiingilia kati EAMWS kiasi cha kuifanya jumuiya hiyo ishindwe kufanya kazi yake vyema na kupitisha maamuzi yake. Hali hii ilijidhihirisha wazi pale kwa kipindi kizima cha mkutano, makachero wa serikali walikuwa wamejitokeza kwa wingi mjini Arusha.
Haukupita muda ikadhihirika kuwa serikali ilikuwa imepania kuivunja EAMWS kwa kuwatumia Waislam wachache walioteuliwa kwa kazi hiyo. Lengo likiwa ni kuanzisha taasisi mpya ambayo serikali itaweza kuiamuru. Ieleweke hapa kuwa kama tulivyokwisha eleza hapo nyuma, serikali nzima ya Tanzani ilikuwa mikononi mwa Wakristo na watendaji hawa walikuwa wapo chini ya Kanisa. Hii ilikuwa na maana kuwa kilichotakiwa kuwepo ilikuwa taasisi ya Kiislam ambayo Kanisa itaweza kuiamuru. Hii ilikuwa ni jambo lazima lifanyike ili kuwadhibiti Waislam kama nguvu inayoweza kuleta mabadiliko ya siasa. Baada ya kuelewa hali hii ndipo sasa tunaweza kuuangalia kile kilichoitwa ‘mgogoro’ wa EAMWS ambao ulidumu kwa miezi mitatu ya mwisho ya mwaka wa 1968.
Ilituweze kuuelewa vyema kisa kizima cha ‘mgogoro’ ni muhimu kwanza kuelewa chanzo chake, hadhi za wahusika wakuu na nafasi zao katika ‘mgogoro’ ule. Mwisho, ni muhimu kuweka bayana na kuchambua nafasi ya Julius Nyerere, serikali yake, chama cha TANU na vyombo vya dola katika ‘mgogoro’ ule. Hii itasaidia kuelewa kama kweli ulikuwepo ‘mgogoro’ katika EAMWS, au ‘mgogoro’ ulibambikizwa na watu katika TANU, serikali na ndani ya Waislam wenyewe ili kuwadhoofisha Waislam kwa nia ya kuwa usije Uislam ukawa na nguvu katika Tanzania hivyo kuwawezesha Waislam kushika madaraka ya nchi.
Mwaka wa 1967 Mwalimu Julius Nyerere alitangaza Azimio la Arusha hatua ambayo iliitia Tanzania katika siasa ya ujamaa. Sera hii mpya ya uchumi ilipokelewa vyema na wananchi. Mtu ambae hata alikuwa hajulikani, tena mwalimu wa shule ya msingi akijulikana kwa jina la Adam Nasibu ambae alikuwa katibu wa Bukoba wa EAMWS, alichukua nafasi hii kwa kuongoza maandamano hadi ofisi ya TANU ya Mkoa kumuunga mkono Mwalimu Nyerere na sera yake mpya ya uchumi ya Azimio la Arusha. Adam Nasibu inasemekana kuwa alisema ujamaa ni sawa na mafundisho ya Qur’an Tukufu. Adam Nasibu hakuishia hapo alikwenda mbele zaidi na kutoa ‘miongozo kwa viongozi wote wa Kiislam wa Bukoba akifafanua Azimio la Arusha’. [39] Wasiokuwa Waislam walimuona Adam Nasibu kama Muislam mwenye mwamko mzuri wa kimaendeleo, na kwa kuwa yeye alikuwa ni kiongozi wa EAMWS, kuunga kwake mkono Azimio la Arusha kulionekana kama kitendo rasmi cha jumuiya hiyo kuunga mkono sera hiyo. Lakini kabla ya yeye kufanya haya, hakuna mtu aliyemjua mwalimu huyu wa shule kama mwanasiasa licha ya kuwa msomi mwenye uwezo wa  kuchambua mambo.
Katika hali ya kawaida, uongozi wa EAMWS pale makao makuu Dar es Salaam ungelikasirishwa kidogo na kitendo cha Adam Nasibu cha ushabiki wa siasa. Lakini uongozi wa EAMWS haukumuonya kiongozi wake wa Bukoba kuhusu jambo lile ambalo dhahiri halikuwa la kupendeza katika jumuiya. Bila shaka uongozi wa EAMWS ulichelea kuwa kwa kufanya hivyo wangelionekana si uzalendo, hasa ukiichukulia jinsi wananchi walivyohamasika na Azimio la Arusha. Hata hivyo Waislam siku zote ndiyo waliokuwa mbele katika kuongoza siasa. Makao Makuu walibaki kimya kama vile hakuna kilichotokea.
Tofauti na mwaka wa 1963 wakati Nyerere alipojaribu kufanya mapinduzi dhidi ya uongozi wa EAMWS, mwaka wa 1967 hali ya mambo yalikuwa yamebadilika sana yakimwendea Nyerere vyema. Serikali ilikuwa imedhibiti vyombo vyote vya habari ukiondoa gazeti la The Tanganyika Standard ambalo bado lilikuwa chini ya Lonrho. Nyerere alikuwa amemuweka Martin Kiama kama mkurugenzi wa radio ya taifa, na Benjamin Mkapa [40] kama mhariri wa magazeti mawili ya TANU, The Nationalist na Uhuru. Adam Nasibu aliandikwa katika magazeti na habari zake kutangazwa katika radio kwa ajili ya kitendo chake, hasa kuhusu yale maneno aliyosema kuwa ujamaa ni sawa na mafundisho ya Qur’an. Katika hali ya mambo kama yalivyokuwa wakati ule hasa jinsi uhasama ilivyokuwapo baina ya serikali na Waislam, baadhi ya Waislam walimuona Adam Nasibu kama kibaraka anaetafuta umaarufu wa bure kwa kujipendekeza kwa TANU, Nyerere na serikali yake. Juu ya haya yote kile kitendo cha katibu wa Bukoba wa EAMWS kitakuja kuwaathiri vibaya jumuiya hiyo na uongozi wake wote pamoja na Mufti Sheikh Hassan Bin Amir.
Kwa wengine Adam Nasibu alionekana kama mzalendo na Muislam mwenye ‘uoni wa mbali’. Kwa ajili hii basi serikali ikamuoana kama kiongozi wa baadae ambayo ingeweza kumtegemea wakati wa shida. Uongozi wa EAMWS makao makuu ukaonekana haupo pamoja na wananchi, wala haujali shida zao na uko mbali sana na sera za serikali. Lakini kwa hakika EAMWS kama taasisi ya dini isingeliweza kujitokeza na kuunga mkono Azimio la Arusha kwa kuwa hayo yalikuwa mambo ya siasa. Kwa kufanya hivyo ingelikuwa inakwenda kinyume na msimamo wake wa kutojiingiza katika siasa. Kwa zaidi ya robo karne toka iasisiwe EAMWS ilikuwa imejiweka mbali sana na mambo ya siasa ikishughulika na masuala ya Uislam tu. Hata hivyo kuwa nje ya Azimio la Arusha kukaonekana kama kitendo cha kukosa uzalendo na kutoa picha kuwa jumuiya hiyo ilikuwa haijali maendeleo na ustawi wa watu wa Tanzania. Mambo yakawa yamevurugika zaidi kwa kuwa rais wa EAMWS, Tewa Said na makamo wake Bibi Titi Mohamed walikuwa katika baraza la mawaziri la Nyerere na wakapoteza nyadhifa zao za ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1965. Kwa  ajili hii basi serikali ikawa inaeneza propaganda kuwa kwa kuwa Tewa  na Bibi Titi walikuwa katika uongozi wa juu wa EAMWS, walikuwa wanatumia nafasi zao kujijengea himaya mpya kutoka kwa Waislam dhidi ya Nyerere. Viongozi hawa ikawa lazima washughulikiwe na kuangamizwa. Mtu wa kufanya kazi hii hakuwa mwingine ila Adam Nasibu katibu wa EAMWS Bukoba, mwalimu wa shule ya msingi ambae elimu yake wala haikuwa kubwa. Adam Nasibu alikuwa tayari keshafanikiwa kufanya mapinduzi dhidi ya rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa. Kutokana na vitendo vyake alikuwa ameidhihirishia serikali kuwa yeye angeweza kuwa mtumishi bora kwa dola kuliko ule uongozi wa EAMWS uliokuwa pale makao makuu Dar es Salaam ambao ulikuwa ukionekana umechoka.
Wakazi wa Dar es Salaam kila mwaka walikuwa wakifanya maulidi katika viwanja vya Mnazi Mmoja kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW). Huu ndiyo toka asili ulikuwa uwanja ambao TANU ilifanya mikutano yake yote wakati wa kupigani uhuru. Mwezi Juni 1968 maulidi mbili katika usiku mmoja zilisomwa kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume (SAW).  Maulidi moja ilisomwa Mnazi Mmoja na nyingine Ilala. Chanzo cha haya yote ni kuwepo kwa kutoelewana kati ya viongozi wa Waislam waliokuwa wanajiona kuwa ni ‘wazalendo’ wafuasi wa TANU na wale na wale viongozi wa EAMWS ambao kambi nyingine ilikuwa ikiwaona kama wapinzani wa TANU. Yale maulidi yaliyosomwa Ilala yalihudhuriwa na viongozi wa EAMWS na yalipata watu wengi na yakafana sana ukilinganisha na yale maulidi ya Mnazi Mmoja, ya wafuasi wa TANU. Uongozi wa TANU ulitishika na hali hii iliyokuwa ikijitokeza kwa maana ilikuwa inaonyesha kuwa chama kilikuwa kinapoteza wafuasi ambao walikuwa  wakijiunga na kambi ya Tewa na Titi iliyokuwa ikisemekana ipo dhidi ya Nyerere. [41]
Tarehe 17 Oktoba, 1968, Adam Nasibu akatokea tena katika magazeti lakini sasa hakuwa tena mgeni machoni mwa watu, alikuwa anafahamika kama katibu mwenye hamasa za siasa wa EAMWS kutoka Bukoba ambae aliunga mkono Azimio la Arusha na kutoa maelekezo kwa viongozi wengine wa Kiislam akieleza vipengele vya azimio hilo. Adam Nasibu alitangaza kupitia radio ya serikali na na magazeti ya TANU kuwa mkoa wake, Bukoba unajitoa kutoka EAMWS.[42] Ghafla Adam Nasibu akawa mtu mashuhuri wa kufahamika nchi nzima, magazeti ya TANU na radio ya serikali ikaanza kumjenga haiba yake pamoja na kuutangaza kile kilichokuja kujulikan kama ‘mgogoro’ wa Waislam. Magazeti ya TANU chini ya Benjamin Mkapa yakawa yamepata habari ya kushabikia: ‘Radio ya serikali na magazeti ya TANU kwa pamoja yanatoa habari kwa uzito wa hali ya juu kuhusu kuhusu kujitoa kwa Bukoba katika EAMWS. Magazeti ya TANU yakiwa yamesheheza vichwa vya habari na maelezo ya mgogoro na picha za Adam Nasibu zikipamba kurasa zake za mbele’. [43]
Ilikuwa baada ya magazeti na radio kutangaza na kuandika habari hizo ndipo Waislam kwa mara ya kwanza wakaja kutanabahi kuwa walikuwa wanakabiliwa na ‘mgogoro’ mkubwa wa nchi nzima. Lakini matatizo yalikuwa yameanza hasa toka siku ile watu wa Dar es Salaam waliposoma maulidi mbili mwezi wa Juni, 1968. Siku tano baadae, yaani tarehe 22 Oktoba, Sheikh Juma Jambia mwanakamati wa halmashauri kuu ya EAMWS kutoka Tanga na yeye akatangaza kuwa Tanga inajitoa katika EAMWS. [44] Mwenyekiti wa EAMWS Tewa Said Tewa akamfahamisha Sheikh Jambia kuwa uamuzi wake ulikuwa ni uamuzi wa mtu mmoja. Jibu la Sheikh Jambia lilikuwa ni kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuvifahamisha uamuzi huo. Sheikh Jambia alitoa taarifa hiyo pamoja na mtu mmoja liyefahamika wa jina la Abdi Matunga. Haukupita muda mrefu, Iringa nayo ikatangaza kuwa inajitoa kutoka EAMWS.
Uongozi wa EAMWS kwa haraka ukaitisha mkutano kujadili hali ile mpya iliyojitokeza. Vyombo vile vya habari, Uhuru na The Nationalist ambavyo vilikuwa vikitumikia wale waliokuwa wanaodai kujitenga na EAMWS, sasa vikawa havitaki kutoa au kuandika habari za viongozi wa EAMWS ambao walikuwa wanapigania umoja wa Waislam. Hapa ikawa ni wazi kuwa serikali ilikuwa inatumia vyombo vya habari, yaani magazeti yaliyokuwa chini ya TANU na radio ya serikali kuwahujumu Waislam na EAMWS. Uongozi wa EAMWS ulipokuja kutanabahi ni nani walikuwa nyuma ya hujuma ile wakawa wamebaini hatari iliyokuwa ikiwakabili, kwa ajili hii basi waliwageukia Waislam kutaka msaada wao.
Kile kikundi kilichokuwa kikidai kujitenga kilitoa sababu nyingi za uamuzi wao huo. Lakini katika sababu hizo zao zote kubwa zaidi ilikuwa katiba ya jumuiya ile ilikuwa haipo sawa na uongozi wa nchi. Walidai kuwa katiba iwe ya Kitanzania na Aga Khan asiwe patroni. Vilevile wakadai kuwa Katibu Mkuu wa jumuiya awe Mwafrika Muislam. (Wakati ule katibu alikuwa Abdul Aziz Khaki, Muismaili na Mtanzania wa asili ya Kihindi). Kikundi kile halikadhalika kilitaka kujua vyanzo vya misaada kwa Waislam na misaada hiyo ilikuwa kitumikaje.[45] Dai lingine na hili likawa zito kwa uongozi wa EAMWS lilikuwa kuwa ‘viongozi wa EAMWS wawe wale wanaoamini malengo ya TANU, wale ambao wanapinga TANU hawafai kuwa viongozi wa Waislam wa Tanzania.[46]  Madai haya yalifikishwa makao makuu ya EAMWS na Adam Nasibu, Muhammad Zoharia na Hamisi Kayamba. Tewa Said Tewa akiongoza Kamati Kuu ya EAMWS alijaribu kuzungumza na viongozi wale lakini hawakutaka maelewano ya aina yoyote. Siku ya pili baada ya kutoa madai haya Adam Nasibu aliitisha mkutano wa waandishi wa magazeti na ndipo akaeleza kuwa  Bukoba imejitoa EAMWS.
Uislam una kanuni na sheria zake za msingi ambazo ndizo zinazowaongoza Waislam katika maisha yao ya kila siku. Madai waliyotoa kile kikundi hayakuwa madai yenye uzito mkubwa kiasi cha kusababisha farka kubwa kiasi kile kwa sababu madai yale yote yangeliweza kujibiwa kwa urahisi kabisa. Kulikuwa na baadhi ya madai ambayo yalikuwa hayajadiliki kwa sababu ya mafunzo ya msingi ya Uislam. Tatizo la katiba lingeliweza kujadiliwa na kumalizwa katika vikao vya kawaida. Lakini kuhoji rangi ya Muislam hilo halijadiliki kwa kuwa Uislam haubagui rangi ya mja kwa kuwa kufanya hivyo kunapingana na ujumbe wa Uislam wa dini moja kwa watu wa ulimwengu mzima. Kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafunzo ya Qur’an Tukufu.
Ilikuwa wazi kuwa wale waliokuwa wanadai utengano katika EAMWS hawakuwa watu wajinga kiasi cha kukosa kujua kuwa hayo waliyokuwa wakidai yalikuwa kinyume na Uislam. Kwa kuwa walikuwa wanang’ang’ania kujitoa katika EAMWS, ilikuwa sasa kitu dhahiri kuwa hiki kikundi cha Waislam waliojawa na ‘hamasa za kizalendo’ walikuwa na mpango maalum uliokuwa ukisaidiwa na serikali wa kuvunja umoja wa umma wa Kiislam ili Waislam wadhoofike na wawe hawana nguvu tena katika siasa. Hata hivyo, tarehe 14 Novemba, 1968, Baraza la EAMWS la Tanzania liliitisha mkutano wajumbe kutoa mikoa yote ya Tanzania kujadili ‘mgogoro’. Pamoja na waliohudhuria ni wajumbe kutoka mikoa ambayo tayari ilikuwa imekwishajitenga na EAMWS. Mkutano huu ulifanyika katika shule ya Kiislam ya Kinondoni.
Hapajatokea katika historia ya Uislam Tanzania mkutano kama ule. Uongozi ulikuwa unaingia katika chumba cha mkutano tayari umeshajeruhiwa vibaya sana na propaganda za magazeti ya TANU na radio ya serikali. Katika moja ya shutuma ambazo zilikuwa zikiandama uongozi wa EAMWS ilikuwa ni matumizi mabaya ya fedha za jumuiya.
Akifungua mkutano ule Tewa aliwatahadharisha wajumbe kuwa makini katika lolote watakaloamua kwa kuwa endapo wajumbe watashindwa kuafikiana basi matokeo yake ni kuvunjika kwa EAMWS, umoja wa Waislam na mwisho ya miradi yote ya elimu pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu.[47] Hisia kali zilitawala mkutano huu na baadhi ya wajumbe wanawake walikuwa wakilia hasa pale baadhi ya wajumbe walipokuwa wakitoa michango yao katika mjadala walipokuwa wakisoma aya za Qur’an Tukufu na kueleza fadhila za kupigana jihad dhidi ya madhalimu na wanafiki. Hisia hizi kali zilitokana na ukweli kuwa wajumbe walikuwa wanafahamu kuwa wale wenzao waliokuwa wakidai kujitenga walikuwa wakitumikia Ibilis tu na wala msimamo waliokuwanao haukuwa wao wala hawakuwa wanayafanya yale kwa mapenzi ya Allah na Mtume wake. Mwenyekiti wa mkutano Tewa Said Tewa aliahirisha mkutano hadi siku ya pili ili wajumbe wapoe na watoe mchango wakiwa katika hali ya utulivu. Katika wajumbe ambao walisimama kidete kutetea umoja wa Waislam walikuwa Sheikh Issa Mchowera kutoka Mtwara, Bilali Rehani Waikela, Hassan Johari na Sheikh Abdallah Said kutoka Kigoma.
Mkutano uliamua kuunda Tume ya Uchunguzi ya watu saba [48] kuchunguza chanzo cha ‘mgogoro’ na kisha itoe taarifa. Mussa Kwikima kijana mwanasheria alichaguliwa kuwa katibu wa tume ile ya uchunguzi. Wakati huo mikoa tisa ilikuwa tayari imeshajitenga na EAMWS na magazeti ya TANU yakawa tayari yamejenga ‘mgogoro’ ule kufikia hali ya kuonekana kuwa ni ‘mgogoro’ wa taifa zima ambao kila mtu anaweza kuuingilia na kusema atakalo. Magazeti ya TANU yakawa yanaandika na kuchapisha mambo ya EAMWS kama wanavyotaka, wakizidi kutia chumvi katika ugomvi ambao tayari ulikuwa umeshaleta hofu na farka kubwa katika jamii. Inasemekana viongozi wengine wa EAMWS walikuwa wanaambiwa wajitoe huku wameshikiwa bunduki. [49]

Pambano Kati ya Nyerere, Tewa na Bibi Titi, 1968
Ili tume ya uchunguzi ya Waislam iweze kufanya kazi yake vyema na bila upendeleo, ilikuwa lazima ile tume ya Waislam iiombe serikali izuie propaganda iliyokuwa ikiendeshwa na wale waliokuwa wamejitenga na EAMWS, wakitumia jukwa la radio ya serikali na magazeti ya TANU. Tume ya Waislam ilikutana na Waziri wa Habari na Utangazaji, Hasnu Makame, ofisini kwake tarehe 20 Novemba, 1968, kujadili tatizo lile. [50] Hii haukusaidia kitu. Propaganda dhidi ya uongozi wa EAMWS iliendelea kwa nguvu zote. Mashambulizi kutoka pande tatu yaliyopangwa vyema yalikuwa kazini. Benjamini Mkapa akitumia gazeti la Nationalist ataandika habari yoyote ya Adam Nasibu, Martin Kiama akitumia Radio Tanzania atatumia habari ile kama habari muhimu katika radio na habari hiyo itatangazwa kutwa nzima huku ofisi ya rais ikiwa kimya kwa fitna ile. Lile kundi la waliojitenga na umma wa Waislam Adam Nasibu akiwa kama msemaji wao mkuu wakawa wakati mwingine kwa mastaajabu makubwa wakawa wanakiuka hata misingi ya akida ya Tanzania, wakitoa madai ya ubaguzi a rangi, wakikazania lazima EAMWS ivunjwe. Adam Nasibu alinukuliwa na The Nationalist akisema kuwa:
Waislam lazima wafahamishwe kwa nini East African Muslim Welfare Society iwe na katiba ambayo inaendana na mwelekeo wa nchi. Hatujui nafasi ya Aga Khan katika nchi yetu na ndiyo maana tunamkataa. [51]
Lakini cha kushangaza zaidi ilikuwa ule ukimya wa serikali kuhusu matakwa ya kundi la Adam Nasibu lililokuwa likidai kuwa Waislam wachanganye dini na siasa katika suala hili, wakati ilikuwa ikijulikana wazi kuwa kufanya hivyo ni mwiko mkubwa katika siasa za Tanzania.  Haya yote mbali, lile la kushangaza hasa na kitu ambacho kilikuwa kigeni katika Tanzania ilikuwa yale madai ya kuingiza ubaguzi wa rangi katika siasa za Tanzania. Ilikuwa inastaajabisha kuona magazeti ya TANU yaliyokuwa na sifa ya kuheshima haki za binadamu yakichapisha na kuzipa uzito wa hali ya juu habari za kundi dogo la Waislam waliokuwa wanawalaumu Waislam wenzao wa Kiismailia kwa kutozaliwa weusi. Miaka kumi iliyopita watu wa Tanganyika, Waislam wenyewe waliokuwa ndiyo walioanzisha na kuijenga TANU, walipambana vikali dhidi ya siasa za kibaguzi za Zuberi Mtemvu na chama chake cha African National Congress. Mtemvu alishindwa na matokeo yake ikawa Tanganyika kuwa na serikali ya watu wote isiyobagua rangi na ikitawala raia wa rangi zote kwa misingi ya haki. Kwa ajili hii nchi ikawa haina msuguano kwa ajili ya ubaguzi wa rangi. Haya matokeo mapya yalikuwa hayaendani na misingi ya TANU.
Ilipofikia hali hii, rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa na makamo wake Bibi Titi Mohamed, waliamua kulipeleka suala hili kwa Juluis Nyerere, Rais wa Tanzania na mwenyekiti wa TANU, chama tawala. Watu hawa walikuwa wakichekeana jino pembe. Lakini ili tuelewa chanzo cha uadui huu inatulazimu turudi nyuma hadi mwaka wa 1963, katika siku za mwanzo za uhuru, katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU [52] uliofanyika Ukumbi wa Karimjee.
Kama ilivyokwishaelezwa hapo mwanzoni kuwa mwaka 1963 ulikuwa mwaka wa mambo mazito. Ilikuwa ndiyo mwaka ambao Kanisa Katoliki liliteua wagombea wake wapambane na wagombea wa TANU waliokuwa Waislam katika uchaguzi wa serikali za mitaa kule Kigoma na Bukoba. Ulikuwa ndiyo mwaka ambao Rais wa TANU, Nyerere alipombana na EAMWS kupitia Bilali Rehani Waikela. Mwaka wa 1963 ndiyo ulikuwa mwaka ambao Halmashauri Kuu ya TANU ilivunja Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa limetawaliwa na Waislam kwa madai kuwa baraza hilo lilikuwa ‘likichanganya dini na siasa’. Mwaka 1963 ulikuwa mwaka muhimu kwa Halmashauri Kuu ya TANU kwa sababu ilikuwa mwaka ambao ilifanya maamuzi nyeti ya kidini. Mwaka ule Bibi Titi na Nyerere walishambuliana kwa maneno ndani ya Halmashauri Kuu yA TANU kuhusu jambo jingine tena la dini lililokuwa likihusu EAMWS.
Wanakamati wawili wa Halmashauri Kuu ya TANU, Selemani Kitundu na Rajab Diwani, waliiomba Halmashauri Kuu ya TANU imjadili Aga Khan na nafasi yake kama patroni wa EAMWS. Kitundu na Diwani walidai kuwa wana habari Aga Khan anataka kuitawala Tanganyika kupitia Waislam na EAMWS. Kwa ajili hii basi wakapendekeza EAMWS ifungiwe. Nyerere aliwaunga mkono Selemani Kitundu na Rajab Diwani. Bibi Titi akasimama kishujaa dhidi ya Diwani, Kitundu na Nyerere, akasema hakuna kati yao aliyekuwa na haki ya kuifungia jumiaya yoyote ya Waislam. Kama walikuwepo watu ndani ya EAMWS ambao walikuwa wanakwenda kinyume na sheria basi watu hao wapelekwe mahakamani na sheria ichukue mkondo wake. Bibi Titi akaendelea na kusema kuwa EAMWS imekuwepo kabla ya TANU na siku zote imekuwa ikitoa huduma kwa Uislam. Inasemekana hasira zilipanda na kukawa na kutoleana maneno kati ya Bibi Titi na Nyerere. Bibi Titi akamwambia Nyerere yeye hamuogopi yeyote ila Allah.
Tuhuma zile dhidi ya Aga Khan na EAMWS hazikuweza kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ya TANU ikaliacha jambo lile kwa wakati ule. Lakini Nyerere alikuwa amefedheheka. Kuanzia hapo akajenga chuki dhidi ya Bibi Titi na kumweka Rajab Diwani na Selemani Kitundu karibu yake. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965 Bibi Titi na Tewa wakapoteza viti vyao kwa watu ambao walikuwa hata hawafahamiki – A.M. Mtanga na Ramadhani Dollah. Iliaminika kuwa Nyerere alikuwa anahusika na kuanguka kwa Bibi Titi na Tewa. Kuanzia hapo mambo yakawa dhahiri. Nyerere alikuwa amewatangazia vita wote wawili, Bibi Titi na Tewa. Nyerere alikuwa sasa ana imani kuwa wale maadui zake wawili walikuwa wamekwisha kisiasa. Lakini kilichokuwa kkimuudhi Nyerere zaidi ilikuwa taarifa ambazo alikuwa akizipata kuwa Tewa alikuwa akipewa mapokezi makubwa sana na Waislam katika ziara zake huko mikoani  kama rais wa EAMWS. [53]
Sasa mwaka wa 1968, Bibi Titi na Tewa walipokwenda kumuona Nyerere kuhusu jambo lililokuwa linawahusu Waislam, Nyerere alikuwa amejitayarisha vyema. Kiwanuka ameueleza mkutano huu vizuri sana:
…Viongozi hawa wawili wa Waislam walimueleza Mwalimu masikitiko yao jinsi radio ya serikali na magazeti ya TANU yalivyokuwa yakiandika habari kuhusu matatizo yale ya Waislam. Walidai kuwa TANU ilikuwa ikichanganya dini na siasa. Waliokuwa wakimtahadharisha kuhusu jambo hilo hawakuwa wengine ila marafiki zake wa zamani na wa kutumainiwa, Tewa na Bibi Titi. Marafiki wa kutumainiwa kwa sababu ilikuwa Titi aliyemuunga mkono Nyerere katika siku za mwanzo za TANU, pale Suleiman Takadir – mmoja wa wazee wa TANU – aliposema kuwa TANU ilikuwa na Ukristo kama Mwalimu na Rupia, rais na makamo wake walivyokuwa Wakristo.  Yeye mwenyewe akiwa Muislam hasa, aliipatia TANU ushindi kwa kuthibitisha kuwa Tanzania, Tanganyika kama ilivyokuwa ikijulikana wakati ule, ilikuwa mbele, na Uislam unafuata nyuma. Leo, alikuwa anazungumzia jambo ambalo yeye mwenyewe alilishinda katika miaka ya 1950. Jibu walilopata kutoka kwa Mwalimu lilikuwa la kusisimua. Mpashaji wangu habari anasema lilikuwa jibu la mkato. ‘Mmeamua kunipiga vita, jiandaeni.’ [54]
Mwalimu Nyerere alikuwa anawaambia Tewa Said Tewa na Bibi Titi Mohamed uso kwa macho wajiandae kwa kile kilichokuwa dhahiri: vita ya msalaba dhidi ya umoja wa Waislam. Sheikh Suleiman Takadir aliyaona haya na aliiomba TANU toka mwaka wa 1958 pawepo na uhakika kuwa Wakristo ambao walikuwa wanapanda migongo ya Waislam na kuchukua uongozi hawatakuja kuwafanyia uadui Waislam pale Waislam watakapokuwa sasa wanataka kugawana madaraka ya kuongoza nchi sawa na Wakristo baada ya uhuru. Tewa Said Tewa, muasisi wa TANU, waziri katika serikali ya kwanza ya uhuru, balozi katika Jamuhuri ya watu wa China na Rais wa baraza la Tanzania la EAMWS, pamoja na Bibi Titi, mwanamke aliowakusanya wanawake wote nyuma ya Mwalimu Nyerere na TANU, walikuwa wakisemwa na Nyerere kama vile watoto wadogo wa shule waliokuwa watukutu kwa sababu tu, walikuja kumfahamisha Rais kuhusu kukiukwa kwa maadili ambayo ilihitaji yeye ashughulikie mara moja na kutoa uamuzi.
Ulipofika mwezi Oktoba, ‘mgogoro’ ukachukua mwelekeo mpya pale Makamo wa Rais wa Tanzania, Abeid Amani Karume, alipoishambulia EAMWS kuwa ni chombo cha unyonyaji. [55] Kutokea hapo Karume akawa anafanya mashambulizi na kutoa shutuma kwa EAMWS, wakati mwingine akijaribu kufafananisha uhusiano wa EAMWS na Waislam katika mtazamo wa Ki-Marxist, akidai kuwa jumuiya ile kilikuwa ‘chombo cha makabaila wakubwa na kilikuwa chini yao kikiwanyonya watu wa chini’. [56] Mgogoro ulipozidi kukua mashambulizi yakahama sasa kutoka EAMWS na kuhamia kwenye mafunzo ya msingi katika Qur’an Tukufu. Katika mkutano wa hadhara Zanzibar, Karume alitoa changamoto kwa Muislam yeyote ajitokeze bila ya woga kupinga kauli zake mbili kuwa ‘Hakuna tofauti kati ya Uislam na Ukristo’, na ‘Kufunga siyo lazima’.
Lakini juu ya mashambulizi dhidi ya uongozi wa Waislam  kutoka serikalini, Nyerere alikuwa hana uwezo wa kumgusa Mufti Sheikh Hassan bin Amir. [57] Sheikh Hassan bin Amir alikuwa na nguvu sana kiasi cha kwamba si Nyerere au yeyote yule kuweza kumgusa kwa wakati ule. Sheikh Hassan alikuwa kwenye siasa kabla ya vijana waliokuwa katika TANU na nafasi yake katika umma wa Kiislam na uzalendo wake ulikuwa hauna shaka. Sheikh Hassan bin Amir aliingizwa TAA kwa mara ya kwanza mwaka 1950 na Abdulwahid Sykes akiwa mwanakamati katika Kamati ndogo ya siasa ya TAA. Kwa ajili hii basi, akawa mmoja wa wale waliotia sahihi ile memoranda iliyotayarishwa na TAA kwenda kwa Gavana wa Tanganyika, Edward Twining kuhusu mabadiliko ya katiba ya Tanganyika. TANU ilipoasisiwa, Sheikh Hassan bin Amir alikuwa akikiwakatia watu kadi za TANU msikitini huku akidarsisha. Baadhi ya wanachama shupavu wa TANU ambao Sheikh Hassan bin Amir aliwaingiza katika TANU ni Sheikh Mussa Rehani ambae alipewa kadi yake ndani ya msikiti Kigoma. Wakati Nyerere alipokuja TAA Dar es Salaam mwaka 1953, alimkuta Sheikh Hassan bin Amir mwenyeji katika siasa. Baada ya uhuru Sheikh Hassan bin Amir alijiuzulu siasa, kutokana na kauli yake alisema kuwa, ili awatumikie Waislam vyema.
Nyerere alifahamu fika kuwa haitakuwa rahisi kwake kumweka Sheikh Hassan bin Amir kizuizini kama alivyofanya kwa Waislam wengine. Sheikh Hassan bin Amir alikuwa ndiyo Mufti wa Tanganyika na Zanzibar na kwa ajili hii alikuwa na hadhi kubwa katika umma wa Waislam. Halikadhalika haikuwa rahisi kwa yoyote kumkiuka Sheikh Hassan bin Amir na kuchukua uongozi wa Waislam.
Mkutano wa Taifa wa ‘Waislam’, 1968
Hadi kufikia juma la kwanza la mwezi wa Desemba, mikoa mitatu kati ya kumi na saba ilikuwa tayari imeshajitenga kutoka EAMWS. Kile kikundi cha Adam Nasibu kikaunda kamati kwa ushirikiano na Kamati ya Maulidi ya Dar es Salaam, Adam Nasib akiwa katibu na Sheikh Abdallah Chaurembo mwenyekiti. Kamati hii ikaitisha mkutano Ukumbi wa Arnatouglo tarehe 3 Desemba, 1968 kujadilia ‘mgogoro’. Aliyetumiwa kutoa tangazo lile alikuwa katibu wa Kamati ya Maulidi na Swala ya Iddi, Y. Osman. Kundi la Adam Nasib lilikuwa na mchanganyiko wa watu waliokuwa wanaungwa mkono na serikali Adam Nasib akiwa kiongozi, halikadhalika kulikuwa na Waislam waliokuwa na nafasi katika TANU kama Sheikh Abdallah Chaurembo na Juma Sued kiongozi wa TANU kutoka Bukoba. Ilikuwa wazi kuwa serikali ilikuwa inamtayarisha Sheikh Abdallah Chaurembo kuchukua nafasi ya mwalimu wake na mtu aliyemfikisha pale alipo, Sheikh Hassan bin Amir. Ikawa sasa lazima Sheikh Hassan bin Amir aondolewe na kupelekwa Zanzibar ili lile kundi la serikali chini ya Adam Nasibu liweze kuchukua uongozi wa Waislam bila ya kipingamizi chochote.
Wakati wa vurugu hizi Kamati Kuu ya TANU ilikuwa inafanya kikao chake Tanga. Sheikh Kassim Juma, [58] Adam Nasibu, Omari Muhaji, Sheikh Abdallah Chaurembo na Saleh Masasi [59] walipanda ndege hadi Tanga kwenda kushauriana na Kamati Kuu ya TANU jinsi ya kumaliza ‘mgogoro’ wa Waislam.  Ujumbe huu ulikwenda Tanga kuonana na Nyerere huku ukiwa na orodha ya Waislam ambao kile kikundi cha Adam Nasibu walikuwa wanataka serikali wakamatwe na kutiwa kizuizini ili msuguano upate kumalizika. Dossa Aziz aliona Nyerere akipewa karatasi wakati kikao kikiendelea lakini hakufahamu ujumbe uliokuwamo ndani ya karatasi ile hadi hapo baadae. Alikuja kutambua habari za karatasi ile baada ya majuma mawili kupita wakati alipofatwa na jamaa yake mmoja na kumuomba aingilie kati ili rafiki yake aliyetiwa kizuizini na Nyerere aachiwe kutoka Jela ya Ukonga. Nyerere alipofahamishwa habari zile na Dossa, alisema kuwa yeye hakufahamu kuwa rafiki yake Dossa alikuwa katika orodha ile ambayo kwa umuhimu wa jambo lile ilibidi aletewe Tanga wakati wa mkutano wa Kamati Kuu. Kwa kejeli Nyerere akamwambia Dossa kuwa yeye huwa hachukuwi tabu ya kusoma majina ya watu anaowaweka kizuizini kwa kuwa anawaamini wale wanaofanya kazi ya kumletea majina yale.
Inspekta Jenerali wa Polisi, Hamza Aziz, mdogo wake Dossa alipopokea amri kutoka kwa rais kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa amkamate Sheikh Hassan bin Amir, hakuweza kuamini masikio yake. Alitaka afahamishwe sababu za kutaka kukamatwa Mufti – kiongozi wa juu kabisa katika safu ya uongozi wa Waislam katika Tanzania. Alipoambiwa kuwa sababu ni kuwa anaihujumu serikali, Hamza Aziz alimwambia Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa huenda kuna makosa katika amri ile. Alimfahamisha waziri kuwa yeye binafsi alikuwa anamfahamu mzee yule toka yeye Hamza alipokuwa mtoto mdogo. Akimfahamu Sheikh Hassan bin Amir kama mwalimu na mtu aliyeshiriki katika ukombozi wa Tanganyika.  Msimamo wake heshima na hadhi yake mbele ya Waislam ipo juu kabisa. Inspekta Jenerali wa Polisi alimwambia waziri kuwa haitawezekana kwake yeye kutii amri ile kwa sababu yeye haamini kuwa tuhuma zile dhidi ya Mufti Sheikh Hassan bin Amir ni za kweli. Nyerere alifahamishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa Inspekta Generali wa Polisi, Hamza Aziz amekataa kutii amri yake ya kumkamata Mufti. Nyerere alitoa amri kwa Usalama wa Taifa kumkamata Sheikh Hassan bin Amir. Hii ilikuwa ni kinyume na utaratibu kwa kuwa Usalama wa Taifa hawana mamlaka ya kukamata watu.
Usiku wa manane siku hiyo hiyo Sheikh Hassan bin Amir alikamatwa na makachero wa Usalama wa Taifa akapelekwa uwanja wa ndege na kurudishwa Zanzibar. [60] Inaelekea kulikuwa na mpango uliokuwa umetayarishwa kabla ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar kumpokea Sheikh Hassan bin Amir. Inasemekana mara kadhaa Karume alipata kumueleza Sheikh Hassan bin Amir kuwa Nyerere alikuwa hamtaki nchini kwake na akawa anamshauri arudi nyumbani Zanzibar. Sheikh Hassan alikataa ushauri ule hadi alipokamatwa na kurudishwa kwa nguvu. Karume alimpa Sheikh Hassan bin Amir hadhi zote alizostahili kama ulamaa na akamruhusu kuendesha madras. Lakini Zanzibar ilikuwa imebadilika.Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa yameingiza katika Zanzibar fikra potofu zilizokuwa zinapinga Uislam. Karume mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kuchoma vitabu vyote vya dini. Nakala za Qur’an Tukufu zilichomwa moto pamoja na taka za mji. Muslim Academy chuo kilichokuwa kikisomesha masomo ya dini kilifungwa. Mashine za kuchapa kwa lugha ya Kiarabu zikatupwa kutoka Government Press. [61] Maulama wengi na wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir walikuwa wamekimbia Zanzibar kwenda kuishi uhamishoni. Zanzibar haikuwa tena kitovu cha elimu na maarifa ya Kiislam. Sheikh Hassan bin Amir akawa sasa mfungwa katika nchi yake mwenyewe kwa kuwa hakuwa na ruhusa ya kuondoka visiwani hapo na kurejea Tanzania bara. Mara baada ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan bin Amir, Adam Nasibu akatangaza kufanyika kwa mkutano ambao ulikuja kujulikana kama Mkutano wa Waislam wa Taifa. Mkutano ambao ilitangazwa utafanyika Iringa kuanzia tarehe 12-15 Desemba, 1968. Agenda kuu ya mkutano ule ilikuwa kujadili katiba kwa ajili ya jumuiya mpya ya Waislam.
Baada ya kukamatwa kwa Sheikh Hassan Bin Amir Tewa Said Tewa gazeti moja la Kiingerezalilimfuata ili afanye mazungumzo nalo. Tewa alimfahamisha mwandishi kuwa kulikuwa na hofu juu ya maendeleo yanayofanywa na Waislam na mikutano mikubwa ya Waislam iliyokuwa ikifanyika nchi nzima.[62] Waislam waliokuwa na vyeo katika serikali walikataa kabisa  kuisaidia Tume ya Kikwima kwa njia yeyote wakidai kuwa kufanya hivyo ni sawasawa na kuchanganya dini na siasa. Waislam hawa walikaa pembeni kama watazamaji huku Nyerere kwa taratibu akivunja uongozi wa EAMWS na  kutayarisha watu wake kuwaongoza Waislam. Kundi la Adam Nasibu lilikataa kukutana na Tume ya Kwikima. Maulamaa wa Kiislam ambao walikuwa na hadhi na uwezo wa kuleta sulhu katika sakata ile hawakuweza kufanya hivyo kwa kuwa walikuwa wanajua fika kuwa aliyekuwa akivunja EAMWS hakuwa Adam Nasibu, yeye na wenzake walikuwa wakitumiwa tu. Kundi la Adam Nasibu lilikuwa halitaki chochote ila EAMWS ivunjwe na badala yake iundwe jumuiya itakayokuwa chini ya kivuli cha serekali. [63] Vilevile kukawa na uvumi kuwa Muislam yeyote ambae atakaejejihusisha na shughuli za EAMWS atawekwa kizuizini na serekali. Tume ya Kikwima haukuweza kupuuza vitisho hivyo kwa sababu serekali ilishawahi kuwaweka vizuizini masheikh.
Tume ya Kwikima ilikuwa inafahamu lile kundi la Adam Nasibu halikuwa na nguvu wala uwezo wa kuivunja EAMWS. Kufuatia kutangazwa kwa mkutano wa Iringa wa kundi la Adam Nasibu, Tume ya Kwikima ilitoa taarifa yake tarehe 11 Desemba – siku moja kabla ya mkutano wa Iringa kuanza. [64] Taarifa ambayo ilitolewa kwa Waislam wote, iliitisha mkutano mkuu wa EAMWS ambao ulikuwa ufanyike mwezi Februari mwaka unaofuata kujadili na kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu ‘mgogoro’. [65] Tarehe ya mkutano ilibadilishwa hapo baadae na kuwa Januari kutokana na umuhimu wa ‘mgogoro’ uliokuwa ukikabili EAMWS. Gazeti la TANU baada ya kusoma taarifa ya Kwikima iliamua kutoa maoni yake kuhusu taarifa ile kwa kusema kuwa haikuwa sawa.[66] Huu ulikuwa mpango uliosukwa mapema kuonyesha kuwa uongozi wa EAMWS ulikuwa na ubadhirifu. Juma lile lile Aga Khan ambae ndiye aliyekuwa akishambuliwa na kundi la Adam Nasibu, baada ya kutambua kuwa EAMWS isingeweza kamwe kuokolewa, akiwa Paris, Ufaransa alijiuzulu nafasi yake kama patron wa EAMWS.[67]
Wakati Tume ya Waislam inasubiri mawazo ya Waislam sasa kundi la Adam Nasibu wakijionesha wazi kuwa serikali na TANU ilikuwa nyuma yao, lilikutana kwa ajili ya kile walichokiita Mkutano wa Waislam wa Taifa ulioanza tarehe 13 Desemba, 1968. Serikali ikifanya kazi nyuma ya pazia ilijitahidi sana kuhakikisha kuwa mkutano ule unafanikiwa. Serikali ndiyo iliyotoa fedha za kufanyia mkutano ule, ukatoa vyombo vyake vya habari kwa ajili ya kuutangaza vizuri na ukatoa ulinzi kwa wajumbe wote. [68]
Wajumbe waliohudhuria mkutano ule walikuwa kama mia mbili.Mkutano huu ulihudhuriwa na Waislam waliokuwa na vyeo katika serikali na TANU, Waislam waliokuwa wakuu wa wilaya na mikoa na Waislam wenyeviti wa TANU. Waislam wote wenye majina walialikwa, pamoja na Waislam waliokuwa katika halmashauri kuu ya TANU na baadhi ya wajumbe wa mkutano walitoka Zanzibar. Ulikuwa mkutano wa wanasiasa Waislam ambao ukitoa majina yao walikuwa hawana chochote katika harakati za Uislam isipokuwa majina yao. Lakini uzito wa mkutano huu ulitokana hasa na kuwa ulikuwa mkutano ambao ulitawaliwa na Waislam waliokuwa hawapendezi mbele ya macho ya umma wa Kiislam. Ni ukweli usioweza kupingika kuwa kama mkutano ule ungelikuwa hasa umetayarishwa kwa ajili ya kumtumikia Allah, ni wazi ungehudhuriwa na Waislam wa kweli na wenye historia ya unyenyekevu na mapenzi kwa dini yao. Waislam wa sifa hizi hawakuwepo katika mkutano ule ukimtoa Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo na wengine wachache ambao kwa kutotambua mambo waliitika mwito. Mkutano ulifunguliwa na Karume na kufungwa na Kawawa. Katika hotuba yake ya ufunguzi Karume alisema maneno haya:
Dini haiwezi kuwa nje ya siasa kwa sababu siasa ndiyo damu inayoipa jamii uhai wake. Wakati wa ukoloni wananchi na daini zao zilikuwa chini ya utawala wa wageni. Hivi sasa watu wamevua mabaki ya ukoloni pamoja na kutawaliwa kwa misingi ya dini. Kuanzaia sasa uongozi wa dini lazima ukwe chini ya wananchi wenyewe bila ya kuongozwa na kiongozi kutoka nje.[69]
Mkutano wa Iringa ulipitisha katiba ya jumuiya mpya ya Waislam, katiba ambayo ilikuwa sawasawa na katiba ya TANU. Hivi ndivyo BAKWATA ilivyoundwa. BAKWATA ikamchagua Saleh Masasi, Muislam tajiri na ambae alikuwa kama mwenyekiti wa mkutano ule kuwa Mwenyekiti wa Taifa na Adam Nasibu akawa Katibu Msaidizi. Nafasi zote za juu katika BAKWATA kama ilivyotegemewa zilichukuliwa na kundi la  Adam Nasibu, kundi ambalo toka mwanzo lilikuwa likidai kuvunjwa kwa EAMWS. Uongozi wa BAKWATA uliomba serikali itambue jumuiya hiyo mara moja na ipige marufuku EAMWS kama jumuiya isiyo halali na mali zake zizuiwe. BAKWATA ilitoa maazimio kadha lakini azimio namba nne ndilo hasa linafaa kuelezwa. Azimio hilo liliomba serikali, TANU na ASP kuwatazama na kufanya uchunguzi wa kina kwa viongozi wote wa EAMWS, hasa Rais, Makamo wa Rais, Katibu wao na baadhi ya viongozi wa mikoa na wilaya ambao wana chuki na hii jumuiya mpya.[70] Uongozi wa BAKWATA katika ushindi wao hawakutaka salama na mawaelewano na Waislam wenzao katika EAMWS wala kuwaonea huruma kama Uislam unavyofundisha, bali ulitaka chama na serikali uwaandame, hasa wale waliokuwa viongozi.
Baada ya kuundwa BAKWATA, ili kuondoa wasiwasi na kuwarudishia imani Waislam, Katibu wa Tume ya Waislam, Mussa Kwikima alitoa taarifa iliyosema:
Hakuna anaeweza kutishia kuwepo kwa EAMWS isipokuwa wanachama wake, sheria na serikali, lakini si watu binafsi…hata ikiwa mikoa yote kumi na saba ikijitoa haitamaananisha kuwa jumiya imekufa kwa kuwa kuwepo kwake hakutokani na kuwepo kwa mikoa hiyo kama wanachama isipokuwa kuwepo kwa wanachama wake, Waislam.[71]
Wakati ilipotoka taarifa hii BAKWATA ilikuwa bado haijaandikishwa rasmi na Msajili wa Vyama. Kisheria ilikuwa haiwezekani kwa kundi la Adam Nasibu kuunda jumiya mpya iliyokuwa na malengo sawa na jumuiya ambayo tayari ishaandikishwa. Kwa muda wa siku tatu BAKWATA na EAMWS zikawepo kwa wakati mmoja. Ilionekana kama kwamba EAMWS itashinda vitimbi vya serikali na vya kundi la Adam Nasibu.
Tarehe 19 Desemba, 1968 serikali kama vile imegutushwa na taarifa ya Kwikima, iliipa BAKWATA Cerificate of Exemption na kuifungia EAMWS.[72]  Waziri wa Mambo ya Ndani Said Ali Maswanya kwa niaba ya serikali alitoa taarifa fupi:
Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kuamriwa na Rais anatangaza kuwa tawi la Tanzania la East African Muslim Welfare Society na Baraza la Tanzania la la East African Muslim Welfare Society ni jumuiya zisizotambulika kisheria chini ya kifungu 6 (i) cha Sheria ya Vyama.[73]
Kwa tangazo hilo la Rais wa Tanzania, Julus Nyerere, Waislam walinyimwa nafasi ya kukutana na kuzungumza kuhusu tatizo ambalo kwa kweli liliwahisu Waislam peke yao. Kwa ajili hii basi Waislam walinyimwa nafasi ya kujadili na kulitolea uamuzi  tatizo hilo.
Viongozi wa EAMWS waliitwa mbele ya Kabidhi Wasii ambae ndiye alikuwa amekabidhiwa na serikali jukumu la kusimamia shughuli za kufunga rasmi shughuli za EAMWS. Viongozi walifahamishwa kuwa chini ya sheria ya vyama mali zote za EAMWS zitauzwa na madeni yatalipwa kutokana na fedha hizo na fedha zitakazobaki watapewa wanachama. Serikali ilikuwa haiwezi kufanya kama sheria ilivyokuwa imeelekeza. Ilikuwa jambo zito sana kwa serikali ya Nyerere kuonekana anasimamia kuuzwa kwa mali za Waislam. Viongozi wa EAMWS walipoitwa kwa Kabidhi Wasii mara ya pili walifahamishwa kuwa serikali imebadilisha mawazo yake kutekeleza amri kama sheria inavyosema kwa ajili hiyo basi imefanya mabadiliko ya sheria ya vyama ambayo yanaiwezesha sasa kutoa mali ya EAMWS na kukabidhi BAKWATA. Hivi ndivyo mali za EAMWS zilivyochukuliwa na kupewa BAKWATA bila ya ridhaa ya Waislam wenyewe. Hivi ndivyo shule zote zilizojengwa na EAMWS pamoja na mradi wa Chuo Kikuu cha Kiislam kilipoanguka katika mikono ya kundi la Adam Nasibu. BAKWATA haikuwa na uwezo wa kuendesha mipango yoyote na taratibu shule na miradi yote ya elimu ikafifia na mwishowe kufa kabisa. Hivi ndivyo halikadhalika moto wa Waislam uliowashwa kwa kupatikana kwa uhuru waliopigania hadi ukapatikana ulivyokufa. Moto huu ulikuja ukawaka tena, lakini hiki ni kisa kingine. Insha Allah Mwenyezi Mungu akipenda tutakuja kukieleza.
Huu ndiyo ukawa mwisho wa kile kilichokuwa kikijulikana kama mgogoro wa Waislam ulivyomalizika. Mgogoro ambao ulianza pale mwalimu wa shule ya msingi asiyefahamika na yeyote alipofanya maandamano katika mitaa ya Bukoba akimuunga mkono Julius Nyerere na Azimio lake la Arusha na ukaishia kwa mwalimu huyu akiwa na nafasi juu katika jumuiya ya Kiislam ambayo ilikuwa ikichukiza machoni mwa Waislam. Mwalimu huyu ambae sasa amekuwa Makamu Katibu Mkuu wa BAKWATA alianza kazi yake kwa kuwashutua Waislam. Katika mkutano wa waandishi wa habari Adam Nasibu aliiomba TANU na ASP kujikinga na watu wanaohujumu umoja wa nchi kupitia dini. Akaendelea na kusema kuwa BAKWATA ni sawa na Baraza la Kikristo la Tanzania. [74] Kwa kuwa Waislam walinyimwa fursa ya kujadili “mgogoro’ hivi sasa kilichobaki na dhana tu, kuwa nini kingelitokea endapo wangeliruhusiwa kufanya mkutano ule ulioitishwa na EAMWS. Waislam wa Bukoba ambao ilitaarifiwa kuwa walifanya maandamano kuunga mkono Azimio la Arusha hawakutayarisha maandamano ya kuunga mkono BAKWATA. Dar es Salaam na katika miji mingi ya Tanzania, neno BAKWATA halina tofauti na tusi. Kumuita Muislam kuwa yeye ni mwanachama wa BAKWATA ni sawa na kumuita Mkristo mfuasi wa Yuda Iscariot, aliyemsaliti Yesu kwa vipande thelathini vya fedha.
Mjumbe mmoja wa Tume ya Waislam inastahili kuelezwa habari zake – Mussa Kwikima. Mussa Kwikima mwaka 1968 alikuwa ameteuliwa kuwa jaji na Rais Nyerere. Yeye ndiye hasa alikuwa nguvu kuu katika tume ya Waislam. Wakati alipojitolea kuisaidia tume katika kupambana na kundi la Adam Nasibu, Waikela alimuonya kuhusu hatari ambayo itamkabili yeye mwenyewe binafsi na kazi yake. Kwikima alijibu kuwa umoja wa Waislam ni muhimu kuliko maslahi yake binafsi. Ilipoundwa BAKWATA na hapo kuwa ndiyo mwisho wa ‘mgogoro’, Kwikima alihamishwa kutoka Dar es Salaam na kupelekwa Mwanza kama Hakimu Mkazai na Rais Nyerere akamvua madaraka ya ujaji wake. [75]
Kilichobakia baada ya kuvunjika kwa EAMWS ilikuwa ni kujaribu kuiweka BAKWATA katika mikoa kama jumuiya inayowakilisha Waislam wote wa Tanzania Bara. Mwaka mzima wa 1969 Adam Nasibu na kamati ya watu wanne walitembea katika mikoa wakiahidi msaada wa fedha kwa katibu yeyote wa zamani wa EAMWS ambae atashirikiana na BAKWATA makao makuu kuisaidia kufungua ofisi katika mkoa wake. Waislam waliipuuza BAKWATA.
Tabora ambayo haikujitoa katika EAMWS, serikali iliwaruhusu Adam Nasibu na kikundi chake kufanya mkutano wa hadhara. Kabla Adam Nasibu hajahutubia Waislam, Maulid Kivuruga mmoja wa wakongwe wa African Association na muasisi wa TANU Tabora, alipanda jukwaani kwa niaba ya Waislam wa Tabora na kuweka sharti kuwa Waislam watakuwa tayari kumsikiliza Adam Nasibu endapo Waikela mjumbe wa Tume ya Waislam iliyokuwa ikitafuta sulhu na yeye ataruhusiwa na serikali kuwahutubia Waislam ili aeleze upande wa pili wa kisa kile. Kivuruga alisema kuwa Waislam wanaomba sharti hili likubaliwe kwa sababu katika Uislam panapotokea mgogoro basi mpatanishi ni lazima asikilize pande zote mbili. Sharti hili lilikataliwa na BAKWATA na serikali. Palepale mbele ya waheshimiwa wa serikali na viongozi wa BAKWATA, Waislam wakaanza kuzomea huku wakitawanyika wakipiga takbir na wengine wakiitikia Allahu Akbar.
Siku chache baada ya tukio hili Waikela aliitwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai kusailiwa kwa nini anaipinga BAKWATA. Wakiwa ndani ya chumba cha Tabora Hotel, Geoffrey Sawaya, Mkrugenzi wa C.I.D, alimpiga maswali Waikela na kutaka kujua kwa nini yeye hayuko tayari kushirikiana na serikali kuipa nguvu na kuieneza BAKWATA. Sawaya akatoa hongo ya shilingi elfu arobaini kwa Waikela ili asaidie kuimarisha BAKWATA. Waikela kama istizai alimuuliza Sawaya kama fedha zile zilikuwa zimetoka bait mal. Waikela alikataa kupokea hongo ile. Sawaya akamtisha lakini Waikela hakutishika. Waikela aliwekwa ndani ya chumba kile akiulizwa maswali kwa kiasi cha saa nne na kisha akaamrishwa kuweka sahihi yake katika makaratasi fulani. Hili alilifanya. Waikela hakufuatwa tena na serikali. Ingawa kulikuwepo na juhudi za chinichini za kuipinga BAKWATA, juhudi hizi hazikushinda kwa kuwa BAKWATA iliweza kufungua matawi yake nchi nzima pamoja na Tabora. Wapo baadhi ya viongozi ambao hawakuweza kuhimili vishawishi vya kupokea ile hongo ya serikali na kwa ajili hii walishirikiana na serikali hivyo kuwezesha ofisi za BAKWATA kufunguliwa, hata kama zipo pale kwa jina tu. Kuangushwa kwa EAMWS kulisababishwa na watu watatu ambao wao ndiyo walikuwa mstari wa mbele kabisa – Adam Nasibu, Sheikh Kassim Juma na Abdallah Chaurembo[76] – na njama hii ikaungwa mkono na Rashid Kawawa na Abeid Amani Karume. Mkono wa Julius Nyerere na Kanisa Katoliki katika njama hii haukuonekana kabisa kama ilivyo kawaida katika njama zote za kupiga vita Uislam na Waislam Tanzania. [77]
Uchambuzi Kuhusu Dhulma
Tasnifu ya Kiwanuka toka ilipochapishwa mwaka 1973 imesimama kama ndiyo ukweli kwa yale yaliyotokea katika ‘mgogoro’ wa Waislam. Msimamo wa Kiwanuka ni kuwa Nyerere na serikali ilikuwa imefanya sawa kwa yale yaliyofanyika ili kudumisha umoja wa taifa la Tanzania. Yeye anaunga mkono dhana ya kuwa siasa na dini zisichanganywe. Vitu hivi viwili lazima vitenganishwe. Kami ilivyokuwa katika maandishi mengi kuhusu historia ya siasa ya Tanganyika, tasnifu imeshindwa kabisa kuunganisha mchango wa Waislam katika kuleta umoja wa Waafrika wa Tanganyika wakati wa kudai uhuru na kwa ajili hii tasnifu imeshindwa kueleza mategemeo ya Waislam katika Tanganyika huru. Tasnifu ya Kiwanuka haielezi ni vipi hawa Wakristo ambao wameshika madaraka katika siasa nyanja nyingine jinsi walivyoyapata na nini msingi wa madaraka hayo. Kiwanuka katika tasnifu yake anawaonyesha Waislam wakiwa katika mapambano na serikali na haonyeshi nafasi ya vyombo vya dola katika mfarakano huo. Kama angelikuwa anaielewa historia ya uhuru wa Tanganyika asingeshindwa kujua sababu za Waislam kupambana na serikali ya Tanganyika huru iliyokuwa imehodhiwa na Wakristo. Halikadhalika angelijua sababu kwa nini serikali ilikuwa inataka sana kuwa na jumuiya ya Waislam ambayo ingekuwa na mamlaka nayo na kuiamrisha kama ilivyokuwa katika taasisi nyingine za umma kama vyama wafanyakazi. Kama Waislam wangekuwa hawataki umoja wa wananchi wangemuunga mkono Sheikh Suleiman Takadir mwaka 1958 alipompinga Nyerere na AMNUT mwaka 1959. Walichokuwa wanakidai Waislam ilikuwa ni fursa sawa kati ya Waislam na Wakristo katika kugawana madaraka ya kuendesha nchi na kuwepo kwa fursa sawa katika kutoa elimu. Huku si kuchanganya dini na siasa. Huku ni kutafuta haki ili taifa lijingengeke katika misingi hiyo.
Mwaka 1963 walimu Wakristo Bukoba wakiungwa mmkono na Kanisa Katoliki, waliwapinga wagombea Waislam walioteuliwa na TANU katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Wagombea Waislam walishindwa katika uchaguzi ule. Kanisa lilikuwa limechanganya dini na siasa kwa kuwapinga Waislam wasichaguliwe kushiriki katika kuongoza nchi. Hakuna taarifa zozote zinazoonyesha kama serikali ya Nyerere ilichukua hatua yoyote dhidi ya Kanisa au dhidi ya wale wagombea Wakatoliki. Lakini Waislam walikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa kukataa utawala wa Kikristo katika TANU – chama ambacho Waislam walikiianzisha na kukijenga ili kiondoe dhulma. Halamshauri Kuu ya Taifa TANU ilifuta katika TANU Baraza la Wazee wa TANU lililokuwa na wajumbe Waislam watupu kwa kile kilichoitwa ‘kuchanganya dini na siasa’.
Kanisa Katoliki Bukoba lilikosa ujanja kwa hiyo njama zake zikaweza kugundulika mapema. Nguvu mpya dhidi ya Uislam na Waislam ilitumia ujanja na mbinu za hali ya juu na hivyo ikafanikiwa kuihujumu EAMWS na kuiweka BAKWATA kuwaongoza Waislam. Vipi serikali ambayo sifa yake ni kupinga ubaguzi wa rangi na kutetea umoja wa kitaifa, itawaruhusu kikundi kisichozidi watu watano kutumia magazeti ya TANU- The Nationalist, Uhuru, Radio Tanzania, polisi na Usalama wa Taifa, vyombo vilivyo chini ya vya dola kuamrisha utengano wa watu na kueneza siasa za ubaguzi  wa rangi. Vipi itaundwa jumuiya ya Waislam ambayo licha kuwa haina ridhaa ya Waislam wenyewe vilevile haina ulamaa hata mmoja ndani ya uongozi wake. BAKWATA haikuundwa kwa maslahi ya kumtumikia Allah. Uongozi wa Kikristo uliokuwa madarakani ulikuwa na hofu ya hali yake ya baadae huku wakikabiliana na Waislam walio huru chini ya jumuiya yao wenyewe iliyo huru na mbali na serikali na Kanisa.
Kwa kuwa serikali haikuonyesha dalili zozote za kutaka kuleta fursa sawa kwa wote katika elimu na kugawana madaraka, ikijizatiti katika kuiacha dhulma ya kikoloni iendelee, ilikuwa wazi awamu ya pili ya harakati itaanzishwa dhidi ya serikali iliyohodhiwa na Wakristo kama vile Waislam walivyopambana na udhalimu wa Kikristo ndani ya ukoloni wa Waingereza. Dalili zilikuwa wazi kuwa harakati zilikuwa zimeenza na hazitakuwa kupitia TANU kwa sababu ndani ya TANU Waislam walikuwa wameshaanza kupigwa vita. Harakati hizi za pili zilikuwa ziwe chini ya umoja wa Waislam wote. Hii ilisababisha hofu kuu kwa serikali na kwa ajili ya woga ule ikawa imejiweka tayari kujikinga na jambo kama hilo lisitokee. Kwa ajili hii serikali ikawa inavamia kila Muislam aliyedhaniwa ni tishio kwa Kanisa. Ni katika hofu hii ndiyo maana hata historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika inaogopwa kuandikwa. Hii ni moja ya njia ambayo serikali inadhani inaweza kujikinga dhidi ya hisia za Waislam.
Wakati kundi lililojitenga kutoka EAMWS huku likiungwa mkono na serikali, likimshutumu Aga Khan kwa kuwa Muasia, hakuna aliyethubutu kuonyesha kidole kwa taasisi za Kikristo katika Tanzania zinazoongozwa na Wazungu na kufadhiliwa na mataifa kadhaa ya Ulaya. Hakuna aliyethubutu kuonyesha kidole kuelekeza kwa Kanisa Katoliki ambalo lina uwakilishi wa kibalozi wa Papa nchini Tanzania. Kwa kuwa inafahamika kuwa Kanisa Katoliki linalazimisha utiifu kwa Kanisa kutoka kwa waumini wake, na kwa kuwa Kanisa lina mawakala wake katika TANU na utumishi wa serikali, ingelikuwa ni Ukristo ambao   ungehatarisha usalama wa nchi na wala si Uislam. Wakati Nyerere anawadhoofisha Waislam kwa hila za wagawe uwatawale, Wakristo walikuwa wanazidi kupata nguvu kila kukicha.
Hadi ilipofika mwaka wa 1970 vumbi la ‘mgogoro’ wa EAMWS likawa limetulia. Mwaka huo Nyerere alihudhuria semina kwa ajili ya dini na viongozi wa siasa. Semina hii kwa ujanja ilitayarishwa na Tanzania Episcopal Conference kamati ya juu kabisa ya Kanisa Katoliki inayotunga sera zote za Kanisa. Katika semina ile kwa mara ya kwanza hadharani Nyerere alizungumza kuhusu TANU na sura yake ya dini. Nyerere alisema ‘Chama chetu, TANU, hakina dini. Ni chama cha siasa tu na hakuna mipango au makubaliano na dini maalum’.[78] Maneno haya yanaweza kuwa na maana moja tu, nayo ni kuwa TANU jinsi miaka ilivyokuwa inapita, imepoteza taswira yake ya Uislam. Kuanzia mwaka 1954 TANU ilikuwa na dini na dini ya TANU ilikuwa Uislam. Historia ya TANU na harakati za kudai uhuru wa Tanganyika ndiyo shahidi wa ukewli huu. Juu ya haya yote, Waislam wanakataa kudhalilishwa na serikali na Kanisa. Waislam hawajaacha harakati za kupambana na serikali na Kanisa kwa njia mbalimbali ambazo serikali inadai ni ‘kashfa na matusi’ kwa Ukristo. Serikali imeshindwa kutuliza hasira za Waislam dhidi yake na dhidi ya Kanisa. Sababu ni kuwa wakati umebadilika. Waislam wamepoteza imani na serikali. Waislam hawaamini kuwa serikali haina dini. Waislam wametambua kuwa wanadhalilishwa na kunyimwa haki kwa kuwa serikali ni ya Wakristo. Salama yao na dini yao kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, ipo katika kuondoa dhulma inayotawala nchi kwa kuwa hivi sasa Ukristo umechukua nafasi ya ukoloni.














Sura ya Tatu
Kusalitiwa kwa Maadili
Tarehe 5 Novemba, 1985 kabla hajastaafu urais, Nyerere aliwahutubia wazee wa Dar es Salaam. Hotuba hii ilijaa simanzi, Nyerere akikumbuka jinsi Waislam walivyompokea Dar es Salaam kwa mapenzi makubwa ingawa yeye alikuwa Mkristo. Wazee hawa wengi wao walikuwa wanachama wa zamani wa TANU waliomuunga mkono Nyerere wakati wa kudai uhuru. Nyerere aliusifia mchango wa Waislam katika kipindi kile kigumu cha kudai uhuru. Nyerere alisema kuwa upogo katika elimu uliorithiwa na serikali yake kutoka kwa Waingereza baina ya Waislam na Wakristo yeye ameuondosha katika kipindi cha utawala wake:
Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo. Sasa nipo katika hali ya kufarahisha kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama Mbunge mpya, Waziri, au Katibu Mkuu katika wizara zetu za serikali, ni Muislam au Mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa utambulisho. Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa dini kwa kuwa tuna Wakristo wenye majina ya Kiislam, na Waislam wenye majina ya Kikristo. Kuvumiliana huku nyie ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia maadili haya kwa niaba yenu.[79]
Hotuba hii ilikuwa ya ulaghai. Ukweli ni kuwa miongo mitatu baada ya uhuru Waislam hawajanufaika chochote wako katika hali ile ile aliyowaacha wakoloni au mbaya zaidi. Sivalon  amefichua kuwa Kanisa limeweza kujenga himaya yake ambayo inahodhi asilimia sabini na tano za viti katika Bunge la Tanzania. Kati ya viti hivyo asilimia sabini vipo mikononi mwa Wakatoliki na vilivyobaki vimegawika kati ya Waislam na Wakristo wa madhehebu nyingine.[80] Baada ya kupatikana uhuru, Kanisa lilipohisi wasiwasi, limeweza kwa urahisi kabisa kuwazuia na kuwadhibiti Waislam. Serikali imeweza kutumia nguvu iliyokuwanayo katika kudhibiti siasa kuzuia harakati za Waislam  kudai fursa sawa na Wakristo katika kugawana madaraka katika serikali. Kanisa limehakikisha kuwa kupinduliwa kwa ukoloni si kizingiti kwa Ukristo, ingawa ingetegemewa kuwa Kanisa lingedhirika kwa kuanguka kwa ukoloni. Katika miaka yake zaidi ya mia moja, Kanisa lilikuwa limestarehe kama muokozi wa nafsi na watu wenyewe. Kanisa lilikuwa salama na halikupambana na msukosuko wowote kutoka kwa serikali kwa kuwa lilikuwa Kanisa ndilo lilishika hatamu ya serikali.
Baada ya kueleza hayo yote ni muhimu sasa kuangalia jinsi ukereketwa wa Kikristo unavyofanya kazi katika serikali na jinsi kazi hiyo inavyoathiri Uislam. Wizara ya Elimu inachukuliwa kama mfano kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii. Katika wizara hii, inaweza kuonekana kwa uwazi kabisa jinsi Ukristo unavyofanya kazi na jinsi udini ulivyoshamiri katika kugawa nafasi muhimu kati ya Waislam na Wakristo. Ilikuwa katika wizara hii katika historia ya Tanzania ndipo kwa mara ya kwanza waziri Muislam alipochaguliwa kuongoza wizara, Kanisa likaingilia kati waziwazi kumpiga waziri vita na kuhoji nafasi nyingine za juu ambazo zilipewa Waislam. Serikali haikuweza kupingana na Kanisa na waziri huyo, marehemu Profesa Kighoma Ali Malima aliondoshwa katika wizara hiyo.
Mwaka 1987 Profesa Malima aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa Muislam wa kwanza kushika nafasi hiyo. Mawaziri wanane waliopita walikuwa Wakristo. Kulikuwa na malalamiko kutoka kwa Waislam kuwa wizara hiyo imegeuzwa jimbo la Wakristo, hasa pale padri alipoteuliwa na Julius Nyerere kuongoza wizara hiyo. Profesa Malima aliposhika wizara hiyo aliona upo umuhimu wa kufanya marekebisho kadhaa ili kurejesha imani ya Waislam katika wizara hiyo. Kulikuwa na tuhuma kuwa Wizara ya Elimu ilikuwa ikiwabagua vijana wa Kiislam kupata nafasi katika vyuo vya elimu ya juu na ilikuwa ikizuia kupanda vyeo kwa Waislam.
Profesa Malima alipoona dhulma ile iliyokuwapo katika wizara ile dhidi ya Waislam, Profesa Malima aliwateua Waislam wanne kushika nafasi katika kurugenzi mbalimbali na akaandika taarifa ya siri kwa Rais Ali Hassan Mwinyi [81]kumtaarifu udini [82] alioukuta katika wizara ile. Katika taarifa ile kwa rais,[83] Profesa Malima alieleza kuhusu kudumazwa kwa Waislam katika mgao wa elimu. Taarifa hii ilivuja kwa vyombo vya habari[84] na kwa Wakristo wengine. Katika watu walioipata taarifa hii ni Rais Mstaafu Julius Nyerere wakati ule akiwa Mwenyekiti wa chama tawala CCM.
Kuwekwa kando kwa Waislam kupo wazi kiasi ya kuwa mtafiti haihitaji hata kufanya utafiti wa kina unaopewa nguvu na takwimu. Mtafiti yeyote wa sayansi ya jamii hatoweza kushindwa kuona ukweli huu kwa macho tu. Hali hii inaonekana katika kila nyanja ya maisha. Utafiti wa kwanza katika tatizo hili la Waislam kudhulumiwa katika ugawaji wa madaraka ulifanywa na vijana wa Kiislam katika jumuiya yao iliyokuwa ikijulikana kama Warsha ya Waandishi wa Kiislam, kwa ufupi ikijulikana kama Warsha.
 Kanisa kwa mara ya pili tokea mwaka 1963 ilipata wasiwasi kuhusu mabadiliko ambayo yalikuwa yanafanyika katika Wizara ya Elimu. Lakini katika miaka ya 1980, hali ya mambo yalikuwa yamebadilika sana.  Waislam walikuwa wamejizatiti nje ya mfumo wa siasa kiasi ya kuwa hapakuweza kupatika kibaraka katika Waislam ambae angekuwa tayari kutumika kulihami Kanisa. Hali ya uhasama wa wazi kati ya Waislam na serikali ilikuwa imejitokeza wazi kabisa. Hata hivyo mawakala wa kanisa katika serikali walimshutumu Profesa Malima kwa kuwa Muislam mwenye ‘siasa kali’. Profesa Malima akatakiwa ahojiwe mbele ya Kamati Kuu ya CCM kwa kuingiza hisia za kidini ambazo zimesababisha uadui baina ya waumini wa dini hizi mbili. Suala hili likajadiliwa Dodoma chini ya uenyekiti wa Julius Nyerere. Lakini badala ya kujadili suala la dhulma kwa Waislam na kulitafutia ufumbuzi, yule anaedhulumiwa ndiye aliyewekwa kizimbani badala ya dhalim anaedhulumu; msukumo wa mjadala ukawa katika uteuzi wa wakurugenzi wanne Waislam aliofanya Profesa Malima katika Wizara ya Elimu. Profesa Malima alionekana amekiuka mwenendo na taratibu zulizodumu katika wizara ile kwa kipindi kirefu ya kuwa ni Wakristo pekee wenye haki ya kushika nafasi za juu katika wizara za serikali. Kwa ajili hii profesa Malima akavuliwa madaraka kama Waziri wa Elimu. Rais Mwinyi alikuwa hana uwezo wa kuhimili nguvu ya Kanisa. Nchi inayodai kuwa ni ya kisekula ilikuwa imeshindwa kwa mara nyingine kuwapa Waislam haki yao waliyohakikishiwa na katiba ya Tanzania.
Kwa nchi ambayo inajigamba kuwa inajali usawa kwa wananchi wake inashangaza kuona kuwa Waislam wanabaki nyuma na juhudi zozote ambazo Waislam watafanya ili kuondoa upogo kati yao na Wakristo na kujiletea maendeleo zinapata upinzani na uadui kutoka na mfumo ule ule unajidai kuwa unasimamisha usawa na haki. Kitu cha kusikitisha ni kuwa hakusimama hata Muislam mmoja katika wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM kumuunga mkono Profesa Malima kwa dhulma ambayo wote walikuwa wanafahamu kuwa imedumu kwa kipindi kirefu. Hata ndani ya Bunge hakuna Muislam aliyekuwa na ujasiri wa kumtetea Profesa Malima.[85] Muislam mmoja, Mwenyekiti wa Mkoa wa Pwani, Masudi Mtandika, aliungana na kambi ya Wakristo katka Kamati Kuu ya CCM kumshambulia Profesa Malima. Msimamo wa Mtandika ulikuwa sawa na ule wa Rajab Diwani na Selemani Kitundu walipomshambulia Bibi Titi Mohamed wakati Kamati Kuu ya TANU ilipokuwa ikijadili EAMWS mwaka wa 1963. Kampeni ya chuki na propaganda dhidi ya Profesa Malima ikaanzishwa na vyombo vya habari ambavyo vyote vilikuwa chini ya miliki ya Wakristo na hivyo chini ya Kanisa.
Aboud Jumbe, [86] rais wa zamani wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania, amefanya utafiti kuhusu nafasi ambazo wameshika Waislam katika serikali, Bunge na vyuo vya elimu ya juu. Takwimu alizoonyesha Aboud Jumbe zinatisha. Katika baadhi ya taasisi Waislam wanaonekana kwa kutokuwepo katika taasisi hizo. Utafiti wa Jumbe ulikuwa wa pili katika kueleza tatizo hili la Waislam na kuliweka wazi kwa matumaini ya kuwa labda serikali ingeweza kuhisi kuwajibika na kujaribu kusahihisha makosa hayo.
Majaribio mengine yamewahi kufanyika huko nyuma na watu kama Sheikh Abubakar Mwilima, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa JUWATA na katika Kamati Kuu ya chama tawala CCM, alijaribu kuieleza serikali tatizo hili la Waislam. Kitu kimoja mashuhuri kwa wote waliojaribu kuliweka tatizo hili mbele ya serikali wote hao walimalizwa kisiasa. Maisha yao katika siasa yalikatizwa – Chifu Abdallah Said Fundikira, Tewa Said Tewa, Bibi Titi Mohamed, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Mussa Kwikima, Sheikh Abubakr Mwilima, Profesa Kighoma Malima na wengine wengi. Ilikuwa kuanzia hapa ndipo Waislam walianza kunong’ona kuhusu njama dhidi yao. Kuwepo kwa njama dhidi ya Waislam kulikuja kudhihirishwa pale watafiti wa Kikristo walipoanza kufanya utafiti kuhusu athari za Ukristo katika utawala wa dola; na bila kujali matokeo ya utafiti kwa hisia za Waislam wakawa wanaeleza jinsi Waislam kwa hila na msaada wa serikali walivyowekwa pembeni katika kugawana madaraka na Wakristo.

Uthibitisho wa Njama Dhidi ya Uislam
Hivi sasa kuna vitabu viwili vilivyoandikwa na Wakristo wenyewe vinavyothibitisha kuwa Wakristo wametumia nyadhifa zao katika serikali kuuhujumu Uislam na Waislam. Jan P van Bergen katika kitabu chake, Development and Religion in Tanzania, (1981) [87] ametoboa siri kuhusu uadui aliokuwa nao Nyerere dhidi ya Uislam na Waislam. Kitabu kinaeleza kwa ufasaha jinsi Nyerere wakati alipokuwa madarakani alivyokuwa akifanya mikutano ya siri na viongozi wa Kanisa kuweka mikakati ya kuupa nguvu Ukristo. Katika mikutano hiyo Nyerere aliwahakikishia viongozi wa Kanisa kuwa anaaunga mkono Ukristo. Kitabu hicho kinaeleza jinsi Nyerere alivyotimiza ahadi yake hiyo kwa Kanisa kwa kuhakikisha kuwa anawapa Wakristo nafasi za juu katika serikali na chama. Kitabu hiki kilikuwa kinauzwa Catholic Bookshop, Dar es Salaam. Lakini ilipokuja kudhihirikia Kanisa kuwa kitabu hiki kilikuwa kinatoa habari nyeti na siri za Kanisa kuhusu njama dhidi ya Waislam, kwa haraka sana kikaacha kuuzwa. [88] Hadi hivi sasa kitabu hicho ni marufuku kuletwa tena Tanzania.
Kitabu cha pili ni cha Dr John C. Sivalon, Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985 (1992). [89] Kitabu hiki kinaeleza njama ndani ya serikali kuuhujumu Uislam. Sivalon anafichua kuwa kuanzia mwaka 1961 baada ya Tanganyika kupata uhuru, Kanisa lilikuwa na hofu mbili. Hofu ya kwanza ilikuwa umoja wa madhehebu za Kiislam kati ya Sunni, Bohora, Ismailia na Ithnasheri. Hofu ya pili ilikuwa kuhamishwa kwa makao makuu ya EAMWS kutoka Mombasa kuja Dar es Salaam. Kanisa lilikuwa linahofu kuwa mali walizokuwanazo Waasia Waislam zikitiwa katika harakati za Waislam ambao walikuwa na nguvu kubwa katika  uwanja wa siasa zitaathiri maslahi ya Ukristo katika Afrika ya Mashariki. Kwa ajili hii Kanisa likatanganza kuwa Uislam ni adui wake na ikaanza mikakati ya hujma dhidi ya Uislam ili kuudhoofisha. [90] Kuna kazi mbili zilizoandikwa na Waislam kuhusu uhusiano baina ya serikali na Waislam. Kazi ya kwanza ni tasnifu ya Kiwanuka, ‘The Politics of Islam in Bukoba District’ (1973); [91] kazi ya pili ni makala ya utafiti ‘Islam and Politics in Tanzania’ (1989) [92] iliyoandikwana mwandishi wa kitabu hiki. Ilikuwa baada ya kusoma tasnifu ya Kiwanuka na kuona jinsi ukweli wa kuvunjwa kwa EAMWS kulivyopoteshwa ndipo kama Muislam na kama ada ya Uislam inavyodai kuwa pande mbili za mgogoro zote lazima zisikilizwe, ndipo nilipoamua kufanya utafiti na kuandika tatizo lile kwa mtazamo wa Waislam. Ukweli ambao kwa miongo miwili ulizuiwa usifahamike kwa Waislam. Kiwanuka anadai na kuafiki kuwa Nyerere alikuwa na haki ya kutumia vyombo vya dola dhidi ya Waislam kwa kuwa kama asingefanya hivyo nchi ingekuwa na mamlaka mbili, yaani ya Waislam na ya serikali. Kwa ajili hii aliamua kuivunja EAMWS ili ‘kulinda umoja wa kitaifa’.
Halikadhalika ipo ‘Kwikima Report’ (1968)[93] ambayo imeeleza kwa ufasaha tatizo la EAMWS, chanzo chake na mchango wa serikali katika kuhujumu umoja wa Waislam. Taarifa hii inafaa kutumika leo kama dira ya kuelewa tatizo la Waislam wa Tanzania kama ilivyokuwa wakati ule ilipotolewa kwa mara ya kwanza. Taarifa ya Kwikima inaeleza jinsi TANU, serikali na Waislam wachache katika TANU walivyodanganyika kudhani kuwa katika kuisaidia serikali kuivunja nguvu EAMWS walikuwa wanatimiza uzalendo na maslahi ya taifa. Rejea hizi tano ni muhimu kwa wanafunzi wa historia ya siasa Tanzania; na kwa mtafiti yeyote anaetaka kujua chanzo cha chuki baina ya Waislam na serikali na chanzo cha hisia kali za kidini zinazoikumba nchi yetu kuanzia miaka ya 1980. [94] Rejea zote hizo za vitabu, makala za utafiti na taarifa mbalimbali, ingawa zimeandikwa na waandishi tofauti na kwa muelekeo tofauti zote hizi zinadhihirisha kitu kimoja – kuwepo kwa njama zinazoendelea kwa zaidi ya karne moja dhidi ya Uislam na Waislam, kwanza zilikuwa zikifanywa na wakoloni walioitawala Tanganyika na sasa zinafanywa na Wakristo wananchi kuhakikisha kuwa Uislam haupati nguvu. Kama hali ndiyo hii vipi Uislam hadi leo bado upo Tanzania na unazidi kupata nguvu kila kuchao? Jibu lipo ndani ya Qur’an.
Hivi sasa Waislam wanamshutumu Mwalimu Nyerere na uongozi wa Kanisa kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na Waislam ambao ndiyo waliopigania uhuru wa Tanganyika. Waislam wa Tanzania hivi sasa ni kama wanazaliwa upya. Kila kukicha wanatafakari hali yao na jinsi historia yao ilivyokuwa ya kishujaa na ya kupendeza kwa namna walivyopambana na wakoloni, kuanzia vita vya Maji Maji mwaka 1905 hadi kuanzishwa kwa African Associatioin mwaka 1929 na TANU mwaka 1954; hadi uhuru ukapatikana mwaka 1961. Waislam wanaamini kuwa baadhi ya majibu ya matatizo yanayowakabili hivi sasa yapo kwenye hii historia yao ya kudai uhuru.
MWISHO


















[1] A.A. Ahmed, ‘Lamu’s Sacred Meadows’, Fountain, April-June, 1995 Vol. 2 No. 10, p.30.
[2] August H. Nimtz Jr, Islam and Politics in East Africa, University of Minneapolis, 1980, p.11.
[3] See Family Mirror, Second Issue, November 1994, uk. 6.
[4] Ali A. Mazrui, ‘African Islam and Competitive Religion: Between Revivalism and Expansion’, in Third World Quarterly Vol. 10. No. 2 April 1988, uk. 499-518.
[5] D.B. Barret, Frontier Situations for Evangilisation in Africa, Nairobi, 1976.
[6] Africa South of the Sahara, Europa Publication, London, No. 20, 1991, uk. 1027.
[7] Utafiti wa kuaminika kidogo ni ule uliofanywa na Dar es Salaam University Muslim Trustee (DUMT), Angalia ‘The Position of Muslims and Islam in Tanzania’, katika Al Haq International, (Karachi) September/October 1992.
[8] Angalia Kiongozi No. 6 June 1950. Kwa maelezo zaidi kuhusu kueneza kwa wamisionari Afrika ya Mashariki, angalia M. Langley & T. Kiggins: A Serving People, Oxford University Press, Nairobi, 1974, uk. 19.
[9] Mengi kuhusu kuingia kwa wamishionari wa mwanzo mwandishi ameandika kwa msaada wa Dr. Hamza Njozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
[10] C.D. Kittler, The White Fathers, London 1959, uk. 22-23 vilevile  R. Clarke (ed) Cardinal Lavigerie and Slavery in Africa uk. 302.
[11] Angalia  ‘Proceedings of CMS 1880-8’, uk. .22-23.
[12] Angalia I.N. Kimambo,  na A.J.A. Temu, History of Tanzania, EAPH, Nairobi, 1969 uk. 126.
[13] Katika kuuhisha vita dhidi ya Uislam serikali ya Tanzania mwaka wa 1993 ilitiliana sahihi mkataba na makanisa, mkataba uliokuja kujulikana kama Memorandum of Understanding makubaliano ambayo yalikuwa serikali kuidhinisha elimu, huduma za jamii na afya ziendeshwe na Christian Council of Tanzania (CCT) and Tanzania Episcopal Conference (TEC) kwa kushirikiana na serikali. Mkataba huu ulitayarishwa kwa siri  na Dr. Costa Mahalu, wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na ukatiwa sahihi na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Mkataba huu ulitiwa sahihi bila ya kuwashirikisha  au kuwafahamisha Waislam. Ili makubaliano haya  yaweze  kutekelezeka, serikali ilibidi ifanye marekebisho kifungu 30 cha  Education Act No. 25, 1978.

[14] H.B Hansen, Mission, Church and State in Colonial Setting: Uganda 1890-1925, London 1984, uk. 26, vilevile angalia Ali M. Kirunda, “Uganda Muslims and their problems,” The Monitor June 4-June 8, 1993.
[15] Abel Ishuwi, Education and Social Change, (1980).

[16] Angalia P. Gerold Rupper, OSB, Pugu Hadi Peramiho: Miaka 100 ya Wamisionari Wabenediktini Katika Tanzania, Benedictine Publications, Ndanda-Peramiho, 1980, uk. 31-42.
[17] Angalia Yusuf Halimoja, Historia ya Masasi, East African Literature Bureau, Nairobi, uk. 163-175. Kwa kupata habari zaidi jinsi Wakristo walivyopigana upande wa Wajerumani katika Vita ya Maji Maji ili kulinda Ukristo dhidi ya kile kilichoonekana kuwa ni jihad, angalia Nimitz, op.cit. uk.12-13.
[18] C.H. Becker, ‘Material for the Understanding Islam in German East Africa’, Tanzania Notes and Records, No. 68, 1968, p. 58.
[19] Al Jamiatul  Islamiyya ‘A’ iliundwa mwaka 1940 kutokana na mgogoro ulioanzishwa na Liwali wa Dar es Salaam wakati ule, Ahmed Saleh akishirikiana na Waingereza.
[20] Congress ilikuwa imegubikwa na matatizo ya ugomvi kati ya viongozi wake. Angalia Reporter (Nairobi), March – June, 1963. AMNUT ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini ilikuwepo tamaa kuwa huenda kikapata nguvu mpya. Kassanga Tumbo aliyekuwa katibu wa TRAU ambae Nyerere alimteua balozi Uingereza, alikuwa amejiuzulu ubalozi akarudi Tanganyika na kuanzisha chama cha upinzani, Tanganyika Democratic Party. (TDP). Kulikuwa na mazungumzo ya kuunganisha TDP na AMNUT. Nyerere alifahamu kuwa endapo Waislam watamuunga mkono Tumbo utawala wake ungekuwa mashakani.Inasemekana kuwa nafasi ilie ya ubalozi Uingereza awali Nyerere alimpa Hamza Mwapachu. Mwapachu aliikataa kwa kuwa alihisi hiyo ilikuwa njama ya Nyerere kumeweka mbali na siasa nchini. Ilikuwa matumaini ya Mwapachu kuwa Nyerere angelimpa uwaziri ili achangie pamoja nae katika kuijenga nchi.
[21] Tanganyika Standard, 2 May, 1961.
[22] Kilichofuata baada ya kupatikana uhuru ilikuwa ni kukamatwa, kuwekwa kizuizini na kuhamishwa kwa masheikh na Waislam wengine waliodhaniwa kuwa wanapinga utawala wa Nyerere. Mashuhuri miongoni mwao walikuwa: Abdillah Schneider Plantan, Sheikh Abdulkarim Abdulwahid, Maalim Popo Saleh, Suleiman Masudi Mnonji, Ali Migeyo, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Sharff Hussein Badawiy, Shariff Mwinyibaba, Shariff Adnan, Bilali Rehani Waikela, Sheikh Jumanne Bias, Maalim Matar, Abdalah Mwamba, Sheikh Hashim Haji Abdallah, Sheikh Nurdin Hussein, Salum Abdallah Popo, Sheikh Mzee Ali Comoriam, Sheikh Al Amin Maftah, Rajab Kiguu cha Mbuzi na wengine wengi.
[23] Tanganyika Standard, 15 April, 1961. Kwa hoja kama hiyo angalia vilevile John Hatch, Two African Statesmen, London, 1976, uk.128.
[24] Press Release B/1629/62 10th December, 1962.
[25] Tanganyika Standard, 12 th March, 1963. 
[26] K. Mayanja Kiwanuka, op. cit. uk. 57-58.
[27] Report ya East African Muslim Welfare Society, January/February 1961.

[28] Kwa maelezo kamili ya mgogoro wa Waislam wa mwaka 1968, angalia M. Said, ‘Islam and Politics in Tanzania’, op. cit. Vilevile angalia ‘Kwikima Report’ katika The Standard, 12 th December, 1968, na katika The Nationalist, 24 th October, 1968.
[29] Mwaka wa 1963 hawa wafuatao ndiyo walikuwa viongozi wa EAMWS: Tewa Said Tewa, Aziz Khaki, Bibi Titi Mohamed, Saleh Masasi, Abdallah Jambia, Khamis Kyeyamba na Bilali Rehani Waikela.
[30] Kwa kiasi cha siku mbili Nyerere alikuwa hafahamiki yuko wapi. Wanajeshi walikuwa wakiwasiliana na Oscar Kambona kujaribu kutatua mgogoro uliokuwepo. Dossa Aziz ndiye aliyemtorosha Nyerere kutoka Ikulu akapita nae lango kuu Nyerere akiwa amejificha katika gari la taka chini ya takataka. Dossa akiwa na bunduki yake alienda na Nyerere hadi Kigamboni kwenye nyumba iliyokuwa ufukweni pwani ambayo ilikuwa ikitumiwa na Gavana kama mahali pa kupumzika. Baadae Rashid Kawawa aliyekuwa makamo wa rais alikwenda pale na wakawa pamoja na Kambona ambae alikuwa kiungo kati ya serikali na wanajeshi walioasi. Nyerere mwenyewe hajakieleza kisa hiki kwa yoyote. Baada ya kujitokeza waandishi wa habari walimuuliza alikuwa wapi wakati wote wa uasi wa wanajeshi. Nyerere kwa ukweli kabisa alijibu, ‘Nilikuwa Dar es Salaam’.
[31] Katika utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi na baada ya kupita miaka zaidi ya thelathini, amri ya kufukuzwa Sharif Hussein ilibatilishwa na akarudi Tanzania. Kwa kauli yake mwenyewe Shariff Hussein alimfahamisha mwandishi kuwa yeye wakati wa uhuru alikuwa akishiriki katika dua nyingi za kumuombea Nyerere mafanikio. Shariff Hussein akasema lakini malipo yake kutoka kwa Nyerere ilikuwa ni kumfukuza nchini.
[32] Viongozi wa EAMWS walitishwa na makachero wa serikali watupe nyaraka na kumbukumbu zote za EAMWS au sivyo serikali itawachukulia hatua. Viongozi wengi walitishika na kuchoma moto majalada yao. Waikela alihifadhi nyaraka na majalada yake yote hadi yakamfikia mwandishi baada ya  zaidi ya miaka ishirini baada ya kufungiwa jumuiya hiyo. Regional Commissioner wa Jimbo la Magharibi wakati ule alikuwa Rashid Heri Baghdelleh yeye alikwenda kuonana na wafungwa wa siasa katika jela ya Uyui akiwa na salamu kutoka kwa Rais Nyerere kuwa wafungwa wa siasa waombe msamaha na yeye atawaacha huru. Waikela alikataa kuomba msamaha na hoja aliyotoa ilikuwa yeye hajatenda kosa lolote kwa hiyo haoni haja ya kuomba msamaha. Baada ya kutoka kizuizini mwaka 1965, Waikela alikuta ofisi ya EAMWS Tabora imefungwa na Waislam wanatishwa na serikali wasiifungue. Waikela aliwashawishi Waislam wakusanye sahihi zao na wamplekee kuomba ofisi ifunguliwe. Hili lilifanyika na ofisi ile ikafunguliwa upya chini ya Waikela na ikaendelea kutoa huduma kwa Waislam kwa miaka mitatu hadi serikali ilipoivunja EAMWS mwaka wa 1968. Hivi sasa Waikela ni mtu mzima na bado anajishughulisha na kuendeleza harakati za kueneza Uislam.
[33] Tabligh ilikuwa imepata mafanikio makubwa kiasi kuwa katika mkutano wa EAMWS wa mwaka 1966 Tewa Said Tewa aliomba kuwa taarifa maalum itolewe katika mkutano ujao kuonyesha takwimu za Wakristo waliorudi katika Uislam.
[34] Tewa Said Tewa, ‘A Probe…’
[35] Tewa op.cit.
[36] Habari katika sura hii zinatokana na mahojiano kati ya mwandishi na Tewa Said Tewa, Bilali Rehani Waikela na Ali bin Abbas mmoja wa wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir. Habari nyingine zinatoka kwenye mswada wa Tewa ambao haujachapishwa, ‘A Probe in the History of Islam in Tanzania’. Tewa aliandika habari hizi kuhusu harakati za Waislam kujiletea maendeleo chini ya EAMWS miaka kumi na nne baada ya aliekuwa rais wa Tanzania Julius Nyerere kuivunja.
[37] Tewa Said, ibid.
[38] Angalia Kiwanuka, op. cit. uk. 75.
[39] Ibid.
[40] Benjamin Mkapa alishinda uchaguzi na kuwa rais wa tatu   wa Jamuhuri ya Tanzania mwaka 1995.
[41] Nyerere alizidi kutishika pale mara baada ya maulidi yale yaliyofanikiwa, mwezi Julai, 1968 Tewa akifuatana na masheikh wawili, Athumani Manzi na Sheikh Minshehe Mgumba akafanya safari ya kutembelea Dodoma, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa, Tabora na Kigoma. Huko kote Waislam walikuwa wakijitokezakwa wingi kumpokea kiongozi wao. Tabora ulifanyika mkutano mkubwa uliohutubiwa na Sheikh Jumanne Biasi na Rehani Bilali Waikela. Kigoma Tewa alifanyiwa mapokezi makubwa akasindikizwa na magari hadi Ujiji msafara ukiongozwa na Sheikh Khalfani Kiumbe. Katika ziara hizi Tewa alikuwa akifungua shule zilizokuwa zimejengwa na EAMWS. Ilikuwa Kigoma ndipo Tewa Said Tewa alipoonyeshwa barua kutoka kwa Adam iliyoambatanishwa na miniti za mkutano kati ya Sheikh Abdallah Chaurembo na Sheikh Ramadhani Chaurembo akiuandikia uongozi wa EAMWS Kigoma akiwaomba Waislam wajitoe kutoka EAMWS kwa sababu ilisoma maulidi Ilala. Aliporudi Dar es Salaam Tewa aliufahamisha uongozi wa makao makuu kuhusu barua ile.
[42]  Taarifa ya Kamati ya Utendaji EAMWS Mkoa wa Tanga 23rd Oktoba, 1968, Ripoti ya Sheikh A.J. Jambia.
[43] Kiwanuka, op.cit., uk. 2.

[44] Angalia Ripoti ya Kwikima katika The Standard, 12th Desemba, 1968. Vilevile The Nationalist, 24 Oktoba, 1968.  
[45] Angalia Ripoti ya Kwikima.
[46] Tewa, ‘A Probe…’
[47] Ujenzi wa Chuo Kikuu ulikuwa umeanza na jiwe la msingi lilikuwa limewekwa na Julius Nyerere rais wa Jamuhuri ya Tanzania.
[48] Tume ya Uchunguzi ya Waislam ilikuwa na wajumbe wafuatao: Mussa Kwikima (Dar es Salaam), Rajab Ukwaju (Mara), Dr. Hussein Lweno (Dar es Salaam), Mussa Nabahani (Lindi), Bilali Rehani Waikela (Tabora), Abdul Karim (Tanga) na Khamis Khalfani (Dodoma).
[49] Tewa ibid.
[50] Barua ya Mwenyekiti Halmashauri ya Uchunguzi Mogogoro ya Waislam kwa Waziri wa Habari na Utangazaji, 21 Novemba, 1968.
[51] The Nationalist, nukuu kutoka kwa Kiwanuka, uk.81.
[52] Maelezo kutoka mwanakamati wa Halmashauri Kuu ya TANU ambae ameomba jina lake listiriwe.
[53] Mwezi Novemba 1967 Tewa Said Tewa alikuwa amefanya ziara ya Mwanza na Bukoba iliyokuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa alifanya majadiliano na viongozi wa Waislam wa huko kama Sheikh Amin Abdallah wa Mwanza, Sheikh Ali Migeyo na Sheikh Suedi Kagasheki wa Bukoba.
[54] Kiwanuka, uk.2-3.
[55] Ibid., p.81
[56] The Standard, 9th November 1968 nukuu kutoka Kiwanuka p. 81. Vilevile angalia The Standard, 20 November 1968.
[57] Sheikh Hassan bin Amir alianza kukosana na serekali mara tu baada ya uhuru pale Kanisa Katoliki ilipotoa vitu vya kukumbuka uhuru vilivyokuwa vimenakshiwa na picha za Kikristo. Sheikh Hassan bim Amir alikereka na hili na hasa pale George Kahama, Waziri wa Mambo ya Ndani, alipokwenda Italia kuweka uhusiano baina ya Tanganyika na Vatikano. Kuanzia hapo, Sheikh Hassan bin Amir, kupitia Daawat Islamiyya na kwa kupitia wanafunzi  wake waliokuwa wameenea nchi nzima alianza kuandika khutba za Ijumaa na kuzisambaza katika misikiti ya nchi nzima na khutba hizo zikawa zinasomwa katika sala ya Ijumaa. Ujumbe wake kwa Waislam ulikuwa Waislam watumie fursa iliyoletwa na uhuru kwa kujielimisha ili wagawane madaraka sawa na Wakristo katika kuiendesha nchi. Sheikh Hassan bin Amir akaanzisha mfuko wa elimu ambao Waislam walitakiwa kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule. Kwa ajili ya kuingia kwake kati pale Nyerere alipotaka kuivunja EAMWS, Sheikh Hassan bin Amir akaonekana ni kikwazo kwa Ukristo kuukalia juu Uislam.
[58] Sheikh Kassim Juma aliitumikia serikali kwa karibu miaka ishirini hadi mwaka 1992 ghafla akaanza kuishitumu serikali na kumtaja Nyerere kama mtu aliyepanga njama za kuuhujumu Uislam. Sheikh Kassim alikamatwa mara mbili na kuwekwa ndani kwa kosa la ‘kuwachonganisha Waislam dhidi ya serikali’. Alipotolewa afya yake ikawa mbaya na akafa mwaka 1993. Historia fupi ya Sheikh Kassim ipo katika Al Haq Newline,(Pakistan) No.1 Muharram/Safar, 1415-A.H. ‘Sheikh Kassim bin Juma bin Khamis 1940-1994’
[59] Baada ya kundi la Adam Nasibu kutoka Tanga masheikh wakaanza kukamatwa na kuwekwa kizuizini na ni wakati huo Saleh Masasi alitangaza kujitoa kwa Iringa.
[60] Miaka mingi baadae Rashid Kawawa alisema kuwa anajuta kuunga mkono kukamatwa kwa Mufti wa Tanganyika na Zanzibar, Sheikh Hassan bin Amir akaelekeza lawama kwa wale waliomshauri kufanya hivyo.
[61] Ali Muhsin, op.cit. uk 87.
[62] Nyaraka za Tewa hazikuonyesha ni gazeti lipi lakini kwa kuwa wakati ule Tanzania magazeti ya Kiingereza yalikuwa mawili, The Nationalist gazeti la TANU na The Standard lililokuwa likimilikiwa na Lonrho, ni wazi gazeti lileThe Standard.
[63] Angalia Kwikima Report.
[64] Pamoja na mambo mengine Taarifa ya Tume ya Kwikima ilipendekeza mabadiliko katika katiba ya EAMWS, kuondolewa kwa nafasi ya Patron, kuasisiwa kwa jumuiya mpya ya Kiislam itakayokuwa haina ubaguzi wa rangi na taarifa ilisisitiza jumuiya mpya kutochanganya dini na siasa.
[65] Ibid.
[66] The Nationalist,15 December, 1968.
[67] Baraza,(Nairobi), 12 Desemba, 1968.
[68] Rashid Kayugwa Afisa wa Usalama Taifa, Dar es Salaam ndiye aliyepewa kazi ya kudumisha mawasiliano kati ya kundi la Adam Nasibu serekali. Kayugwa ndiye aliyekuwa akielekeza kundi la Adam Nasibu mbinu za propaganda na nini kifanyike na kwa wakati gani ili kuvunja umoja wa Waislam. Kayugwa alikuwa amepata mafunzo yake ya ukachero Israel, Checkoslovakia na Marekani. Katika kuhakikisha mafanikio ya mkutqano wa Iringa, Kayugwa ambae ni mzaliwa wa Iringa alipendekeza mkutano wa Waislam wa Taifa ufanyike Iringa kwa kuhofu vurugu na upinzani kutoka kwa Waislam wa Dar es Salaam. Baada ya kusoma kitabu cha Padri John Sivalon kilichoeleza kuwa Kanisa baada ya uhuru liliendesha hujuma dhidi ya Uislam na Waislam kwa kupitia serikali, ndipo ilipomdhihirikia ukweli na kuona kuwa alipokuwa akitumiwa kuhujumu EAMWS hakuwa akitumikia serikali kama alivyokuwa anadhani bali alikuwa akilitumikia Kanisa, kama kuomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu, aliamua kueleza mchango wake katika kuwahujumu Waislam na Uislam ili iwe fundisho na onyo kwa Waislam watakao kuwa katika utumishi wa vyombo kama hivyo siku za usoni. Kabla ya kufa kwake alieleza masikitiko yake kwa kukandamizwa kwa Waislam na akatoa mfano wake mwenyewe wa kutopandishwa cheo katika Usalama wa Taifa kwa sababu tu yeye alikuwa Muislam.
[69] Tewa ibid.
[70] Angalia Kiwanuka, uk.85. Vilevile Proceedings of the Iringa Conference 12th – 15th December,1968 katika Maktaba ya Chama cha Mapinduzi, Dodoma. Vilevile The Standard, 18th December, 1968.
[71] The Standard,18th December, 1968.
[72] The Standard, 20th December 1968.
[73] Ibid.
[74] Tewa, ibid. Vilevile angalia The Standard, 20th December 1968.
[75] Kiwanuka, uk. 86. Habari nyingine kuhusu Mussa Kwikima zimepatikana katika mazungumzo na yeye mwenyewe Kwikima pamoja na maelezo kutoka kwa Bilali Rehani Waikela. Katika mabadiliko makubwa na bishara Mussa Kwikima ndiye alisimama mahakamani kumtetea Sheikh Kassim Juma wakati aliposhtakiwa kwa ‘kuwachonganisha Waislam na serekali’. Sheikh Kassim Juma alikuwa akimpiga vita Kwikima wakati akiwa katibu wa Tume ya Waislam chini ya EAMWS, Kwikima alipokuwa akitafuta sulhu baina ya pande mbili.
[76] Pamoja na watu hawa watatu wengine waliokuwa katika mpango ule walikuwa: Omari Muhaji, Juma Jambia, Juma Swedi
[77] Baada ya miaka mingi ya Waislam kuisusia BAKWATA ikafika mahali ikawa inashindwa hata kufanya mikutamo ya uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wakatiba yake. Kwa hali kama hiyo ilikuwa kwa Msajili wa Vyama kuivunja. Serikali ilipooona imekabiliwa na hali hiyo ikachukua jukumu la kutayarisha mkutano ili kuihuisha BAKWATA. Tarehe 28 Aprili 1993 Waziri wa Mambo ya Ndani na Makamo Waziri Mkuu Augustine Mrema aliitisha mkutano kati ya Waislam na Wakristo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Mkutano ulikuwa hauna agenda. Kanisa lilipeleka ujumbe wa hali ya juu kabisa. Waislam hawakutokea isipokuwa BAKWATA. Katika mkutano ule Mrema alieleza kuwa uchaguzi katika BAKWATA umechelewa sana kwa kukosa faedha.Kanisa paleplale lilijitolea fedha kuipa BAKWATA ili ifanye uchaguzi wake. Halikadhalika Mrema alisaidia kukusanya fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwa ajili ya uchaguzi wa BAKWATA. Mkutano ulifanyika Dodoma tarehe 10th -12th Mei. Badala ya kufanya uchaguzi BAKWATA ilirekebisha katiba yake ili iweze kumpa ruhusa Sheikh Mkuu wa BAKWATA haki ya kufukuza na kumweka katika uongozi au kumtoa mtu yeyote bila ya kipingamizi.

[78] Angalia Bergen, uk. 238.
[79] Daily News, 6th November 1985.
[80] Sivalon, op.cit. uk.49.
[81] Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Jamuhuri ya Tanzania mwaka 1985-1995.
[82] Warsha ndiyo jumuiya ya kwanza katika historia ya Tanzania baada ya uhuru kuanza kuwaanda Waislam na kupambana na dhulma zilizokuwa zikifanyiwa Waislam. Kwa kipindi chote cha uhai wake serikali ilikataa kukipa usajili. Hii ilikuwa heri kwao kwa kuwa kiliendesha kampeni zake chini kwa chini, kampeni ambazo zilileta mafanikio makubwa hasa katika kuwaelimisha Waislam kuhusu mbinu za adui. Warsha iliweza kufikia hatua ikachukua uongozi wa BAKWATA. Warsha haikudumu katika uongozi kwa muda mrefu. Serikali ikimtumia Adam Nasibu kwa mara ya pili iliweza kuwapiga marufuku vijana hawa wasishugulike na uongozi wowote katika jumuiya yoyote ya Kiislam. Hata hivyo athaari za Warsha zingalipo hadi sasa. Vongozi wengi wa jumuiya za Kiislam hivi sasa wamepata uamsho na mafunzo yao ya awali ya uongozi katika Warsha. Mwaka wa 1981 Warsha walifanya utafiti ambao ulikuwa haujawahi kufanyika kabla, Warsha walifanya utafiti katika elimu ya Waislam Tanzania. Utafiti ulionyesha Waislam walikuwa wana nafasi chache katika vyuo vya elimu ya juu. Taarifa ya utafiti huu ilisambazwa kwa Waislam wote wa Tanzania.
[83] Angalia Kiongozi, Julai 15-31, 1993.
[84] Hali ya Waislam katika Tanzania ni ya kusikitisha inapokuja suala la kueneza habari au propaganda. Vyombo vyote vya habari, vya serikali na vilivyo chini ya wamiliki binafsi vyote vipo katika mikono ya Wakristo. Vyombo hivi vinatumika vyema katika kupiga vita Waislam.
[85] Nje ya vyombo hivyo vya serikali, Profesa Malima alikuwa na jeshi kubwa ka Waislam waliokuwa nyuma yake, wengi wao wakiwa vijana. Wakiwa hawana vyombo vya habari wanavyovimiliki, Waislam walichapa makaratasi na kuyatawanya nchi nzima yakimuunga mkono Profesa Malima huku yakieleza udhalimu wa serikali, mengine yamkitaja Julius Nyerere na Kanisa Katoliki kama washiriki katika kuwadhulumu Waislam. Kwa ajili hii Profesa Malima alipendeza machoni mwa Waislam. Profesa Malima akawa anaalikwa katika kila hafla muhimu ya Waislam. Katika hafla zile Profesa Malima aliwahutubia Waislam kuhusu madhila wanayoyapata.

[86] Aboud Jumbe, The Partner-Ship, Amana Publishers, Dar es Salaam, 1995, uk. 125-138.
[87] Jan P van Bergen, Religion and Development in Tanzania, (Madras, 1981) passim.
[88] Kitabu hiki hivi sasa hakipatikani na kulikuwa na uvumi kuwa Usalama wa Taifa walikuwa wakikitafuta ili kikusanywe na kuteketezwa kwa kuwa kilikuwa kinahatarasha umoja na mshikamano wa wananchi na kwa ajili hiyo amani ya nchi.
[89] John C. Sivalon, Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985, (Ndanda,1992)
[90] Ibid. uk. 37.
[91] K. Mayanja Kiwanuka, The Politics of Islam in Bukoba District (1973), B.A. Thesis, University of Dar es Salaam.
[92] Mohamed Said, ‘Islam and Politics in Tanzania’ (1989) makala hii ilichapishwa tena kwa jina hilo hilo katika Al Haq International (Karachi) Vol. 1 No. 3 August-December 1993.
[93] ‘Kwikima Report’ imo ndani ya The Standard, 12th December, 1968, vilevile The Nationalist, 15th December, 1968. Angalia vilevile Bergen, uk. 238.
[94] Angalia, USAID/Tanzania ‘Tanzania Flash Points Study’, April, 1999.


No comments: