Monday, 8 February 2016

MAALIM SEIF AJIVUA LAWAMA ZANZIBAR - GAZETI KA JAMHURI


Sasa ni dhahiri. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, ametabiri hatari ya mgawanyiko unaoweza kuikumba Zanzibar, lakini asingependa alaumiwe kwa uamuzi utakaochukuliwa Zanzibar.
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Serikali ya Mapinduzi wametangaza kurudia uchaguzi Machi 20, mwaka huu.
Wakati kiongozi huyo wa CUF akitabiri mabaya, kwa upande wake amejivua lawama kwa lolote linaloweza kutokea kwa kuwa hajahusika kupanga programu yoyote licha ya kwamba yeye ni mmoja wa viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi.
Maalim Seif amekiri na kuiambia JAMHURI kuwa amefanya mawasiliano na mabalozi kadhaa na viongozi wa kimataifa juu ya hali ya siasa Zanzibar, na kusema: “Kwa hatari yoyote nisihusishwe. Naipenda Zanzibar, Wazanzibari wanajua hivyo, lakini watu wa CCM na Serikali yao wana yao.”
Anasema: “Nimewaambia mabalozi na marais wa nchi nyingi tu nimewaandikia kwamba nisingependa kuingizwa kwenye lawama kwa chochote kitakachojiri Zanzibar.”
Maalif Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alihojiwa swali la msingi na JAMHURI kuwa ni kiongozi wa juu wa Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Kwa msingi huo, Maalim Seif aliyepata kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, anasema: “Sijahusika kupanga au kuratibu huo uchaguzi. Sisi CUF tulitoa msimamo mapema kwamba hatukubali kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu.
“Hakuna sababu ya kurudia uchaguzi. Nasisitiza tena nasema kwamba hoja ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza kuzaa fujo na vurugu…
“Nami nasema jambo moja kuu kwako leo. Sitaki kubeba lawama kwa lolote litakalotokea Zanzibar. Kwa lolote baya litakalotokea visiwani, waulizwe CCM, aulizwe Dk. Shein, aulizwe Dk. Magufuli na wengine, lakini si mimi.”
Anasema Zanzibar inaweza kuibua mzozo mpya na mkubwa wa kikatiba na wa kisheria, na kwa upande wake hadhani kama itakuwa busara kufanya uchaguzi uliotangazwa na ZEC hivi karibuni kwamba utafanyika Machi 20, mwaka huu.
Anasema wanadiplomasia wengi wakiwamo Bernard Membe na Amina Salum Ali, wamemtaka kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kuiepusha Zanzibar na machafuko.
Anasema jitihada za kuutafutia ufumbuzi mkwamo wa kisiasa Visiwani humo ungepatikana baada ya yeye kujitokeza mara kadhaa kwenye meza ya mazungumzo, “lakini wenzangu walikuwa na nayo. Hawataki kufuata taratibu.”
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, anasema alikuwa na imani na kujaa matumaini kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi wa haki unaoheshimu uamuzi wa wapiga kura wa Zanzibar walioufanya Oktoba 25, mwaka jana.
Anasema yanayofanywa na Membe na Amina ni kuhangaika kwani tayari CUF imetoa msimamo wa kutoshiriki na kuwataka wanachama wake wasifanye hayo.
Mbali na mabalozi hao, anasema jitihada nyingine zinafanyika kwa kuhusisha na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zikiwamo Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na nchi kadhaa ambazo ni marafiki wa Tanzania.
Maalim Seif anasema tayari takwimu za ushindi wake zilionekana hata kwa waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi huo.
Maalim Seif ameshatoa msimamo wake na chama chake baada ya mazungumzo ya siri ya kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.
“Ni CCM wanaong’ang’ania uchaguzi, hoja zao ni kama hoja mfu kwa sababu hazina msingi, haikubaliki kwa sababu nilizipangua kwenye vikao kama 10 nilivyoketi na makada wa CCM,” anasema.
Anasema kuwa ikitokea Uchaguzi Mkuu ukarudiwa, zipo changamoto nyingi za kikatiba ambazo zitakwamisha uchaguzi huo, hivyo uchaguzi huo hautawezekana.
“Nani anatoa fedha za uchaguzi? Nani anapitisha fedha za kugharamia uchaguzi na Baraza la Wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa limefikia ukomo wake?” Anahoji Maalim Seif.
Amemtaja Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kuwa ni tatizo Zanzibar na kwamba kama ikitokea damu inamwagika, ‘itasambaa’ kwenye akili ya kiongozi huyo kwa muda mrefu akidai kwamba ndiye kinara wa vurugu za Zanzibar kwa sasa.
Jecha ndiye aliyetangaza kufutwa kwa matokeo, jambo ambalo Maalim Seif anasema si halali kwa kuwa hakuwa na nguvu kikatiba kuchukua uamuzi huo ambao kwa sasa unaleta mjadala.
Tayari wadau wa maendeleo zikiwamo nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani, wameelezea masikitiko yao kutokana na ZEC kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema ZEC imechukua hatua hiyo bila kuwahusisha wadau wote kwenye mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa ulioikumba Zanzibar.
“Tunatoa wito kwa Serikali ya Tanzania na Rais Magufuli kuhakikisha kumefanyika mazungumzo yanayohusisha pande zote ili kupata suluhisho la mzozo huo wa Zanzibar,” ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na msemaji wa wizara hiyo, John Kirby.
Kirby anasema kwamba Marekani ingependa kuwa mwangalizi wa uchaguzi huo. Alitaka pande zote mbili ziimarishe amani na kuja pamoja kwa moyo wa kujitolea “kwa sababu Wazanzibari na Watanzania wote wana haki ya kupata suluhisho kwa mzozo huo, ambalo litatilia maanani matakwa ya wapiga kura na kuashiria kujitolea kwa Serikali kuimarisha maadili ya kidemokrasia.”
CHANZO: Gazeti la Jamhuri la tarehe 8 Februari 2016

No comments: