Kambi
Rasmi ya Upinzani inasema kuwa Dk. Ali Muhammed Shein hana uhalali wa kushika
nafasi hiyo kwa sababu matokeo ya Uchaguzi wa Marejeo yana kila dalili kuwa
yalikuwa ni ya kupanga kitakwimu. Kwa mfano katika Jimbo la Malindi, Dk Shein
alipata kura 2,334 katika Uchaguzi wa Oktoba, lakini katika Uchaguzi wa Machi
20 akapata kura 5,873 ikiwa ni ongezeko la kura 3,539. Na kwa Jimbo la
Mwanakwerekwe, Dk. Shein alipata kura 4,003 Oktoba, lakini akaibuka na kura
9,5,97 hapo juzi ikiwa ni ongezeko la kura 5,594. Majimbo yote hayo Maalim Seif
aliongoza kwa kura Oktoba.
KAULI YA WAZIRI KIVULI WA WIZARA YA MUUNGANO NA
MAZINGIRA KUHUSU UCHAGUZI WA MAREJEO ZANZIBAR
March 31, 2016
Wana Habari,
Tunaelewa sote kuwa Uchaguzi wa Marudio umefanyika
Zanzibar na hivi sasa kuna harakati zinazoendelea kuunda Serikali kutokana na
uchaguzi ambao umekosa uhalali wa kikatiba na kisheria.
Kambi Rasmi ya Upinzani inatamka wazi kuwa
haitautambua uongozi huo wa Serikali ya Zanzibar na wala haitatoa ushirikiano
wowote kwayo.
Uongozi mzima wa Serikali ya Zanzibar hauna uwezo wa
kikatiba na kisheria kushiriki katika suala lolote la Muungano kwa sababu
umekosa ridhaa ya Wazanzibar kutokana na kufutwa uchaguzi halali tarehe 28
Oktoba 28, 2015 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya ZEC na pia hapakuwa na
uhalali wa kikatiba na kisheria kuwepo kwa Uchaguzi wa Marejeo wa Machi 20,
2015.
Ieleweke kuwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar una
athari ya moja kwa moja kwa upande wa Jamhuri ya Muungano, na Kambi Rasmi ya
Upinzani inapinga kwa vyovyote vile uchaguzi huo kuhusishwa na mambo ya
Muungano na itapinga na kulaani kitendo chochote kitachoelekeza hivyo.
Mnasaba wa Uchaguzi huo na Muungano ni katika maeneo
yafuatayo ambayo kwa hali ilivyo kwa sasa yameingia katika mashaka na mgogoro
wa kikatiba:
Pamoja na mamlaka ya Zanzibar kutajwa katika Katiba
yake ya 1984 lakini pia yanatajwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Kifungu
cha 4 (2) na hapana shaka Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua misingi ya
demokrasia na kwa hivyo kwa utawala wa sasa kuingia madarakani kwa misingi
isiyo halali na kufanya teuzi zinazohusu Baraza la Mawaziri, Mahakama na Baraza
la Wawakilishi kunatia katika utata Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani hatutalikubali
jambo hilo la kutiwa doa na kuipuuza Katiba ya Jamhuri ya Muungano na tutafanya
kila njia kuonyesha kutoridhishwa kwetu kunajisiwa kwa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano.
Uchaguzi Mkuu wa Marejeo na unyakuaji madaraka
uliofanywa huko Zanzibar unakwenda kinyume kabisa na Malengo Muhimu na Msingi wa
Mwelekeo wa Shughuli za Serikali kuhusu Serikali na Watu inasemwa katika
Kifungu 8 (2):
“Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali
ya
Mapinduzi ya Zanzibar, au wa chochote kati ya vvyombo vyake
na uendeshaji wa shughuli zake utatekelezwa kwa kuzingatia
umoja wa Jamhuri ya Muungano na haja ya kukuza umoja wa
kitaifa na kudumisha heshima ya Taifa”
Uchaguzi wa kihuni uliofanywa Zanzibar huawezi kabisa
kuwa unaakisi kifungu hiki cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano si kwa kuzingatia
umoja wa kitaifa wala si kwa kudumisha heshima ya kitaifa.
Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani watalisimamia jambo
hili kwa nguvu zote kuhakikisha kuwa Uchaguzi wa Marejeo hautasimama mbele ya
macho ya sheria na katiba na tukijua kuwa kutakuwa na tishio la kutetereka
umoja wa kitaifa..
Wala Wabunge wa Kambi ya Upinzani hawatakubali
Tanzania ipate aibu mbeleya wananchi wake lakini pia mbele ya macho ya
kimataifa ambapo jina la Tanzania limekuwa kubwa, la kuaminika na la kusifika
lakini linaweza kabisa kuharibiwa na aibu hii.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Kifungu 54
(1) Rais wa Zanzibar anakuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri wa Muungano, na kwa
hivyo atatarajiwa kula kiapo kushika nafasi hiyo.
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema Dk. Ali Muhammed Shein
hakushinda katika taratibu zinazoendana na misingi ya demokrasia kwanza kwa
kuhusika kwa kiasi kikubwa kwa nguvu za kijeshi kupitia vitisho vilivyokuwa
vikionekana na kujiri hata majeshi yetu kuvaa soksi za usoni.
Dk. Shein amechaguliwa katika kipindi ambacho
kamatakamata ilikuwa kubwa ambapo katika kipindi kabla ya Uchaguzi wa Oktoba
zaidi ya watu 100 walikamatwa na katika kipindi cha baada ya Oktob hadi Machi
20 watu zaidi ya 150 wamekamatwa pamoja na kukamatwa na kuhojiwa viongozi wa
Chama cha Wananchi CUF.
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa Dk. Ali Muhammed
Shein hana uhalali wa kushika nafasi hiyo kwa sababu matokeo ya Uchaguzi wa
Marejeo yana kila dalili kuwa yalikuwa ni ya kupanga kitakwimu. Kwa mfano
katika Jimbo la Malindi, Dk Shein alipata kura 2,334 katika Uchaguzi wa Oktoba,
lakini katika Uchaguzi wa Machi 20 akapata kura 5,873 ikiwa ni ongezeko la kura
3,539. Na kwa Jimbo la Mwanakwerekwe, Dk. Shein alipata kura 4,003 Oktoba,
lakini akaibuka na kura 9,5,97 hapo juzi ikiwa ni ongezeko la kura 5,594.
Majimbo yote hayo Maalim Seif aliongoza kwa kura Oktoba.
Kwa mujibu wa majimbo ambayo Tume ilikuwa imeyatangaza
mpaka Oktoba 28, 2015 ambayo yalikuwa ni 31, ZEC inaonekana imemuongezea Dk.
Shein kura za chini kabisa kwa kiasi cha 61 na za juu kabisa ni 5,594 jambo
ambalo halielekei, halina mantiki na haliwezekani. Maana hata majimbo yote ya
Pemba, Dk. Shein amepata kura za ziada.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 66 (1) (c) Wajumbe 5 wa
Baraza la Wawakilishi huingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na hushiriki
katika shughuli zote za Bunge kama vile kutunga sheria na kushiriki katika
Kamati mbali mbali za Bunge.
Pia kama itampendeza Rais wa Jamhuri ya Muungano ana
uwezo wa Kikatiba wa kumteua yoyote mmoja wao au wote kushika nafasi ya Uwaziri
katika Jamhuri ya Muungano. Katika Uchaguzi huo wa Marejeo pia alipigiwa kura
Mbunge pekee aliyekuwa amebakia Shamsi Vuai Nahodha wa Jimbo la Kijitoupele.
Ushiriki wa Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi
utalivunjia hadhi Bunge kwa kuwa watakuwa wanatokana na uchaguzi ambao
haukukidhi vigezo vya kidemokrasia na inawezekana pia wakatoka katika majimbo
ambayo hata Uchaguzi wa Oktoba majimbo wanayoyashika sasa yalikuwa yamekwenda
kwa upinzania na kukabidhiwa vyeti vya ushindi na ZEC.
Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga ushiriki wa Wajumbe
hao wa Baraza la Wawakilishi kwa sababu wameshiriki katika zoezi zima la kubaka
demokrasia pia wanatokana na Baraza la Wawakilishi ambalo uhalali wake
unakwenda kinyume na matakwa ya katiba na sheria kwa kupokea Wajumbe ambao
hawakupitia mchakato unaokubalika wa kikatiba.
Kambi ya Upinzani inaonya kuwa kutakuwa na migongano
kadhaa ya Kikatiba katika suala hili bila ya kuwepo na ulazima isipokuwa
itatokea kwa sababu Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeamua kuitia kwenye
mbeleko Serikali ya Drk Shein ili kuendeleza ubabe wa CCM kuitawala Zanzibar
kwa nguvu na kudhihirisha nia ya Serikali ya Jamhuri kutokubali kuruhusu
maamuzi ya kidemokrasia huko Zanzibar.
Kambi ya Upinzani inasema wazi kuwa kubebwa kwa utawala
wa Dk. Shein kutozorotesha uimara wa Muungano na kuutia mtihani mkubwa hasa kwa
vile matokeo ya Uchaguzi wa Marejeo yameshindwa kujenga mazingira ya Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ambayo ilileta utulivu na kuupa pumzi Muungano, lakini hali
hii mpya inatoa fursa kwa upinzani kudai kwa nguvu zote kuwepo kwa Katiba Mpya
ambayo tutaidai kwa nguvu zetu zote.
Ally Saleh (Mbunge)
Waziri Kivuli wa Muungano na Mazingira
Machi 31, 2016
0715 4300 22 / 0777 4300 22
No comments:
Post a Comment