DOKTA DAU KUTEULIWA BALOZI:
JE,
AMEPENDELEWA AU AMEONEWA?
| Sheikh Muhammad Iddi |
Kabla ya kuianza Kauli
yangu ya leo yenye anuani tajwa hapo juu, niwaombe wasomaji wangu tufanye mambo
matatu:
(a)
Tukumbushane Waislamu kwamba ni haramu ‘kupendelewa’ kwani kupendelewa ni
dalili ya huyo anayependelewa kutostahiki katika jambo fulani. Na pia
kupendelewa kunalazimisha kudhulumiwa mwengine ili wewe upate huo upendeleo,
jambo ambalo si zuri kwani Uislamu hautaki Muislamu amdhulumu mwengine kwa
maslahi yake binafsi au ya jamii ya Kiislamu. Ieleweke kwamba Uislamu si dini
ya usawa bali Uislamu ni dini ya uadilifu.
(b)
Tushirikiane Watanzania wote kumuombea Rais wetu, Dokta John Pombe Jospeh
Magufuli, Mwenye ezi Mungu amuepushe na tuhuma nzito ya kuwabagua Wislamu na
Wakristo wasiokuwa katika dhehebu lake la Kikatoliki, na kuwapendelea zaidi Wakristo
Wakatoliki na haswa wanaotokea ‘nyumbani’.
Tuhuma hizi hazifanani
naye hata chembe kwani tabia yake ya kumuweka Mwenye ezi Mungu mbele na kumtaja
sana kwenye hotuba zake inaonyesga ‘uchamungu’ ambao haukubaliani na tabia ya
ubaguzi kwa misingi ya udini, madhehebu na ukanda.
Tumuombe sana Mwenye ezi
Mungu amuepushe Rais wetu na tuhuma hizo.
(c)
Tumpongeze sana Dokta Ramadhan Kitwana Dau kwa kuwa ‘mkimya’ baada ya kuipokea
kwa mikono miwili taarifa ya kupewa ubalozi. Tunapaswa kumpongeza kwa hilo kwa
sababu vyombo vya habari vimepokea kwa hisia tofauti uteuzi wa yeye kuwa
balozi, na yameandikwa yakuandikwa pamoja na kusemwa yaliyosemwa.
Kitendo cha yeye kuwa
mkimya, mtulivu na msikilizaji zaidi kumeonyesha ukomavu wake katika kuufahamu
vyema mfumo wa uongozi.
Tukirudi katika anuani
ya leo, jambo la msingi ni mjadala usio rasmi juu ya kitendo cha aliyekuwa
Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dokta Ramadhan Dau,
kuteuliwa kuwa Balozi, tukio ambalo ndio linahitimisha utumishi wake uliotukuka
katika shirika hilo kubwa nchini.
Watanzania kupitia
vyombo vya habari na mijumuiko isiyo rasmi wametofautiana sana juu ya uteuzi
huo. Wapo walioupongeza na wapo walioubeza. Wale walioupongeza wanadai kwamba
Dokta Dau amependelewa, na wale walioubeza wanadai kwamba Dokta Dau ameonewa.
Tukianza na wale
walioupongeza uteuzi huo kwa hoja kwamba Dokta Dau amependelewa, wanadai
kwamba:
(1)
Dokta Dau amedumu katika shirika hilo kwa muda mrefu pengine kuliko mtu yeyote
kwani ameweka historia ya kuwa Mkurugenzi wa Shirika aliyetumikia kwa muda
mrefu. Aliteuliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin William
Mkapa, kuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo mnamo mwaka 1997, na akaweza kulitumikia
katika kipindi chote cha Mheshimiwa Mkapa kuanzia mwaka huo hadi alipoondoka
madarakani mwaka 2005.
Ilipoingia Awamu ya nne
chini ya Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, bado Dokta Dau
aliendelea kuwa Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa mihula yote miwili (miaka kumi)
ya uongozi wa Mheshimiwa Kikwete. Na hatimaye kuteuliwa kuwa Balozi
katika Awamu hii ya tano chini ya Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli.
Kutokana na utendaji
wake uliotukuka na uliosheheni mafanikio makubwa, kwa hakika isingependeza
kumpumzisha kwa kutengua nafasi aliyokuwa nayo bila ya kupewa nafasi nyengine
yenye hadhi na heshima.
(2)
Dokta Dau amependelewa kwa sababu Shirika hilo ni kubwa sana na kwa kuwa yeye
ndiye aliyekuwa Mkurugenzi wake (na kwa kuwa ni mwanaadamu) ni makosa makubwa
sana kumpa sifa ya umalaika kwamba eti ni mtakatifu aliyefanikisha tu na wala
hana kasoro yoyote katika utendaji wake.
Hilo kamwe sio kweli
kwani endapo ukipitishwa upembuzi yakinifu yanaweza kupatikana ‘majipu’ ambayo
kama yakitumbuliwa yanaweza kumaliza uhai wa mgonjwa. Katika mazingira hayo
halafu anapewa ubalozi, wanaamini Dokta Dau amependelewa sana.
(3)
Dokta Dau amependelewa na wala hisia za kuondolewa kwake kuhusishwa na udini ni
hoja isiyo na ‘mashiko’ kwa kuwa aliyemteua ni Rais Mstaafu, Mheshimiwa
Benjamin William Mkapa, ambaye ni Mkatoliki na aliyemuondoa hapo ni Mheshimiwa
Rais, Dokta John Pombe Magufuli, ambaye ni Mkatoliki pia.
Kama leo hii
wanalalamikiwa Wakatoliki kwa kumuondoa Dokta Dau, ni vizuri kwanza
zikatangulia pongezi kwa Wakatoliki hao kwani ndio waliomuweka pia.
Amma kuhusu hoja za
wanaolaumu kwamba Dokta Dau ameonewa, msingi wa hoja zao umejengekea kutokana
na historia njema ya Dokta Dau katika utumishi wake kwa Taifa la Tanzania.
Wanadai kwamba Dokta Dau
ni miongoni mwa Waislamu wachache ambao hawauoni ‘kinyaa’ Uislamu wao, ni msomi
aliyebobea mwenye uwezo na hadhi ya kimataifa. Pia ameongoza katika maeneo
kadhaa ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) na kadhalika, kwa mafanikio na ufanisi mkubwa.
Pamoja na usomi wake na
hadhi yake katika nafasi ‘nyeti’, bado anaona fakhri na heshimwa kubwa
kujulikanwa na jamii kwamba yeye ni Muislamu. Na kamwe haoni tatizo kuvaa kanzu
na koti siku ya Ijumaa, na wala haoni kwamba vazi hilo linampunguzia hadhi na
heshima katika jamii ya kisomi (kama walivyojiweka Waislamu wengine ambao ni
wasomi wa kisekula).
Kwa kipindi kirefu Dokta
Dau amekuwa mkarimu sana kupitia mshahara wake na stahiki zake mbalimbali hadi
kufikia kiwango cha kusifiwa hata na watu wasioijua hata sura yake.
Dokta Dau ni
mnyenyekevu, anayehudhuria hafla na matukio mbalimbali ya dini yake ya Kiislamu
huku akiwa na bashasha (mchangamfu) anapokutana na rafiki zake bila
ya kujali wadhifa na uwezo alio nao.
Kutokana na hulka yake
hiyo njema, Dokta Dau ni miongoni mwa Watanzania mwenye wapenzi wengi mnoo.
Na kutokana na yeye kuwa
kinyume na Waislamu wengine wasomi wa kisekula kwa kujipamba vyema na
kutounyanyapaa Uislamu wake, sehemu kubwa ya Waislamu, Wazee kwa Vijana,
wanampenda sana Dokta Dau kwani anaondoa ‘ ombwe’ walilo nalo Waislamu wengi
wasomi wa kisekula ambao wanaunyanyapaa Uislamu wao. Amejijengea himaya kubwa
ya wapenzi kupitia tabia zake njema na wema anaowatendea wenzake.
Dokta Dau kwa utendaji
wake uliotukuka katika Shirika la NSSF ameonyesha njia kwamba Waislamu nao
wanaweza, tatizo linalowakumba ni kubaguliwa kutokana na wivu wa kiimani.
Kundi hili la Waislamu
na baadhi ya wanajamii linaona kwamba Dokta Dau ameonewa kwa sababu:
(1)
Pamoja na kuwa Rais Kikatiba anao uwezo wa kutengua uteuzi na kuteua upya
katika eneo lolote ambalo ana mamlaka nalo, lakini alipaswa kuyafikiria
mafanikio ya Shirika la NSSF na mchango mkubwa wa Dokta Dau katika mafanikio
hayo.
Kitendo cha Mheshimiwa
Rais, Dokta John Pombe Magufuli, kutengua uteuzi wa Dokta Dau kama Mkurugenzi
wa Shirika hilo katika wakati huu ambao umepewa jina la ‘msimu wa utumbuaji wa
majipu, kinailazimisha jamii hiyo iamini kwamba lipo lengo la kumdhalilisha Dokta
Dau na huo ni uonevu kwa mtendaji huyo.
(2)
Pamoja na heshima ya kazi ya ubalozi lakini kutokana na uwezo na utendaji
uliotukuka wa Dokta Dau, baadhi ya wanajamii waliamini kwamba Mheshimiwa Rais
Magufuli angemtumia msomi huyo bobezi kwa kumpa ubunge na kumteua kuwa waziri
ili awatumikie zaidi Watanzania badala ya kwenda ‘kumficha’ ubalozini ambapo
atasahaulika na jamii kwa muda mfupi sana.
Wanaendelea kuhoji
kwamba: Hivi katika Baraza la Mawaziri la Mheshimiwa Rais Magufuli, hakuna
nafasi ambayo Dokta Dau anaimudu? Kumpa Dokta Dau ubalozi ni ‘kumpandisha’
kimataifa lakini ni ‘kumfinika’ kijamii.
(3)
Pia wapo wanaohoji kwamba; Je, haraka ya Mheshimiwa Rais Magufuli kumtoa upesi
Dokta Dau imesababishwa na nini? Vipi ameshindwa hata kumvumilia afanikishe
ufunguzi wa Daraja la Kigamboni na ndipo amteue kwa wadhifa huo wa Balozi?
Kwani pamoja na wengi watakaotambuliwa kufanikisha ujenzi wa daraja hilo lakini
Dokta Dau angekuwa ‘kinara’ wa sifa hizo. Je, ni kipi alichokiogopa Mheshimiwa
Rais Magufuli mpaka akaharakisha ‘kumnyofoa’ Dokta Dau kwa kasi hiyo?
Kutokana na uharaka wa
kumuondoa, utumishi wake uliotukuka kwa Taifa na kumuepusha na mafanikio ya
Daraja la Kigamboni linalotarajiwa kufunguliwa mwezi huu wa Machi, Dokta Dau
ameonewa na inaonekana ni mwanzo wa safari ya kuizima nyota yake katika jamii
ya Watanzania.
Je, ni nini sababu ya
kuyafanya hayo? Hicho ni kitendawili ambacho ni vigumu kukitegua kwa haraka
kwani ni mapema mnoo kusema kwamba kilichotumika ni ile kanuni ya upangaji
foleni kwamba ili ‘namba mbili’ awe namba moja, ni lazima ‘namba moja’ asiwepo;
au kusema ni miongoni mwa ‘kampeni baridi’ kwamba wakati wa ‘Waswahili’
Waislamu umepita madhali ‘Mswahili Mkuu’ kamaliza muda wake basi na wa chini
yake wamfuate huko huko mapumzikoni.
Yote kwa yote, niendelee
kumhimiza Dokta Dau aendelee na ukimya wake pamoja na utii kwa mamlaka ya juu
ya nchi yake, na Inshaallaah (Mwenye ezi Mungu akipenda) aende katika kituo
chake atakachopangiwa na kamwe asikate tamaa na wala asipunguze hata
nukta moja ya utiifu wake kwa Serikali ya nchi yake.
Popote awapo ayakumbuke
maneno ya Wakale waliosema: “Udi kila ukichomwa ndio huzidi kutoa
harufu nzuri”, “Dhahabu ikitaka kutengenezwa kitu kizuri huchomwa”,
na “Mitihani ndio tanuri la kuyafikia mafanikio”.
Hii ndio Kauli yangu ya
wiki hii na mjadala umefunguliwa.
Mwandishi
wa makala haya ni Mwenyekiti wa ARRISAALAH ISLAMIC FOUNDATION
Unaweza
kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.
No comments:
Post a Comment