Sheikh Muhammad Iddi |
MAGUFULI ANATEUA HATUMBUWI
Msamiati
wa utumubaji wa majipu umepata umaarufu mkubwa haswa katika awamu ya tano ya
Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli. Msamiati huo kama tungekuwa
tumemsikiliza vyema mwenyewe Mheshimiwa Rais Magufuli, tungejua ni wapi unafaa
kutumia na ni wapi haufai kutumia.
Watanzania
tunayo tabia pindi msamiati mpya ukienea katika jamii huwa tunautumia bila hata
ya kuangalia kama ni sahihi au sio sahihi hapo tunapounasibisha. Mheshimiwa
Rais John Magufuli anapotamka msamiati wa kutumbua majipu anachokusudia ni
kumfukuza au kumuwajibisha yule mtendaji ambaye amehusika moja kwa moja na
ubadhirifu katika nafasi husika.
Lakini
pia kwa mujibu wa utendaji wa Serikali inayoheshimu misingi ya sheria na
utawala bora, bado chombo kikuu chenye mamlaka ya kumtia mtuhumiwa hatiani ni
Mahakama na si vyenginevyo.
Kwa
bahati mbaya sana katika uongozi wa awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais,
Dokta John Pombe Magufuli, kila mabaye uteuzi wake unatenguliwa au
anastaafishwa basi jamii inaaminishwa kwamba huyo alikuwa ‘jipu’ na sasa
ametumbuliwa. Jambo hili linavunja heshima waliyojiwekea watendaji Serikalini
kwa miaka kadhaa na kibaya zaidi ni kwamba wanahojiwa huku tayari
wameshahukumiwa.
Ipo
mifano kadhaa amabayo kwa kweli ni muhimu sana kuitazama kwa jicho la ndani
zaidi kwani kama hatutokuwa makini Mheshimiwa Rais John Magufuli pamoja na kazi
njema yenye nia njema kwa nchi yake anaweza kuweka historia ya kuwa Rais wa
kwanza Afrika kupendwa mwanzoni na hatimaye kuchukiwa sana mwishoni.
Tukiyaangalia
matukio ya tngu Mheshimiwa Rais John Magufuli aingie madarakani tutaona wazi
kwamba yapo matukio matatu yaliyoshudiwa na kupokewa kwa hisia kubwa sana na
wananchi.
(a)
Lipo tukio la Mheshimiwa Rais John Magufuli kuwawajibisha baadhi ya wafanyakazi
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hatimaye watendaji hao kufikishwa
mahakamani. Lakini mtendaji mkuu (Kamishna) wa mamlaka hiyo uteuzi wake
ulitenguliwa. Kwa kuwa huyu hakufikishwa mahakamani, msamiati wa kutumbuliwa
‘jipu’ kwake ni uonevu kwani yapo matukio kadhaa ambayo ni vigumu kuyahusisha
na yeye moja kwa moja haswa ukilinganisha yaliyokuwa yakiri na mfumo wa
kuyahusisha kwake.
Lakini
kutokana na mfumo tulio nao, utaona yakitajwa hayo yanayoitwa ‘majipu’ maneno
yanajirudia rudia kwa kila ambaye kwa sasa ameondolewa katika nafasi yake ya
kiutendaji Serikalini au katika Mashirika ya Umma.
(b)
Tumeshuhudia tukio la Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA)
akifanyiwa kama ya Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kuitwa
‘jipu’ kwa sababu tu ametenguliwa wadhifa wake aliokuwa nao. Jambo baya zaidi
ni tukio la hivi karibuni la uteuzi wa Wakuu wa Mikoa Wapya.
Hapo
ndipo tunapoona Watanzania tukumbushane kwamba Mheshimiwa Rais John Magufuli
anateua, hatumbuwi ‘majipu’.
Amma
hii dhana nzima ya utumbuaji wa majipu inahitaji ufafanuzi au urekebishwaji
mkubwa sana. Mfanyakazi aliyeitumikia Serikali au Shirika la Umma kwa muda
mrefu, kibinaadamu anayo mafanikio na pia anazo changamoto kadhaa.
Anaposimamishwa kazi kwa ghafla kwa ubadhirifu alioufanya, huo ni upande mmoja
wa shilingi. Lakini kwa upande wa pili wa shilingi ni vizuri kuchunguza pia kwa
miaka yote hiyo ameiingizia Serikali au Shirika kiwango gani cha mafanikio.
Tunawaona
watendaji wa Serikali wakipigwa mapicha katika vyombo vya habari na huku wakipewa
majina ya uhalifu, hilo linaweza kupunguza ari ya watendaji waliopo kwani
haiwezekani aliyetumikia miaka takriban thelathini kazini halafu leo hii mema
yake yote yasahauliwe na yakumbukwe mapungufu tu tena ambayo bado
hayajathibitishwa na vyombo husika.
Ni
vizuri dhana hii ya utumbuaji wa majipu tukaiunga mkono kwani inaonyesha ina
dhamira njema, lakini ni muhimu pia kuuangalia mfumo mzima wa utumbuaji ili
jamii ibakie salama pamoja na kuwalindia watendaji hao heshima zao
walizojiwekea kwa miaka mingi katika uongozi.
Kwa
kuanzia, katika zile nafasi ambazo Mheshimiwa Rais John Magufuli anaonekana
anao uwezo wa kutengua uteuzi na kumteua mwengine, falsafa ya jipu hapo isipewe
nafasi kwani kumteua mtendaji na kumuacha mwengine ni jambo la kawaida. Na yule
anayeachwa wala haimaanishi kwamba ni ‘mchafu’ sana bali ni utaratibu katika
uongozi kupokezana vijiti katika nafasi.
Nihitimishe
Kalamu yangu wiki hii kwa kumpa nasaha Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa John Pombe
Magufuli, kwamba:
- Kiongozi bora hapimwi kwa umahiri wa kuwaadhibu waliokosea katika uongozi uliopita kwani yapo baadhi ya makosa yanamlazimu mtawala kuyaachia kutokana na mazingira ya wakati husika. Fikra ya ‘kuchimbua’ makosa yote yaliyotokea na kufanywa katika uongozi uliopita ili wakosaji waadhibwe inaweza kukosa nia njema au mwisho mwema. Katika uungwana na ustaarabu wa utawala bora ni kuheshimu mema ya mtangulizi wako na kuufungulia mlango wa dharura kwa yale ambayo yanaonekana ni makosa. Kuendelea ‘kuchimbua’ yote yanayoonekana yamekosewa kutazalisha mfumo mpya wa uongozi katika nchi yetu wa kutoheshimu mazuri ya mtangulizi wako. Aidha, uchambuzi huo unaweza kufikia katika wizara ambazo wewe Rais wetu uliziongoza na hatimaye kutuletea vurugu nchini kwa wanachi kutaka ‘ujitumbue’ mwenyewe wakati sisi bado tunakuhitajia sana.
- Kwa siasa za Kitanzania zilivyo kila tukio unaloendelea nalo imma linaleta wingi wa kura au linapunguza idadi ya kura katika Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2020. Ingawa wewe ni Rais wa Watanzania wote bila ya kujali vyama, lakini umeletwa kwenye uwanja wa kura kupitia chama chako. Kwa muktadha huo, ni vyema sana kutaka ushauri kwa viongozi wa chama chako ili ‘mruke’ pamoja.
- Watanzania wanayo tabia ya kumpenda mtu kwa ‘mkupuo’ (bila ya sababu) na pia kumchukia mtu kwa ‘mkupuo’. Tayari mapenzi ya Watanzania umeyaona, hiyvo ni vizuri pia ukajiandaa kupokea watakavyokuchukia.
Ukweli
ni lazima usemwe! Mheshimiwa Rais John Magufuli ameteua katika maeneo mengi tu
na kamwe dhana ya utumbuaji majipu haipo.
Naomba
kuwasilisha.
Mwandishi
wa makala haya ni Mwenyekiti wa ARRISAALAH ISLAMIC FOUNDATION.
Unaweza
kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.
No comments:
Post a Comment