Wednesday, 30 March 2016

UCHAGUZI WA MARUDIO ULIOFELI ZANZIBAR NA ADVOCATE AWADH ALI SAID


awadh
Awadh  Ali Said 

Katika mfumo wa kidemokrasi, uchaguzi wowote ni utaratibu wa kupata viongozi wa kikatiba wa nchi husika kama yalivyo mahitaji ya katiba ya nchi hiyo. Mfano wake ni kama dhana maarufu ya ‘’mahitaji na kukidhi’’ yaani  ‘’demand and supply.’’ Katiba inakuwa na mahitaji yake na uchaguzi unayakidhi mahitaji hayo. Endapo Uchaguzi umefanyika na matokeo yake yameshindwa kukidhi matakwa ya katiba nchi hiyo katika kupata uongozi uliotimia basi huo huwa ni uchaguzi uliofeli.
Zanzibar ilifanya Uchaguzi Mkuu tarehe 25 October 2015 kwa madhumuni ya kukidhi matakwa ya kikatiba ya kupata uongozi kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Uchaguzi ule ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi tarehe 28 October 2015. Mengi yamesemwa, tena kwa usahihi na uthibitisho wa kikatiba na kisheria kuwa kitendo kile hakikuwa na mashiko yoyote kikatiba na kisheria na ulikuwa uamuzi binafsi uliosukumwa na utashi wa kisiasa.
Pamoja na ukakamavu katika kujitia hamnazo na kutafuta hifadhi katika tafsiri zinazotia kichefuchefu za vifungu vya katiba na sheria lakini ni wazi ukweli ulithibiti. Ila hilo tuliwache kwa wakati huu.
Uchaguzi Mkuu wa Marudio ukaitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na ukafanyika tarehe 20 March 2016. Matokeo yametolewa. Kwa nafasi ya urais, mgombea wa CCM, Dr Ali Mohamed Shein ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 91.4 ya kura zote na kuwapita kwa mbali sana wapinzani wake wote 13 waliobakia, ambao wote kwa pamoja wameambulia chini ya asilimia 10 ya kura zote. Kwa upande wa viti vya uwakilishi chama kilicho madarakani cha CCM kimeshinda viti vya majimbo yote 54.
Sasa tuyaangalie matokeo haya kama yalivyo na pia tuyaangalie matakwa ya katiba ya Zanzibar ya 1984 tuone kama uchaguzi huu umefanikiwa kuipatia Zanzibar uongozi kwa mujibu wa matakwa ya katiba yake.
Katiba ya Zanzibar imeunda nafasi 3 za Uongozi wa juu katika serikali, nazo ni Rais, Makamo wa Kwanza wa Rais  na Makamo wa Pili wa Rais. Hawa wanapatikana kwa utaratibu kuwa katika uchaguzi unaowashirikisha wagombea zaidi ya mmoja, mgombea anaekuwa wa kwanza kwa kura nyingi ndiye anakuwa rais.
Chama kilichoshika nafasi ya pili kinatoa Makamo wa Kwanza wa Rais na Makamo wa Pili wa Rais anatoka chama kilekile cha Rais. Lakini kwa hii nafasi ya Makamo wa Kwanza Katiba imeweka kizingiti kuwa pamoja na kuwa itakwenda kwa chama kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa kura za urais lakini wingi wa kura zake usipungue asilimia 10. Ikiwa upili wake uko chini ya hiyo asilimia 10 (au kama mgombea wa urais alikuwa hana mpinzani katika kinyang’anyiro cha urais) basi nafasi ya Makamo wa Kwanza itakwenda kwa chama kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya uwakilishi majimboni.
Baada ya kukamilika kwa viongozi hao watatu wakuu, rais kwa kushauriana na hao makamo wawili ataunda baraza la mawaziri ambapo wizara zitagawiwa kwa vyama vilivyo na uwakilishi majimboni kwa kutumia utaratibu wa uwiano kutegemea na wingi wa viti ambavyo chama kimeshinda katika uchaguzi wa wajumbe wa baraza la wa wakilishi majimboni. Yaani chama kinapata mgao wake wa wizara kwa kutumia kigezo cha asilimia ya ushindi wake katika uchaguzi wa uwakilishi majimboni. Kwa mujibu wa katiba na kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi hakuna utata kwa nafasi ya urais na nafasi ya makamo wa pili. Kitahanani kipo katika kumpata huyu makamo wa kwanza.
Kwa vipi?
Chama kilichoshika nafasi ya pili hakikutimiza asilimia 10 kama lilivyo sharti la katiba. Katika hali hiyo katiba imeelekeza kuwa nafasi hiyo iende kwa chama kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa viti vya uwakilishi majimboni. Nacho hakipo, maana viti vyote vimechukuliwa na CCM. Vilevile hakutakuwa na mgao wa wizara maana hakuna vyama vilivyopata viti vya uwakilishi majimboni zaidi ya CCM.
Wakati yakijiri hayo katiba inaelekeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa ni ya muundo wa Umoja wa Kitaifa. Ibara ya 9 (3) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaweka wazi hili:
Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.
Changamoto kubwa ni kuwa katiba haikutoa jibu la nini cha kufanya pale inapotokezea hali kama iliyopo wakati huu. Watunzi wa Katiba ile ni wazi waliongozwa na uzoefu wa kawaida wa mwenendo wa siasa na chaguzi za Zanzibar. Hawakutegemea kutokea haya yaliyotokezea, na ndio maana hawakuweka vifungu vya akiba.
Dhahir kabisa, endapo kutakuwa na dhamira ya kuizingatia na kuiheshimu katiba katika kuunda serikali basi  matokeo ya Uchaguzi huu hayatoi nyenzo za uundwaji wa serikali hio.
Unapoisoma katiba hii kwa ujumla wake unagundua waziwazi kuwa watunzi wake hawakufikiria mazingira ya kuwa na baraza lenye wajumbe wote kutoka chama kimoja au serikali inayoundwa na chama kimoja pekee. Chukulia mfano mwengine mdogo juu ya muundo wa Baraza la Wawakilishi.
Baraza hili huundwa na wajumbe wa kuchaguliwa majimboni, Wajumbe wa Viti Maalum Wanawake na Wajumbe 10 wa kuteuliwa na Rais (pia Spika anakuwa ni Mjumbe kama amechaguliwa mtu ambae hakuwa Mjumbe wa kuchaguliwa jimboni na pia Mwanasheria Mkuu naye anakuwa Mjumbe). Hawa wajumbe 10 wa kuteuliwa na Rais Katiba, Ibara ya 66 inatamka:
Kutakuwa na Wajumbe kumi wa kuteuliwa wa Baraza la Wawakilishi ambao watateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoelezwa na kifungu  cha 68 (a) na (c) cha Katiba ambao wakiteuliwa watafaa kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Isipokuwa kwamba Wajumbe wasiopungua wawili watateuliwa na Rais kwa kushauriana na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi au kwa kushauriana na Vyama vya Siasa vyenye uwakilishi ndani ya Baraza la Wawakilishi iwapo hakuna Kiongozi wa Upinzani.
Kwa hali ilivyo hakutakuwa na kiongozi wa upinzani, maana wajumbe wa upinzani hawapo na vyama vyenye uwakilishi barazani pia havipo isipokuwa CCM.
Mifano ya chaguzi zinazofeli na zikarudiwa ipo mingi. Mathalan, kwa nchi ambaz20o katiba zao zinatamka kuwa mshindi wa nafasi ya urais anatakiwa apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa, na ikatokezea katika uchaguzi husika hakwuna aliefanikiwa kufikisha kiwango hicho (ambacho ndio matakwa ya katiba) basi uchaguzi huo huchukuliwa kuwa umefeli kwa kutokukidhi mahitaji ya katiba. Hili linapotokea uchaguzi hurudiwa ili mahitaji ya katiba yafikiwe. Kwa hali hii ni wazi kuwa Uchaguzi wa Marudio umeshindwa kutoa uongozi kwa mujibu wa matakwa ya katiba na hivyo ni uchaguzi uliofeli. Kwa pale penye dhamira ya utawala wa sheria ni wazi kuwa uchaguzi mwengine kwa Zanzibar ungekuwa dhahir na usingeepukika.
Awadh Ali Said
Mwanasheria

Zanzibar

Msikilize Awadhi Ali Said na Fatma Karume wakizungumza kuhusu uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 2015:

No comments: