ACT WAZALENDO
TAARIFA KWA UMMA
UAMUZI WA BODI YA WAKURUGENZI YA MCC WA KUSITISHA
MAHUSIANO NA TANZANIA YATAWAUMIZA WANANCHI WA VIJIJINI
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeupokea kwa masikitiko
makubwa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa wa MCC wa kusisitisha mahusiano na
Tanzania.
MCC ni ?Shirika la misaada la Marekani lilianzishwa na
Bunge la Nchi hiyo mwaka 2004 kwa lengo la kusaidia miradi ya maendeleo katika
nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya ?kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi.
?Tangu kuanzishwa kwake, shirika hili limesaidia
miradi mingi ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa barabarani na usambazaji wa
umeme vijijini kwa sasa miradi ya aina hiyo inaendelea sehemu mbali mbali hapa
nchini? na miongoni mwao ni pamoja na mradi wa REA,miradi ya barabara kama ile
ya Tnduma Sumbawanga pamoja na Tanga katika barabara ya Horohoro.
Pamoja na vigezo vingine, kigezo mama kwa nchi kufuzu
kupata misaada ya MCC ni kwa nchi husika kuzingatia misingi kidemokrasia
ikiwemo kufanya uchaguzi ulio huru na haki.
Jana tarehe 28 Machi 2016 Shirika la MCC lilitangaza
kusitisha mahusiano na Tanzania kutokana na serikali ya Chama cha Mapinduzi
(CCM),kubariki kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika tarehe
25 Oktoba 205 na kubariki kurudiwa kwa uchaguzi huo tarehe 20 Machi 2016 katika
mazingira ambayo hayakuzingatia misingi ya demokrasia ya vyama vingi na kuvunja
matunda ya mwafaka wa kisiasa na kikatiba uliojengwa kwa gharama kubwa visiwani
humo.
Chama cha ACT-Wazalendo kinapigania nchi yetu
kujitegemea kiuchumi kama msingi wa kujenga utu na uhuru endelevu wa kisiasa na
kijamii. Hata hivyo tunatambua kwamba katika kipindi hiki nchi yetu inahitaji
mahusiano mema na Jumuiya ya Kimataifa na wadau mbalimbali wa maendeleo
duniani, likiwemo shirika la MCC, katika kuendeleza miradi? ya maendeleo.
Shirika la MCC limekuwa mdau mkubwa katika miradi ya barabara na kusambaza
umeme vijini.
Uamuzi huu wa Bodi ya Wakurugenzi wa MCC utawaumiza na
kukwaza juhudi za wananchi wa vijijini katika kujikwamua na umaskini.
Tunasikitika kwamba ubabe wa Serikali ya CCM na woga
wake wa kushindana kidemokrasia umesababisha nchi yetu ikose pesa za MCC ambazo
zingesukuma mbele juhudi za kupambana na umaskini.
Tunatoa wito tena kwa Serikali ya chama cha Mapinduzi
kuacha ubabe na kufifisha juhudi za miaka ishirini za ujenzi wa demokrasia hapa
nchini. Tunatoa wito maalumu kwa wadau wote wa siasa visiwani Zanzibar kurudi
mezani na kutatua mgogoro wa kisiasa kwa njia za kistaraabu na katika hali
ambayo itarudisha heshima ya nchi yetu katika kukuza demokrasia nchini.
Imetolewa na
Theopister Kumwenda
Makamu Mwenyekiti, Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo
ya Nje
29/03/2016
No comments:
Post a Comment