Wednesday, 6 April 2016

DK. SHEIN WAZANZIBARI HAWAKUIKATAA SUK WALIKUKATAA WEWE

Utangulizi

Mmoja wa michezo maarufu ya William Shakespeare niipendayo ni ''Richard The Third.'' Mchezo huu unamuonyesha vipi kupitia ulaghai, mateso na ujanja Richard aliweza kupora taji la ufalme wa Uingereza. Utawala wake haukudumu kwa muda mrefu mara akajikuta yuko katikati ya vita kukilinda kiti alichopora. 

Richard anapigana dhidi ya jeshi la wapinzani wake na farasi wake aliyepanda kauawa katika mapigano yale.

Richard akiwa katika uwanja wa vita anajiona yuko chini hana farasi anatembea kwa miguu anahangaika kutafuta farasi huku akinadi, ''Farasi, farasi, ufalme kwa farasi,'' Richard kapagawa ghafla imeshamdhihirikia kuwa bila ya farasi atauawa na ufalme utamtoka. Katika mtafaruku uliomkumba kaona ufalme si chochote mbele ya farasi. Farasi kawa bora kuliko himaya nzima. 

Nilipokuwa nasoma hapo chini utabiri wa Mohamed  Ghassany kuhusu Dr. Shein ilinijia picha ya Richard the Third na mkasa wa farasi wake vitani. Namwangalia Dr. Shein kama Richard the Third, Dr. Shein akiwa katika taharuki akipiga mayowe akijinadi yeye ndiye mtu fulani, mimi mkubwa wa ufalme huu, wananchi ndiyo walioniweka katika kiti hiki nk. nk. 

Huu mfano umesadifu na mayowe wa Richard akitafuta farasi apande apate kuendelea na vita. Shein yeye mayowe yake anataka kuwakumbusha wananchi kuwa yeye ndiye rais wa Zanzibar. 

Richard the Third alipiga mayowe ya ''farasi,  farasi, farasi kwa  kwa ufalme.'' 

Dr, Shein yeye kelele zake ni, ''“Mimi si Ali tu. Mimi ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nimechaguliwa na umma miye. Kwa kishindo!”
Mohamed Said 

DK. SHEIN WAZANZIBARI HAWAKUIKATAA SUK WALIKUKATAA WEWE

Takribani wiki tatu zilizopita, nilimtabiria Dk. Ali Mohamed Shein kuwa ataiishi miaka yake hii mitano kwenye Ikulu ya Mnazi Mmoja kwa mateso makubwa nafsini mwake. Nilitumia taswira ya mtu ajitazamaye kiooni na kuuona uhalisia kuhusu yeye, huku mwenyewe akitaka kuwaaminisha wengine kuwa yu mtu tafauti.
Hata mwezi mmoja bado haujatimia, tayari kioo kimeanza kumuambia ukweli huo Dk. Shein. Naye, kama utabiri unavyosema, ameanza kugombana nacho kwa kuja nje akipiga makelele huku nje. “Mimi si Ali tu. Mimi ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nimechaguliwa na umma miye. Kwa kishindo!”
Ndiyo muakisiko wa hotuba yake ya juzi kwenye jengo la Baraza la Wawakilishi mjini Unguja, ambapo miongoni mwa mengi yanayoashiria mwangwi wa ugomvi wake huo na kioo, ni pale anapotamka kuwa wananchi wa Zanzibar wameamua kuukataa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kukipa ushindi wa kishindo Chama chake cha Mapinduzi (CCM) tarehe 20 Machi 2016. Sitaki nikumbushie kile kilichosemwa na msaidizi wake mkuu, Balozi Seif Ali Iddi, wiki moja tu kabla ya hapo, kuwa “serikali ya umoja wa kitaifa itaendelea kuwapo”, lakini nakumbusha kuwa matokeo anayoyataja Dk. Shein kuwa yaliukataa muundo wa SUK ni yale yale ambayo hapa tuliyaita “Miujiza ya Jecha iliyomgeuza chura kuwa Mwana Mfalme”.
Kwa kila hali, hayo hayakuwa matokeo yaliyowasilisha wala kuwakilisha sauti ya Wazanzibari. Vyombo vya habari vya ndani na nje vilivyopata nafasi ya kuyaripoti matukio ya Machi 20 vilionesha vituo vingi vya kura kote Unguja na Pemba, vikiwa vitupu. Mitandao ya kijamii pia ilijaa picha za wapiga kura wakionesha kile hasa walichokuwa wakikifanya kwenye vyumba vya kura. Kuna waliopewa karatasi zaidi ya moja za kura – kama mke wa ndugu yangu ambaye pia ni mwalimu wa skuli moja ya wilaya ya Magharibi, lakini wakaishia kuziandika “Allah Akbar” – Mungu Mkubwa. Huyu alirudi nyumbani akilia akimuambia mumewe kuwa anajihisi ameisaliti Zanzibar kwa kuamua kwenda kupiga kura kwa kuwa tu analinda kibarua chake. Kuna waliotuma vidio zinazoonesha wakimpelekea ujumbe Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), kwa kumuandikia: “Jecha, tambua kuwa dhuluma haidumu!” Na hao si kidogo.
Alimradi, kwa mara ya kwanza kwenye siasa za Zanzibar, teknolojia ya mawasiliano ya kisasa ikatumika kuiumbua ZEC, Jecha na CCM kwa pamoja. Uchaguzi walioutisha kwa mbwembwe na hamasa za kuwakomoa wapinzani wao, Chama cha Wananchi (CUF), ukamalizika kwa hizaya kubwa. Kuna ambao wanahoji kwamba lau CCM ilijuwa haya yangelitokea, basi wasingeliruhusu matangazo ya moja kwa moja ya televisheni na redio kutoka vituo vya kura wala wapigakura kuingia na simu za mkononi. Lakini sikio la kufa huwa halisikii dawa!
Mtumiaji mmoja wa mtandao, ambaye kwa hakika ni mwana-CCM aliyekwenda kupiga kura kwa hiyari yake, aliniandikia hivi: “Nimeondoka nyumbani kwangu Mwembenjugu saa 8:00 mchana kwenda kupiga kura kituo cha Kidongo Chekundu na saa 8:30 nikawa nisharejea nyumbani. Hii unajuwa maana yake ni nini, Mohammed?” Nikamjibu sijui. Akaniambia: “Inamaanisha kuwa hata sisi wana-CCM tumegomea uchaguzi huu. Hapa Mwembenjugu, Sogea, Kwahani, Kidongo Chekundu pote hapa ni CCM watupu. Lakini vituo vilikuwa vitupu.”
Ndiyo maana wengine tukasema matokeo yaliyotangazwa na Jecha na kumpa Dk. Shein kura 299,982 sawa na asilimia 91.4 ya kura zinazoitwa halali, ulikuwa mchezo wa mazingaombwe. Inavyoonekana Dk. Shein mwenyewe anaujuwa ukweli wa nini hasa kilifanywa na Jecha kupatikana kwa nambari hiyo.
Kwa hivyo, Dk. Shein anafahamu fika kuwa Wazanzibari hawajaukataa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ambavyo anapiga kelele dhidi ya kioo chake huku nje, bali waliyemkataa ni yeye kuwa kiongozi mkuu wa serikali hiyo. Anajuwa kuwa walifanya hivyo kwa mara ya kwanza tarehe 25 Oktoba 2015, pale walipoamua kumuambia kwa heshima na taadhima kwamba: “Ahsante kwa kutusimamia kwa miaka mitano, lakini ulionesha kiwango kidogo cha uongozi wa Zanzibar yetu. Kwa hivyo, kaa chonjo. Tunamuweka mwenzako!”
Kwa kuwa Dk. Shein na CCM yake hawautambui msamiati wa kukataliwa na umma kwa njia za amani, kama ambavyo wamekuwa wakisema mara kadhaa huko nyuma, wakaamua kutokukubali kukataliwa huko na wakayapindua maamuzi halali ya umma. Vyombo vya dola, ambavyo viko chini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vikaingia njiani kula njama ya kuyahujumu maamuzi yenyewe, na kwa baraka na muongozo wa uongozi wa juu, wakaitisha kile walichokiita “uchaguzi wa marudio wa Machi 20”.
Ni kwenye tukio hili la Machi 20 ambapo Wazanzibari walipata nafasi ya mara ya pili kumkataa Dk. Shein, na mara hii wakamuambia pasina tone la heshima wala haya: “Hatukutaki Dk. Shein kuwa kiongozi wetu!” Wazanzibari walimkataa makamu mwenyekiti huyu wa CCM kuwa rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na wala sio kwamba waliukataa muundo huo. Na kwa kuwa Dk. Shein na CCM wanaujuwa ukweli huo, ndio maana bado ile kampeni yao ya pigapiga, vunjavunja na kamatakamata inaendelea kwenye maeneo kadhaa Unguja na Pemba.
Laiti ingelikuwa Dk. Shein anajiamini kuwa Wazanzibari wamempa ushindi anaosema wamempa, basi angelikuwa na uthubutu wa kuwakabili uso kwa macho popote pale na wakati wowote ule. Angelikuwa shafii na swafii kwao. Lakini kwa kuwa anafahamu ndani ya nafsi yake kwamba walikamtaa, ndio maana anapambana nao kwa kila hali, huku akiapa na kujiapiza kuwa atailinda Katiba dhidi ya yeyote anayeichezea. Kijembe kilioje!
Ni kijembe kwake kusema kuwa Wazanzibari wameukataa mfumo huo, ilhali hata hiyo Katiba anayoapa kuilinda inautambua muundo huo tu wa serikali ya Zanzibar. Ukweli kuwa amemteua Balozi Seif Ali Iddi kuwa makamu wa pili, unatumia mantiki kuwa kulitakiwa awepo makamu wa kwanza, maana huwezi kuwa na wa pili bila ya kuwa na wa kwanza. Lakini umma umemkataa Dk. Shein, tena kwa katao baya kabisa.
Nakumbuka siku ile ya tarehe 25 Oktoba 2015 pale Bungi Miembe Mingi, wilaya ya Kusini Unguja, mara baada ya kupiga kura yake, waandishi wa habari walimuuliza Dk. Shein kwa nini alikuwa anaamini Wazanzibari wangelikuwa na sababu za kumchagua tena kuwa rais wao, naye akataja sababu kadhaa, lakini kubwa yote akasema ni mafanikio yake kwenye kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Akajisifia kuwa hata mataifa ya nje yanakuja Zanzibar kujifunza namna Wazanzibari walivyoweza kuijenga na kuiendesha serikali hiyo. Akamalizia kuwa chochote kizuri ambacho alikuwa amekifanya kwenye miaka ile mitano ya awali ya uongozi wake, kilitokana na mashirikiano ya pande zote mbili, CUF na CCM, na hivyo hivyo kama ni kukosea, basi wamekosea kwa pamoja. Leo hii ni ajabu kwamba kiongozi ambaye hadi miezi mitano nyuma alijisifia na kujipa heshima kwa SUK, anauvunja muundo huo wa serikali kwa kuwa tu aendelee kuwatawala wananchi asiokuwa na ridhaa yao!
Narudia kwa kumalizia. Ukweli ni kuwa Dk. Shein anafahamu fika kuwa Wazanzibari hawajaamua kuyakataa Maridhiano yao. Hawajaamua kuivunja Katiba yao. Hawajaamua kuirejesha nchi yao kwenye zama za ujahili. Walichokuwa wamekiamua ni kumkataa yeye kama kiongozi wao. Na hilo ndilo linaloendelea kuyafanya maisha yake ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano kuwa jehanamu ya duniani.
Inayumkinika kuwa baina ya 2010 na 2015, Dk. Shein aliishi kama kiongozi asiyekubalika miongoni mwa viongozi wenziwe kwenye CUF na hata CCM yake, lakini alisalia kuwa kiongozi anayeheshimika kwa wote. Wananchi ambao waliamini kabisa kuwa hakuwa mshindi halali wa uchaguzi wa 2010, waliamua kumpa heshima yake kama kiongozi aliyekaa madarakani kwa moyo wa Maridhiano; na ikawa hivyo. Lakini urais anaouanza sasa unakumbana na yote mawili – kutokukubalika na kutokuheshimiwa. Sio tu wapigakura wa CUF wanaomuona kuwa huyu ni mtawala aliyejitwalia madaraka kwa mtutu wa bunduki uliopachikwa kikaratasi cha kura kwenye sime yake, bali hata kwa wana-CCM wenzake ambao wanajuwa kuwa iliwabidi kufanya mapinduzi mengine kurejea madarakani, lakini sio kwa kura za wananchi.

No comments: