Wednesday, 6 April 2016

MAPITIO YA KITABU: Maisha na Nyakati za Abdulwaheed Sykes na Simon Noel


Maisha na Nyakati za Abdulwaheed Sykes


Historia isiyosimuliwa ya harakati za Waislamu dhidi ya ukoloni wa Uingereza nchini Tanganyika ni kitabu kilichoandikwa na mwandishi maarufu nchini Tanzania aitwaye Mohammed Said na kimebeba historia nzito sana juu ya harakati za kupigania uhuru wa nchi ya Tanganyika.

Mwandishi amezaliwa na kukulia katika kitongoji maarufu cha Gerezani Kariakoo eneo ambalo ndilo lilikuwa chimbuko la mapambano dhidi ya ukoloni wa waingereza nchini Tanganyika (rejea hotuba ya Mwalimu Nyerere wakati akiwaaga wazee wa Dar es salaam.

Endapo utabahatika kukisoma kitabu hiki basi utaona hazina kubwa iliyopo ndani yake na utaweza kabisa kuthubutu kusema kuwa vitabu vyote vilivyowahi kuandikwa juu ya historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika vilikuwa ni porojo tupu na viliandikwa kwa kusudi maalum lenye lengo la kumnufaisha mtu fulani au kikundi fulani cha watu na sio kuelezea historia kamili ya uhuru wa Tanganyika.

Katika kila alichokiandika mwandishi ameweka ushahidi makini tena wenye kueleweka ipasavyo hivyo ni dhahiri kabisa kuwa mwandishi alifanya utafiti mkubwa sana kabla ya kuanza kuandika kitabu.

Mwandishi amezielezea koo mbili za Sykes na Dosa Aziz kama koo zilizokuwa mashuhuri na zenye kuheshimika sana jijini Dar es salaam katika miaka ya 50.

Pia mwandishi alielezea jinsi askari wa Tanganyika waliopigana Vita ya Pili ya Dunia walivyopanga kuanzisha harakati za kupigania uhuru na pia kuanzisha chama cha siasa. Vyote hivi vilifanyika chini ya uongozi wa Abdulwaheed Sykes.

Mwandishi ameeleza vizuri kabisa kuwa baada ya Hamza Mwapachu na Abdulwaheed Sykes kufanya fujo katika makao makuu ya T.A.A mwaka 1950 ambapo tukio hili lilianzisha enzi mpya ya harakati za vijana katika mapambano dhidi ya ukoloni wa Uingereza. Kwani siku chache baadae uchaguzi uliitishwa na Dr Vedasto kyaruzi alichaguliwa kuwa rais wa T.A.A na Abdulwaheed Sykes akachaguliwa kuwa katibu (ukurasa wa 92)

Miezi michache baadae Dr Kyaruzi alihamishiwa Nzega kikazi na hivyo Abdulwaheed Sykes alikaimu nafasi ya urais.

Chini ya uongozi wa Abdulwaheed Sykes T.A.A ilifanikiwa kutatua matatizo makubwa yaliyowasibu watanganyika ikiwemo swala la Ardhi lililowasibu wameru na hatimaye TAA iliweza kumpeleka Japhet Kirilo UNO kuwasilisha madai ya wameru kunyang'anywa ardhi.

Mwandishi pia ameeleza namna vijana na wazee wa Dar es salaam walivyoanza harakati za kupinga ukoloni wa Waingereza mapema kabla hata TANU haijaundwa.

Pia ameeleza jinsi Mwalimu Nyerere alivyojiunga nao na hatimaye kuchaguliwa kuwa rais wa TAA na baadae wote kwa pamoja wakaasisi TANU.

Mwandishi ameeleza vizuri kuwa Nyerere alikuwa amemzidi Abdulwaheed na hivyo aliweza kumshinda katika urais wa TAA katika uchaguzi wa mwaka 1953.

Pia mwandishi ameeleza vizuri juu ya uamuzi wa busara wa Tabora ulivyofanikisha kuleta uhuru wa Tanganyika mapema.
  
MAPUNGUFU
Kiuhalisia hakuna kazi yoyote ile ya fasihi inayokosa mapungufu. Kitabu hiki ni moja kati ya vitabu vichache sana vyenye kiwango kidogo sana cha mapungufu. Na hii ni kwa sababu mwandishi alifanya utafiti wa kina kabla ya kuandika kitabu hiki.

Sehemu pekee niliyoiona ina mapungufu katika kitabu hiki ni ukurasa wa 60 ambapo mwandishi ameeleza jinsi Abdulwaheed Sykes na askari wenzake wakiwa nchini Burma katika mji wa Imphal ambapo kwa pamoja walikubaliana kuunda chama cha siasa na walikipa jina la TANU.

Nadhani mwandishi hakulielezea kwa kirefu tukio hili muhimu sana kwa taifa letu. Niliwahi kumsikia Mzee mmoja aliyepigana vita kuu ya pili ya dunia ambaye nae alikuwa mmoja wa washiriki wa tukio hilo akisema kuwa wakiwa nchini Burma waliunda chama cha siasa na walidhamiria kwa dhati kupigania uhuru wa nchi yao pindi watakaporudi nyumbani. Kwa muda huo wakipanga hayo walikuwa jirani kabisa na askari wenzao kutoka Kenya ambao wao pia walidhamiria kuanzisha harakati za kupigania uhuru pindi wakirudi nchini kwao na ndipo waliporudi wakaanzisha Mau Mau (Rejea Mau Mau ilianzishwa na askari 40 waliopigana vita kuu ya pili ya dunia)

Mzee huyo alisimulia kuwa wao askari kutoka Tanganyika walifikia hadi hatua ya kuunda wimbo wa Taifa mahsusi kwa ajili ya Tanganyika pale uhuru utapopatikana.

Wimbo wenyewe ndio ule wa Tanzania Tanzania nakupenda kwa moyo wote, kwa wakati huo waliimba Tanganyika Tanganyika nakupenda kwa moyo wote. Kwa bahati mbaya au nzuri wimbo huo haukutumika kama wimbo wa Taifa baada ya uhuru.


HITIMISHO
Kitabu hiki ni moja kati ya vitabu bora kabisa vya historia ya uhuru wa nchi yetu. Historia kamwe haiwezi kudanganya maana hueleza matukio ya kweli yaliyotokea siku zilizopita. Nathubutu kabisa kusema kuwa yaliyomo ndani ya kitabu hiki ndio historia rasmi ya uhuru wa nchi yetu.

Pongezi kwa mwandishi kwa kuweza kufanya kazi kubwa sana kutafuta ukweli wa historia ya harakati za kudai uhuru wa nchi yetu.

Simon Noel
B A Development Studies
University of Dodoma

No comments: