UKURUGENZI
MKUU NSSF 1997 – 2016
HIVI
DOKTA DAU HANA JEMA HATA MOJA?
Kabla
ya kuanza kuandika chochote kuhusu maudhui yenye anuani hiyo hapo juu,
niwakumbushe wasomaji wangu ‘kisa’ kimoja nilichohadithiwa na rafiki yangu
ambaye alikishuhudia yeye mwenyewe katika nchi moja (sipendi kwa leo kumtaja
wala kuitaja hiyo nchi).
Dereva
wa gari ambaye ni mzaliwa wa nchi hiyo aligonga gari ya mwenzake ambaye ni raia
wa kigeni kwa dhahiri shahiri. Huyu dereva mzalendo ndiye aliyevunja utaratibu
lakini cha ajabu yeye akawa akimlaumu, akimgombesha na kumtukana matusi mazito
mazito yule aliyemgonga.
Yule
aliyegongwa baada ya kuona watu wamejaa katika eneo la tukio akauliza: “Jamani!
Katika hali hii mimi hapa kosa langu ni lipi?” Yule mzalendo aliyemgonga
akamjibu hivi (na hapa ndipo kwenye nukta ninayoikusudia): “Kosa lako wewe ni kuwepo hapa nchini petu kwani kama ungekuwa kwenu, Je
ningekuja kukugonga huko?”
Kisa
hiki kinanikumbusha kwamba kuna baadhi ya makosa yanasababishwa na kumchukia tu
mtu mwenyewe na wala si kuangalia kosa kama kosa katika mizania ya sheria.
Katika
muktadha huo, ni vizuri tukajiuliza maswali kadha wa kadhaa juu ya ‘mlipuko’ wa
baadhi ya wanahabari kumshambulia kwa kasi kubwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika
la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dokta Ramadhan Dau. Kulikonii? Au kosa lake ni kwamba alikalia mahala pa
watu ambapo leo pamerudishwa kwa wenyewe?
Baadhi
ya Watanzania wamestaajabishwa sana na ‘mlipuko’ huo mkubwa wa kumtangaza na
kumshambulia Dokta Dau kwa tuhuma za ufisadi kwa sababu:
a) Hao
‘washika bango’ wa kuutangaza huo waliokwishauhukumu kuwa ni ufisadi
hawaonekani kama wana lengo la kuhabarisha bali wamejipa kabisa mamlaka ya
kuhukumu kwa kiwango ambacho hata hawakuhitajia kumhoji huyo wanayemtuhumu,
jambo ambalo linaitia kasoro taarifa yao hiyo kwa jamii.
b) Wakati
wanamjengea ‘kuchafuka’ huko katika jamii ya Kitanzania wamesahau kwamba ndio
‘wanamkejeli’ Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta John
Pombe Magufuli, kana kwamba hana vyombo makini vya kumpa taarifa na ‘akapotoka’
kwa kumteua kuwa Balozi mtu ambaye kwa mtazamo wao ni ‘mhalifu’ anayehukumiwa
hata bila ya kustahiki kuulizwa na kujitetea.
c) Wakati
washika bango hao wakikazia kumchafua Dokta Dau huku wakisahau kwamba katika
uhalifu wowote ambao ni ‘shirikishi’ kumng’ang’ania mtu mmoja tu tena kwa
kumtuhumu tuhuma nzito huku wakiwaacha wengine, ni dalili ya kuwepo ‘ajenda’
zilizofichwa nyuma ya mpango huo.
d) Washika
bango hao wanastaajabisha kwa ufahamu wao juu ya taarifa za Dokta Dau lakini
‘wakazikalia’ mpaka alipoondolewa ndipo ‘wapumue’ kwa kuzitoa. Je,waliogopa
nini kuzitoa hapo awali? Na kwanini sasa hawaogopi kuzitoa taarifa hizo?
Kama
ni kweli kwamba chanzo chao kikuu cha taarifa ni Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) (Ripoti ambayo tayari Ofisi ya CAG
imeshaikana), hivi Watanzania leo hii tumefikia kuifanya taarifa ya ukaguzi
kuwa ndio hukumu halafu eti huo tuuite ndio utawala bora unaofuata sheria? Hivi
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inajadiliwa kwanza na
wanahabari kisha wafikie au iwafikie watuhumiwa katika kadhia husika?
Amma
kwa upande wa pili ndipo linapozalika swali ambalo huenda lingekuwa ndio
ufumbuzi wa dhana ya chuki ‘binafsi’ dhidi ya Dokta Dau. Nayo ni kwamba huyo
Dokta Dau aliyetumikia katika Shirika la NSSF kwa zaidi ya miaka kumi; hivi
hana hata jema moja linalofaa kutangazwa?
Hivi
jicho lenye uadilifu linaweza kuangalia mapungufu ambayo ni dhana na likawacha
mafanikio ambayo ni hakika? Je, washika bango wanakitazama Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM) kwa mtazamo upi? Je, wanaitazama miradi ya ujenzi wa nyumba za
makazi inayofadhiliwa na NSSF kwa mtazamo upi? Je, wanalitazama Daraja la
Kigamboni kwa mtazamo upi? Je, hayo na mengineyo kwa mtazamo wao ni mafanikio au
mapungufu?
Hivi
utendaji wa Dokta Dau katika Shirika la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF) kutokea mwaka 1997 hadi 2016 mwanzoni, hakuna jema hata moja linalofaa
kutamkwa kabla ya kupekua kinachoonekana kuwa ni mapungufu?
Watanzania
lazima tuwe wakweli na kamwe tusiache kujifunza kutokana na msemo wa Waswahili
usemao: “Mnyonge mnyongeni lakini haki
yake mpeni.” Kitendo cha kusahau kabisa mambo mema na mafanikio ya Dokta
Dau katika Shirika hilo, hapo ndipo inapopata nguvu ile dhana kwamba Waislamu katika
Tanzania hawatarajiwi kuwa raia wa daraja sawa na wenzao wa dini nyengine. Kwa
hiyo, Muislamu ‘msomi’ katika Tanzania akishika wadhifa wowote katika serikali
au shirika la umma hata kama atafanikisha mafanikio makubwa, anaonekana
amefanikiwa kwa bahati mbaya tu kwa sababu sio matarajio Muislamu kutegemewa
kuwa na uwezo katika utendaji.
Tumeshuhudia
mara zote ambazo Waislamu wamekuwa viongozi wa juu katika nchi hii au katika idara,
taasisi na mashirika mbalimbali ya serikali wamekumbana na matatizo na
vizingiti kadha wa kadhaa mpaka walipobadilishwa na kupewa ‘wenyewe’ nafasi
hizo, hapo sasa ndipo utulivu hupatikana.
Katika
nchi yenye uwiano wa kukaribiana kiidadi raia wake kiimani ni aibu kubwa kuona
kila eneo katika idara, taasisi na mashirika ya serikali kujazwa na raia wa
dini fulani na akipatikana mmoja tu wa dini nyengine katika idara, taasisi au shirika
lolote la serikali ‘atachimbwachimbwa’ mpaka ang’olewe na akishang’olewa kwa
sababu tu amekalia sehemu ya ‘watu’ atachafuliwa ili jamii iaminishwe kwamba
alistahili kuondolewa.
Katika
hali ya ubaguzi wa aina hiyo, Watanzania Waislamu wanajiuliza: Hivi kweli
tatizo ni kuwa Waislamu ‘hawakusoma?'
Hivi
kwa nchi iliyo huru kwa takriban miaka hamsini sasa yule aliyewabagua raia wake
kwa misingi ya dini mpaka kundi moja likapewa fursa ya elimu na kundi jengine
likanyimwa; Je, huyo ni mzalendo au ni mbaguzi? Na Je, ni kweli kwamba Waislamu
hawakusoma? Je, hawa Waislamu waliofikia viwango vya kushika urais, uwaziri,
ukatibu mkuu wa wizara, ukurugenzi na kadhalika, sio Watanzania?
Ukweli
ni vizuri ukasemwa kwamba Dokta Dau ashukuriwe kwanza mpaka Watanzania
wajiridhishe kwa mafanikio haya makubwa yanayoonekana kabla ya kugeukia hayo
yanayoitwa mapungufu. Huo ndio uungwana na ndio ustaarabu.
Katika
hali hiyo sio vyema kukaa kimya kwani jamii kama inavyobadilika kitabia basi
inabadilika kiuvumilivu na viwango vya subra.
Hivi
ni kweli Dokta Dau hana jambo jema hata moja katika utumishi wake kama
Mkurugenzi wa Shirika la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kiasi cha
kuandamwa na ‘kusulubiwa’ namna hiyo? Na kama lipo, basi litajwe kwanza kwa
sababu jema lipo wazi na linaonekana lakini mapungufu ni dhana inayohitaji
ushahidi uliothibitishwa katika vyombo husika.
Hii
ndiyo kauli yangu ya wiki hii na mjadala uko wazi.
Mwandishi
wa makala haya ni Mwenyekiti wa ARRISAALAH ISLAMIC FOUNDATION.
Unaweza
kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749.
No comments:
Post a Comment