Friday, 15 April 2016

SHEIKH HASSAN BIN AMIR NA BEN RIJAL


Sheikh Hassan Bin Ameir-7

Na Ben Rijal


Sheikh Hassan Bin Ameir ni msomi wa kujivunia, akiwa  ni tunu aidha ni nuru iliyoweza kung’ara katika ukanda wa Afrika Mashariki na nje ya mipaka yake. Sheikh Hassan bin Ameir hakuvitenganisha vitu viwili baina ya Dini na Siasa alivyweka vitu viwili hivo kama ni pacha kutokana na Uislamu kutovitafautisha vitu viwili hivi. Alikuwa Mufti wa Tanganyika na kuchangia pakubwa katika Uhuru wa Tanganyika, aidha alisambaza umoja kwa watu wa dini zote, hayo yote mema aliyoyafanya anapambana na Persona non Grata na PI ndani ya nchi ya Tanzania.

Katika makala mbili zilizopita niliwazungumzia Masheikhe wawili ambao walikuwa ni wanaharakati na wenye misimamo tafauti na wengi wa Masheikhe wa nyakazi zao na hata wa nyakati hizi za sasa, Masheikhe hao ni Sayyid Mansab na Sheikh Ali Bin Khamis bin Salim Al-Barwany, wao waliweza kukinzana na watawala, aidha kupenda kujisomea na kuandika, utapomsoma Sheikh Hassan bin Ameir utamuwona hayuko mbali na watangulizi hawo Sayyid Mansab na Sheikh Ali bin Khamis.

IMG-20140808-WA0039
Mufti Sheikh Hassab bin Ameir

Shekh Hassan bin Ameir bin Mazi bin Haji bin Khatib Al-Shirazy amezaliwa mwaka wa 1300 AH (1880 CE). Sheikh Hassan bin Ameir alikuwa alimu mkubwa wa Zanzibar na Afrika Mashariki kwa jumla, akiwa mzaliwa wa Mkoa wa Kusini Unguja katika kijiji cha Mtegani, Makunduchi, alianza masomo yake ya Qur’an hapo kwao Mtegani, hakudumu muda mrefu kustakimu na kusoma hapo kijijini kwao akahamia kijiji cha Dunga amabapo nako huko alikuwa akisoma chuwoni na kujifunza dini akiwa mwenye umri mdogo. Kujifunza dini katika umri mdogo  ndiyo desturi ya watoto wa Kiislamu visiwani na duniani kote.

Kutoka Dunga Sheikh Hassan bin Ameir akahamia katika kijiji cha Upenja ambapo alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi waliokuwa wakimudu fani ya Tajwidi, aliendelea kukaa Dunga kwa muda kisha akaelekea mjini ambapo alipata fursa ya kusoma kwa Maulamaa wa nyakati hizo ambao kwa leo tutaweza kuwaita Ma-Professa, kwani walimu hao waliomiminia elimu walikuwa kila mmoja wao akimwambia mwenzake nipishe. Mashekhe aliosoma kwao ni  Sheikh Hamdani bin Abdulkadir Al-Qahtan, Sheikh Said bin Dahman, Sheikh Muhammed bin Abdaulla bin Wazir, Sheikh Ali bin Mandhry huyu alisoma kwake huko Pemba, Sheikh Abdulrahman bin Mahmoud, Sheikh Abdulrahman bin Hassan, Sheikh Muhammad bin Ali Khamis Al-Barwany, Sheikh Abdallah bin Amour bin Muhammed al-Mendhry na Sheikh Abdulla bin Amour al-Azzi.

Mbele ya mashekhe hao alisoma ilimu zote ikiwa pamoja na Fiqh, Tafsiri ya Qur’an, fani zote za lugha, Sayansi ya hadithi za Mtume Muhammad (SAW). Maulamaa wote ambao  waliomsomesha walimkubali kuwa mwanafunzi wao ataweza kuendeleza kile walichomfunza.

SHEIKH+HASSN+BIN+AMEIR+MWANZA
Sheikh Hassan bin Ameir na baadhi ya wanaharakati

Sheikh Hassan bin Ameir alianza kazi ya kusomesha kabla ya kujiunga na Mahkama ya Kadhi, na alipokuwa anasomesha aliweka madrsa yake katika mtaa wa Misufini madrasa iliyokuwa ikijulikana kwa jina la “Madrasa el-Shirazi”, watu wengi walinufaika na madrasa hiyo, ingawa kwanza ilikuwa na wanafunzi wengi kutoka sehemu za kwao Makunduchi lakini kipindi kisichokuwa kirefu  wanafunzi walikuwa wakifurika kutoka sehemu mbalimbali za Unguja, Pemba, Mrima na baadhi ya sehemu nyenginezo za maeneo ya Afrika Mashariki na kati kwenda kusoma kwa alimu huyu.

Ingawa Sheikh Hassan alikuwa ameshapea na kuwa mwalimu lakini alikuwa hajasita na kusoma sio kwa kujisomesha mwenyewe tu lakini ilikuwa yupo tayari kwenda popote pale panapotolewa elimu kwenda kujifunza, ndipo alipokuja Unguja Sheikh Abdulbari Al-Aziy kutoka Misri, Sheikh Hassan bin Ameir  alikuwa mmmoja katika wanafunzi waliojiunga kwa kupata taaluma kwa mwalimu huyo, na kati ya mengi aliyoyasoma hapo ilikuwa pamoja na uandikaji wa khati, inasemekana Sheikh Hassan alikuwa na khati nzuri sana za Kiarabu kwa maandishi ya “nusha” na “rika”, vile vile alisoma masomo ya hesabu ambayo ni muhimu katika fani ya mirathi, mmoja aliyowahi kusoma kwake alifika kueleza kuwa “ulipokuwa ukiingia mlango wa mirathi kila mmoja akisikia raha kutokana na namna Shekhe alivyokuwa akimudu mada ya mirathi”. Sheikh Hassan alijifunza Kiswahili cha skuli kwa mwalimu wa Kiengereza Mr. River Smith, na alipomaliza msomo hayo akapatiwa cheti kilichomruhusu kusomesha katika skuli za Serikali na kuweza kufanya kazi popote pale anapotakiwa mtu wa elimu ya dini.

Wakoloni wa Kiengereza walijaribu kutaka kuweka mfumo ambao walimu wa Chuwoni waweze kujikimu katika kazi zao za usomeshaji na katika mpango huo uliwawezesha wengi wao kusomesha katika skuli za serekali (Rejea: Between Social Skills and Marketable Skills, The Politics of Islamic Education in Zanzibar in 20th Century Zanzibar-Roman Loimeier). Sheikh Hasasan alisomesha skuli nyingi kisiwani Unguja na Pemba za mjini na mashamba  ikiwa pamoja na skuli ya Makunduchi, Muyuni, Kiembe Samaki, Chake Chake Pemba na kwengineko.

Wengi kati ya wanafunzi wake walishika nyadhifa mbalimbali katika sehemu zao walizokuwa wakiishi akiwemo Mufti wa Ngazija Muhammed bin Abdulrahman, Sheikh Fatawi bin Issa aliyekuwa kadhi baada ya kuwacha ukadhi Sheikh Abdaalh Saleh Farsy na kuhamia Kenya, Sheikh Ameir Tajo Al-Shirazi naye pia alikuwa kadhi mkuu wa Zanzibar, Sheikh Rashid bin Haji Al-Shirazi wa Tabora, Sheikh Abdalla Iddi Chaurembo wa Mrima, Sheikh Ramadhan Abass wa Mrima, Sheikh Masoud bin Khatib wa Rufiji, Sheikh Abdulmuhsin bin Kitumba wa Ujiji-Kigoma, na wengi wengineo.

Sheikh Hassan bin Ameir aliwacha kazi ya ualimu na kujiunga na Mahkam akiwa kama karani, na nyakati hizo zilikuwa sio elimu yako tu ndio inakubalika lakini shakhsia yako nayo ilikuwa ni kiegezo cha kuweza kupata kazi, aliifanya kazi vilivyo na kwa uadilifu kabisa na hakuna yeyote yule aliyewahi kumtia ila juu ya kazi yake.

Sheikhe Hassan bin Ameir kuelekea Bara na Safari zake
Sheikh Hassan alielekea bara kwa kustakimu na kufanya kazi kubwa ya tabligh, kuna wengine wanaosema kuwa kule bara aliitwa kwenda kuokoa jahazi, kuna wengine wanasema alikwenda kwa hiari yake. Kuna kauli nzito inayoelezea kuwa kuhama kwake Zanzibar na kuelekea Tanganyika nikutokana kuombwa na Al-Habib Syd Umar bin Sumeit kufanya hivyo.

ANd9GcQDHeQPG3CgbU4VQ8v1YKNWxNNvMmgtGb9MqAdy9pJnfuDxTi5ayw
Sheikh Hassan bin Ameir mwenye miwani na Al-Habib Syd Umar bin Sumeyt

Alipokuwa Tanganyika alifanya kazi kubwa sana ya kusomesha na ilipoundwa Jumuia ya Waislamu wa Afrika ya Mashariki “The East African Muslim Welfare Society”  (EAMWS) iliyokuwa chini ya ulezi wa kiongozi Mohammed El Husaini Aga Khan iliyoasisiwa katika mwaka wa 1945, Sheikh Hassan bin Ameir alikuwa katika washauri wakuu wa jumuia hii na kusimama kwa jumuia ilikuwa kutoakana na mchango wake mkubwa wa kifikra na uongozi.

Kushamiri utendaji wake wa kazi na kuanza kujulikana umahiri wake wa taaluma nje ya Afrika Mashariki kuliandaliwa msafara wa wajumbe wa EAMWS kwenda nchi za Misri, Lebnon na nchi nyengine za Kiislamu kwa kutafuta msaada wa kujenga Chuo Kikuu Cha Kiislamu katika Afrika ya Mashariki, msafara huo ulijumuisha masheikhe na wanasiasa akiwemo Tewa Said Tewa, Mwinyi Baraka na wengineo maelezo zaidi ya msafara huo na kazi zake za Mrima pitia kitabu cha Ndugu Muhamed Said “Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes 1924-1968.” Safari hio inasemekana kuwa ilikuwa ya mafanikio makubwa sana na ilizaa matunda kwa kukubalika kujengwa kwa Chuo Kikuu hicho katika mji wa Zanzibar katika mtaa wa Kwa Mtipura, ardhi iliotolewa kwa ujenzi wa Chuo Kikuu hicho ni cha  watoto wa Sheikh Muhammad Nassor Lemki na watoto wa Masoud bin Ali Riyami maarufu Bwana Udi (Rejea: Conflicts and Harmony in Zanzibar –memoirs-Ali Muhsin Barwany.)

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjiG4LYaww5b-wRO6WFIHq-GrczRcoScCwGnBO9wQDwN_vf1X9dA1tHoI5uukMiImNGvoGjAR2aIVAsn43d9tM9wmz_2HZZj_akOLKUi534yT7KrxjwvmdzTbozOsjoJdlMwYP6lIF5LJo/w674-h577-no/20140430_150609.jpg
KutokaKushoto: Sheikh Hassan bin Ameir, Mwalimu Nyerere, Sheikh Abdalla Chaurembo, Rashidi Kawawa

Sheikh Hassan bin  Ameir alitimiza nguzo ya Hijja kama wanavyotakiwa Waislamu wenye uwezo kwenda Makka kuhiji mara mmoja katika maisha yao. Aliporejea kutoka Makka marejeo yake alizuru Chuo Kikuu na kikongwe duniani chuo cha Al-Azhar huko aliweza kupatiwa fursa ya kutoa mhadhara mdogo ambao wengi walishtuka kuona mtu ambaye amesoma Unguja tu na Pemba yake kuweza  kuwa na umahiri na umilikaji mkubwa wa lugha ya Kiarabu na kumpelekea Sheikh Mahmoud  Zuttuti kumkubali na kusema kuwa “Afrika Masahariki imepata lulu”.

Yaliompoza Sheikh Hassan bin Ameir
Mara nyingi mtu huponzwa kwa mabaya, lakini mara nyengine hata mazuri nayo humponza mtu, Sheikh Hassan bin Ameir yeye aliponzwa kwa mazuri aliyoyatenda. Mambo matatu tunaweza kusema ndio yaliomponza Sheikh Hassan bin Ameir na kubidi kurejeshwa Unguja na kutotakiwa kuonekana katika ardhi hapo ishakuwa inaitwa Tanzania Bara. Moja kati ya hayo mambo matatu ni ziara yake ya Kongo, Kinshasa (Congo, DRC kwasasa), mchango wake katika hotuba ya Maalim Nyerere aliyoitoa Umoja wa Mataifa na mchangao wake mkubwa katika kuisimamisha Jumuia ya Waislamu wa Afrika ya Mashariki. (Rejea: Mazungumzo na Sheikh Ahmed.)

Moja katika safari zake za Kongo, Kinshasa aliweza kuwahamasisha Waislamu juu ya elimu na umuhimu wake, Waislamu wa Kongo walihamasika na kuchangishana fedha nyingi kumpa kwa furaha yao kuweza kuwaunganisha na kuwaongoza, Sheikh Hassan alipokabidhiwa kitita cha fedha zimsaidie kwa safari yake na matumizi huko nyumbani anakorudi, kwa mastaajabu ya wengi hakuchukua hata faranga mmoja,  kwetu huku tutasema hakuchukua hata shillingi na badala yake akawataka Waislamu pesa zile alizopewa zijengewe Skuli wala sio Madrasa, habari zikamfika Gavana wa Kibelgiji, kusikia hayo akataka kumuoana huyo mtu aliopewa pesa akazikataa na kutaka kujengwe Skuli, walipokutana na kuzungumza Sheikh Hassan bin Ameir alisisitiza kuwa elimu ni muhimu, elimu ya dini wataipata Misikitini lakini ni muhimu kusoma elimu ya dunia kuweza kuwasaidia vijana wa Kiislamu kuweza kupata nafasi za uongozi serikalini, Gavana huyo hapo hapo akaandika waraka na kupiga mhuri wake kuwa Sheikh Hassan anaweza kuingia Kongo wakati wowote ule bila ya Viza, hilo ni moja katia yaliomponza, jambo la pili ni pale mwalimu Nyerere alipotoka Glasgow aliporudi Tanganyika alishauriwa huko Scotland kuwa asiwache kuzungumza na Sheikh Hassan bin Ameir kuweza kupata ushauri kati ya mambo atakayoyazungumzia huko Umoja wa Mataifa, hilo ni la pili kati ya liomponza na la tatu ni kuwa mshauri na kiongozi wa Jumuia ya EAMWS hili ndilo lilokuwa kubwa ambalo alitoa mchango mkubwa kuweza kupatikana kujengwa kwa Chuo cha mwanzo cha Waislamu Afrika mfano wa Al-Azhar.

Mambo matatu hayo yalimponza na kuonekana ni mtu adui na hatari, hapo ndipo alipotiliwa chonza na kupewa amri kuwa mtu asiotakikana Persona non Grata na kurejeshwa Zanzibar kutotakiwa kuoneka kurudi katika ardhi ya Tanganyika na kuwa asiotakikana kabisa Prohibited immigrant (PI), hayo yalimkuta katika mwaka wa 1968, Sheikhe anarudishwa kwao na kumkuta yaliowakuta watu kama Imam Ahmad bin Hambal.



Picture+008

Sheikh Ali bin Abbas mwanafunzi wa Sheikh Hassan bin Amir wakati alipokuwa anasomesha Dar es Salaam katika miaka ya 1950 akiwa na mtafiti wa Kimarekani James Brenan

Sheikh Hassan bin Ameir alifanya kazi ya Daawa kwa upana kabisa pamoja na kuwahamasisha watu kujiunga na TANU, Sheikh Hassan alikuwa ni msomi aliokuwa na imani kuwa watu wote ni sawa na alikuwa hakubaliani kabisa watu kujigawa kwa misingi ya kidini.

Viatabu alivyoviandika

Sheikh Hassan alibarikiwa kupata fursa ya kuandika vitabu na kati ya vitabu alivyoviandika ni:
*      Wasialatul Rraja (Shrerehe ya Safinatul Najaa)
*      Fathul Kabir (Sherehe ya Mukhtasarul Kabir)
*      Idhanil Maani Fi-Asamail Husana (Sherehe ya Taibatil Asmai)
*      Musliku Karib Fi mughnil Muhtaj (Sherehe ya Maslaqul Qarib)
*      Madarijul Ulaa (Sherehe ya Tabaraka Dhul Ulaa).
            Kuna  baadhi ya vitabu alivyoviandika na kutochapishwa ni pamoja na :

No comments: