Friday, 1 April 2016

KITENDAWILI CHA UHURU NA MADARAKA “ASIYOYASEMA MOHAMED SAID KWENYE UANDISHI WAKE WA HISTORIA MPYA YA NCHI YETU “ NA KAMARA KUSUPA

Kamara Kusupa's Profile Photo
Kamara Kusupa

Kupitia makala hii sikusudii kulumbana na Mohamed Said wala kubeza chochote kinachohusu uandishi wake, ila nataka kuuweka wazi ukweli ulio nyuma ya pazia. Najua Mohamed Said anasomwa na wengi, binafsi nimesoma maandiko yake mengi vikiwemo vitabu alivyoandika katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili.

Nakiri kwamba anafanya kazi njema, anachimbua na kuwaletea wasomaji yasiyoandikwa kwenye vitabu vinavyotumika kufundishia historia ya nchi yetu. Kazi ya kupata nyaraka za zamani si ndogo inahitaji mtu aliyejitoa “committed” pia anayeaminiwa na hao wenye nyaraka.

Niliwahi kumwona Bibi Titi Mohamed enzi za uhai wake akiwa bado ana kumbukumbu zake, nilikusudia kumshawishi anieleze ukweli anaoujua kuhusu Nyerere kujiuzulu uwaziri mkuu baada ya siku 42 tu tangu aupate na kwanini alimwachia Rashid Kawawa na si mwana TANU mwingine.  Nilitarajia angesema niliyosikia kwa Oscar Kambona na Mzee Kajunjumere, lakini alinijibu kijumla.

Nilichobaini Bibi Titi hakuniamini pia alihofia kunukuliwa vibaya, baada ya misukosuko aliyopitia ya kuwekwa ndani na utawala wa Nyerere hakupenda tena kusikika akisema lolote lenye mwelekeo hasi.

Mohamed Said anapowazungumzia mashujaa waliopigania uhuru wa Tanganyika anainua zaidi dini yao kuliko uzalendo wao, naamini waliopigania uhuru pamoja na kuwa Waislamu, lakini hawakusukumwa na dini yao walisukumwa na uzalendo.

Waliipenda nchi yao uzalendo wao ndio unaotufanya hata sisi tusio Waislamu tuwaenzi.
Jingine linalojitokeza kwenye kalamu ya Mohamed Said ni picha anayochora, anajitahidi kuonyesha Waislamu walivyoshiriki harakati za uhuru wa Tanganyika, Waislamu walivyofanya jitihada za kuung’oa ukoloni, Waislamu walivyofanikisha upatikanaji wa uhuru wa nchi yetu, lakini baada ya uhuru likatokea janga kwao Waislamu hawakutendewa haki kwa namna moja au nyingine na utawala uliofuata baada ya kuondoka mkoloni.

Mohamed Said kupitia uandishi wake ni kama anachora picha na kuwaachia wasomaji watoe hitimisho, kila ninapoyasoma maandiko yake nakumbuka kisa cha wachoraji wawili kwenye mji mdogo wa Moravian nchini Ujerumani, walioishi karne ya 16 wakati Martin Luther (mwasisi wa dhehebu la Lutherani) alipoendesha mapambano ya kuupinga utawala wa Papa wa Roma.

Papa alikuwa na ziara ya kuitembelea Ujerumani, wachoraji wawili wakaenda kwenye lango la jiji wakachora picha mbili moja ilimwonyesha Papa aliyepanda farasi akiingia mjini na vazi lake la kifahari lenye wasindikizaji 24 kumi na mbili upande wa kulia na kumi na mbili upande wa kushoto.  Wakachora picha nyingine iliyoonyesha Yesu akiingia Yerusalemu akiwa amepanda punda. Kisha wachoraji wakaandika maneno na kuyawekea alama ya kuuliza kati ya hawa wawili nani BWANA?

Picha hiyo ilitosha kuwafikirisha watu na kuleta mapinduzi, kila aliyekwenda kuitazama alirudi na fikra mpya za kumwasi Papa wa Roma, mwisho likaibuka kundi lililomuunga mkono Martin Luther.

Hao walipowasiliana na wenzao waliokuwa maeneo mengine ya nchi yao, waliandikiana barua “kwa ndugu zetu wa Moravian” na huo ukawa mwanzo wa dhehebu la Moravian. Hadi leo Wajerumani wanapoadhimisha kumbukumbu ya Martin Luther huwakumbuka pia wachoraji wawili, Wajerumani hawamkumbuki Luther kama kiongozi wa dini bali wanamkumbuka na kumuenzi kama shujaa aliyeongoza mapambano ya kupinga ukoloni wa Papa nchini Ujerumani.

Ninachotaka kieleweke katika mada hii ni ukweli ulio nyuma ya pazia kuhusiana na dhana ya uhuru, haitoshi watu kusadikishana kwamba tulipigania uhuru na baada ya uhuru kupatikana hatukutendewa haki. Kimsingi uhuru ulifanana na herufi “6” hii ikiwekwa katikati ya wawili walioketi pande mbili zinazotazamana wanaweza kubishana wasifikie mwafaka, kwasababu upande mmoja utaisoma kama “9” na upande mwingine uataisoma kama 6.

Ili kuupata uhalisia watu wanalazimika kulitazama  hilo moja kutoka pande zote, maana yangu ni kwamba sisi Waafrika tunaweza kuendelea kusadikishana kwamba tulipigania uhuru wa nchi zetu na kuaminishana kwamba tafsiri ya uhuru ni hali ya kuondoka kwa wakoloni nchini na kurudi kwao Ulaya wakiiacha  dola mikononi mwa Waafrika wenyewe.

Tafsiri hii haijitoshelezi inabidi kuzama ndani zaidi kuona kama kweli kilichotolewa ni uhuru ama ni kitu kingine kisichojulikana hata jina lake wala kuonekana kwa sura yake?
Upande wa mpokeaji herufi inasomeka tisa, kwamba alipokea vingi wakati upande uliotoa ukijua ulitoa sita na kwahiyo ulitoa vichache, wapokeaji waliona wamepokea kikubwa cha kuwatosha lakini watoaji waliijua wametoa kidogo na kisichotosha.
Ili kuujua mtizamo wa upande mwingine ni kuiona Tanganyika ndani ya Afrika na ndani ya dunia, hapo historia inabadilika inaanzia 1884 kwenye kikao cha dhuluma katika mji wa Berlin.

Mabeberu walikutanika mwezi Novemba ili wagawane Afrika kwa amani wakaweka ramani zao pamoja, walidhani kikao chao kingeisha ndani ya siku chache lakini wakajikuta wanaendelea wiki, baadaye mwezi, ilipofika Desema wakaahirisha kikao kwenda kusherehekea Krismas na Mwaka Mpya. Waliporudi wakaendelea hadi Aprili 1885, walipomaliza wakapumua na kunywa mvinyo, huku wakikiri kikao kimekuwa cha kihistoria kwasababu kilichukua muda mrefu kuliko walivyotazamia. Marekani na Urusi zilialikwa, Urusi ilihudhuria kama mtazamaji lakini Marekani iligoma ilihoji uhalali wa kikao kisichowashirikisha Waafrika.

Baada ya kumalizika kikao hatua iliyofuata Afrika ilivamiwa, Waafrika wakachinjwa kwa sababu tu utajiri wao ulitakiwa na Wazungu wa Ulaya Magharibi, watawala wa jadi waliposhindwa vita Afrika ikawa chini ya ukoloni.

Lakini dhuluma haidumu ilipofika mwaka 1914 ikiwa ni miaka 30 tangu kifanyike kikao cha Berlin, Wazungu wa Ulaya wakaanza kupigana chokochoko ilianzia Zanzibar. Wazungu walipigana hadi 1918, wao kimakosa  wanaita Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kwa sababu waliamini dunia ni Ulaya na Ulaya ndio dunia.

Ujerumani ilishindwa vita ikanyang’anywa makoloni yote Rwanda, Urundi, Tanganyika na Namibia, pia iliamuliwa katika mkataba wa Marsaille ilipe fidia.

Fidia iliwauma sana Wajerumani kwa sababu raia walitozwa kodi kubwa kugharamia vita iliyowafanya wapoteze makoloni yao, walijiona wanaoendelea kupoteza, wakawa wakisubiri aibuke mkombozi wa kuwaokoa.

Alipoibuka Adolf Hitler kila Mjerumani alimwona kama jibu walilolisubiri kwa muda mrefu, ilipofika 1939 ikiwa ni miaka 20 tangu kumalizika kwa vita ya kwanza, Wazungu wa Ulaya wakaanza tena kupigana. Hawaweki wazi kilichosababisha wapigane, lakini uhalisia ni mgawo wa 1884, Ujerumani iliona Ufaransa na Ubeligiji wamejitwalia maeneo makubwa katika Afrika kuliko wao.

Hitler alikuwa na uchungu mwingi na mali za Tanganyika waliyokuwa wameipoteza baada ya vita ya kwanza. Kufikia 1944 Hitler alikuwa amefanikiwa kuzikalia nchi zote za Ulaya isipokuwa mbili tu Uingereza na Urusi (USSR), Uingereza haikuwa na nguvu za kumzuia Hitler, ililazimika kuomba msaada kwa Marekani. Rais wa Marekani kwanza alikataa  akisema ni vita ambayo Marekani haina maslahi yoyote, lakini baadae Marekani ikaingia vitani kutokana na hila za Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill.

Kabla Marekani haijaingia vitani kummaliza Hitler, Rais wake aliweka sharti kwamba baada ya kumalizika kwa vita dola zote za Ulaya zinazomiliki makoloni zitoe uhuru kwa makoloni. Marekani ilikuwa na hesabu rahisi kwamba makampuni ya nchi hiyo yanaweza kufanya biashara ama uwekezaji kwenye nchi iliyo huru kuliko kwenye nchi iliyo chini ya ukoloni.

Kwao Marekani ilikuwa rahisi kunufaika na rasilimali za Afrika ikiwa huru kuliko Afrika iliyo chini ya ukoloni wa dola za Ulaya kwa hiyo waliingia vitani wakijua baada ya vita nchi za Afrika itakuwa huru.

Uingereza ilijua baada ya vita itayaachilia makoloni yake, mwaka 1945 iliunda wizara ya makoloni ikajiwekea ratiba ya kutoa uhuru ndani ya miaka 20 koloni la mwisho kupata uhuru 1965.

Mwaka huo1945 Uingereza ilipobadilisha asasi yake iliyoitwa “British Empire” ikaitwa “Commonwealth of Nations” yalikuwa maandalizi ya kukabidhi madaraka lakini papo hapo kuhakikisha maslahi yaliyowafanya waivamie Afrika yabakie yalivyokuwa. Hapa ndipo penye kitendawili cha uhuru na madaraka, waliotawaliwa waliona wanapigania uhuru lakini wao waliotawala waliuchukulia uhuru kama mradi mpya wa kukabidhi madaraka kwa watu wanaowaamini.

India na Pakstani ziliijua siri ya makubaliano baina ya Uingereza na Marekani zikadai na kupewa uhuru wao mapema 1947 na 1949. Waafrika wakiwa hawaijui siri hiyo, ilipofika 1950 Shirika la Ujasusi la Marekani “CIA” lilianza kuwatafuta Waafrika waliosoma popote walipo na waliokuwa vyuo mbali mbali vya Ulaya na Marekani likiwahamasisha kupigania uhuru wa nchi zao.

CIA ndiyo ilimtafuta Kwame Nkrumah na kumwelimisha dhana ya uhuru kwa Waafrika pasipokutumia nguvu za kijeshi, CIA ndio iliwakutanisha watu wazima Jonathani Kamau (Jomo Kenyatta) kutoka Kenya, Osagyefo Kwame Nkrumah kutoka Gold Coast (sasa Ghana) na Dk Hastings Kamuzu Banda kutoka Nyasaland, wakati huo akiwa tayari amehitimu masomo akifanya kazi ya kuutibu ukoo wa kifalme nchini Uingereza.
Ikatokea Nkrumah akawa mhamasishaji mzuri wa wanafunzi waliokuwa vyuo vya Ulaya na Marekani, CIA ndiyo iliyotoa fedha za kugharamia mkutano wa kwanza wa PAFMECA yaani “Pan African Movement for Freedom in East and Central Africa” uliofanyika mwaka 1950 mjini Manchester nchini Uingereza. Haya yanapatikana kwenye hati iliyopewa anuani hii “Nkrumah’s policy of USA against Europe.”
Katika siku zake za awali Nkrumah aliamini kwamba Marekani ilikuwa kinyume na Ulaya, hakujua kuwa Marekani ni dola inayoweka mbele maslahi yake, haina rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu bali ina maslahi ya kudumu.

Ghana ilipopata uhuru mwaka 1957 Nkrumah aliiga mengi kutoka Marekani ukiwamo mfumo wa Rais mtendaji, Nkrumah alidhani Afrika ingeweza kuwa na mfumo wake usiofanana na “ukomunisti” wa USSR wala ubepari wa Marekani, hapa ndipo uhusiano wa Nkrumah na CIA ulipoingia dosari.

 Marekani haikuuelewa Ujamaa wa kiafrika ikamwona Nkrumah mkomunisti, CIA ikatoa andishi lake “save Africa from communism” wakaazimia kwamba kiongozi yeyote “radical” aidha auawe, ama apinduliwe, au apelekewe vita kwa kuanzishiwa uasi nchini mwake ama yote matatu.

CIA ikaorodhesha kuanzia “radical” wa kwanza hadi wa mwisho, Patrice Emery Lumumba wa Congo Kinshasa akaonekana wa kwanza akifuatiwa na Amilcar Cabral wa visiwa vya Cape Verde wa tatu akiwa Nkrumah na wa nne Banda.


Baadhi ya marais waliipata mapema taarifa ya CIA kuwaondoa madarakani, wakaamua kuachana na ukali wao na kuendeleza mifumo waliyoikuta.
Itaendelea toleo lijalo

No comments: