Kuna makala uliandika na ukaiweka hapa JF lakini kwa haraka sana
ikaondolewa lakini nilikuwa nishatoa jibu.
Anaependa kufuatilia mjadala huo nilioutaja hapo juu na aingie hapa:
Dkt Muhammed Seif Khatib na Mohamed Said wazungumzia siasa za Zanzibar
Safari hii umerudi na mengine kuhusu ''makosa'' ya Maalim Seif Sharif
Hamad.
Umesema mengi na naamini kwa hadhi ya Maalim Seif Sharif itakuwa
vigumu kwake kukujibu kwa sababu zilizo wazi kabisa.
Kwa ajili hii basi hatutoweza hapa kupata ukweli wa nini kilipitika kati ya
Maalim Seif na Mzee Abdul Wakil ingawa yoyote ajuaye siasa za Zanzibar
hatopata tabu kuhisi nini lilikuwa tatizo.
Dkt. si kweli kuwa mpasuko kati ya Pemba na Zanzibar chanzo chake ni Maalim
Seif kama ulivyosema.
Sote tunaijua historia ya Zanzibar na Dkt. ukipenda ingia hapa uone sababu ya
mpasuko huo:
Mohamed Said: PEMBA: THE FIRE NEXT TIME
Kwa kuwa wewe ni mtu wa fasihi naamini umemsoma James Baldwin: The Fire
Next Time kwa hiyo utaelewa kilio cha jamii inayodhulumiwa.
Sote tunaijua historia ya Zanzibar.
Kuna mengi umesema lakini sioni sababu ya kujibu yote khasa kwa kuwa baada
ya uchaguzi wa marejeo ukweli sasa uko wazi.
Wazanzibar walikataa kupiga kura na kama ulivyogusia walimsikiliza kiongozi wao
na wakabaki majumbani mwao kwa amani na salama.
Itoshe tu kwa msomaji anetaka kujua nguvu ya Maalim Seif kuingia hapa na
kujisomea mwenyewe kujionea kuwa CCM Zanzibar haiwezi kupambana na
Maalim Seif katika uchaguzi wowote Zanzibar kwani atawashinda hata iweje:
Mohamed Said: TAKWIMU ZA USHINDI WA DK. SHEIN NI ''FAIRY TALE'' HADITHI ZA KUWALAZA WATOTO USINGIZI - MOHAMED GHASSANY
Mohamed Said: UCHAGUZI WA MARUDIO ZANZIBAR - ALICE IN WONDERLAND
Mwisho ningependa kusema kuwa Maalim Seif ni kiongozi hodari ambae juu ya
vigingi vyote alivyowekewa ameweza kuijenga CUF kuwa chama makini chenye
nidhamu ya juu na kuweza kuwapata vijana ambao ndiyo wapiga kura walio wengi
kukipenda chama na kuleta ndani ya chama elimu zao na ujuzi wao ambao umekuwa
msaada mkubwa kwa CUF na Zanzibar.
Kuwa Maalim Seif alijitangaza mshindi wala si hoja ya maana.
Ukweli ushajulikana.
Sina haja ya kusema kuwa Maalim Seif ameshinda kila chaguzi iliyofanyika Zanzibar toka
1995 na hii si siri.
Haikutushangaza wengi kuwa katika uchaguzi wa 2015 Maalim Seif alimshinda Dkt. Shein.
Dkt. analifahamu hili kama mimi na wengi tunavyolifahamu.
Sina sababu ya kueleza barua ya Ali Ameir ya 1995 iliyokataa ushindi wa Maalim Seif wala sina haja ya kukumbusha uchaguzi wa 2010 na juhudi za Mzee Hassan
Nassor Moyo.
Dkt. nina hakika unafahamu kuwa kama si busara ya Maalim Seif usiku ule Bwawani
wazazi Zanzibar wangezika vijana wao wengi.
Zanzibar ingepata si yale ya Pemba 2001 bali bali ingepata Amritsar (1919) na Sharpville yake (1960).
Naamini Dkt. uliona vipi siku ile jinsi hali ya Bwawani, Amritsar na Sharpville ilivyoshabihiana.
Nataka nikufahamishe kitu.
Siku mbili baada ya Bwawani na Dr. Shein kuapishwa rais wa Zanzibar nilikuwa mgeni
wa mmoja wa viongozi wakubwa Zanzibar.
Alinambia maneno haya, ''Sisi tunamshukuru Maalim Seif kama si yeye wewe leo
usingekuja Zanzibar ingawa serikali ingekuwa mikononi mwetu.''
Atakae hukumiwa na historia hakika si Maalim Seif...
Wenyewe wanajijua na tayari wameshasimamishwa kizimbani na dunia.
Dkt. asipoteze muda wake kwa kukimbilia chombo kinachozama.
Nyakati zimebadilika sana na hawatoweza kuwategemea Ton Ton Macoute kwa
muda mrefu.
Wakati umefika kwake na kwa wahafidhina wenzake wakajiuliza nini kinasababisha
wao kukataliwa na Wazanzibari katika kila uchaguzi kitu kinachowafanya kuchukua
serikali kwa kutumia mtutu wa bunduki?
No comments:
Post a Comment