Wednesday, 22 June 2016

KALAMU YA MOHAMMED K GHASSANI INAPOANDIKA



Siwachi Kusema ni diwani yangu ya pili kuchapishwa baada ya Andamo (Buluu Publishing, 2016) ikiwa na tungo 70 zenye bahari na mitindo mbalimbali. Ambapo Andamo ni hadithi za maisha yangu ya mwanzoni mwa ujana baina ya 1993 na 2001, Siwachi Kusema ni muedelezo wa hadithi hizo baada ya mwaka 2001. Ni namna yangu ya kusema na kuyasemea yale yanayotokea mbele ya macho yangu – iwe kwenye uwanja wa siasa, jamii au hata katika kiwango cha binafsi – na yakaniathiri au kuacha alama kwa mazingira yaliyonizunguka. Ninasema na sitaki kuwacha kusema kwa kuwa kusema ni haki yangu na kwa kuwa ni tabia muhimu kwenye jumla ya mambo yanayouumba utu na ubinaadamu wangu. Ninasema kwa kuwa kuna mambo yanahitaji kusemwa, ili nipumuwe na nijipapatuwe dhidi ya kabari ya roho. Ninasema kwa furaha na kwa matumaini pale mambo yanapoonekana kwenda njia sahihi, lakini pia ninasema kwa hasira na kuvunjika moyo pale yanayopindishwa na kuchukuwa njia ya machakani; na kamwe sitaki kuacha kusema. Nimeuchagua ushairi kuwa moja ya njia ambazo naweza kuyasema na kuyawasilisha hao na mengine kama hayo na bado nikabakia na nafasi na wakati na nishati ya kuyasema mengine. Na bado nikabakia mimi mwenyewe.

No comments: