Friday, 8 July 2016

FAROUK ABDULLA (1945 - 2016)

Photo
Farouk Abdulla
(1945 - 2016)

Nimejuana na Farouk mwaka wa 1999 nilipokwenda Muscat kwa mwaliko wa marehemu mzee wetu Sheikh Ali Muhsin Barwani. Ikasadif na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unikute huko. Farouk tulipendana tulipotiana machoni na hatukuachana kuanzia mwaka ule hadi alipofariki jana. Nimekuja Muscat nikitokea Tanga sina nimjuae kwa sura ila kwa kusikia majina tu…Farouk, Dr. Harith Ghassany, Mutta, Walid, na wengineo. Baadhi kama Mutta nilikuwa tayari nishawafahamu baada ya kupita Dubai kabla sijakwenda Muscat. Niliyekuwa namfahamu kwa kumuona kwenye picha kisha kumsoma alikuwa Sheikh Ali Muhsin na ndiyo kwanza kitabu chake mashuhuri, ‘’Conflict and Harmony in Zanzibar,’’ kilichochcpwa mwaka 1999 kilikuwa kimefika Tanzania kwa njia za panya. Mimi nilipata photocopy ya kitabu kutoka kwa marehemu Ahmed Rashad Ali. Kitabu hiki kilikuwa kikipatikana kwa watu wachache sana. Akikuomba mtu unamwambia bora tupige photocopy na hii kwa hofu huenda kitabu kisirudi tena. Nyakati zile zilikuwa ngumu.

Leo kwa juhudi za ndugu zetu wenye kutafuta kheri kwa huu umma tunasoma kila toleo la kitabu kutoka Oman au Dubai kwa kununua katika maduka ya vitabu na vingine vikiletwa kama sadaka. Nakala hii ya photocopy ya kumbukumbu za Sheikh Ali Muhsin ninayo hadi leo na ingawa nina kitabu chenyewe hivi sasa nakala hii ya photocopy ni hazina kubwa kwangu ambayo kama ilivyo kawaida kwa vitu vya vinavyogusa hisia, thamani yake haikadiriki hivyo kiko katika shubaka kwa ajili ya maonyesho. Na kila ninapokiangalia kitabu hiki nilikuwa namkumbuka Faruouk, Sheikh Ali Muhsin Barwani na Ahmed Rashad Ali. Sasa katika kumbukumbu zangu ameongezeka rafiki yangu Farouk Abdulla Barwani (ambae kabla hakuwako)na sababu kubwa ni kuwa ni yeye Farouk ndiye aliyefanya tafasiri ya kitabu kwa Kiswahili, ‘’Kujengwa na Kubomolewa Zanzibar,’’  ili kisomwe na wengi na kwa hakika nilipopokea nakala ya Kiswahili kitabu hakikukaa madukani kilinunuliwa kwa kasi ya ajabu na hadi leo kitabu hiki nakala ya Kiswahili inaulizwa na watu wengi wasomaji na wauza vitabu.

 

Nimeuleta utangulizi huo hapo juu kwa mukhtasari ili msomaji asiyemjua Farouk ajuwe na picha ya Farouk alikuwa mtu wa namna gani na aliishi katika kipindi kipi na watu wa wa namna gani imjie. Nilijuana na Farouk katika kipindi cha wasiwasi. Kipindi cha kuanzia mwanzoni 1990 kilikuwa kipindi cha aina yake katika historia ya Tanzania na hasa Zanzibar. Kilikuwa kipindi ambacho Zanzibar ilikuwa kama vile inaamka kutoka katika usingizi mzito wa Rip Van Winkle. Baadhi ya Wazanzibari walikuwa wakitazama mbele na kuona kitundu kidogo cha nuru katika mabadiliko ya siasa yalikyokuwa yamebisha hodi visiwani na Afrika nzima kwa ujumla. Siasa ya vyama vingi ilikuwa imeingia. Uchaguzi wa vyama vingi vya siasa Zanzibar ulikuwa tayari umeshaashiria mabadiliko makubwa yatakayoleta utangamano, maendeleo na kung’arisha visiwa na watu wake. Hili halikuwa. Kwa watu waliokuwa na mapenzi na nchi yao kama Farouk hali ya Zanzibar ilimpa changamoto kubwa kwani hata kwa kutembea katikati ya mpaka nako kulikuwa na hatari zake.


Farouk naweza kusema kwa kile kipindi kifupi nilipokuwa mgeni wa Sheikh Ali Muhsin haikuniwia tabu kutambua kuwa alikuwa ndiyo mkono wa kulia wa Sheikh Ali. Haikuwa vilevile tabu kwangu kutambua kuwa Farouk licha ya kuwa mkono wa kulia wa sheikh pia alikuwa ndiyo sikio la sheikh. 

Jina la Farouk lilikuwa halipungui kwenye kinywa cha Sheikh Ali. Kwa ule muda niliokuwa Muscat Farouk alikuwa kivuli changu na mie nikawa kivuli cha Farouk. Akinipeleka kila mahali na nikiwanae muda wote tunaachana usiku wakati wa kwenda kulala. Nakumbuka nilikuwa nalala nyumbani kwa marehemu Sheikh Salum na nyumba ilikuwa tupu wenyewe walikuwa wamekwenda umra. Nilikuwa naishi kwenye jumba lile mimi na mtumishi aliyekuwa masikini akihakikisha kuwa daku yangu naila ya moto kwa wakati niutakao mwenyewe. Kama nilivyoeleza mwanzo mara baada ya kuwasili Muscat mwezi ukaandama na mfungo ukanikutia huko. Farouk akichukua adha ya kuacha kufuturu kwake akija nyumbani kwa Walid Badr alipokuwa Sheikh Ali Muhsin ili afuturu na mie. Pale nyumbani ndipo nilipojuana na Sheikh Said Badr na Sheikh Issa bin Nasser Al-Ismaily aliyeandika kitabu, ‘’Zanzibar Kinyang’anyiro na Utumwa.’’ Hiki ni kitabu cha aina yake katika kuijua historia ya Zanzibar. Kiliingia Dar es Salaam wakati wa uchaguzi wa mwaka wa 2000. Mamlaka ilikizuia bandarini na hakikuachiwa mpaka baada ya uchaguzi kupita. Nazikumbuka email za Farouk kuniuliza lini kitabu kitatoka wakati mwingine akiwa na hofu huenda kikapotea kabisa.


Nikiwa peke yangu na Farouk Muscat ndipo alipokuwa akinisomesha yote kuhusu watu niliokutananao. Hii ilikuwa darsa tosha. Kila niliyekutananae alikuwa na historia ya pekee ya kuhadithiwa kuhusu nini kilitokea Zanzibar wakati wa mapinduzi. Kwangu mimi hii ilikuwa shule mpya ambayo ninsingeweza kuisoma popote duniani. Hii ilikuwa historia iliyokuwa inasubiriwa kuandikwa na kila alyekuwa na cha kusema.

Lakini mazungumzo yetu mengi yalikuwa yale ambayo Sheikh Ali Muhsin akitusisitiza kwayo – kutia juhudi ya kusomesha dini. Wakati ule Sheikh Ali Muhsin alikuwa ndiyo anafanya tafasiri ya Qur'an na alinieleza na kuniahidi kuniletea nigawe nchi nzima. Sheikh Abdulla Muhsin yeye alikuwa anafanya tafasiri ya Sahih Bukhari. Sheikh Ali akisema,’’Dini ikikaa vyema kwenye nyoyo za watu na siasa itakaa vizuri pia.’’ Kama vile lile darsa la Sheikh Ali Muhsin lilikuwa halitoshi kwetu sote, Farouk alikuwa akiniuliza na kutaka kujua mengi kuhusu Waislam hasa wa Bara vipi tutaweza kuvisaidia vyuo na walimu wake. Hayakuwa maneno matupu. Ikawa baada ya kurejea Tanga sasa nikawa naanza kupokea vitabu kuanzia mashafu tafsiri ya Sheikh Ali Muhsin, ‘’Al Muntakhab’’ vitabu vya fiqhi, ‘’Fiqhi Iliyowepesishwa,’’ iliyotarjimiwa na yeye mwenyewe Farouk Abdulla, hadith ‘’Tarjuma ya Sahih Al-Bukhari’’ hii imetarjumiwa na Sheikh Abdulla Muhsin Al-Barwani. Pamoja na vitabu hivi Farouk alinitumia vitu vingi kwa ajili ya umma tukilenga vijiji vya pembezoni. Wakati huu Farouk akiniandika kwa anuani aliyoiita ‘’Umoja Baraka.’’ Pamoja na haya Farouk siku zote akinisisitizia kufanya kila niwezalo kalamu yangu iwe kalamu ya kuuleta umma katika umoja. Iwe katika email alizokuwa ananiandiki au katika mazungumzo ya simu, Farouk akinitia moyo na kunihimiza sana kusamabaza ilm ya dini katika umma na nihakikishe kuwa vitabu ninavyopokea vinawafikia Waislam bure bila ya kutozwa chochote.


Shehena ya vitabu vya dini Bandari ya Dar es Salaam

Kubwa kwangu ni kuwa Farouk ndiye mtu aliyenijulisha kwa Dr. Harith Ghassany. Naikumbuka siku hii kama jana. Naikumbuka kwa sababu moja kubwa nayo ni kuwa kwa Farouk kunijulisha kwa Dr. Ghassany kulifungua mlango mwingine khasa katika kujuana na kufanya yale ambayo wazee wetu na sisi sote tukiyaendea mbio, nayo ilikuwa kuleta utangamano katika jamii. Farouk akipenda kusema kuwa Zanzibar kuna historia ya kutosha kwa Wazanzibari kujifunza kutorudia makosa ya nyuma. Hii pia ilikuwa ndiyo lugha ya Dr. Ghassany na ndipo aliponifahamisha kuwa ana mpango wa kutafiti upya historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. 


Yaliyofuatia sasa ni historia kwani utafiti ulifanyika na kitabu kimeandikwa, ‘’Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.’’ Ilikuwa katika kukutanishwa huku na Dr. Ghassany na Farouk ndipo nilipomdokeza Dr. Ghassany kuhusu tetesi na uvumi wa nafasi ya Tanga, mji niliokuwa nikiishi na kufanya kazi, katika mapinduzi ya Zanzibar. Nilidokezwa kuwa kulikuwa na kambi ya mamluki kijiji kimoja nje ya Tanga kilichotumika kuwapa mafunzo mamluki kuvamia Zanzibar wakati wa mapinduzi. Jina la kijiji hiki ni Kipumbwi.

Nilimfahamisha Dr. Ghassany uvumi niliokuwa nimedokezwa kuhusu kambi hii na nikamshauri aje Tanga kufanya utafiti kupata ukweli. Dr. Ghassany alifika Tanga na alifanya utafiti mkubwa Tanga mjini na Sakura na Kipumbwi kwenye mashamba ya mkonge ambayo ndiko walikotoka askari mamluki walioingia Zanzibar kusaidia mapinduzi. Kwa miaka saba Ghassany alikuwa akija na kurudi Tanga kiasi akaja hata kujulikana na wenyeji kuwa ni mgeni wangu.  Farouk pia alinitembelea Tanga baada ya Dr. Ghassany keshaanza utafiti wake. Tulizunguka pamoja katika misikiti mingi ya mjini na mara zote akinambia kuwa hali iliyoko Bara kwa Waislam haijatofautiana sana na hali ya visiwani.

Kushoto:Farouk Abdulla, Mwandishi, Sheikh Ali Muhsin na Sheikh Abdalla Muhsin
Muscat 1999
Mwaka jana mwezi December 2016 nilikuja Muscat na safari hii haikuwa Farouk aliyenipeleka nyumbani kwa Dr. Ghassany. Dr. Ghassany alikuja mwenyewe uwanja wa ndege kunipokea. Safari hii ni Farouk ndiye aliyenichukua mimi na Dr. Ghassany katika gari yake tukenda kwake. Allah alikuwa kanipa ndugu. Nilikuwa nimerudi Oman baada ya miaka 15. Ukimtoa Dr. Ghassany mimi na Farouk tulikuwa sote tumeota mvi katika vichwa vyetu na Farouk akaniletea mjukuu wake mchanga mtoto wa mwanae Hamid nimshike. Nilipokuja Muscat mwaka wa 1999 Hamid alikuwa mtoto mdogo akija na baba yake nilipofikia kunichukua kwenda kusali sala ya Alfajir. Sasa Hamid alikuwa ni baba. Bahati mbaya sikubahatika kukutana na Hamid kwani alikuwa kazini. Wakati tunakuja kwake Farouk alisimamisha gari tukatoka nje akanionyesha nyumba ya marehemu Sheikh Salum niliyoishi nilipokuja mwaka wa 1999. Farouk alipiga fatha na tukaomba dua.

Huyu ndiye Farouk siku zote Allah alikuwa mbele ya kila kitu chake.
Allah amghufirie madhambi yake na amweke mahali pema peponi.

Amin.


Mwandishi na Farouk Abdulla nyumbani kwake Muscat December 2015

No comments: