Tuesday, 26 July 2016

RAJAB ATHMANI MATIMBWA MUAISISI WA KWAYA YA TANU 1954

Rajab Athmani Matimbwa

Rajab Matimbwa katoka Chole, Uzaramo kaja Dar es Salaam kijana mdogo kutafuta maisha. 

Rajab Bi. Titi ni shangazi yake na akikaa nyumbani kwake Shauri Moyo. 

Harakati za kudai uhuru zilipoanza Dar es es Salaam Rajab akajikuta ana kibarua cha kuuza maji kwenye bomba moja lililokuwa linatazamana na ofisi ya TANU New Street (sasa Lumumba Avenue). 

Kabla ya kufanya kazi ya kuuza maji tayari Rajab alishapewa kibarua na John Rupia cha kuuza mgahawa pembeni ya Pugu Road na ikatokea akaelewana vizuri sana na Mzee Rupia na familia yake yote akawa mtoto wa nyumbani. 

Rajab anawakumbuka watoto wa Mzee Rupia, Paul na dada yake Kipanya, Mpuya (Stephen) na kaka yao mkubwa Albano. 

Mzee Rupia alikuwa na lori lake limeandikwa, ''Msichoke'' likibeba mijengo. 

Mikutano ya hadhara ya TANU ilipoanza Rajab aliwakusanya vijana wenzake wanne wakaanzisha kwaya ya kwanza ya TANU Rajab akiwa kiongozi na mtunzi mkuu wa nyimbo za kuhamasisha watu kujiunga na TANU na nyimbo za kuwasema Waingereza. 

Wanakwaya wenzake walikuwa Said, Abdallah, Juma, Binoga na Katumbwele. 

Said akatunga nyimbo ya kwanza iliyokuwa ikisema, '' Watanganyika njooni tuchanganyike tukisifie chama chetu cha TANU Mola akipenda tupate uhuru.'' 

Rajab akatunga, ''Sikia wana kuteseka nchi ni shida tupu yatukalia sisi Watanganyika tunateseka kutawaliwa ni fedheha.'' 

Hizi nyimbo zilipokuwa zikiimbwa pale Mnazi Mmoja kabla Nyerere hajapanda jukwaani zilikuwa zikiwajaza hamasa wananchi. 


No comments: