Utangulizi
Japhet
Kirilo na Earle Seaton wameandika kitabu, ‘’The Meru Land Case,’’ kuhusu
mgogoro wa ardhi ya Wameru ambayo ardhi yao ilichukuliwa na Wazungu bila fidia.
Mimi nimekieleza kisa hiki kufuatana na jinsi Abdulwahid Sykes akiwa kiongozi
wa TAA alivyokishughulikia akishirikiana na Earle Seaton na Japhet Kirilo kwa
nia ya kuongeza ufahamu wa mkasa huu. Naweka hapo chini kipande kidogo kutoka
kitabu cha maisha ya Abdul Sykes:
Wakwanza aliyekaa kushoto ni Japhet Kirilo na Wanne waliosimama ni Abdul Sykes
Picha ya Waasisi wa TANU
1952
Baada
ya Dr Kyaruzi kuhamishiwa Nzega nafasi ya rais ikawa wazi. Abdulwahid akakaimu
nafasi hiyo sasa akiwa katibu na kaimu rais wa TAA. Mgogoro wa ardhi ya Wameru
ulikuwa umekwishaanza lakini bado haujalipuka kuwa suala lililowahusu
Watanganyika wote. Umoja wa Mataifa ulipotuma ujumbe wake wa pili kuzuru
Tanganyika mwaka wa 1950, Wameru waliwasilisha rasmi malalamiko yao kwa ujumbe
huo. Abdulwahid aliwaomba wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria washirikiane na
TAA katika kutatua baadhi ya matatizo yanayokabili jamii ya Waafrika.
Abdulwahid alifadhaishwa na wajumbe Waafrika katika Baraza la Kutunga Sheria
pale waliposhindwa kuipinga Wilson Report ambayo ilipendekeza kuondolewa kwa
wananchi wa Meru kutoka kwenye ardhi yao. Katika barua aliyoiandikia Meru
Citizenís Union, Abdulwahid, kwa niaba ya makao makuu ya TAA, aliwahakikishia
watu wa Meru kuwa tatizo lao llilikuwa tatizo la Watanganyika wote.
Abdulwahid
aliamua kutumia mgogoro wa ardhi ya Wameru kuwaunganisha Watanganyika wote
dhidi ya serikali ya kikoloni. Uamuzi wa serikali juu ya mapendekezo ya TAA kwa
Constitutional Development Committee ulikuwa bado umo akilini mwake. Alitambua
kwamba uamuzi wa Gavana ulikuwa ni mpango wa muda mrefu wa kuwadhalilisha
Waafrika katika utumwa wa daima. Abdulwahid sasa akiwa na ghera kubwa alianza
kufanya kazi ya kuwahamasisha watu wa Tanganyika chini ya vuguvugu la
kuunganisha umma dhidi ya utawala wa Waingereza. Abdulwahid aliwasiliana na
Earle Seaton mjini Moshi kutaka ushauri wa kisheria juu ya tatizo la Meru.
Seaton alikuja Dar es Salaam na kukutana na Abdulwahid na uongozi wa TAA.
Ilikubaliwa na pande zote mbili kuwa makao makuu ya TAA, Meru Citizenís Union
ikiongozwa na Japhet Kirilo na Seaton lazima waunganishe shughuli zao katika
kesi hiyo na kwa pamoja watume rufaa yao kwenye Baraza la Udhamini la Umoja wa
Mataifa huko New York. Kwa sasa uongozi wa chama cha TAA ulitambua kwamba
nusura yao ilitegemea uwezo wao wa kudhibiti na kushawishi matukio na maamuzi
ndani ya Baraza la Kutunga Sheria. Ili
kuweza kufanya hayo shinikizo lilitakiwa kuwekwa katika Baraza la Udhamini huko
New York, nchini Amerika na siyo katika Ofisi ya Makoloni pale London Uingereza.
Tawi
la chama cha TAA la Tabora lilichukua changamoto hiyo kwa kupitia juhudi za Kandoro
aliyeuona mgogoro wa ardhi ya Wameru kama jukumu lake binafsi. Kandoro
aliitisha mkutano wa matawi ya TAA ya Mwanza, Kigoma na Tabora kujadili suala
hilo. Mwanza iliwakilishwa na Bhoke Munanka, Mzee Mkama Mlaji na Mohamed Kihaka
Kitenge; kutoka Kigoma mjumbe aliyekuja alikuwa Jumanne Mawimbi na Tabora
iliwakilishwa na Sheikh Kinana, Kandoro na George Magembe kama rais wa TAA tawi
la Tabora. Mkutano wa Tabora uliahidi
mshikamano wa pamoja na watu wa Meru katika mapambano dhidi ya walowezi.
Mgogoro
wa ardhi ya Meru ni wa pekee katika historia ya Tanganyika. Ilikuwa kupitia
katika mgogoro huo ndiyo Mtanganyika, Japhet Kirilo, akifuatana na Earle Seaton
kama mkalimani na mshauri wa sheria, kwa mara ya kwanza alizungumza mbele ya
Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa huko New York, na kuonyesha udhalimu wa
ukoloni. Mnamo November, 1952 Kirilo alizungumza mbele ya Kamati ya Nne ya
Baraza Kuu. Watu wa Tanganyika sasa walikuwa wanayachukua mapambano yao toka
mipaka yao hadi kwenye kumbi za Umoja wa Mataifa, mjini New York kutafuta haki.
Lakini Kirilo alirudi mikono mitupu. Rufaa ya mgogoro wa ardhi ya Wameru
ilitupiliwa mbali. Kirilo aliuhakikishia Umoja wa Mataifa kuwa watu wake kamwe
hawatachukua silaha kuikomboa ardhi yao kama Wakikuyu wa Kenya walivyojaribu
kufanya. Kwa kweli hapakuwa na sababu ya kutoa kauli hii, kwa kuwa uhakikisho
wa kutokuwepo mapambano uliwafanya walowezi washushe pumzi na kujiona wako
salama. Tangu mwanzo wa mgogoro wazalendo nchini Kenya kama Fred Kubai na
Kung'u Karumba walikuwa wakitoa ushauri kwa Meru Citizenís Union kwa kuwa wao
walikuwa na ujuzi zaidi wa matatizo ya walowezi kuliko watu wa Tanganyika.
Kwa
mtazamo wa juu juu mtu anaweza kudhani kuwa Abdulwahid alikuwa akipata kipigo
kutoka sehemu zote alizojaribu kuipenyeza TAA kutoka mwaka wa 1948 katika enzi
za chama cha makuli, kufikia marekebisho ya katiba hadi kumalizikia kwa mgogoro
wa ardhi ya Wameru. Kushindwa huku si kwa sababu TAA ilikuwa ina viongozi
dhaifu au ilikuwa haiuingwi mkono na umma. TAA ilikuwa haifanikiwa katika madai
yake kwa sababu serikali ya kikoloni ilikuwa imeamua kutosikiliza lolote kuhusu
matatizo ya Waafrika. Matokeo ya hali hii ilimfanya Abdulwahid aamue kuwa njia
iliyobakia ya Tanganyika kujitoa katika makucha ya Waingereza ni kuuandaa umma
wa Tanganyika chini ya chama cha siasa. Mara tu baada ya Kirilo kurejea kutoka
New York, mpango wa kuanzisha chama cha siasa cha kushirikisha umma wote
ulianza.
Uongozi
wa TAA Makao Makuu ulianza kampeni ya nchi nzima kuueleza umma matokeo ya
safari ya Kirilo kwenye Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa ardhi ya Wameru na
vilevile kuchangisha fedha za kupeleka msafara mwingine katika Umoja wa Mataifa
kuueleza umoja huo kuwa Tanganyika ilikuwa chini ya udhamini na Watanganyika
walikuwa sasa na haki ya kudai uhuru wao. Kamati ya TAA ya watu watatu
iliyowajumuisha Kandoro, Kirilo na Abbas Sykes iliundwa kwa ajili hiyo. Ally
Sykes akiwa mweka hazina msaidizi wa TAA aliombwa ampelekee Kirilo hawala ya
posta Usa River kama nauli ya kumwezesha kusafiri hadi Dodoma kujiunga na ile
kamati ya watu watatu. Kulikuwa hakuna huduma ya fedha katika posta ya Usa
River na fedha zile zilikaa hapo kwa muda bila ya kuchukuliwa hadi hapo
zilipopelekwa posta ya Arusha mjini ambako Kirilo alizichukua.Kuanzia tarehe 26
Septemba, 1953 kwa takriban mwezi mmoja ile kamati ilitembelea na kuhutubia
mikutano ya hadhara, ikikusanya fedha Dodoma, Mwanza, Bukoba, Ukerewe, Tarime,
Musoma na Shinyanga. Rais wa chama cha TAA, kanda ya ziwa, Paul Bomani
aliipokea ile kamati ya watu watatu na kuhutubia mikutano pamoja nao katika
jimbo lote. Bomani aliwaambia wanachama wa TAA na wananchi wote mjini Mwanza
kuhusu umuhimu wa kuchanga fedha kwa kwa kusudio hilo.
|
Katika miaka ya 1950 Cosy Cafe ilikuwa hotel ikipendwa sana na viongozi wa TAA |
Kushoto Abdul Sykes na Mwandishi Nyumbani kwa Japhet Kirilo Usa River, Arusha 1989 |
No comments:
Post a Comment