Thursday, 11 August 2016

KUTOKA JF: SAIGON FC SIKUKUU STREET DAR ES SALAAM 1960s NA CLUB NYINGINE




Kitulo,
Zamani Dar es Salaam mitaani kulikuwa na vilabu vingi sana vya mpira.
Hizi club zilikuwa za watoto wadogo shule ya msingi hadi sekondari kiasi.

Huwezi amini takriban zote zilikuwa na viwanja vya mazoezi Jangwani.
Vilabu hivi vikifanya mashindano ambayo yakisisimua mji.

Kulikuwa na African Temeke na Good Hope Temeke hawa ni kama Yanga
na Sunderland.

Wakicheza Temeke yote inasimama na vijana hawa walikuwa wakipata
makamo wanakwenda Sunderland au Yanga.

Buguruni kulikuwa na Roverfire club ya wahuni.
Hii ndiyo sifa yao.

Karikaoo kulikuwa na Brazil kilabu nyingine ya wahuni.
Hii ndiyo sifa yao.

Club hizi hazimalizi mechi kwa salama kwani walikuwa washari sana.
Lakini walikuwa na soka la kuvutia ila tatizo ni hilo, wagomvi.

Kulikuwa na club za waungwana vijana wastaarabu kama Young Boys,
LIverpool, Young Kenya, Doncaster Rovers, New Port, Fulham nk.

Hii Fulham ilikuwa club ya mtaani kwangu Kipata.

Mimi sikuweza kucheza club hii kwa sababu ya umri wangu wakinioa ati
kiduchu.

Nakumbuka siku moja ilikuwa 1965 katika uwanja wa Shule ya Nanak
hii ilikuwa shule ya Singa Singa nimekwenda ili nami nifanye mazoezi
Adam Kingui akanifukuza nakumbuka maneno yake vizuri hadi sasa,
''Huyu ataweza wapi kucheza...''

Kimo changu kilimtia wasiwasi.

Naweka hapa chini picha yake na jamaa wengine ambao wote walikuwa
wachezaji wazuri:

[​IMG]
Kulia Adam Kingui, Abdallah Mgambo (Cosmo, Taifa Cup, East African Community Team), Kleist Sykes yeye alisoma Carlton University, Canada kwa scholarship ya mpira)

Katika hizi kulikuwa na club moja ya kipekee kabisa - Cuba Rovers.

Cuba Rovers wao walikuwa ''Wazungu,'' ndani ya mechi wanazugumza
Kiingereza, ''On him.'' ''Pass the ball,'' ''Cool down.'' etc. etc.

Jezi zao zilikuwa punda milia.

Si haya tu wakipenda muziki wa The BeatlesHelen Shapiro, Cliff
Richard 
na Sal Davis.

[​IMG]
Sal Davis akifanya onyesho Ujerumani 1960s

[​IMG]
Mwandishi na Sal Davis Chef Pride Lumumba Street, Dar es Salaam 2006

Club yao ilikuwa Mtaa wa Mkunguni.

Hawa baadhi yao walikuwa watoto wa ''upper class,'' ya Dar es Salaam
ya wakati ule.

Nimeleta mkadama huu mrefu ili kumpa msomaji picha ya Dar es Salaam
ambayo mimi nimekulia.

Saigon ilikuja baada ya kutokea mgawinyiko kweye club ya Everton. 
Haikupita muda Everton ikafa.

Sasa Saigon ipo na baadhi ya wanachama waasisi wa club ile miaka ya
1960 wakiwa watoto wa umri wa shule ya msingi bado wapo na sasa
imekuwa barza maarufu ya mazugumzo.

[​IMG]
Saigon Club Mtaa wa Sikukuu 1970s kushoto ni marehemu Ahmed AbdallahMwandishi na Boi Risasi.

No comments: