Yanga mie ''nawapenda,'' kwa namna yangu ya ajabu kabisa.
Rafiki zangu wengi hadi wachezaji walikuwa ''Kuala Lumpa,'' kama
Elias Michael, Sunday Manara, Juma Matokeo, Leonard
Chitete lakini tukielewana vizuri sana.
Hili jina Yanga watani zetu tuliwapa kwa sababu Kuala Lumpa kulitokea
machafuko na kila radio katika taarifa ya habari inaanza na habari za
huko.
Sasa tukapatapo silaha ya kuwapigia watani wetu tukawapa jina hilo
Kuala Lumpa.
Elias na mimi sote tulikuwa wapenda kusoma vitabu kwa hiyo
tukiazimana vitabu.
Ahsante kwa picha:
Kuna wengi nawatambua na wengine ni walikuwa wazungumzaji
wangu kama Said Walala, Adam Athmani, Hamisi Kisiwa,
Mbaraka Salum Rwando, Hamisi Kilomoni, Arthur Mambeta,
Hamisi Fikirini, Hamisi Kibunzi na Emmanuel Mbele.
Wengine hapo ni Haji Lesso Simba wakimuita ''Kiuno,'' Lased,
Mustafa Choteka...
Enzi hizo tukiwapa Yanga bao nne kila wakitia pua Ilala Stadium
sasa sisi tukawaongezea watani wetu jina lingine, ''four, four,'' sawa
na Peugeot 404.
Katika picha yuko na mshabiki mkubwa sana wa Sunderland -
Jumanne Kisukari.
Kisukari siku za mwisho za uhai wake alikuwa muadhin wa msikiti
wa jirani na nyumbani kwake Magomeni.
Udongo unameza watu.
Kisukari alikuwa akichangamsha na kuweka morali ya wachezaji
juu maana yeye anatangulia mbele na bendera ya Simba kuingia
uwanjani kuanzia enzi ya Ilala Stadium hadi Uwanja wa Taifa.
Bendera yetu ilikuwa na maneno haya, ''Daima Mbele Nyuma Mwiko,''
maana yake sisi tutapambana haturidishi majeshi yetu nyuma.
Hili Yanga wakilijua sana.
Kuna wakati alinunua ''sports car,'' nyekundu.
Yanga walipata sana shida na gari ile.
Na unajua kuwa unazi wa enzi zile ulikuwa wa kufanyiana vitimbi
wala hakuna chuki ndani ya nafsi maana wote wakijuana toka utoto
wao.
Siku moja Yanga wamepigwa mbao na Sunderland na Salum Ali
Sunderland wakimuita, ''Jini,'' alitingisha nyavu kama mara mbili hivi.
Hiyo kombe uwanjani Ilala Stadium.
Siku hizo Yanga wapo Mtaa wa Sukuma karibu na chuo cha Sharif
Abdulrahman.
Usiku Yanga wako club pale wamejikunyata, wanawaza mabao
tuliowapiga.
Salium Ali kachukua kikombe anakuja kwa miguu hadi Sukuma.
Sunderland siku hizo club yao iko Mtaa wa Kongo.
Kushtuka, Yanga wanamuona Salum Ali huyu hapa keshawasimamia
mbele yao kama jini aliyetumwa.
Salum Ali anawaambia Yanga, ''Nyie Makwala haya nimekuleteeni
kikombe hiki chukueni...''
Yanga wako kimya wanajifanya kama hawamsikii vile.
Basi Salum Ali katamba sana pale na jamaa sasa wamejazana pale
club wanacheka.
Kisha huyo kabeba kombe lake anaondoka anawaambia, ''Haya kama
hamkitaki kikombe mimi nakwenda zangu.''
Jamaa mmoja wa Yanga akasema, ''Wallahi leo Jini katuweza kweli
kweli lakini huyu Salum wewe mwachie tu siku tukiwafunga mimi
nitakwenda kukesha nyumbani kwake namuudhi kama alivyotuudhi
sie leo.''
Washabiki wapenda mpira hawa leo hawapo na Dar es Salaam ile pia
imekwenda zake.
Miaka mingi imepita na nimepoteza mapenzi ya mpira.
Jirani yangu kuna rafiki yangu anaitwa Kambi Kilago, Mzaramo
na sijui kwa nini Wazaramo wanapenda Yanga labda kwa kuwa
viongozi wa juu enzi zile walikuwa Wazaramo kama Kondo Kipwata
kisha Mangara Tabu.
Kambi ana genge jirani yangu anauza matunda na mimi mteja wake
mkubwa.
Nikifika pale namuona Kambi anavyowagaragaza Simba wenzangu
anawafunga mdomo hawana majibu.
Anavyotunanga roho inaniuma lakini nikasema nasubiri hawa Yanga
wafungwe nakwenda kwa Kambi kuweka ligi na yeye, huyu hanijui
mimi.
Basi siku ya siku nikenda kumkomesha.
Weee!
Kafunga mdomo.
Vijana wa mtaani walijazana pale kunisikiliza.
Siku hizi rafiki yangu Kambi kaja na mpya akiniona yuleee nakuja
anajidai anasikiliza simu.
Sikumuacha nikenda kwanza nikapiga wito kuwaita jamaa wanisikize
ninavyomtoa raha Kambi Kilago.
''Kambi rafiki yangu kipenzi ongea na simu lakini najua hiyo ni geresha
unanisikia vizuri sana.
Kama ulivyosema kuwa sisi Simba hatuna mpira wala hatutakwea pipa
kwa muda mrefu na mechi zetu tutaishia na Mtibwa.
Sawa nimekubali lakini nakupa taarifa kuwa tumeagiza majoho mekundu
na vuvuzela nyekundu kutoka bondeni hizi makhsusi kwa kukuzomeeni kila
mkicheza na lazima mfungwe tu.''
Sasa nikimaliza hasira zangu namuuliza Kambi bei ya ndizi.
Ananitajia huku machozi yanamtoka kwa kucheka.
''Kambi mbona unanifanyia aghali mtani wangu au ndiyo haya maneno
yangu?
Usiwasikize hawa jamaa fitna wanataka kutugombanisha mbwiga...''
No comments:
Post a Comment