TAAZIA
ABOUD
JUMBE 1920 - 2016
Mzee Aboud Jumbe na Mwandishi |
George Githii alikuwa
Mhariri Mkuu wa gazeti la Nation. Githii aliandika taazia ya Jomo Kenyatta
wakati Kenyatta yu hai hajafa. Bahati mbaya sana kwa Githii, Kenyatta akapata
taarifa kuwa kaandikiwa taazia mapema inamsubiri afe tu Githii aichape.
Kenyatta hakufurahishwa na habari ile hata kidogo na inasemekana alimwita
Githii Gatundu kwa ‘’mazungumzo.’’ Kenyatta hakupendezwa na kitendo kile kwa
kuwa yeye akiogopa kifo na akiogopa kukutana na malaika wa mauti, hakutaka mtu
amkumbushe kifo.
Aboud Jumbe alikuwa na
yakini ya kukutana na Mola wake na hakusubiri mtu kumkumbusha hilo. Aboud Jumbe
alijikumbushs mwenyewe kifo na akaandika kwa mkono wake mwenyewe usia wake na
vipi angependa mazishi yake yawe. Hii ndiyo tofauti kubwa kati ya viongozi hawa
wawili. Aboud Jumbe alikitegemea kifo muda wowote na akajitayarisha na siku
atakayokutana na Mola wake. Usia wa Jumbe vipi azikwe umewashtua wengi katika
serikali ya Tanzania kwani alikataa kuzikwa nje ya taratibu za Kiislam. Kwa ajili hii basi Aboud Jumbe alizikwa kama Uislam
ulivyofundisha na kuwa kiongozi wa kwanza wa juu katika historia ya Tanzania kuhitimishwa
nje ya utaratibu uiiozoeleka wa ‘’sherehe.’’
Nimejuana na Mzee Jumbe
katika takriban miaka ishirini na tano ya mwisho wa maisha yake. Huu usia ambao
umezunguka sana katika mitandao ya jamii na kuzungumzwa sana mara tu
ulipotolewa hadharani, mimi na wenzangu tuliusikia kutoka kinywani kwake
mwenyewe. Mimi na wenzangu tulikuwa nyumbani kwake Mji Mwema na Mzee Jumbe
akawa anatukumbusha sisi kama wanae hatari ya mja kutekwa na dunia akaisahau
akhera kama vile iko mbali sana. Hiyo ndiyo siku alipotueleza kuhusu usia huu.
Alituambia kuwa baada ya kuandika usia wake akamwita kiongozi mmoja wa juu
katika Serikali ya Muungano kumfahamisha kuhusu usia ule na vipi angelipenda
azikwe umauti utakapomfika. Alimweleza kuwa yeye angependa kuzikwa kama
wanavyozikwa Waislam kwa mujibu wa sharia na akamsisitizia kuwa asingependa
afanyiwe yale yaliyoko nje ya Uislam, mojawapo likiwa jeneza lake kufunikwa
bendera. Mzee Jumbe akatueleza kuwa jibu alilotoa yule kiongozi lilimshangaza.
Anasema yule kiongozi alimwambia Mzee Jumbe kuwa asiwe na hofu yote aliyoagiza
katika usia wake watatekeleza. Mzee Jumbe akasema kwa masikitiko kuwa yeye
hakutegemea jibu hili peke yake bali alitegema kuwa na yeye kwa kuwa ni Muislam
angemuunga mkono na kusema kuwa hata yeye angependa kuzikwa kama Mtume (SAW)
alivyofundisha. Hili kiongozi yule hakulisema. Msisitizo wake ulikuwa kwenye
utekelezaji wa usia wa Mzee Jumbe, yeye atazikwa kwa, ‘’sherehe’’ na bendera
juu ya jeneza lake. Hivi ndivyo iliyotokea miaka michache baadae. Kiongozi huyu
alifariki ghafla na akazikwa kwa, ‘’sherehe,’’ na jeneza lake likafunikwa
bendera ya CCM. Bahati mbaya sana kwake usia wa Mzee Jumbe haukumzindua.
Kenyatta alisoma taazia
yake mwenyewe yungali hai akaghadhibika akamuita George Githii Gatundu kwa
makemeo. Kiongozi huyu aliusoma usia wa Mzee Jumbe lakini yeye aliona haumuhusu.
Hivi ndivyo Mzee Jumbe alivyokuwa, tofauti mno na viongozi wenzake. Kuna
mwandishi mmoja katika taazia aliyomwandikia Mzee Jumbe, kwa kutoelewa maisha
ya Mzee Jumbe kawapa wasomaji wake picha ya kuwa Mzee Jumbe amekufa akiwa
‘’mpweke.’’ Hii si kweli watu walikuwa hawapungui nyumbani kwake Mji Mwema. Nimekuwa
nikienda nyumbani kwa Mzee Jumbe mimi na wenzangu mara ambazo hata siwezi
kuzihesabu na sikupata hisia hata kidogo kama kuwa Mzee Jumbe alikuwa mpweke.
Geti lake lilikuwa wazi ingawa kulikuwa na askari na silaha wakilinda pale.
Ukiwa pale nyumbani kwake muda wote utawaona majirani zake wakiingia na kutoka
ndoo kichwani wakija kuteka maji, akina mama na watoto mgongoni na wengine
wakiwa na watoto wadogo wamewatangulia au wako nyuma yao. Askari walinzi
wakiwaachia waingie na kutoka kama watu wa nyumbani. Nyumba ya Mzee Jumbe
haikuwa nyumba iliyojiinamia. Sikuenda kwa Mzee Jumbe nikakuta lile geti
limefungwa hata siku moja. Nyumba ilizidi uchangamfu kwa wavuvi kuingia na
kutoka kuja kufata barafu kwani Mzee Jumbe alikuwa na mtambo wa kisasa kabisa
wa kutengenzeza vinoo vya barufu kwa ajili ya uvuvi. Wakati wote wavuvi
walikuwa wakipita nyumbani kwake kuja kununua barafu. Siku moja katika
mazungumzo Mzee Jumbe katika hulka yake ya kutuchekesha alituambia kuwa yeye
hakutaka kuwa tegemezi akae kusubiri hundi ya pensheni maana alisema huenda
siku bwana fedha akasahau kukutumbukizia hundi yako. Yeye kwa ajili hii akaamua
ajishughulishe kidogo na ndiyo akaleta mtambo wa barafu. Mzee Jumbe
akatumalizia kwa kusema alichagua biashara ile ya barafu kwa sababu alijua
itawasaidia sana nduguze wavuvi. Si wengi wenye kulijia hili lakini ukweli ni
kuwa babu yake mkuu Mzee Othman Kitamaguru aliondoka Mji Mwema na kuhamia
Chukwani Zanzibar kuendeleza shughuli zake za uvuvi.
Aboud Jumbe hakuwamo
katika mpango wa mapinduzi. Huenda hili likawashangaza watu wengi. Labda kwake
yeye hii ni kheri kubwa sana na ilimpa utulivu wa nafsi kwani wale wachache
kutoka Zanzibar na Tanganyika waliohusika na mipango ya mapinduzi, hawakutaka
baada ya mapinduzi majina yao yanasibishwe na mapinduzi yale. Kwani ni muda
mfupi tu baada ya mapinduzi, mauaji na unyama uliofanyika Zanzibar ukajulikana
dunia nzima. Kulikuwa na kambi Kipumbwi, nje kidogo ya Tanga ambapo kuliwekwa
mamluki wengi wao Wamakonde kutoka mashamba ya mkonge ya Sakura. Hawa ndiyo
waliovushwa na kuingia Zanzibar kusaidia mapinduzi na inasemekana kuwa hawa Wamakonde
waliua watu wengi sana hasa Waarabu. Kila Mzanzibari kiongozi niliyezungumzanae kuhusu
mamluki hawa au hata kuwapo kambi yao Kipumbwi alisema hana taarifa hizo. Lakini
kwa sasa hii si siri tena kwani kitabu cha Dr. Harith Ghassany, ‘’Kwaheri
Ukoloni Kwaheri Uhuru,’’ kimeeleza kila kitu. Aboud Jumbe bila shaka alishukuru
kuwa hakuwa na mkono katika mpango huu kwani imeshadhihirika hivi sasa kuwa mauaji
yale yalikuwa mauaji ya kimbari.
Swali ambalo litakuja ni
kuwa nani aliidhinisha kuwepo kwa kambi hii katika ardhi ya Tanganyika? Baada
ya swali hili kujibiwa ndipo yatafuata maswali mengine ambayo historia ya
Zanzibar na Aboud Jumbe akiwa mmoja wa walioandika historia hii ataweza kutupa
majibu. Hivi ni kweli Mwalimu Nyerere alisaidia kuipindua serikali ya Waziri
Mkuu Mohamed Shamte kwa kuwa ilikuwa serikali dhalim au kulikuwa na sababu
nyingine ambayo wanamapinduzi hawakuijua?
Inajulikana wazi kuwa
mgongano wa Nyerere na Aboud Jumbe umetokana na Jumbe kuhoji muungano. Hiki ni
kisa maarufu. Bahati mbaya hakuna mwandishi aliyekwenda zaidi ya hapo na
kueleza kwa nini suala la Zanzibar kuwa na uhuru lau kidogo wa kujiamulia mambo
yake likawa jambo kubwa sana kwa Nyerere? Suala la Zanzibar kuwa huru lilikuwa
jambo zito kwa Nyerere kwa sababu ikiwa Zanzibar itatoka mikononi kwake itakuwa
yeye alifanya kazi ya bure kusaidia mapinduzi ya Zanzibar. Kwa Aboud Jumbe
kuitaka iwe huru pawepo na serikali tatu hii ilikuwa vita ya wazi dhidi ya
Nyerere. Lakini muhimu kujiuliza Aboud Jumbe alifika vipi katika hali ile ya
kuidai Zanzibar kutoka kwa Nyerere? Katika kitabu chake Dr. Harith Ghassany
anaeleza Ali Muhsin anavyoieleza Zanzibar kama Ngome ya Kusini ya Uislam ambayo
maadui wa Uislam walidhani wakiiangusha ngome hiyo basi na Uislam nao
utaanguka. Ilimchukua muda gani kwa Aboud Jumbe na yeye kuliona hili ambalo
wale waliopinduliwa waliliona zamani? Ni kweli kuwa Zanzibar ile kabla ya
mapinduzi si Zanzibar hii ya mapinduzi.
Ili kumwelewa Aboud Jumbe
hadi kufikia pale ambapo aligongana na Nyerere ni vyema kwanza ijulikane kuwa
Aboud Jumbe aliupenda Uislam wake kama vile Nyerere alivyokuwa anaupenda
Ukatoliki wake ila tofauti kati yao ilikuwa moja tu. Wakati Nyerere alifanya
mipango yake ya kusaidia dini yake kwa usiri wa hali ya juu, Jumbe yeye
alifanya juhudi zake waziwazi bila ya kificho. Aboud Jumbe alisaidia kuanzishwa
kwa Baraza la Misikiti Tanzania (BAMITA) mwaka wa 1984. Hii ni miaka 12 baada
yeye kuwa rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania. Historia ya Nyerere
inaonyesha kuwa hapajatokea kiongozi katika serikali yake akajinasibisha na
Uislam na Waislam akanusurika. Aboud Jumbe kwa kule kujinasibisha na Uislam
alikuwa tayari kwa fikra ya Nyerere kamtangazia vita. Nyerere alitoa, ‘’Presidential
Notice,’’ akionya kuhusu viongozi wa serikali kufanya shughuli za dini.
Kwa hakika haikuwa
‘’viongozi wa serikali,’’ onyo lile lilikuwa kwa Makamu wa Rais Aboud Jumbe
moja kwa moja. Uislam lilikuwa suala nyeti sana kwa Nyerere na alitumia nguvu za
dola kuwamaliza wote walijaribu kuutia nguvu Uislam Tanzania. Sheikh Hassan bin
Amir, Tewa Said Tewa, Bi. Titi Mohamed, Abubakar Mwilima na Prof. Kighoma Malima
wote hawa walishughulikiwa barabara na wote wakajikuta nje ya siasa za
Tanzania, achilia mbali wale waliowekwa kizuizini. Uislm lilikuwa jambo
linalotisha na hakuna kiongozi aliyekuwa na ujasiri wa kuleta agenda hiyo
mezani.
Aboud Jumbe alikuwako katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM siku Abubakar Mwilima alivyomkabili
Nyerere uso kwa macho kama Rais wa Tanzania na mwenyekiti wa CCM na kumuuliza
imekuwaje Waislam wako nyuma wakati wenzao wanasongambele. Nyerere alikuwa
kimya. Ukumbi mzima vilevile ulikuwa kimya. Wajumbe walikuwa wameshika roho zao
mkononi. Swali hilo hakuna aliyekuwa hajui kuwa ni mwiko mkubwa kuulizwa. Kwa
sekunde chache ilikuwa kama vile dunia imesimama, haizunguki, imetuwama mahali
pamoja. Nyerere aliahirisha kikao wajumbe wakanywe chai. Aboud Jumbe alikuwako
na alishuhudia jinsi wajumbe wa mkutano walivyomkimbia Mwilima. Hakuna
aliyetaka kumkaribia wala kuongea na yeye. Mwilima alikaa mezani akinywa chai
peke yake. Wenzake wote hata wale marafiki zake wa siku zote walimkalia mbali. Waliporudi
kikaoni Nyerere aliendelea na mkutano kama vile hakuna kilichopitika. Nyerere
hakutaka kulijibu swali la Sheikh Mwilima.
Haukupita muda Sheikh
Abubakar Mwilima aliitwa kuhojiwa kuhusu kuuza dola za Kimarekani kinyemela.
Haukupita muda na yeye kama wenzake waliomtangulia akajikuta yuko nje.
Siku moja Mzee Jumbe
alitupa kisa cha, ‘’The Long Letter.’’ Hii barua ndefu ilikuwa ile barua
iliyotayarishwa na Bashir Swanzy Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar ndani yake yakiwa
mashtaka dhidi ya Muungano kuhoji uhalali wa wa Muungano. Barua hii
ilikuwa imekusudiwa iwasilishwe kwenye
Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Mzee Jumbe alikuwa akitualika
mara kwa mara nyumbani kwake na yeye akipenda sana kuandalia. Mzee Jumbe
akikualika nyumbani kwake kula, inabidi ujitayarishe vyema kwani alikuwa
akichafua uwanja. Ilikuwa katika moja ya barza zetu kama hizi ndipo siku hiyo
akatuhadithia yale yaliyotokea Dodoma kati yake na Nyerere kupelekea yeye
kujiuzulu nyadhifa zake zote. Mzee Jumbe alikuwa ana namna ya kuhadithia jambo
hata liwe zito vipi, wewe msikilizaji likakufikia kwa wepesi na wakati mwingine
katika njia ya kukufanya ucheke. Alikuwa keshatuhadithia jinsi mashtaka yale
yalivyokuwa yametayarishwa na hapo ndipo alipokuja na jina hilo la, ‘’The Long
Letter,’’ na sisi ikawa huo waraka tunauita, ‘’Long Letter,’’ kama yeye
mwenyewe, katika njia ya utani alivyopenda kuita.
Mzee Jumbe alipokuwa
anaeleza kupotea kwa waraka ule na ukaibuka mikononi kwa Nyerere Dodoma, Mzee
Jumbe alikuwa akituchekesha alivyokuwa akitueleza jinsi Nyerere
alivyoinga’nga’nia, ‘’The Long Letter,’’ na akawa anasoma vipande alivyovipenda
yeye na Jumbe akimwambia endelea na soma na mahali pengine, Nyerere alivyokuwa
hataki akishikilia hapo hapo kama mtoto mdogo aliyepewa pipi na sasa anahisi anataka
kunyang’ang’anywa. Huku tukishusha biryani na juisi baridi, hakika ilikuwa ni
burdani ya aina yake. Mzee Jumbe akicheka na sisi wasikilizaji tukicheka pia. Mzee
Jumbe Uislam na kukubali qadar ya Allah kulikuwa kumemweka pazuri sana. Mzee Jumbe hakuwa mtu aliyejuta kutoka katika
uongozi kiasi alikuwa sasa anatushekesha kuhusu madhila ya uongozi. Akawa siku
zote tukiizungumza na yeye kuhusu, ‘’The Long Letter,’’ masikitiko yake ni kuwa
kuikosa, ‘’The Long Letter,’’ hawezi kuandika kitabu kuhusu matatizo ya Muungano.
Siku zikenda na miaka
ikapita. Siku moja tuko kwake akatuangushia bomu lililotuacha midomo wazi. Mzee
Jumbe akatuambia kuwa, ‘’The Long Letter,’’ kaiona nyumbani kwake Migombani
kwenye, ‘’Study Room,’’ yake. Tulimuuliza Mzee Jumbe kaiona vipi? Yeye
akatujibu kuwa na yeye amepigwa na mshangao kama tulivyopigwa sisi. Akatuambia
kuwa na keshaanza kuandika kitabu. Siku zile Mzee Jumbe tayari alikuwa
keshaanza kupoteza nuru ya macho na akiandika na kusoma kwa msaada wa ‘’lens.’’
Iko siku mimi na mwenzangu sasa tukihariri mswada wa kitabu cha Mzee Jumbe
kilichokuja kujulikana kama, ‘’The Partner-ship: Tanganyika-Zanzibar Union 30
Turbulent Years.’’ alitualika nyumbani
kwake Zanzibar Migombani na tulisafiri meli moja. Siku ile alituingiza katika
‘’Study Room,’’ yake na akatuonyesha ‘’desk,’’ alipoikuta, ‘’The Long Letter,’’ikimsubiri,
imerejeshwa kama ilivyoibiwa ofsini kwake Ikulu Zanzibar. Kwangu mimi binafsi
ilikuwa furaha ya pekee. Nakumbuka wakati tumekaa tunajiuliza ni nani
aliyeirudisha, ‘’The Long Letter,’’ nyumbani kwa Mzee Jumbe na asionekane na
mtu. Hakika kilikuwa kitendawili. Mzee Jumbe alikuwa mtu wa kupenda kuandalia
chakula kama nilivyosema hapo awali. Wakati sote tumeinamisha vichwa
tunamsikiliza jinsi alivyoiona, ‘’The Long Letter,'' ghafla wakaingia watu wa ‘’catering,’’ na mavazi yao meupe
wamebeba sahani za vyakula wanatuandalia. Ilikuwa kiasi cha saa kumi na moja
jioni.
Kile ambacho Aboud Jumbe
hakupewa nafasi kukisema Dodoma Allah akamuwezesha kukisema miaka kumi baadae
kupitia kitabu chake, ‘’The Partner-ship: Tanganyika-Zanzibar Union 30
Turbulent Years.’’ Mzee Jumbe alikuwa mtu wa vichekesho sana. Tulikuwa
tunachagua picha za kitabu sasa tukawa tunaangalia picha moja Karume na Nyerere
wamepanda gari la wazi. Mmoja wetu akamuuliza Mzee Jumbe, ‘’Hii picha tuweke,
‘’caption gani?’’ Mzee Jumbe mara moja hapo kwa hapo akajibu, ‘’Karume being
taken for a ride by Nyerere.’’ Sote tuliangua kicheko.
Nadhani hapa tulipofika
panatosha. Huwezi mtu ukammaliza Mzee Jumbe. Nina mengi ningeweza kueleza
kuhusu Aboud Jumbe na juhudi zake za kuwasaidia Waislam khasa wa Bara. Mzee
Jumbe alikuwa karibu sana na viongozi wa Waislam Bara na alijitahidi sana
kuwasaidia kwa hali na mali akifanya mambo yake kimya kimya. Darul Iman
walipofanyiwa hujuma wasijenge shule ya ufundi Kibaha. Darul Iman walifunga
virago na fedha zile wakataka kuzipeleka Somalia. Mzee Jumbe hakukubali
aliwaambia kuwa ikiwa watafanya hivyo watakuwa wamewadhulumu Waislam wa
Tanzania kwani hizo fedha zimetolewa kwao. Mzee Jumbe akawaambia kuwa Tanzania
ni nchi mbili, ikiwa bara Waislam wanazuiliwa kujengewa hiyo shule hizo fedha
zipelekwe Zanzibar na yeye atahakikisha kuwa ardhi inapatikana na shule
inajengwa. Mzee Jumbe alipotuambia kuwa kanifanikiwa kuzirejesha fedha za Darul
Iman na shule itajengwa Zanzibar, tulimshauri kuwa itakuwa bora badala ya shule
kijengwe Chuo Kikuu. Hivi ndivyo ilivyokuja kujengwa Zanzibar University,
Tunguu.
Allah tunakuomba
umsamehe dhambi zake mzee wetu huyu na umweke mahali pema peponi.
No comments:
Post a Comment