Ndugu zangu,
Kila watu
duniani wana mila na dasturi zao ambazo ni muhimu kuzilinda iwapo sharia
hizo ni nzuri kwa jamii kwa jumla na zina manufaa kwa umma na iwapo haziwanyimi
haki zao walio wachache. Sharia iliyowekwa na wakoloni wa Kiingereza
ilitokana na Waislamu wenyewe walio wengi kutaka pawe na kizuwizi
ambacho alitakiwa Muislamu akaombe na atoe sababu za kutaka kuingia
madhambini kwa kulewa. Ilikuwa kama kuhakikisha kuwa huyo Muislamu anayetaka
kulewa ana akili zake timamu. Ofisi ya D.C. ikiona kweli ana akili timamu,
basi hupewa hiyo rukhsa ya kujitia madhambini. Khiyari ni yake mwenyewe. Pili,
sharia hiyo ilitokana na Wazanzibari wake waliolalamika kuwa waume zao
hutumia kipato chao kikubwa sana au chote katika ulevi na wake zao na watoto
wakawa hawana hata chakula; na kuna sababu nyinginezo pia.
Iwapo mtu alikuwa
si Muislamu, sidhani kuwa naye pia alitakiwa kuwa na liseni kununua ulevi. Na
iwe iwavyo. Hapa kuna haki mbili zilikuwa zikilindwa. Ya kwanza ni haki ya
anayetaka kulewa, na ya pili ya umma -- ambao sehemu kubwa kabisa ilikuwa
ni ya Waislamu -- ambao mara nyingi husoneneka kwa vitendo na vitimbi
vya walevi. Iwapo mtu ni mlevi na baada ya kulewe hufanya visa na miqasa ya
kuudhi watu mitaani kwa maneno yake na vitendo vyake kama kutoa nyuchi
zake hadharani na kwenda haja na huku wazee na vijana huyaona makruhi
ayafanyayo, kiumbe kama huyo huwa hafai kulewa wala kupewa rukhsa ya kulewa
maana haki yake ya kulewa inaingilia, pakubwa sana, haki ya umma wenye kuudhiwa
na vitendo vyake vyenye kuvujna muruwa wa jamii. Na vijana wa kike na kiume
huoneshwa vituko na kusikilizishwa kwa wasiyofaa kuyaona na
kuyasikia kwa mujibu wa mila yetu. Na mila na dini yetu huwa zinapigwa
dharaba kubwa na chafu bila ya sababu. Uhuru wa mtu kulewa haina maana ya wengi
kunyimwa uhuru wao wa kuishi maisha ya muruwa kwa kuingiliwa mitaana
mwao na machafu ya walevi, hata iwapo si wote.
Fikiria jambo moja
jingine muhimu linalokhusu uchumi wa mkoloni. Mkoloni wa Kiingereza
alikuwa na mashirika yake mengi ya kutengenezea ulevi wa kila aina tokea
kwao Uingereza mpaka katika makoloni yake. Wala hakuwa na lolote linalomkataza
kuuza ulevi. Kwa hakika, mashirika ya ulevi yaliipatia Uingereza faida kubwa
sana ya biashara ya ulevi. Hivyo basi, kwa nini Mkoloni ajinyime faida
hiyo kwa kutunga sharia ya kuzuia raia zake katika makoloni wasiweze kununua
ulevi ilakwa kibali? Waliowalazimisha Wakoloni Zanzibar ni idadi kubwa ya
Waislamu waliokuwepo na madai yao ya kuwa na sharia hiyo, si jinginelo.
Wazanzibari Waislamu walikuwa wakilinda ya dini yao na mila yao bila ya
kuwanyima wengineo haki zao. Muingereza hakuwa na shida ya kuyakubali matakwa
ya Wazanzibari wengi kwa sababu Zanzibar ni nchi ndogo sana na kibiashara
ikuwa haiwashi wala haizimi ukiangalia idadi ya makoloni iliyokuwa nayo.
Tulikuwa na mila njema
kabisa Duniani, kwa uadilifu wake, usalama, upole, mapenzi na kusaidiana kwa
kila njia. Ukisikia mtu ameuliwa au amejiua, Zanzibar nzima ilikuwa
ikistaajabishwa. Leo kuuwa kumekuwa kitendo kisitostaajabisha tena. Ulevi
uliwekewa vikwazo na watu wakawa wanajihishimu na kuhishimiana. Mtu akipotelewa
na kipochi chake ama hupelekewa nyumbani au hupelekwa polisi na akatafutwa
mwenye haki yake. leo unatafutiwa kila njia ya kuchomolewa haki
yako. Kulikuwa hakuna madanguro, na kama yalikuwepo basi yalikuwepo kwa
siri kabisa, leo tembelea Forodhani na katika fukwe nyingi uwaone mabarobaro na
washichana, na wasichana wengine hata hawawajavunja ungo (baleghe)
wanavyojiuza. Kwa ufupi sana, khasara kubwa kabisa iliyoikumba Zanzibar si ya
kutawaliwa tu na wale wasiokuwa na dini za kisawasawa Tanganyika, na
kuunyakuliwa uhuru wake, bali pia ya kuuwawa kwa lugha, mila, dasturi, utu
na kila kilichokuwa Zanzibar kikijivunia nacho, na kutoudhibiti uhuru
wa kulewa mtu apendavyo ni sehemu moja ya kuwa hatujitambui na hatutambuliwi
wala hatutambulikani Duniani.
No comments:
Post a Comment