Sunday, 18 September 2016

BI. MAUNDA BINTI LUKOYO MKE WA AFANDE PLANTAN NA WANAE


...kwa kweli jina la Kizulu la Affande Plantan lilikuwa Shangaan. Hili jina lilitokana na kijiji katika Inhambane Msumbiji, walikotoka Sykes Mbuwane na Affande Plantan. Chini ya Herman von Wissman Wajerumani waliwaajiri Wazulu 400 kutoka Msumbiji kama mamluki na kujanao ndani ya manowari hadi Pangani ili wapigane na Abushiri na Chifu Mkwawa. Hii ilikuwa katika miaka ya mwisho ya 1800...'' 

Photo
Bi Maunda Binti Lukoyo mke wa Affande Plantan kabila Mmanyema, Mkusu kutoka Belgian Congo
Mama yao na Thomas, Schneider na Mashado Plantan
(Picha kwa hisani ya Bi. Maunda Plantan mjukuu wa Affande Plantan na Maunda Binti Lukoyo)
''...pamoja na Kleist katika mji wa wa Dar es Salaam walikuwepo ndugu wa mbali watatu, Mwalimu Thomas Plantan, (hilo jina Mwalimu alipewa kwa sababu alikuwa Mwalimu wa shule), Schneider Abdillah Plantan na Ramadhani Mashado Plantan. Hawa Wazulu waliweza kutambulika kwa urahisi kutokana na majina yao ya Kikristo ingawa wao wenyewe walikuwa Waislam. Majina hayo yalikuwa na mchanganyiko wa majina ya Kijerumani, Kireno na Kiingereza; kama vilevile Kleist na Schneider ni majina ya Kijerumani; Mashado ambalo ni jina la Kireno na Thomas ni la Kiingereza. Wote hao, Kleist, Mwalimu Thomas, Schneider na Mashado baadaye walifanya kazi kubwa katika kupiga vita ukoloni na katika kuupeleka mbele Uislamu, kabla na baada ya uhuru. Bahati mbaya majina haya ya Kiislamu ya wazalendo hawa hayakujitokeza sana na badala yake  walijulikana zaidi kwa majina yao ya Kizungu waliyoyarithi kutoka Wajerumani kupitia wazee wao wa Kizulu...''

Mwandishi akizungumza na Bi. Maunda Plantan nyumbani kwa Bi. Maunda Magomeni Mikumi
Bi. Maunda ni mwanamke wa kwanza kutangaza Sauti ya Dar es Salaam radio ilipoanzishwa
Tanganyika 1952
''...baada ya kuwashinda wananchi wa Tanganyika, Wissman alitunzwa na serikali yake na akafanywa Gavana wa German East Africa kati ya mwaka wa 1895 na 1896. Wazulu nao kwa kuwa walichangia katika ushindi huo na wao hawakutoka mikono mitupu, Wajerumani walitunza. Kwa kuwa Mohosh hakuweza kudai uchifu ugenini alifanywa kuwa mkubwa wa jeshi la polisi la Wajerumani (Germany Constabulary) katika mji wa Dar es Salaam na hapo ndipo alipopata jina hili la Affande Plantan. Wazulu katika jeshi la Wajerumani walikuwa wakilipwa mishahara mizuri na hali zao zilikuwa bora ukilinganisha na wenyeji. Wenyeji wengi waliajiriwa na serikali katika jeshi kama vibarua. Hii ndiyo sababu hasa iliyomfanya Kleist apate malezi ya hali juu yaliyompelekea kupata elimu, kazi nzuri na mwishowe kuwa mmoja wa watu mashuhuri katika mji wa Dar es Salaam.

Thomas Soudt Plantan
Baba Yake  Bi Maunda Plantan

Kleist alipelekwa kusoma shule ya Wajeruman iiliyokuwa OceanRoadHospital ambako alijifunza Kijerumani, kupiga chapa na hati mkato, ujuzi adimu na wa thamani sana kwa Mwafrika enzi zile. Katika nyumba ya Affande Plantan, Kleist alilelewa pamoja na watoto wa Affande Plantan mwenyewe, Schneider Abdillah, Ramadhani Mashado na Thomas Soudtz mtoto wa ndugu yake wa mbali kidogo. Watoto hawa wote walipata elimu nzuri ambayo iliwawezesha kuwa watu muhimu. Mashado Plantan alikuja kuajiriwa kama askari akiwa na cheo kilichomtabulisha kama ''English Speaking Policeman,'' yaani askari anaezungumza Kiingereza,  na baadae alikuja kuwa mhariri wa magazeti aliyoyamiliki mwenyewe. Gazeti lake la kwanza likiitwa ''Dunia.'' Hii ilikuwa kabla ya 1938 na. wakati wa Vita Vya Pili Vya Dunia mwaka wa 1938 akaanzisha gazeti lililoitwa ''Zuhra.'' Thomas Saudtz alikuja kuwa mwalimu wa shule, Schneider alikuwa mkulima na katika siku za mwisho wa uhai wake aliungana na Sheikh Hassan bin Amir kama katibu wa Daawat Islamiyya (Mwito kwa Waislam).

Vita ya Kwanza ya Dunia (1914-1918)
''...ilikuwa wakati bataliani ya Schneider na Kleist ipo Korogwe, mji uliopo maili chache kutoka Tanga, katika kijiji kiitwacho Semanya ndipo Kleist alipopokea habari kuwa Affande Plantan, baba yake Schneider amefariki Dar es Salaam. Plantan alikuwa amekufa kwa homa ya matumbo tarehe 11 December 1914. Wajerumani walisimamisha vita kwa siku saba kwa heshima ya Affande Plantan...

Waarabu waliungana na Waingereza kuwatimua Wajerumani Tangayika. Bado baadhi yao walikuwa na kumbukumbu ya kitendo cha kikatili cha Wajeruani kwa shujaa wao Abushiri ambae walimnyonga mwaka 1889. Historia ikajirudia upya; Kleist na Schneider waliingia katika mapigano Mwele Ndogo dhidi ya adui wa zamani wa baba yao na adui wa Wajerumani ñ Waarabu. Mapambano haya yalifanyika siku ya mkesha wa Krismasi mwaka wa 1915 katika sehemu ile ile ambayo Sykes Mbuwane na Affande Plantan mamluki wa Kizulu waliteremka kwenye meli kuja kuwaongezea nguvu Wajerumani waliokuwa wakipigana na Waarabu na Abushiri bin Salim na Mkwawa... 

Mashado Ramadhani Plantan alikuja Tanganyika kutoka Mozambique akiwa mtoto mdogo mwaka 1905 wakati nchi ipo katika vita vya Maji Maji dhidi ya Wajerumani. Mwaka 1924 alirudi Msumbiji na alisafiri kwenda Lisbon kwa pasi ya Kireno. Wale waliomfahamu wanasema kwa kiwango cha miaka ya 1950, Mashado Plantan alikuwa mtu mjuzi wa mambo. Alikuwa miongoni mwa wanachama wa mwanzoni wa African Association ilipoanzishwa mwaka 1929 na miongoni mwa wanachama wa awali kujiunga na TANU pale ilipoasisiwa mwaka 1954.

Vita Kuu ya Pili 1938-1945
Askari wa zamani waliopigana katika jeshi la Wajerumani dhidi ya Waingereza katika ardhi ya Tanganyika wakati wa Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia kati ya mwaka 1914-1918 walimuunga mkono Hitler, ingawa si wazi wazi kwa kuwa kufanya hivyo kungekuwa usaliti na uhaini dhidi ya Himaya ya Waingereza. Hata hivyo hilo halikumzuia Schneider, askari wa Kijerumani wa Vita Kuu ya Kwanza vya Dunia, kutembea huku na kule katika mitaa ya Dar es Salaam akiwachochea watu wasimuunge mkono Winston Churchill katika vita vyake dhidi ya Adolf Hitler. Schneider alikamatwa na kuwekwa kizuizini huko Mwanza, na hakufunguliwa hadi mwisho wa vita mwaka 1945...


Tanganyika African Association (TAA) 1950
Mwaka wa 1949,  Mwalimu Thomas Plantan ndiye aliyekuwa rais wa TAA.  Katibu wake alikuwa Clemet Mohammed Mtamila.

Unahitaji tu kuzipitia tahariri za Mashado Plantan katika gazeti la Zuhra ili kuweza kufahamu mambo yalivyokuwa nchini Tanganyika katika miaka ya 1950. Naye Mwalimu Thomas Plantan na damu yake ya Kizulu ya kupenda vita, baada ya kuwa yupo kwenye nchi yenye amani, aliielekeza banduki yake porini kuwinda wanyama. Hakuwa na muda kama rais wa TAA kushughulika na siasa. Uhodari wake katika kuwinda bado hadi leo unaweza kushuhudiwa nyumbani kwake Mtaa wa Masasi, Mission Quarters. Kuta za nyumbani kwake zimeshamiri mafuvu ya vichwa vya wanyama aliowaua huko porini. Kwa sabau alitumia wakati wake mwingi porini akiwinda,  hakuwa na muda wa kuitisha mikutano au kushughulikia mambo ya TAA...

Tanganyika African National Union (TANU) 1954
''...John Hatch wa Labour Party ya Uingereza alipokuja Dar es Salaam kwa mwaliko wa TANU Nyerere alikuwa kwao kijijini. Tutaona hapo baadae kidogo jinsi mgeni huyu Mwingereza alivyomgutusha Schneider kuhusu  TANU kuwashirikisha wanawake katika harakati za kudai uhuru.

Ali Mwinyi Tambwe alikuwa mkalimani wa Hatch. Denis Phombeah pamoja na katibu mkuu wa TANU, Oscar Kambona vilevile walihutubia halaiki ile. Hatch akiwa anaunga mkono ukombozi wa watu weusi aligundua kuwa TANU haikuwa na tawi la akina mama. Katika dhifa ya chai iliyoandaliwa na TANU kwa heshima yake, Hatch alilieleza tatizo hili kwa Schneider Plantan na John Rupia. Hatch alimwambia Schneider kwamba ili kuwa na chama chenye nguvu TANU isiwaache akina mama nyuma. Hatch alimwambia Schneider kwamba huko Uingereza Chama cha Labour kilikuwa kimejikita kwa wanawake kama moja ya nguzo yake kuu. Schneider alimwendea Bibi Tatu binti Mzee akamwomba kuanzisha tawi la akina mama kwa ajili ya TANU. Bibi Tatu binti Mzee alimpendekeza Bibi Titi Mohamed ndiye afanye kazi hiyo kwa sababu ya tabia yake ya ucheshi na kupenda kuchanganyika na watu...''

No comments: