Sunday, 4 September 2016

KUTOKA JF: JECHA, BARAKA SHAMTE NA QUISLING








CMP,
Inawezekana ikawa hapana kosa kwa Jecha kufikiriwa kupewa nishani.
Haya mambo yanafata jinsi taifa lilivyojenga utamaduni na historia yake.

Labda tujikite zaidi Zanzibar tuangalie historia yake baada ya mapinduzi.

Tukishaijua historia yake lau kwa uchache haitakuwa shida kuelewa kwa
nini ni muhimu sana Jecha kuenziwa hasa kwa wakati huu.

Tuanze na historia ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964.

Hapa ningependa nifanye rejea katika kitabu cha Dr. Harith Ghasany,
''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.''

Kitabu hiki katika makubwa kilichotufahamisha ni kuweko kwa kambi
Kipumbwi, Tanga iliyokuwa imeanzishwa makhsusi kwa kuwapa mafunzo
mamluki wa Kimakonde kuvamia Zanzibar na kusaidia katika kupindua
serikali ya Sheikh Mohamed Shamte.

Hawa mamluki walivushwa hadi Zanzibar na walishiriki katika mapinduzi
na inasemekana hawa mamluki ndiyo walioua Waarabu wengi.

Swali la kujiuliza ni nani walihusika na kambi hii.

Majina yaliyojitokeza katika kitabu cha Dr. Ghassany ni Ali Mwinyi
Tambwe,Jumanne Abdallah, Mohamed Omari Mkwawa 
na Abdallah
Kassim Hanga.


Mwaka wa 2014 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa nishani za mapinduzi
katika kuadhimisha miaka 50 ya mapinduzi.

Katika vinara wa mapinduzi kutoka Kambi ya Kipumbwi ni Ali Mwinyi Tambwe
peke yake aliyepewa Nishani ya Mapinduzi wengine wote hadi Kassim Hanga
hawakupewa heshima ile.

Lakini kitu cha ajabu ni kuwa ake wakati wa uhai wake Ali Mwinyi Tambwe 
alikuwa hataki jina lake lihusishwe na mapinduzi.

Inasemekana Ali Mwinyi alimkatalia  kumwambia Prof. Haroub Othman 
lolote kuhusu mapinduzi.

Taarifa nyingine zinasema alimfukuza nyumbani kwake.

Muhimu ni kujiuliza kipi kilimfanya Ali Mwinyi achukie jina lake kuhusishwa na
mapinduzi.

Je, ni yale mauaji?

Baada ya mapinduzi Abeid Amani Karume alizungumza na wale mamluki wa
Kipumbwi na aliwashukuru kwa kazi nzuri waliofanya.

Hakuna hata mmoja katika mamluki wa Kipumbwi ambae alipewa tuzo yoyote
ya kushiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar labda kwa sababu hakuna katika viongozi
wa Zanzibar anaekubali kuwa ilikuwapo Kambi Kipumbwi.

Baraka Shamte, mtoto wa Sheikh Mohamed Shamte ambae serikali yake ndiyo
iliyoangushwa yeye amepewa nishani ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mtu unaweza ukajiuliza iweje Baraka Shamte apewe nishani ya mapinduzi Hanga
anyimwe?

Nini sifa ya mtu kupewa nishani ya mapinduzi?

Mfano huu wa Baraka Shamte ni mfano mmoja tu ningeweza kueleza mengi na habari
za wengi waliofanya makubwa kukamilisha mipango ya mapinduzi lakini hawatambuliwi
hadi sasa.

Jecha...
Jecha kafanya jambo kubwa, zito na linalohitaji ujasiri wa kikomo.

Mtu yeyote jasiri wa mfano wa Jecha anastahili kuenziwa.

Ni Bahati mbaya sana Quisling yeye aliishia pabaya lakini ni kwa kuwa Manazi
walishindwa.

Laiti kama Manazi wangeshinda Quisling angevaa medali kifuani.
Juu ya haya Quisling kapata heshima ya aina yake.

Jina lake limekuwa msamiati wa Kiingereza ingawa kwa kweli haupendezi.

Quisling juu ya hayo hakukosa kila kitu ukifungua ''dictionary,'' utamkuta.
Jecha naye hatokosa kitu...

Jecha huenda akavaa medali katika kifua chake na akamshinda Quisling kwa kuwa
licha ya medali ataingia vilevile katika msamiati wa Kiswahili na jina lake litakuwa ndani
ya Kamusi.

Haya ndiyo maajabu ya historia.

Suala la Jecha linataka utulivu wa fikra ukajihangaisha na kutazama nyuma ili ujifunze
kwayo yale yaliyotangulia.

Kwa historia ya Zanzibar ilivyo haitoshangaza kwa Jecha kupewa medali.
Ikiwa Baraka Shamte kapewa kwa nini Jecha anyimwe?

No comments: